|
Bwana Mtume- Allah amshushie Rehema na Amani- mara baada ya kuzaliwa alinyonyeshwa
na mama yake Bi Amina Bint Wahab kwa siku kadhaa. Kisha akanyonyeshwa na Bibi Thuwaybatul
Aslamiyyah ambaye alikuwa ni mjakazi wa wa Ammi yake Mtume Abuu Lahab. Baada ya hapo ndipo
waliamua kumtafutia mlezi na mnyonyeshaji kama ilivyokuwa ada na desturi ya Waarabu wakati
huo. Wakampata Bibi Haliymah Assaadiyyah, Bibi huyu alimchukua Bwana Mtume na kwenda
kuishi naye katika kitongoji cha Baniy Saad kwa muda wa miaka miwili akimnyonyesha.
Akamuachisha ziwa baada ya miaka miwili, na hili liliashiria kuisha kwa mkataba na
kulazimika kumrudisha mtoto kwa mama yake.
Kutokana na jinsi mama huyu mlezi alivyompenda mwanawe huyu wa kumlea kwa sababu
ya baraka walizozipata tangu kuanza kumlea mtoto huyu alimsihi sana mama yake Mtume
amruhusu aendelee kuishi na kumlea mtoto huyu mwenye baraka. Kitongoji cha Baniy Saad
kilikuwa ni ardhi iliyo na upungufu mkubwa wa mvua, lakini mara tu baada ya kufika Bwana
Mtume katika kitongoji kile, hali ilibadilika kabisa, ukame ukatoweka, ardhi ikaotesha
mimea, mazao yakakithiri, wanyama wakapata malisho mengi na hivyo kutoa maziwa ya kutosha.
Hali na afya za watu wa kitongoji kile zikaboreka kutokana na baraka za mtoto huyu yatima.
Kwa kuyazingatia yote haya mama yake Mtume alimkubalia Bibi Haliymah aendelee kumlea Mtume
kwa kipindi kingine cha miaka miwili. Ada na desturi hii ya waarabu kuwapeleka watoto
kulelewa mashambani ilijengeka juu ya sababu mbili kuu :
MOSI Mashambani ndiko kuna mazingira safi yaliyosheheni hewa safi yenye afya.
Kutokana na hewa hii safi na chakula freshi watoto huwa na afya njema.
PILI Wakazi wa mashambani ndio waliokuwa wakizungumza lugha fasaha. Hivyo mtoto
alipata fursa ya kujifunza na hatimaye kuzungumza lugha fasaha.
Bibi Haliymah alikuwa akiishi na mumewe Bwana Abuu Kabshah. Bibi huyu anasimulia
ukuaji na tabia za mtoto huyu wa ajabu, anasema : "Mtoto huyu alikuwa akikuwa haraka
haraka kuliko kawaida ya watoto, alikuwa akizungumza maneno fasaha ilhali yungali mtoto
bado, kila aliyemuona alimpenda na kuvutiwa naye. Alikuwa halii na kupiga makelele kama
wafanyavyo watoto wengine ila akiachwa bila ya nguo. Akipatwa na mshtuko ghafla wakati wa
usiku nilikuwa nikitoka naye nje ya nyumba, naye huziangalia nyota mbinguni kwa muda mrefu
mpaka akalala". Haya ni machache tu miongoni mwa mengi aliyoyaeleza Bibi Haliymah juu
ya mtoto huyu yatima.
iii) TUKIO LA KUPASULIWA KIFUA
Katika kipindi hiki ambacho Bwana Mtume alikuwa chini ya ulezi na uangalizi wa
Bibi Haliymah alitokewa na tukio muhimu sana. Hili lilikuwa ni tukio la kupasuliwa kifua
chake na kutolewa fungu/uchafu wa shetani ili shetani asiwe na nafasi ya kumlaghai,
kumshawishi na hatimaye kumpotosha.
Tukio hili lilikuwa kama ifuatavyo :
Mwenyezi Mungu alimpelekea Mtume wake wake naye akingali mtoto malaika wawili.
Wakati huo Mtume alikuwa akichunga mbuzi na kondoo pamoja na nduguze wa kunyonya (Watoto
wa Bi Haliymah) jirani na makazi yao. Malaika wale wakambeba Mtume wakamlaza chali na
kumpasua kifua chake, wakautoa moyo wake na kuukosha. Baada ya kuukosha wakaurudisha
mahala pake na pale pale kifua kikawa kama kilivyokuwa mwanzo bila ya athari yeyote. Yote
haya yalitendeka mbele ya macho ya watoto wenzake, wakakimbia haraka kwenda kumueleza mama
yao yaliyompata ndugu yao huyu. Bibi Haliymah na mumewe wakatoka mbio kwenda kuangalia
kulikoni, wakamkuta Mtume amesimama, wakamkumbatia na kumuuliza yaliyomsibu naye
akawahadithia tukio zima lilivyojiri. Wakamshukuru MwenyeziMungu kwa kumsalimisha salama
lakini wakachelea yasije kumpata tena kama haya yaliyompata leo, hivyo wakaamua kumrudisha
kwa mama yake.
|