|
Miongoni mwa mateka alikuwemo Abul-Aaaswi Ibn Rabee, huyu
alikuwa ni mkwewe Mtume kwa bintie Zaynabu. Ibn Is-haaq-Allah
amrehemu–anasema: “Abul-Aaswi alikuwa ni miongoni mwa watu wa Makah walio
wachache wa mali, amana na biashara. Watu wa Makah walipowatuma watu kwenda
kuwakomboa ndugu zao kwa kutoa fidia Zaynabu Binti ya Mtume wa Allah nae
alimpa mtu mali kwenda kumfidia Abul-Aaswi Ibn Rabee (mumewe). Katika mali
hiyo aliyotoa kilikuwemo kidani chake alichopewa na Bi. Khadijah mama yake
(mkewe Mtume) siku ya harusi yake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie–
alipokiona kidani cha mkewe yalimjia makiwa na huruma akasema: “Mkiweza
kumuacha huru mateka wake na kumrudushia mali yake, basi fanyeni hivyo.”
Mashwahaba wakasema: Naam, ewe Mtume wa Allah wakumuachia na kumrudishia mali
yake. Nae Mtume akachukua ahadi kwa Abul-Aaswi ya kwamba amuachie (amruhusu)
Zaynabu kuhamia Madinah Abdul-Aaswi akaahidi kulitekeleza hilo”.
KUFIDIWA KWA ABBAAS.
Abbas Ibn Abdul-Mutwalib-Ami yake Mtume, nae alikuwa ni
miongoni mwa mateka wa vita vya Badri. Huyu alitumai kupata ihsani ya Mtume,
aachiwe huru bila ya kutoa fidia. Lakini mambo hayakuwa kama alivyodhania,
Bwana Mtume hakukubali kumuachia ila kwa kujitolea fidia yeye mwenyewe pamoja
na jamaa nao. Zuhriy–Allah amrehemu–amepokea kwamba: “Makurayshi
waliwatuma watu kwa Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie kwenda
kuwatolea fidia mateka wao. Watu wote wakawafidia mateka wao kwa namna
walivyokubaliana. Abbas akasema: “Ewe Mtume wa Allah, kwa yakini tayari
nilishakuwa muislamu”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie–akamwambia: “Allah ndiye mwenye kujua zaidi uislamu wako
(kusilimu kwako), ukiwa kama usemavyo basi hakika Allah atakujazi (atakulipa).
Na lililo juu yetu sisi ni dhahiri yako ilivyokuwa, kwa hivyo jifidie nafsi
yako na wana wa nduguyo; Naufal Ibn Al-Haarith Ibn Abdul– Mutwalib na Uqayl
Ibn Abuu Twaalib Ibn Abdul–Mutwalib. Na umtolee fidia mshirika wako Utbah
Ibn Amrou ndugu wa Banil-Haarith Ibn Fihr”. Akasema (Abbas): “Mimi nina
mali gani ya kutoa fidia, ewe Mtume wa Allah?” (Mtume) akamwambia: “I wapi
ile mali uliyoizika wewe na Ummul-Fadhli? Wewe ulimwambia (mkeo): Nikiuwawa
katika safari yangu hii, basi mali hii niliyoizika ni ya wanangu; Al-Fadhli,
Abdullah na Quthm.” Akasema (Abbas): “Wallah, ewe Mtume wa Allah, hakika
kwa yakini natambua kwamaba wewe ni Mtume wa Allah! Hakika jambo hili halijui
ye yote ila mimi na (mke wangu) Ummul–Fadhli (tu). Nakuomba ewe Mtume wa
Allah, unifikirie katika mali mliyoiteka kwangu, nipeni wakia (ounce) ishirini
kutoka katika mali niliyokuwa nayo.” Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akasema: “Hapana, hicho ni kitu alichotupa Allah kutoka kwako.”
Hatimaye Abbas akajifidia yeye mwenyewe, wana wa nduguye ma mshirika wake.”
SURA YA VITA ILITOA VIGEZO VYA USHINDI NA VIGEZO VYA USHINDWA
Tumeona waislamu wakiibuka washindi katika vita vya Badri
pamoja na uchache wao, maandalizi dhaifu na zana duni ukilinganisha na
mahasimu wao. Kadhalika tumeona Makurayshi waliokuwa wengi, wenye maandalizi
ya kutosha na zana nyingi na imara za vita, wakiendeshwa mbio na kushindwa
vibaya sana. Wewe mpenzi msomaji wetu, unafikiri nini zilikuwa sababu za
ushindi na ushindwa huu pamoja na tofauti kubwa na ya wazi iliyokuwepo baina
ya makundi mawili haya; kundi dhaifu na kundi lenye nguvu? Nini ilikuwa siri
ya ushindi wa kundi hili dogo tena dhaifu dhidi ya kundi kubwa lenye nguvu na
maandalizi ya kutosha? Ushindi uliowashangaza si tu washindwa bali hata
washindi pia. Ushindi unaovibatilisha vigezo vya ushindi kama vilivyokuwa
katika fira za watu, na natija ya vita kuwa kinyume na mazoea ya watu. Hapana
shaka yo yote kwamba ushindi huu wa kishindo wa waislamu, ulitokana na msaada
wa Allah. Allah aliwasaidia waumini kwa nguvu zake zisizoshindika,
akawateremshia majeshi ya malaika kuwasaidia bila ya wao kuyaona: “….NA
AKATEREMSHA MAJESHI (ya malaika) AMBAYO HAMKUYAONA NA AKAWAADHIBU WALE
WALIOKUFURU NA HAYO NDIYO MALIPO YA MAKAFIRI.” (9:26)
Allah akawaandikia waumini ushindi ikiwa ni jazaa ya subira na
ukweli wao pamoja na ustahamilivu waliouonyesha katika machungu yote
yaliyowafika kwa ajili ya dini ya Allah. Na kujitoa kwao muhanga kuinusuru
dini ya Allah na Mtume wake na kusimama kwao kidete katika kuilinda Imani yao.
