|
Yahudi
Ka’ab Ibn Al-Ashraf akarejea Madinah kutoka Makah alikokwenda kuchochea
fitna na uadui dhidi ya Mtume na waislamu. Akarudi hali ya kuwa uadui na chuki
yake kwa Mtume wa Allah ukiwa umerudufika kuliko ilivyokuwa kabla hajaenda
Makah. Na akawa na ulimi mchafu mno usiostahamilika kwa wanawake wa Kiislamu,
kiasi cha kumfanya Mtume kuwa na dhiki kubwa ya moyo na akatamani kupumzika na
shari la mtu huyu muovu. Akasema Mtume–Rehema na Amani zimshukie–kuwaambia
maswahaba wake: “Nani atakaye nipumzisha na shari ya Ibn Al-shraf?”
Muhammad Ibn Maslamah Al-Answaariy
akamwambia: “Mimi nitakutoshea nae, ewe Mtume wa Allah, mimi nitamuua.”
Mtume akamwambia: “Fanya hivyo ukiweza.” Akasema Ibn Maslamah: “Ewe
Mtume wa Allah, hakika ya mambo yalivyo hatuna budi kusema maneno ya uongo ili
tumpate.” Mtume akamwambia: “Semeni yatakayokudhihirikieni, nyinyi mna
uhalali wa kufanya hivyo.” Wakajikusanya katika jukumu la kumuua Ka’ab Ibn
Al-Ashraf, Muhammad Ibn Maslamah mwenyewe na wenzake. Wenzake hawa
walikuwa Ubbaad Ibn Bishri, Al-Haarith Ibn Ausi, Abuu Iysa Ibn Jabri na
Silkaan Ibn Salaamah, huyu alikuwa ni ndugu wa kunyonya wa Ka’ab Ibn Al-Ashraf.
Ibn
Is-haaq-Allah amrehemu–anasimulia hali ilivyokuwa katika harakati za kumuuwa
adui huyu wa Mtume na waumini: “Kisha (baada ya kupata baraka za Mtume)
wakamuendea adui wa Allah; Ka’ab Ibn
Al-Ashraf. Wakabakia nje
akaingia Abuu Naailah (Silkaan Ibn Salaamah), akamjia akazungumza nae kitambo
na wakiimba mashairi. Abuu Naailah ndiye aliyekuwa muimbaji wa mashairi hayo.
Kisha akamwambia: Ole wako ewe Ibn Al-Ashfraf! Mimi nimekujilia na
jambo nataka kukuambia, basi nifichie siri. Akajibu (Ibn Al-Ashraf): Nitafanya
hivyo. Akaendelea kusema: Kuja kwa mtu huyu (yaani Mtume) kwetu imekuwa ni
balaa juu ya balaa! Waarabu wametufanyia uadui kwa sababu yake na
wametukusanyikia na kutupiga
vita. Na wametukatia njia mpaka familia zimekosa matunzo na nafsi zimehangaika.
Ka’ab akasema: Mimi ndiye mtoto wa Ibn Al-Ashraf ama wallah, nilikuwa
nikikuambia ewe Ibn Salaamah kwamba mambo yatakuwa kama nisemavyo. Silkaan
akamwambia: Kwa yakini mimi nataka utupe ahadi nasi tukuweke rahani ili
tukuamini nawe ututendee wema katika hili. Akasema (Ibn Al-Ashraf) Mtaniwekea
rahani watoto wenu? Akasema (Silkaan): Unataka kutufedhehesha, mimi ninao
wenzangu wenye fikra kama zangu na ninataka nikuletee uwape ahadi na ufanye
wema katika hilo. Nasi tukuwekee rahani silaha za kutosha ili kutekeleza ahadi
zetu kwako. Akasema (Ibn Al-Ashraf): Hakika katika kuweka rehani silaha ni
kutekeleza ahadi.
Ibn
Is-haaq anaendelea kusimulia:
Silkaan akarejea kwa wenzake (aliowaacha nje) akawapa khabari ya
waliyozungumza yote. Akawaamuru
kwenda kuchukua silaha, kisha warudi wakutane nae usiku.
Wakakutana kwa Mtume–Rehema na Amani zimshukie–akaenda nao mpaka
sehemu iitwayo “Baqi’il-gharqad”, kisha akawaelekea na kuwaambia:
“Enendeni kwa jina la Allah, ewe Mola wa haki wasaidie”.
