|
Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie akaondoka pale Rauhaa alipolakiwa na maswahaba wake kuendelea
na safari yake ya Madinah. Alipofika mahala panapoitwa “Al–Uthayl”
akawakagua mateka na akaamuru kuuliwa wawili miongoni mwao ambao ni
An–nadhwru Ibn Al–Haarith na Uqbah Ibn Abiy Muaitw. Hawa walikuwa ni
miongoni mwa mashetani wa Makuraishi waliokuwa na maudhi makubwa kwa Mtume na
maswahaba kuliko wengine. Hawa walikuwa wakikizulia kitabu cha Allah na Mtume
wake. Mtume wa Allah wakati akiwakagua mateka wale alimtupia An–nadhwru Ibn
Al–Haarith jicho lililoupapatisha moyo wake mateka yule An-nadhwru
akamwambia mateka aliye pembeni mwake: “Wallah, Muhammad ataniua kwani
amenitazama kwa macho yanayoashiria mauti”. Mwenziwe akamwambia “Wallah,
hiyo ni khofu yako tu, hatafanya hivyo. An–nadhwru akaanza kutafuta mtu
atakayemuombea kwa Mtume asiuawe, akamuendea swahaba Musw’ab Ibn
Umeir–Allah amuwiye radhi. Musw’ab ndiye muislamu aliyekuwa ndugu yake wa
nasabu mwenye nasabu ya karibu nae kuliko waislamu wengine Akamwambia: “Hebu
zungumza na mtu wako huyu (Mtume) anijaalie kama ye yote miongoni mwa
Makuraishi. Kwani yeye, Wallah ataniua tu kama hukuzungumza nae. Musw’ab
akamwambia: “Hakika wewe ulikuwa ukisema katika kitabu cha Allah na Mtume
wake kadha wa kadha na ulikuwa ukiwaadhibu maswahaba wake”.
An-nadhwru–akasema: “Lau Makuraishi wangelikuteka wewe, kamwe
wasingelikuua maadam mimi ni hai”. Musw’ab akamjibu: Wallah, hakika mimi
sikuoni wewe kuwa ni mkweli, isitoshe mimi si kama wewe (si kafiri) na Uislamu
umekwishakata ahadi na makafiri”. Huyu An–nadhwru alikuwa ni mateka wa
Al–Miqdaad Ibn Amrou–Allah amuwiye radhi, swahaba huyu aliposikia
mazungumzo yanayojiri juu ya kuuliwa mateka wake akapiga ukelele akisema :
An–nadhwru ni mateka wangu”. Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie–akamwambia: “Ipige upanga shingo yake. Ewe Mola wa haki wee!
Mtajirishe Al– Miqdaad kwa fadhila zako”. Akauawa An–nadhwru kwa pigo la
upanga wa Al–Miqdaad.
Ama Uqbah Ibn Abiy
Muaitw, Mtume aliamuru auliwe walipofika mahala paitwapo ‘Arqid–dhwabyah,
Uqbah akapiga mayowe kwa kupapatika: “Nani atawaangalia wanangu ewe Muhammad
(nikiuwawa)?
“Mtume akamjibu:
“Moto”. Imepokelewa kutoka kwa Sha’abiy kwamba Mtume alipoamuru kuuliwa
kwa Uqbah, alisema Uqbah: “Hivi unaniua mimi miongoni mwa makurayshi hawa
(yaani katika wote hawa hukumuona wa kumuua ila mimi tu)?” Mtume akamjibu:
“Naam, je, mnajua huyu alinifanyia nini mimi? Huyu siku moja alinikuta
nimesujudu, akanikanyaga shingoni na kusigina (kukandamiza) hakuuondoa mguu
wake mpaka nikadhani kwamba macho yangu yatatoka kutokana na mkandamizo ule wa
nguvu Mara nyingine tena akaja na matumbo ya mbuzi akanitupia kichwani nami
nikiwa nimesujudu. Akaja Fatmah binti yangu akayaondosha. Kisha kusema hivyo
akaamuru auliwe, akauawa. Baada ya kuuawa, huyoo Mtume wa Allah–Rehema na
Amani zimshukie–akashika njia kuendelea na safari yake ya Madinah . Akaingia
mjini Madinah kabla ya mateka wale kwa siku moja akitokea upande wa njia ya
Thaniyah. Hiyo ilikuwa ni siku ya Jumatano mwezi ishirini na
mbili–Ramadhani, watu wakamlaki na kumpongeza kwa ushindi aliopewa na Allah.
