|
Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-ndiye aliyekuwa na imani thabiti kushinda watu wote kwamba
ushindi na nusra ya Allah itakuwa upande wao. Maswahaba wake wakapatwa na
usingizi wakalala kutokana na uchovu wakati ambapo yeye Mtume alikesha
akiswali na kumuomba Mola wake amtimizie ahadi yake ya kumnusuru. Aliendelea
kuwa katika hali hiyo mpaka kuchomoza kwa alfajiri, hapo ndipo akawaamsha
maswahaba wake kujiandaa kwa ajili ya swala. Akawaswalisha na baada ya swala
akawahamasisha na kuwahimiza kupigana kwa ajili tu ya kutaraji radhi za Allah.
Baada ya khutba hiyo fupi ya uhamasisho, kisha haraka akatoka na baadhi ya
maswahaba kuelekea kwenye eneo la maji ili kuwatangulia Mkurayshi. Alipofika
sehemu ya mwanzo ya Badri yenye maji, akaamrisha ipigwe kambi hapo kuzunguka
maji. Miongoni mwa maswahaba alioambatana nao alikuwa ni Al-Hubaab Ibn
Al-Mundhir; huyu alikuwa ni mtaalamu wa mambo ya maji, akasema: “Ewe Mtume
wa Allah, hivi haya ndio mashukio (kambi) aliyokuamrisha Allah kushukia. Au
hii ni rai yako na mbinu ya vita tu?” Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-akamjibu: “Hii ni rai tu na mbinu za vita (sio amri ya Allah)”.
Hapo ndipo Al-Hubaab akasema: “Ewe Mtume wa Allah, hapa si mahala panapofaa
kupiga kambi (mashukio), waondoshe watu tuende mpaka karibu kabisa na sehemu
ya maji iliyo karibu na watu (Makurayshi). Mimi ninaijua sehemu yenye maji
mengi ya kutosha kabisa, tupige kambi hapo na tuvifukie visima vingine vyote
visiweze kutoa maji. Hapa sisi tutajenga hodhi (birika kubwa la maji) na
kulijaza maji tele, kwa mbinu hii sisi tutapata maji ya kunywa na wao
watakosa”. Baada ya Al-Hubaab kumaliza kutoa ushauri wake huo, ndipo
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamuunga mkono kwa kusema: “Hakika umetoa
rai njema kabisa yenye kufaa”. Bwana Mtume akaamuru waondoke wote na kwenda
kupiga kambi mahala aliposhauri Al-Hubaab, wakawa karibu kabisa na mahasimu
wao. Hapana baina yao kizuizi cho chote zaidi ya mafungu ya mchanga. Kazi yao
ya kwanza waliyoifanya mara tu baada ya kupiga kambi ilikuwa ni kujenga hodhi
la maji mahala ambapo aliposhauri Al-Hubaab. Kisha wakaviziba kwa mawe na
mchanga visima vyote vilivyokuwa nyuma yao.