Kisha Mtume akarudi nyumbani kwake katika usiku wa mbalamwezi. Wakaenda
mpaka wakafika katika boma la Ibn Al-Ashraf, Abuu Naailah (Silkaan) akampigia
ukelele wa kumjulisha kuwa wamekuja kwa ajili ya ahadi yao. Kusikia hivyo
akalichupia guo lake la kujitanda, mkewe akashika ncha ya guo hilo na
kumwambia: Hakika wewe ni mtu mshindani unayewaniwa na kukamiwa na watu wa
vita huwa hawatoki nje saa hizi (usiku). Akamjibu mkewe: Huyo ni Abuu Naailah
(ndugu yangu wa kunyonya), lau angenikuta nimelala asingeliniamsha Mkewe
akamwambia: Wallah, mimi naona kuna shari katika sauti yake hiyo. Ka’ab akamwambia mkewe: Lau kijana shujaa aitiwa mchomo wa
mkuki basi angeitika tu wito huo (shujaa haogopi) Akatoka akazungumza nao
kitambo, kisha wakamwambia: Waonaje ewe Ibn Al-Ashraf tukienda mpaka
Shi’ibil–Ajuuz, tuzungumze hapo usiku kucha? Akajibu: Mkitaka. Wakaenda
wakitembea, wakatembea kitambo kidogo Abuu Naailah akamshika Ibn Al-Ashraf
kichwani, kisha akaunusa mkono wake na kusema: Sijapata katu kunusa manukato
yenye kunukia sana kama haya ya usiku wa leo. Kisha wakaenda kitambo kidogo,
akarudia kufanya vile vile kama mwanzo kwa mara ya pili. Wakaenda tene kitambo
kidogo, akarudia tena mara ya tatu, sasa akamkamata barabara nywele za utosi
kisha akawaambia wenzake: Mpigeni panga adui wa Allah, Panga zao zikamuangukia
moja baada ya nyingine.”
Hiki
ndicho kisa cha adui wa Allah; Ka’ab Ibn Al-Ashraf kama alivyokipokea
mwanasira Ibn Is-Haaq, kadhalika wamekipokea wanasira wengine katika vitabu
vya sira kwa riwaya inayoshabihiana na hii. Kwa mauji haya ya Ka’ab Ibn Al-Ashraf,
Allah akawa amewapumzisha waislamu na shari ya mtu muovu huyu ambayo alikuwa
ameikusudia kwao. Baada ya mauji haya wakaenda kumpa khabari Mtume aliyewatuma
kuifanya kazi hii ya kuuhami Uislamu na waislamu Mauaji haya yalikuwa katika mwezi wa Rabiul-Awwaal (Mfunguo
sita) wa mwaka wa pili tangu Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–alipohamia
Madinah.
TANBIHI:
Waandishi wengi wa kimashariki (Orientalists) walioandika katika uwanja
wa sira ya Mtume, wanayatazama na wanayafasiri mauaji haya ya Ibn Al-Ashraf
kwamba ni “Mauaji haramu ya kihaini/kisaliti.” Wakayashikia bango mauji
haya na kuyafanya kuwa mada ya kumtukana na kumvunjia heshima Mtume wa Allah Wakafikia kusema kwamba tukio hili liliitia doa jeusi
historia nyeupe ya Mtume. Hebu na
tuitumie lugha yao na tuyaite mauji haya kama wayaitavyo wao kuwa ni “Mauaji
haramu”, kwa kuwa yalikuwa ni ya kushtukiza. Kadhalika tukubaliane nao
kwamba yalisimama katika misingi ya kihaini na usaliti. Kisha baada ya
kuzungumza lugha yao na kukubaliana nao, sasa tuwaulize:
-
Je
mauaji haya haramu ya kisaliti alifanyiwa nani; adui au walii (mtu mtukufu
aliye kipenzi cha Allah)? Na
-
Je,
alikuwa adui huyu anataka vita au amani? Na
-
Je,
ni lipi kati ya makundi mawili haya; waislamu na mayahudi lililoanza
kutumia njia ya uhaini? Na
-
Je,
ni kundi lipi kati ya mawili haya lililoanza uadui na kuuonyesha waziwazi
na likavunja mkataba wa amani waliokubaliana? Na
-
Je,
ni kundi lipi lililomshakizia na kumchochea mwenzake maadui wamkusanyikie
kuja kumpiga?
Mashwali
haya yanahitaji jawabu linalotaka elimu ya kuwaza kwa akili halisi inayotoa
hoja. Elimu inayotegemea na
kuegemea uhalisia wa kihistoria na matukio yake ya kweli si ya kubuni ili
kukidhi matakwa ya muandishi na kushibisha malengo yake.
Ni kwa msingi wa jawabu la namna hii ndio tunaweza kulihukumu suala
hili la mauji ya Ibn Al-Ashraf.
NI
KUNDI LIPI LILILOVUNJA AHADI (MKATABA) YA AMANI?