Ukiziachilia mbali sababu hizi, bila ya shaka kwa mchunguzi na mzingatiaji wa
mambo atagundua sababu nyingine za ziada. Sababu ambazo zinaweza kuonekana
machoni kuwa ndogo lakini kwa hakika zilitoa mchango mkubwa katika kufikia
ushindi. Tunaweza kuzielezea sababu hizo kama ifuatavyo:
WAISLAMU WALIPIGANA KWA NIA NA SHAURI MOJA
Waislamu walitoka Madinah kuelekea Badri wakiwa na nia na
shauri moja chini ya kiongozi mmoja. Wakiwa na lengo moja tu nalo si jingine
bali ni kuuteka msafara wa biashara wa makurayshi. Walipobaini kwamba msafara
umewaponyoka na kwamba Makurayshi wamewatokea kuja kuwasagasaga. Msimamo wao
ukabadilika na udhaifu ukazipenya safu zao, kiongozi na kamanda wao Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie–akalidiriki hili. Akawarejesha katika nguvu
na ari na akawakusanya pamoja juu ya nia moja kiasi cha kutoweza kujitoa
katika jamaa mtu ye yote. Wakateremka katika uwanja wa mapambano wakiwa
wamejawa mori na ari ya haki ambayo wanayoipigania na kuitetea. Na lengo lao
wakati huo lilikuwa ni moja tu, nalo ni dini ya haki kuzishinda dini zote
potofu, na neno la Allah kuwa juu ya kila neno. Wakajitoa muhanga katika
kulitimiza lengo hili na waumini wakayasahau kabisa mapambo (starehe) ya
maisha ya dunia. Kila mmoja akawa hawanii na wala hapanii ila kufa shahidi kwa
ajili ya dini ya Allah.
B) MAKAFIRI WALIPIGANA NA IL-HALI NYOYO ZAO ZIMETAPANYIKA
(HAWAKO PAMOJA)
Mushrikana kwa upande wao, walitoka wakiwa wamechangukana
hawaunganishwi na uongozi mmoja. Wala haiwakusanyi pamoja nia na lengo moja.
Lilikuwepo kundi miongoni mwao lililokuwa na lengo la kulipa kisasi kwa
Muhammad; Mtume wa Allah–na maswahaba wake na kundi lingine halikutoka ila
kwa lengo la kuhami na kuuokoa msafara wao wa biashara. Hawa zilipowafikia
khabari za kunusurika kwa msafara wao wakagawika makundi mawili. Kundi moja
likaona hakuna tena mantiki ya vita likajitoa na kuamua kurejea Makah na kundi
jingine pamoja na kutoona sababu ya vita lakini likalazimika kuwemo kundini
kwa kuona vibaya kujitenga na wenzao. Haya yalikuwa kabla ya kuanza kwa
mapambano. Mkundi mawili yalipokutana katika uwanja wa mapambano, makafiri
wakaona nyusoni mwa waislamu utayarifu wa kujitolea muhanga, ukadhihiri
mgawanyiko kwa mara nyingine tena. Baadhi ya wakubwa wao wakaanza
kuwahamasisha kuingia vitani. Yakakhitilafiana makundi mawili haya kiasi cha
kuzozana viongozi wao na kuwafanya waingie vitani wakiwa na chuki wao kwa wao
na nyoyo zilizogawika. Kadhalika lilikuwemo mapambanoni kundi ambalo
halikudhamiria uadui na mfundo si kwa Mtume wala kwa waumini. Hili lilikuwa ni
kundi la Baniy Haashim na washirika wao. Hawa kidhahiri walikuwa pamoja na
mushriki, lakini nyoyo zao zilikuwa pamoja na waislamu. Ni kwa sababu hii ndio
Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–akawausia maswahaba wake wasimuue
ye yote miongoni mwa watu wa kundi hili. Kwa hali hii utawaona mushrikina
wameingia katika uwanja wa mapambano wakiwa si wamoja; nyoyo zao zimetengana
na malengo tofauti. Uongozi wao ukiwa umeparaganyika, hawana kiongozi mmoja
mwenye kutiiwa na kukubalika na wote. Wakati ambapo waislamu walipambana nao
wakiwa na lengo moja, moyo mmoja chini ya kiongozi mmoja.
|