|
I/.
MTUME WA ALLAH AFICHA DHAMIRA YAKE.
Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasonga mbele na maswahaba wake mpaka akafika
katika bonde la Badri. Hapo akapiga kambi kando ya bonde lililo karibu na
Madinah. Bwana Mtume alikuwa katika hadhari kuu, akalifanya suala na makusudio
yake kuwa ni siri kubwa. Alifanya hivyo ili khabari isije kuvuja na kuwafikia
wanafiki na majasusi wa Makurayshi. Alifanya hivi ili kuficha mikakati na
muelekeo wake, hiyo ikiwa ni mojawapo ya mbinu za vita. Akaamrisha zikatwe
kengele walizofungiwa ngamia shingoni na akawa kila anapopiga kambi mahala
hupeleleza khabari za Makurayshi. Akiuliza khabari zao kwa uficho na hadhari
kuu.
Ibn
Is-haaq na wanazuoni wengine wa Sira-Allah awarehemu- wamepokea kwamba Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipiga kambi karibu kabisa na Badri.
Akampanda mnyama yeye na mmoja wa maswahaba wake, wakaenda mpaka kwa mzee
mmoja muarabu. Mtume akamuuliza khabari zilizomfikia za Makurayshi, Muhammad
na maswahaba wake. Yule mzee akamjibu: “Ukitupa khabari utapata khabari”.
Mtume akamwambia: “Ni nipe nikupe?”. Akajibu: Naam, yule mzee akaanza
kusema: :Hakika imenifikilia khabari kwamba Muhammad na maswahaba wake
wametoka siku kadha kadha. Ikiwa mtu aliyenieleza amesema kweli, basi hapana
shaka wao leo watakuwa wamefika mahala kadha kadha. Ikasadifu kuwa ndio mahala
khasa alipopiga kambi Mtume na maswahaba wake. Na khabari zilizonifikia ni
kwamba Makurayshi nao wametoka siku kadha kadha. Ikiwa huyo aliyenipasha
khabari amesema kweli, basi wao leo watakuwa wamefika mahala kadha. Ikasadifu
kuwa ndio mahala khasa walipo Makurayshi wakati ule. Yule mzee alipomaliza
kueleza khabari zake, akamuuliza Mtume: “Nyinyi ni watu wa wapi?” Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamjibu: “Sisi ni watu wa sehemu zile zenye
maji”, huku akiashiria kwa mkono wake upande wa Iraq, kisha wakaondoka. Yule
mzee akabaki akijisemea: “Hawa si watu wa pande zile zenye maji, kweli ni
watu wa pande za maji za Iraq, hata!” Mtume akarejea kuungana na maswahaba
wake pale walipopiga kambi.
Jua
lilipokuchwa na kiza kikaanza kuingia akawatuma Aliy Ibn Abiy Twaalib, Zubeir
Ibn Al-Awwaam, Sa’ad Ibn Abiy Waqaasw na kundi la maswahaba wake kwenda
katika eneo lenye maji la Badri. Waende wakapeleleze khabari za Makurayshi,
walipofika hapo wakawakuta watekamaji wa Makurayshi wakichota maji.
Wakawakamata vijana wawili miongoni mwao, wakawaleta mpaka kwa Mtume nae akiwa
anaswali. Ikawa wao wanawauliza vijana wale: Nyinyi ni watumishi wa nani?
Wakitaraji kwamba vijana wale ni miongoni mwa watekaji maji wa msafara wa
Makurayshi. Wale vijana wakajibu: Sisi ni wateka maji wa Makurayshi (waliotoka
Makkah), wametutuma kuja kuwatekea maji. Maswahaba wakadhania kuwa vijana wale
wanaongopa, wakaanza kuwapiga huku wakiwauliza nao wakisema: Sisi ni wateka
maji wa Makurayshi (sio wa msafara). Walipozidiwa na kipigo wakasema: Sisi ni
wateka maji wa Abuu Sufyaan, wakaacha kuwapiga. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alipomaliza kuswali akawaambia: “Walipokuambieni ukweli mliwapiga
na walipokuongopeeni mkawaachia! Wallah, wamesema kweli wao ni wateka maji wa
Makurayshi”. Kisha Mtume akawauliza khabari za Makurayshi, wakamjibu: Wao
wallah wako nyuma ya hili fungu la mchanga unaloliona kando ya bonde hili
lililo mbali na Madinah. Mtume akaendelea kuwauliza: “Wako watu wangapi?”