BWANA MTUME AWATAKA
USHAURI MASWAHABA WAKE KUHUSIANA NA KADHIA YA MATEKA.
Mateka walipowasili
Madinah, Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie-akawagawa baina ya maswahaba
wake na kuwaambia: “Usianeni kuwatendea wema mateka hawa”. Maswahaba
wakaipokea kwa mikono miwili amri hii ya Mtume wa Allah, wakawakirimu mateka
wao kiasi cha kuwapendelea wao chakula kizuri kuliko wanachokula wao. Abuu
Aziyz Ibn Umay, mmoja wa mateka anasema katika riwaya iliyopokelewa na Ibn
Is–haaq: “Nilikuwa katika kundi la Answaar wakati waliponileta mateka
kutoka Badri, wakawa wanapoleta chakula chao cha mchana na usiku, hunikhusisha
mimi kwa kunipa mkate na wao wakala tende kwa ajili ya kuutekeleza wasia wa
Mtume wa Allah aliowapa kwetu. Hakikuangukia kipande cha mkate mkononi mwa ye
yote miongoni mwao ila alinipa. (Akaendelea kusema): Basi mimi huona haya na
kumrudishia naye hunirudishia bila ya kukila”. Kisha Mtume wa Allah–Rehema
na Amani zimshukie–akawataka ushauri maswahaba wake wakubwa kuhusiana na
suala la mateka, wawafanyeje. Ushauri uliotolewa na baadhi yao ulikuwa ni
kuwauwa kwa kukatwa shingo zao na panga au kwa kuchomwa moto. Sababu ya hukumu
yao hii kali ni kwamba walimwambia Mtume hawa ni mashina ya ukafiri na
viongozi wa upotevu na waliwanyanyasa sana waislamu na kuwatesa walipokuwa
Makah. Baadhi ya maswahaba wakawapinga wenzao katika shauri hili la kuwauwa
mateka, wao wakasema tukiwauwa hatutafaidika na cho chote, bora ni kuwapa
fursa ya kujikomboa kwa kutoa fidia. Ili watakachokitoa kisaidie katika
kuimarisha nguvu ya Waislamu. Na huenda Allah akazielekeza nyoyo zao katika
Uislamu, wakasilimu na kutubia. Mtume wa Allah akausikiliza kwa makini ushauri
uliotolewa na makundi mawili haya ya maswahaba wake na ukamuathiri zaidi
ushauri wa fidia kuliko ule wa kuua. Hii ilitokana na hali ya dhiki na ufakiri
waliokuwa nayo maswahaba wakati huo. Amepokea Imamu Ahmad–Allah
amrehemu–kutoka kwa Abdallah Ibn Masoud–Allah amuwiye radhi-amesema:
Alisema Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–siku ya vita vya Badri:
“Mnasemaje katika suala la mateka hawa?” Abuu Bakri-Allah amuwiye
radhi-hawa ni kaumu yako na ni ndugu zako (Makurayshi wenzako)! usiwauwe, wape
nafasi (muda) huenda Allah akawakubalia toba yao”. Na Umar–Allah amuwiye
radhi- akasema: “Ewe Mtume wa Allah, hawa walikutoa (walikufukuza) Makah na
wakakukadhibisha! Wasogeze karibu uzipige shingo zao kwa panga”. Abdullah
Ibn Rawaahah–Allah amuwiye radhi–nae akasema: “Ewe Mtume wa Allah,
angalila jangwa (bonde) lenye kuni nyingi uwaingize humo kisha uwawashie moto
(wafilie mbali)” (Akaendelea kusema Ibn Masoud): Mtume wa Allah akaingia
ndani bila ya kusema lolote. Watu wakasema: Atafuta kauli ya Abuu Bakri na
wengine wakasema atafuata kauli ya Umar. Kundi jingine likasema atafuata kauli
ya Abdallah Ibn Rawaahad. Mara Mtume akawatokea na kuwaambia: Bila shaka Allah
atazilainisha atazilainisha nyoyo za watu kwake mpaka zitakuwa laini zaidi
kuliko maziwa (yanapokuwa tumboni). Na bila shaka Allah atazifanya nguvu nyoyo
za watu kwake mpaka ziwe ngumu zaidi kuliko mawe. Na nyinyi ni mafakiri (hamna
kitu) basi asibakie asibakie ye yote ila kwa kutoa fidia (na kama hana) na
ipigwe upanga shingo yake.”
