|
Mayahudi wa kabila la Baniy Qayunqaa, ndio waliokuwa wa mwanzo
kabisa kuwadhihirishia waislamu uadui. Hii ni kwa sababu wao ndio waliokuwa
mashujaa kuliko makabila yote ya kiyahudi na ndio walikuwa majirani wa karibu
wa waislamu. Hawa waliishi baina ya waislamu katika kitovu cha mji wa Madinah.
Ama mayahudi wa kabila za Banin-nadhwiyr na Baniy Quraydhwah, hawa waliishi
viungani na pembezoni mwa mji wa Madinah. Ujirani na ushujaa huu ndio
uliowafanya Baniy Qayunqaa kuwa maadui dhahiri wa mwanzo wa waislamu kuliko
mayahudi wengine. Na yahudi aliyekuwa shadidi mno katika kujihirisha uadui kwa
waislamu kuliko wenzake, huyu hakuwa mwingine ila Ka’abu Ibn Al-Ashraf. Huyu
alikuwa ni miongoni mwa washairi na mabwana wakubwa wao. Huyu alianza
kuwacheza shere waislamu, akamsingizia uongo Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-na kuwahamasisha watu kumuua. Kadhalika alijitia kuwaombolezea
makurayshi watukufu waliouawa na waislamu ili kuwachochea makurayshi kulipa
kisasi kwa waislamu. Hakutosheka kuyafanya haya pale Madinah tu, bali
alikwenda mpaka Makah kuwachochea watu kumuua Bwana Mtume. Ili kuwachochea
zaidi watu na kuwapandisha mori, aliimba mashairi na kujitia kuwalilia watu wa
kisima. Hawa ni wale makurayshi waliouawa katika vita vya Badri, miongoni mwao
akiwa ni Abuu Jahli. Hivi ndivyo hali ya hewa ilivyosheheni uadui baina ya
waislamu na mayahudi, nyoyo za watu zikajaa mifundo na chuki. Jambo lo lote
dogo la kipuuzi tu lilitosha kabisa kuwa ni sababu ya kuwasha moto baina ya
makundi mawili haya yenye kukamiana. Cheche zilizouwasha moto huu mkubwa,
hazikuwa nyingine bali ni lile tukio la mwanamke wa kiislamu. Huyu alikwenda
katika soko la Baniy Qayunqaa kwa ajili ya kujipatia mahitaji yake. Akaliendea
duka la sonara, hapo ndipo myahudi mmoja akamfanyia mwanamke huyu wa kiislamu
kitendo cha kumdhalilisha na kumvunjia heshima. Mmoja wa waislamu aliyekuwa
mahala hapo na akashuhudia namna muislamu mwenzake anavyodhalilishwa, hakuweza
kuvumilia kuliona tendo baya lile. Akamuendea yule myahudi aliyemdhalilisha
mama wa kiislamu na kumuua. Kuona hivyo mayahudi wakamkusanyikia muislamu yule
mmoja na kumuua kulipa kisasi cha myahudi mwenzao aliyeuliwa naye. Hapa tena
waislamu wakawa wanaitana kuja kupambana na mayahudi na mayahudi nao wakaitana
kuja kukabiliana na waislamu. Hali ya hewa ikachafuka kiasi cha kutaka
kugeuzwa mahala hapo kuwa machinjioni, lau zisingekuwa hekima na busara za
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuzizima cheche hizi.
Bwana Mtume akawaita viongozi wa mayahudi na kuwatahadharisha
na kuwaonya juu ya matokeo ya dhulma waifanyayo na kuvunja kwao ahadi
(mkataba) ya amani. Akawaambia: “Enyi kusanyiko la mayahudi, tahadharini na
Allah isije ikakufikeni kama nakama (adhabu) iliyowafika makurayshi.
Nakutakeni msilimu, kwani nyinyi mnajua fika kwamba mimi ni Mtume (wa kweli).
Haya mnayapata ndani ya kitabu chenu na agano la Allah kwenu nyinyi”.
Kusikia hivi, mayahudi wakamkunjia uso Bwana Mtume na kumwambia kwa ukali
kabisa:”Ewe Muhammad wee! Hivi unadhania sisi ni kama hao jamaa zako
(makurayshi wenzio)? Kusikughuri kupambana na watu wasio na ujuzi wa vita,
ukapata fursa ya kuwashinda. Hakika sisi, wallah tukipigana na wewe
utatutambua kwamba sisi ni watu kweli (wala sio kama jamaa zako)! Ibn
Ishaaq-Allah amrehemu-anasema hawa ndio mayahudi wa mwanzo kuvunja mkataba wa
amani na ujirani mwema waliotiliana saini na Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie.
KUVAMIWA NA KUSHAMBULIWA BANIY QAYUNQAA.