Wamekongamana wapokezi wa sira juu ya kwamba Mtume wa Allah alifanya
maagano na Mayahudi alipofika Madinah. Akaandikiana
nao mkataba wa amani na kwamba Mtume awaache na dini yao na wao wamuache
wasimbughi na wala wasimuingilie
katika dini yake. Wakakubaliana
kwamba wasimuunge mkono wala kumsaidia adui wa Mtume na kwamba watashirikiana
na waislamu dhidi ya adui atakayeivamia Madinah. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu–anatunakilia
sehemu ya vipengele vya mkataba huo: “Mayahudi waendelee kufuata dini yao na
waislamu waachiwe kuabudu kwa mujibu wa imani ya dini yao.
Ila atakayefanya dhulma au dhambi, huyu hataingamiza ila nafsi yake na
watu wa nyumbani kwake. Na kwamba ni juu yao kunusuriana dhidi ya ambaye
atakayempiga vita mmojawapo wa wana mkataba huu (waislamu/mayahudi). Na kwamba
Makurayshi na washirika wao wasipewe ushirikiano/msaada dhidi ya waislamu. Na
kwamba atakayetoka Madinah kwa khiyari yake ameaminika (ana amani) a
atakayebakia ameaminika pia, ila atakayefanya dhulma na dhambi. Kwa yakini
Allah atamuhifadhi na kumpa amani atakayefanya wema na kumcha.”
Mkataba
huu uliwadhaminia mayahudi kuishi na waislamu kwa amani na salama, kwa sababu
vipengele vyake vilibainisha wazi haki na wajibu wa kila kundi kwa mwenziwe.
Na msingi wa mkataba huu ulikuwa ni kusaidiana (ushirikiano) na kila mmoja
kuwa mkweli kwa mwenziwe na kunusuriana dhidi ya dhalimu au mchokozi yo yote.
Je, mayahudi walikuwa ni wakweli kwa waislamu kwa mujibu wa mkataba huu? Allah
Mjuzi mno wa siri za nafsi anawashuhudia kuwa hawakuwa wakweli na
akawatahadharisha waislamu kuwaamini katika kipindi hiki cha mpito. Anasema:
“ENYI MLIOAMINI! MSIWAFANYE WASIRI WENU WATU WASIOKUWA KATIKA NYINYI: HAO
HAWATAACHA KUKUFANYIENI UBAYA. WANAYAPENDA YALE YANAYOKUDHURUNI. BUGHUDHA (yao
juu yenu) INADHIHIRIKA KATIKA MIDOMO YAO NA YANAYOFICHWA NA VIFUA VYAO NI
MAKUBWA ZAIDI. TUMEKUBAINISHIENI DALILI (zote) IKIWA NYINYI NI WATU WA
KUFAHAMU. OH! NYINYI MNAWAPENDA (maadui zenu hao), HALI WAO HAWAKUPENDENI!
NANYI MNAAMINI VITABU VYOTE (chenu na vyao) NA WANAPOKUTANA NANYI HUSEMA:
TUMEAMINI LAKINI WANAPOKUWA PEKE YAO WANAKUUMIENI VYANDA KWA UCHUNGU (wa
kukuchukieni) SEMA: KUFENI KWA UCHUNGU WENU (huo), HAKIKA ALLAH ANAYAJUA (hata)
YALIYOMO VIFUANI. IKIKUPATENI KHERI HUWASIKITISHA NA IKIKUPATENI SHARI
WANAIFURAHIA NA KAMA NYINYI MKISUBIRI NA MKAMCHA ALLAH, HILA ZAO
HAZITAKUDHURUNI KITU HAKIKA ALLAH ANAYAJUA VIZURI YOTE WANAYOYATENDA.”
(3: 118-120)
Ndani
ya aya hizi mna taswira na picha halisi ya undani wa mayahudi na uadui wao
waliouficha nyoyoni mwao dhidi ya waislamu. Matendo ya mayahudi ni ushahidi
tosha juu ya haya; ni kwa nini ushindi wa waislamu dhidi ya makurayshi katika
vita vya Badri uliwakera na kuwaudhi?! Hivi ushindi huu haukustahiki
kuwafurahisha, kwa sababu ni ushindi wa washirika na jirani zao na isitoshe ni
ushindi wa watu wanaoshabihiana nao kiitikadi. Hivi tendo lao hili si kuvunja
mkataba walioandikiana na waislamu na wao kuuridhia? Kwa hakika tunaweza
kusema kwa majumuisho kwamba ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa
Ka’ab Ibn Al-Ashraf alijiua mwenyewe kwa kujitengenezea mazingira
yaliyosababisha kuuawa kwake. Huu
ndio ukweli na haki, tumeikubali au tumeikataa bado historia itaendelea
kuikiri.
|