III/. UTOZAJI WA FIDIA
KWA MATEKA
Allah Mola mjuzi wa siri
na dhahiri akamlaumu Mtume wake –Rehema na Amani zimshukie kwa kitendo chake
cha kukubali kupokea fidia kuliko kuwauwa mateka, akasema: “HAIMPASII NABII
(ye yote) KUWA NA MATEKA MPAKA APIGANE (sana) NA KUSHINDA (barabara) KATIKA
NCHI (ndipo achukue mateka). MNATAKA VITU VYA DUNIA HALI ALLAH ANATAKA (mpate
thawabu za) AKHERA! NA ALLAH NI MWENYE NGUVU (na) MWENYE HEKIMA. ISINGALIKUWA
HUKUMU ILIYOTANGULIA KUTOKA KWA ALLAH (kuwa mwenye kujitahidi mwisho wa
jitihada yake hateswi) BILA SHAKA INGELIKUPATENI ADHABU KUBWA KWA YALE
MLIYOYACHUKUA.” (8:67–68) Wapokezi wanasema kwamba Mtume wa Allah–Rehema
na Amani zimshukie–alilia sana na Abuu Bakri iliposhuka aya hii na akatamani
lau angelifuata rai ya kuwauwa mateka. Kutokana na kwamba Allah alimsamehe
Mtume wake kwa kosa hili kama inavyosema aya, akamuhalalishia yeye na waislamu
ile ngawira waliyoitwaa, akasema:“BASI KULENI KATIKA VILE MLIVYOTEKA
(vitani) NI HALALI (yenu sasa) NA VIZURI, NA MCHENI ALLAH. HAKIKA ALLAH NI
MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU.” (8:69) Bwana Mtume–Rehema na
Amani zimshukie akawafanyia ihsani kubwa mateka walio mafakiri kwa kuwaacha
huru bila ya kuwatoza fidia. Akafanya fidia ya wanaojua kusoma na kuandika ni
kila mmoja wao kuwafundisha kusoma na kuandika watoto kumi wa Kiislamu. Ama
mateka waliokuwa matajiri, aliendelea kuwashikilia mpaka waje kukombolewa na
ndugu zao kwa kutoa fidia. Fidia ya kila mmoja wao ilikuwa ni kati ya Dirham
alfu moja mpaka Dirhamu alfu nne. Fidia hii ilizingatia hali na uwezo wa
mateka binafsi au ndugu zake mateka huyo.
Miongoni mwa watu
waliofanyiwa ihsani ya kuachwa huru bila ya fidia na Bwana Mtume, alikuwa ni
Abuu Azzah;Umar Ibn Abdillah Al- Jumahiy. Huyu alikuwa fakiri mwenye watoto wa
kike, akamzungumza Mtume wa Allah akamwambia: “Ewe Mtume wa Allah, bila
shaka wewe wajua vema kwamba mimi sina mali na unajua mimi ni fakiri na nina
familia inayonitegemea, basi nakuomba unifanyie ihsani.” Mtume wa Allah
akamkubalia ombi lake hilo na kumuacha huru bila ya fidia nae akaipokea ihsani
na ukarimu huu wa Mtume kwa kumuahidi kwamba hatamuunga mkono wala kumsaidia
kwa namna yo yote ile mpinzani wake.
|