Hali ya ujirani na mahusiano mema baina ya waislamu na
mayahudi ikavunjika. Baniy Qayunqaa wakageuka na kuwa maadui wakubwa wa
waislamu baada ya kuwa walikuwa marafiki wema siku za kisogoni. Isitoshe wao
ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kufanya mambo na kusema maneno
yanayopelekea kwa namna moja au nyingine kuvunjika kwa amani. Wakatumia kila
njia kuhakikisha kuwa amani iliyokuwepo baina yao na waislamu inatoweka kwa
kuchochea kulipuka kwa vita ili wapate fursa ya kutoa chuki zao. Je, katika
hali kama hii waislamu watakuwa na amani kwa upande huu wa mayahudi? Hapa
ndipo Allah Mola Mwenyezi akamshushia Mtume wake: “NA KAMA UKIOGOPA KHIANA
KWA WATU (mliofanya nao ahadi) BASI WATUPIE (ahadi yao) KWA USAWA, HAKIKA
ALLAH HAWAPENDI WAFANYAO KHIANA”. [8:58]
Naam, imekwisadhihiri khiana machoni pa mayahudi, kwani tayari
wamekwishavunja ahadi walizoagana na Mtume wa Allah na wakaanza kuingilia
mambo ya Mtume na maswahaba wake. Wakatafuta sababu za kuwachokoza waislamu na
kuwaudhi, wakawa sasa hawaaminiki kwa upande wa amani na ilhali
wanajiranikiana na waislamu katika maskani na wanachanganyika nao katika kazi
na shughuli mbalimbali. Hawa wanajua mambo mengi ya ndani ya waislamu na
kuzichomozea siri zao nyingi, kwa hivyo watu hawa ni watu hatari sana kwa
waislamu. Kwa hali hii, ikawa hapana budi ichukuliwe hatua mkataa (decisive)
itakayowahakikishia amani na utulivu waislamu. Hivi ndivyo alivyofanya Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza na kuwatupia ahadi yao kama
walivyotangulia wao kufanya hivyo. Akawatangazia uadui waziwazi na
kuwatahadharisha na khatari ya kukabiliwa na vita vikali kabisa. Mayahudi
walipoyakinisha kwamba Mtume hafanyi mzaha katika hili, wakajitia katika ngome
zao ili kujilinda na mashambulizi yanayotegemewa kutoka kwa waislamu. Kuona
hivi Mtume wa Allah akaamua kuwazingira, akawazingira kwa kipindi
kisichopungua siku kumi na tano. Katika kipindi chote hicho alihakikisha kuwa
hawapati chakula, maji, nguvu wala msaada wa aina yo yote ile kutoka nje.
Bwana Mtume alifanya hivi ili kuivunja nguvu yao na hatimaye wajisalimishe
wenyewe bila ya kumwagika damu. Hawa Baniy Qayunqaa walikuwa ni washirika na
ndugu wa yamini wa Ubaadah Ibn Swaamit na Abdullah Ibn Ubayyi (wenyeji wa
Madinah). Mayahudi hawa walipodhihirisha uadui wao waliokuwa wameuficha,
Ubaadah Ibn Swaamit akawakana na kuwakataa. Ama Abdullah Ibn Ubayyi, yeye
aliendelea kuwa mtiifu kwao na hakuwakana kama alivyofanya Ubaadah. Na alikuwa
akisema: “Mimi ni mtu ninayechelea mageuzi ya mambo na wala sijiaminishi na
zama”.
Kujitia ngomeni kwa mayahudi hakukuwasaidia cho chote, kwani
hakuna ye yote aliyeweza kuwapa msaada katika kipindi chote hiki cha mazingiwa
(blockade). Wala ndugu zao (mayahudi wenziwao) wa kabila la Banin-Nadhwiyr na
Baniy Quraydhwah hawakuweza kuja kuwaokoa. Pengine hili la kutokusaidiwa hata
na mayahudi wenziwao linathibitisha khiana yao na kwamba wao ndio waliofanya
jeuri na dhulma. Na wakatangaza vita kwa kuvunja kwao ahadi na maagano,
wakaudhihirisha uadui na upinzani wao kwa Mtume na maswahaba wake. Mazingiwa
yaliporepa (yaliporefuka) na wakashindwa kupambana wao wenyewe na waislamu,
ikawapata khofu kuu. Wakamsihi Bwana Mtume awaruhusu kuondoka Madinah, wao,
wake zao pamoja na watoto, nae Mtume na maswahaba wake wachukue mali na silaha
zao zote. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawakubalia ombi lao hilo
na akawapa muda wa siku tatu na akamuwakilisha Ubaadah Ibn Swaamit kusimamia
utokaji na uondokaji wao. Wakaondoka na kwenda sehemu iitwayo
‘Adhri’aat’ katika nchi ya Shamu na waislamu wakaichukua ngawira mali na
silaha zao zilizokuwa nyingi. Ikumbukwe kwamba mayahudi hawa walikuwa ni
masonara na walikuwa ni watu wenye mapenzi makubwa katika ulimbikizaji wa
silaha. Mtume wa Allah akahodhi khumsi (moja ya tano 1/5) ya ngawira hii kwa
ajili ya Allah, Mtume wake, jamaa za Mtume, mayatima, masikini na wasafiri
walioharibikiwa. Na sehemu iliyosalia, yaani nne ya tano (4/5) akaigawanya
miongoni mwa maswahaba wake.
Kuvamiwa huku kwa Baniy Qayunqaa kulikuwa katikati ya mwezi wa
Shawwal (mfunguo mosi) wa mwaka wa pili wa Hijrah. Bwana Mtume akampa ukhalifa
(ugavana) wa mji huu wa mayahudi, Abuu Lubaabah Al-answaariy na bendera yake
akampa ami yake Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib. Hivi ndivyo Baniy Qayunqaa
walivyotolewa Madinah kwa sababu ya uasi na jeuri yao sambamba na kuanza kwao
uadui na uchokozi dhidi ya waislamu.
|