|
C/. WAISLAMU WALIKUWA CHINI YA UONGOZI WENYE HURUMA NA BUSARA,
WAKATI AMBAPO MUSHRIKINA WALIKUWA CHINI YA UONGOZI MPUMBAVU (USIO NA BUSARA)
WENYE KIBURI.
Tukichukulia kwamba Abuu Jahli ndiye aliyekuwa kiongozi wa
Makurayshi kwa sababu ya fikra na mawazo yake kushinda fikra zote zilizotolewa
na viongozi wengine. Na ni yeye ndiye aliyewaongoza Makurayshi katika halaki
na maangamivu haya yaliyowasibu. Hebu sasa tuwe na mizani tupime baina ya
nyongozi mbili hizi; uongozi wa waislamu kwa upande mmoja wa kitanga cha
mizani na ule wa Makurayshi kwa upande mwingine. Mizani yetu itatuonyesha kuwa
waislamu walikuwa chini ya uongozi wenye huruma na busara. Na zaidi ya yote ni
uongozi uliopendwa, kukubaliwa na kutiiwa na wote. Wakati ambapo mizani yetu
inatuonyesha kuwa mushrikina waliongozwa na uongozi usio na busara. Uongozi
uliojaa kiburi, uongozi unaotumia nguvu zaidi katika kufikia maamuzi. Huyu
hapa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anajiweka sawa na maswahaba wake
katika kila kitu na kuwafanya wahisi haki sawa baina yao. Anawataka ushauri
maswahaba wake katika mambo mengi na kuuthamini na kuuenzi ushauri wao huo.
Akiupokea kwa mikono miwili ushauri bora zaidi na akiwarejesha msatarini kwa
upole na hekima kila wanapoteleza na kukosea. Akiwanyenyekea bila ya
kujidhalilisha kiasi cha kumpa nafasi ya kulipa kisasi kwa ye yote
aliyemdhulumu au kumkosea miongoni mwao. Na yule Abuu Jahli akitumia udikteta
katika kufikia maamuzi, hawapi watu wake nafasi ya kutoa fikra na mawazo yao.
Anamuona adui na kumpiga vita kila aliyeonyesha upinzani dhidi yake mpaka
amuunge mkono na kuwa chini ya twaa yake. Kiongozi asiyemuheshimu mkubwa kwa
ukubwa wake wala kumuhurumia mdogo kwa udogo wake. Wala hafikirii natija na
matokeo ya matendo yake, kwamba nikifanya au nikisema hivi itakuwaje. Katika
hali na mzingira kama haya, unafikiri ni uongozi upi ulio na nafasi ya
kushinda kuliko mwingine?!
D/. WAISLAMU WALIPIGANA KWA MIKAKATI MAALUMU WAKATI AMBAPO
MUSHRIKINA WAKIPIGANA BILA YA MBINU WALA MIKAKATI.
Tukiyaangalia maandalizi na matayarisho (mobilization) ya
makundi mawili haya; kundi la haki na kundi la batili katika vita vya Badri.
Tutawaona waislamu wamepangwa katika safu zilizoungana mithili ya jengo imara
lililokamatana barabara: “KWA YAKINI ALLAH ANAWAPENDA WALE WANAOPIGANA
KATIKA NJIA YAKE, SAFUSAFU (mkono mmoja); KAMA KWAMBA WAO NI JENGO
LILILOKAMATANA BARABARA” [61:4]. Wakachagua mahala na upande munasibu wa
kuelekeza mashambulizi yao dhidi ya hasimu wao, wakalipa mgongo jua na
kuwafanya kutolielekea. Kadhalika tunawaona hawamfuati adui yao pale
aliposonga mbele kuwajia, bali walithibiti katika sehemu zao walizopangiwa,
wakiwa wamekita magoti yao. Wakimrushia adui yao mvua ya mishale kama
alivyoamrisha kamanda wao mkuu. Waliendelea kurusha mishale mpaka pale adui
alipowavaa na kukabiliana nao ana kwa ana. Hapo ndipo kwa pamoja walichomoa
panga zao na kupiga pigo la mtu mmoja wakiwa wamejenga ukuta imara bila ya
kutapanyika huku na huko. Kwa weko na mkao huu wa kivita uchache unaweza
kufanya maajabu yasiyoweza kufanywa na wingi usio na mpangilio. Hivi ndivyo
walivyojipanga waislamu katika uwanja wa vita, wakiitii na kuisikiliza amri ya
kamanda wao.
Ama kwa upande wa mushrikina mambo yalikuwa kinyume kwani
walikuwa shaghlabaghla. Walikuwa wengi waliotapanyika, hawana mikakati na
utaratibu katika mashambulizi yao. Wakipigana bila ya kuwa na kamanda
anayekubalika na wote, kila kundi likielekeza mashambulizi yake kwa mujibu wa
maelekezo na amri ya kamanda wake. Walipigana huku jua likiwapiga nyusoni mwao
na maji yakiwa katika udhibiti wa adui yao. Pamoja na yote haya, Makurayshi
wanaanza vibaya vita, kwani kabla hawajaanza kusonga mbele tayari wanawapoteza
viongozi wao wanne kwa kuuawa na waislamu.