Wakamjibu: wengi tu, akawauliza tena akawaambia: “Nataka idadi yao ni
wangapi?” Wakamjibu hatujui. Akawauliza: “Wanachinja ngamia wangapi kila
siku?” Wakasema: siku moja huchinja ngamia tisa na siku nyingine kumi. Hapo
ndipo Mtume aliposema: “Watu hawa ni kati ya mia tisa na alfu”. Kisha
akawauliza tena: “Nani miongoni mwa watu watukufu wa Makurayshi yumo
humo?” Wakaanza kumtajia majina ya watukufu wao wote. Mtume akawaeleza
maswahaba wake, akawaambia: “Haya hii sasa ndio Makkah imekutupieni vipande
vya maini yake (wanawe watukufu)”. Waislamu wakatambua kutokana na kauli
hiyo ya Bwana Mtume kwamba sasa ni vita tu, hakuna njia ya kuviepuka. Wakajua
kuwa hawana budi kupambana na adui mwenye nguvu zaidi na maandalizi ya kutosha
kuliko wao. Hebu tuipe nafasi Qur-ani Tukufu nafasi itueleze hali ilivyokuwa
katika uwanja wa vita: “...SIKU YALIPOKUTANA MAJESHI MAWILI (siku ya vita
vya Badri-jeshi la waislamu na jeshi la makafiri). NA ALLAH NDIYE MWENYE UWEZA
JUU YA KILA KITU. (Kumbukeni) MLIPOKUWA KANDO YA BONDE LILILO KARIBU (na
Madinah) NAO (makafiri) WALIKUWA KANDO YA BONDE LILILO MBALI, NA ULE MSAFARA
(wa Makurayshi uliokuwa na mali yao) ULIPOKUWA CHINI YENU (upande mwingine
kabisa) NA KAMA MNGELIPEANA MIADI MNGALIKHITILAFIANA. LAKINI (mmekutana hivi
hivi na jeshi lao la vita) ILI ALLAH ALIPITISHE JAMBO LILILOKUWA LAZIMA
LITENDEKE; KUSUDI YULE AANGAMIAYE (akakhitari ukafiri) AANGAMIE KWA DALILI
ZILIZO DHAHIRI (alizokataa kuzifuata) NA ANAYEHUIKA (yaani anyeufuata Uislamu)
AHUIKE KWA DALILI DHAHIRI. NA HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUSIKIA MWENYE KUJUA”.
[8:41-42]
SHETANI
APATA UPENYO KATIKA NYOYO ZA BAADHI YA WAISLAMU.
Hapa
sasa ndipo shetani-mlaaniwa-alipopata upenyo akaziingia baadhi ya nyoyo za
watu dhaifu wa imani. Akaanza kuwasawirishia udogo (uchache wa idadi yao) na
silaha duni walizonazo pamoja na maandalizi dhaifu. Akawasawirishia Makurayshi
walivyotoka na nia ya vita, wakiwa wengi na zana nyingi na bora za vita.
Wakawaweka mbele ya jeshi wakati wa kutoka watukufu wao kama dalili na ishara
ya kuwakinaisha waumini kwamba wao wamejiandaa kwa vita virefu. Shetani
akazidi kuwasawirishia, akawanong’oneza mioyoni mwao, haya mnafikiri natija
itakuwa nini yatakapokutana majeshi mawili haya?! Jeshi hili lenu limetoka
bila ya maandalizi na jeshi la wenzenu lina maandalizi ya kutosha kabisa.
Hapana shaka natija na matokeo ya kukutana kwa majeshi mawili haya yako wazi
kwamba nyinyi mtashindwa tu na si vinginevyo. Hivi ndivyo shetani alivyopenya
na kuingia katika nyoyo za waislamu waliokuwa madhaifu wa imani.
Sehemu
waliyopiga kambi waislamu ilikuwa mbali na maji, hapo walipokuwa na yalipo
maji kulikuwa na tambarare ya mchanga ambayo miguu huzama ndani yake mtu
atembeapo. Waislamu wakaishiwa na akiba ya maji waliyokuwa nayo, wakapatwa na
kiu kikali kabisa kiasi cha kushindwa kustahamili tena. Walikuwa katika hali
ngumu sana, hawana maji ya kunywa wala ya kujitwaharishia ili wapate kuswali
na wakati huo bado kulikuwa hakuna rukhsa ya kutayamamu. Hali hii ngumu ikampa
shetani upenyo mwingine, akaanza kuwatia wasiwasi waislamu na akatia chuki
mioyoni mwao. Na akawatishia kufa kwa kiu kabla hawajafyekwa na Makurayshi na
wengine kuchukuliwa mateka na kufanywa watumwa na adui. Ni vema
tukakumbuka kwamba maji jangwani ni asili ya uhai mbali ya kuwa yanaweza
kutumika kama silaha ya ushindi dhidi ya adui. Jeshi linalokosa maji jangwani
hupoteza nguvu zake kabla ya kupoteza uhai wake. Nyoyo zinazoingia mapambanoni
katika hali na mazingira kama haya huingiwa na kiwewe na kizaizai kikubwa.
MSAADA
WA MBINGUNI.
Katika
hali ya mkanganyiko na kukata tamaa, ndipo ulipokuja msaada kutoka mbinguni.
Allah Mola Muweza akateremsha mvua, waislamu wakanywa na kujitwaharisha,
wakajaza maji vyombo vyao na kuwanywesha wanyama wao. Mchanga ukashikamana,
miguu yao ikathibiti katika ardhi baada ya kuwa ilikuwa inazama na wakaweza
kutembea na kwenda bila ya taabu kama mwanzo. Waislamu wakastarehe na
kupumzika kutokana na hali ya shida iliyowasibu, ukawapata usingizi wakalala.
Hawakuzinduka kutoka usingizini mwao ila na hali yao ikawa imebadilika, khofu
yao ikawa ni amani na wasiwasi wao ukageuka kuwa utulivu. Uoga wao ukabadilika
na kuwa ujasiri na uthabiti, tahamaki wakawa ni watu wengine kabisa sivyo kama
walivyokuwa punde tu. Allah Karimu anaizungumzia hali hii ndani ya Qur-ani
Tukufu, hebu na tumtegee sikio: “(Kumbukeni) ALIPOKULETEENI USINGIZI
ULIOKUWA (alama ya) SALAMA ITOKAYO KWAKE, NA AKAKUTEREMSHIENI MAJI MAWINGUNI
ILI KUKUTWAHARISHENI KWAYO NA KUKUONDOLEENI UCHAFU WA SHETANI NA KUZIPA NGUVU
NYOYO ZENU NA KUITHUBUTISHA MIGUU YENU CHINI (isiwe inazamazama mchangani)”.
[8:11]
|