|
MAKURAYSHI
WAFANYA JARIBIO LA KUREJESHA HESHIMA YAO ILIYOPOTEA KWA KUSHINDWA KWAO KATIKA
VITA VYA BADRI.
Ulipoingia mwezi wa Dhul-Hijjah (Mfunguo wa tatu) yaani baada ya kupita
takriban miezi miwili na nusu tangu kumalizika kwa vita vya Badri. Alitoka
Abuu Sufyaan na askari wapanda wanyama mia mbili wa kikurayshi, kuwafuata
mayahudi wa Banin–nadhwiyr. Wakamgongea Huyay Ibn Akhtwab kumuulizia khabari
za Mtume na maswahaba wake, naye akakataa kuwafungulia.
Wakaondoka wakaenda kumgongea Sallam Ibn Miksham, huyu akawafungulia,
akawakaribisha na kuwakirimu. Kisha
akawapa khabari zote anazozifahamu juu ya Mtume. Wakabakia pale mpaka usiku wa maladaku (karibu na alfajiri),
ndipo Abuu Sufyaan akatoka na jeshi lake mpaka mahala panapoitwa “Uraydhw,”
hii ni sehemu iliyo umbali wa maili tatu kutoka Madinah. Hapo akafanya uharibifu na ukatili mkubwa, akamuua mmoja
katika Answaar na mtumishi wake, akachoma nyumba kadhaa na chakula cha mifugo.
Kwa kitendo chake hiki haramu akaona tayari ameshatekeleza yamini (kiapo)
yake, huyoo akakimbia kurudi Makah Turejee nyuma kidogo tuone asili ya yamini
hii ya Abuu Sufyaan iliyompelelekea kufanya unyama huu.
Ikumbukwe kuwa miongoni mwa waliouawa katika vita vya Badri walikuwemo
Utbah Ibn Rabeii ambaye ni baba mzazi wa Hindu (mkewe Abuu Sufyaan), ami na
kaka ya Hindu pia waliuawa. Kwa msiba huu mkubwa uliompata Bi. Hindu akaapa
kulipa kisasi kwa Mtume na maswahaba wake kutokana na watu wake hawa waliouawa. Ili kuonyesha hisia zake za uchungu akakihama kitanda cha
mumewe Abuu Sufyaan na akajiharamishia manukato mpaka alipe kisasa cha watu
wake hawa. Nae Abuu Sufyaan
katika kumuunga mkono mkewe katika machungu yake hayo, akaapa maji kutokugusa
kichwa chake (hataoga) mpaka awalipie kisasi makurayshi na kurejesha heshima
yao baina ya waarabu. Ni kiapo
hiki (yamini) ndicho kilichomsukuma Abuu Sufyaan kufanya yote aliyoyafanya “Uraydhw.”
Haya sasa na tuendelee, khabari za shambulizi hili zikamfikia Mtume wa
Allah–Rehema na Amani zimshukie. Akawaita
maswahaba wake, akatoka na watu mia mbili katika Muhajirina na Answaar
kuwafuatia maadui hawa. Huku Abuu
Sufyaan na watu wake wakijitahidi kwenda mbio kadri wawezavyo ili wasikutwe
njiani kabla ya kuingia Makkah. Ili
wawe wepesi katika kukimbia kwao wakawa wanatupa njiani baadhi ya mizigo
iliyobebwa na wanyama wao. Wakatupa
vyombo vilivyobeba chakula chao kikuu kilichojulikana kama “Sawiyq”; hii
ni aina ya chakula kinachotengenezwa kwa unga wa ngano/shayiri mithili ya
chapati. Waislamu wakapita
wakikiokota chakula hicho bila ya kukutana nao, kwani tayari walikuwa
wameshaingia katika himaya yao. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie–akarejea Madinah
baada ya siku tano tangu alipotoka kufuatia uchokozi huu wa Makurayshi.
Na alikuwa amemtawalisha Abuu Lubaabah Bishri Ibn Al-Mundhir kushika
nafasi yake kwa kipindi chote alichokuwa nje ya Madinah.
Katika shambulizi hili waislamu walijikusanyia
Sawiyq nyingi na ndio ikawa sababu ya kuitwa shambulizi hili kwa jina
hili la “Shambulizi la Sawiyq”.
Machoni
mwa Makurayshi kukimbia huku kwa Abuu Sufyaan ilikuwa ni sawa na kushindwa na
kuwapa ushujaa waislamu. Ili
kufuta mawazo na fikra hizi wakaanza matayarisho kabambe kwa vita vikubwa.
Vita vitakavyowarudishia heshima na tisho lao miongoni mwa makabila ya
Waarabu. Haikuwa heshima/utukufu
pekee ndio uliowapelekea kutaka kuingia vitani tena.
Bali ilikuwepo dharura nyingine, dharura ya usalama wa misafara yao ya
biashara kwenda Shamu na kurudi Makah. Kwani
sasa njia iliyozoeleka haina amani kutokana na waislamu kuivizia kwa lengo la
kuiteka. Ikawa hapana budi
kupanga mikakati itakayowahakikishia usalama wa misafara yao hiyo.
MAKURAYSHI
WAUPITISHA MSAFARA WAO WA KIBIASHARA KATIKA NJIA IELEKEAYO IRAQ.