Ujenzi wa hodhi la
maji ilikuwa ni rai ya Al-Hubaab iliyomfungulia mlango wa kutoa rai Sa’ad
Ibn Muaadh. Huyu alishauri Bwana Mtume ajengewe kibanda katika uwanja wa
mapambano. Kutokea kibandani humo atakuwa akishuhudia maendeleo ya vita na
kutoa maelekezo ya nini cha kufanya ili kufikia ushindi. Kadhalika kibanda
hicho kitasaidia kumkinga kamanda mkuu (Bwana Mtume) dhidi ya mashambulizi ya
adui. Yatakayoelekezwa kwake kwa lengo la kummaliza ili kukata mzizi wa fitina
kama walivyodai. Akasema Sa’ad: “Ewe Nabii wa Allah, unaonaje tukikujengea
kibanda ukawa ndani yake na tukakuwekea tayari vipando vyako. Kisha sisi
tukawa mbele yako tukipambana na adui yetu, Allah akitupa ushindi dhidi ya
adui yetu, hilo ndilo tulipendalo. Na kama mambo yatakuwa kinyume na matarajio
yetu tukashindwa, wewe utaweza kupanda kipando chako na kwenda kujiunga na
ndugu zetu tuliowaacha huko nyuma. Kwani waliobakia huko nyuma ni watu ambao
sisi hatuwashindi kwa kukupenda; wao wanakupenda zaidi kuliko sisi. Lau
wangelijua kuwa kutatokea vita, bila ya shaka wasingelibakia nyuma yako na
Allah angekunusuru kwa kuwatumia wao”. Sa’ad alipomaliza kutoa ushauri
wake, Bwana Mtume akamsifia na kumuombea dua njema ikiwa ni ishara ya
kuukubali na kuuridhia ushauri na rai yake hiyo. Maswahaba wakautekeleza
ushauri wake huo, wakajenga kibanda kwenye kilima kinacho chomozea uwanja wa
mapambano na wakamuandalia kipando bora kabisa.
BWANA MTUME AWAPANGA
MASWAHABA WAKE TAYARI KWA MAPAMBANO HUKU AKIWAHIMIZA KUWA NA SUBIRA NA
IKHLAASWI.
Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-akasimama na kuanza kupanga safu za vita na kuelekeza namna ya
kujihami na kushambulia. Akampa bendera yake ya vita Musw-ab Ibn Umeir, nae
akaitwaa na kwenda kuiweka mahala alipomuamrisha kuiweka. Kisha Mtume
akasimama kuziangalia safu namna alivyozipanga, akaziamuru kuelekea upande wa
magharibi ili jua liwe kwa nyuma yao. Majeshi ya mushrikina yakawa
yanalielekea jua. Kabla ya kuanza kwa mapambano, Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-aliwakhutubia maswahaba wake akiwahimiza kupigana na kuwaraghibisha
ujira adhimu. Akamuhimidi Allah na kumsifia, kisha akasema: “Ama baad,
hakika mimi ninakuhimizeni kile kile alichokuhimizeni Allah na ninakukatazeni
kile kile alichokukatazeni. Bila shaka Allah Mtukufu anaamrisha mema na
anapenda ukweli na huwapa kheri watu wa kheri kwa mujibu wa daraja zao mbele
yake. Bila ya shaka nyinyi mmepambaukiwa kuwa katika daraja miongoni mwa
daraja za haki ambapo Allah hakubali cho chote kwa ye yote ila tu kile
kilichofanywa kwa kuikusudia dhati yake Allah pekee. Na hakika kusubiri katika
sehemu za vita na dhara ni miongoni mwa mambo ambayo Allah huleta faraja kwayo
na kuwa ni sababu ya kupata uokovu akhera. Mnaye miongoni mwenu Mtume wa Allah
akikutahadharisheni na kukuamrisheni. Basi leo oneni haya kumuonyesha Allah
jambo ambalo litamghadhibisha na kumfanya akuchukieni, kwani hakika Allah
anasema: “...BILA SHAKA KUKUCHUKIENI ALLAH NI KUKUBWA KULIKO KUJICHUKIA
NYINYI NAFSI ZENU...” [40:10]
Jitahidini
kumuonyesha Mola wenu katika meneo haya ya vita jambo litakalokuwajibishieni
kile alichokuahidini miongoni mwa rehema na msamaha wake. Hakika miadi yake ni
ya haki, kauli yake ni kweli na adhabu yake ni kali kabisa isiyowezwa. Na
hakika si vinginevyo mimi na nyinyi ni milki yake Allah Mwenye uhai wa maisha,
Msimamizi wa kila jambo. Ni kwake yeye ndiko tulikotegemeza migongo yetu na
kwake yeye tu tunajilinda na kutegemea na marejeo yetu sote ni kwake yeye.
Allah anighufirie mimi na waislamu wote”.
|