E/. WAISLAMU WALIKUWA NI UCHACHE UNAOMTEGEMEA MOLA WAKE NA
MUSHRIKINA WALIKUWA NI WINGI ULIOGHURIKA NA NGUVU ZAKE.
Haya hebu sasa tuichunguze na kuiangalia roho na nafsi
iliyokuwa ikilitawala kila kundi wakati wa mapambano. Tunawakuta waislamu
wakipigana huku wakiamini kwamba wao wanaipigania na kuitetea haki ambayo
Allah na Mtume wake wanaipenda. Walikuwa na yakini kwamba hafai kuipigania
haki ila aliyeiamini na kuikubali haki hiyo. Wakisadikisha miadi na ahadi ya
Allah ya kwamba atainusuru haki na kulinyanyua neno lake. Ni imani na yakini
hii ndio iliyowafanya waukatae msaada wa mushriki ye yote na uchache wao
haukuwakatisha tamaa kusonga mbele. Allah pekee walimtegemea awasaidie katika
kuinusuru dini na Mtume wake. Hii ndio roho na ari iliyowatawala waislamu
katika uwanja wa mapambano.
Ama kwa upande wa mushrikina, wao walitoka majumbani mwao kwa
fakhari na kujionyesha kwa watu, hivi ndivyo inavyosema Qur-ani Tukufu:
“WALA MSIWE KAMA WALE WALIOTOKA KATIKA MAJUMBA YAO (miji yao) KWA FAKHARI NA
KUJIONYEHSA KWA WATU NA KUZUILIA (watu) NJIA YA ALLAH...” [8:47]. Wakatoka
wakiwa wamejawa na kiburi, majivuno na majigambo wakighuriwa na wingi wa idadi
yao na nguvu yao. Hawakusudii katika kutoka kwao huku ila kusikiwa na watu na
kuzungumzwa ushujaa wao. Wakiamini kabisa kwamba ushindi unatokana na wingi,
fikra hizi ndizo zilizowafanya wamwambie Iymaai Ibn Rukhswah alipotaka kuwapa
msaada wake: “Ikiwa tunapigana na watu (waislamu), basi sisi si dhaifu mbele
yao na kama tunapigana na Allah kama anavyodai Muhammad, basi hakuna mwenye
ubavu (nguvu) wa kupambana na Allah”. Allah Mola Mwenyezi anaisawirisha hali
yao hiyo kwa kauli yake: “NA (kumbuka) SHETANI ALIPOWAPAMBIA VITENDO VYAO
(wale makafiri) NA KUSEMA: LEO HAKUNA WATU WA KUKUSHINDENI, NA MIMI NI MLINZI
WENU. LAKINI YALIPOONANA (yalipokutana) MAJESHI MAWILI (shetani) ALIRUDI NYUMA
NA KUSEMA: MIMI SI PAMOJA NANYI, MIMI NAONA MSIYOYAONA, MIMI NINAMUOGOPA ALLAH
NA ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU”. [8:48] Haya hili ndilo kundi dogo lenye
imani linaloipigania haki na kuutegemea msaada wa Allah pekee. Na lile ni
kundi kubwa kafiri lenye kuhadaiwa na wingi wao, likisukumwa na jeuri, uadui
na kujionyesha kwa watu.
Ukiziachilia mbali sababu hizi kuna sababu nyingine nyingi tu
ambazo anaweza kuzidiriki mchunguzi wa mambo. Vyo vyote zitakavyokuwa sababu
hizi, zote zitakuwa zinarejea kwenye asili moja, nayo si nyingine bali ni
msaada wa Allah aliouthibitisha na kuwapa waislamu: “...NA ALLAH ANAPENDA
KUTHUBUTISHA HAKI KWA MANENO YAKE NA (anapenda) KUIKATA MIZIZI YA MAKAFIRI.
ILI KUTHUBUTISHA HAKI NA KUONDOA BATILI, HATA WAKICHUKIA WATU WABAYA.
(Kumbukeni) MLIPOKUWA MKIOMBA MSAADA KWA MOLA WENU, NAYE AKAKUJIBUNI KUWA: KWA
YAKINI MIMI NITAKUSAIDIENI KWA MALAIKA ELFU MOJA WATAKAOFUATANA MFULULIZO
(wanaongezeka tu). NA ALLAH HAKUFANYA HAYA ILA IWE BISHARA (khabari ya furaha)
NA ILI NYOYO ZENU ZITUE KWAYO. NA HAKUNA MSAADA (wa kufaa) ILA UTOKAO KWA
ALLAH. HAKIKA ALLAH NI MWENYE NGUVU (na) MWENYE HEKIMA”. [8:7-10]
|