Siku moja Swafwaan Ibn Umayyah alisimama na kuwaambia Makurayshi
wenzake: “Hakika Muhammad na watu wake wametuharibia biashara yetu, hatujui
tuwafanyeje nao bado wameweka vizuizi katika njia yote ya pwani. Na wenyeji wa
pwani wamefunga nao ahadi na isitoshe wengi wao wameshawafuata, hatujui tuishi
wapi sasa? Tukiendelea kubakia katika miji yetu tutakula rasilimali yote mpaka
kisisalie kitu. Na bila ya shaka
maisha yetu hapa Makah yanategemea kwa kiasi kikubwa biashara ya Shaam katika
majira ya kusi na ile ya Habashah (Abyssinia) majira ya Kaskazi.”
Al-Aswad Ibn Mutwalib akainuka na kumwambia: “Cha kufanya sasa ni
kuiachilia mbali njia hii ya pwani na tuitumie njia ya Iraq, kwani hiyo ni
ardhi ya uwanda wa juu haipiti njia hii ye yote miongoni mwa watu wa
Muhammad.” Akamfahamisha juu ya
mtu mmoja wa kabila (ukoo) la Baniy Bakri Ibn Waail aitwaye Furaat Ibn Hayaan
ili amuongoze katika njia hiyo. Swafwaan
akajiandaa tayari kwa msafara wa kupitia njia hii mpya iliyopendekezwa na Al-Aswad,
akakusanya fedha (madini) na
bidhaa mbalimbali zenye thamani ya Dir-ham alfu moja (hizi ni pesa nyingi sana
kwa wakati huo). Msafara ukaanza safari huku ukiamini kwamba khabari ya kutoka
kwao haitavuja na kuwafikia mahasimu wao; waislamu lakini kumbe bila ya kujua
mmojawapo wa majasusi wa Kiislamu tayari alikuwa ameshainusa khabari hiyo.
Na bila kuchelewa akautimiza wajibu wake akaifikisha kwa Bwana Mtume
nae bila ya kufanya ajizi akaanza kuifanyia kazi khabari ile.
Akamtuma Zayd Ibn Haarithah kukiongoza kikundi cha wapandaji mia moja
miongoni mwa Muhajirina na Answaar. Wakaenda
mpaka wakautokezea kwa ghafla msafara ule katika eneo liitwalo “Al-Qaradah”.
Hili ni eneo lenye maji la Najid, wanamsafara ule wakatimua mbio
kutokana na khofu ya kushitukizwa walikokuwa hawakukutarajia kabisa.
Wakakimbia wakiuacha msafara na mali zake zote na kutoa fursa kwa
waislamu kuichukua ngawira baridi isiyo na vita/mapambano.
Hii ndio ngawira nono ya kwanza waliyoipata waislamu bila ya kuitolea
nguvu. Bwana Mtume akaipiga
mafungu matano na kuigawa baina ya maswahaba wake.
Jaribio
hili la waislamu lililofanikiwa likawa ni miongoni mwa sababu zenye nguvu
zilizowafanya Makurayshi kufanya juhudi za makusudi kutaka kuwaonyesha
waislamu nafasi yao. Suala sasa
likawa si tu suala la kulinda hadhi na kurejesha heshima yao, bali suala la
ama kufa au kupona. Ama
Makurayshi waendelee kuwa dhalili na dhaifu mbele ya Muhammad na watu wake na
kukubali hili bila shaka ni kuchagua kuangamia.
Au wajiandae kutoa pigo la kusambaratisha litakalo wahifadhia maisha
yao na kuwarejeshea kitisho chao (awe) baina ya makabila ya Waarabu.
Kwa hivyo Makurayshi wakaanza kukusanya nguvu zao tayari kabisa
kuwavamia waislamu Madinah kwa lengo la kuwasagasaga kabisa na kukata mzizi wa
fitna. Katika kipindi hiki cha
mpito kuelekea vita vikali vinavyopikwa na makurayshi yalitokea mapambano ya
hapa na pale baina ya waislamu na baadhi ya makabila yaliyokuwa yakiishi
jirani na Madinah. Mapambano
yaliyoishia kuwapa ushindi na ngawira waislamu ambao sasa walianza kuonekana
kama wababe wa vita wanaochukua nafasi ya Makurayshi katika medani hii ya
vita. Kila mara Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–alipopata khabari
ya kujikusanya kikundi cha watu hawa dhidi yake.
Alikitokea ghafla na maswahaba wake kabla hakijajiandaa na kukifagilia
mbali na kuwaacha wakikimbilia majabalini. Mapambano haya ni pamoja na
shambulizi la “Ghatw-faan,” sehemu za Najid katika mwezi wa Rabiul-Awwal (Mfunguo
sita) mwaka wa tatu wa Hijrah. Na
shambulizi la Baniy Sulaym katika sehemu ya “Bahraan”, lililofanywa katika
mwezi wa Jumaadal-Uula (mfunguo nane) wa mwaka huo huo.
Baadhi
ya wanahistoria wanaieleza sababu ya machafuko haya yaliyofanywa na makabila
haya kuwa ni kutokana na ushirika wao na makurayshi. Wengine wanasema yalikuwa
ni ya kulinda na kutetea maslahi yao, kwa sababu kwa kiwango kikubwa maisha
yao yalitegemea kodi ya njia iliyotolewa na misafara ya kibiashara ya
makurayshi inayopita kwao wakati wa kwenda na kurudi.
Waislamu walipowakatia makurayshi njia yao hii, makabila haya
yakajichelea dhiki na taabu.
|