|
SOMO
LA KWANZA.
I/.
MAKURAYSHI WAANZA KUJIANDAA NA VITA.
Fikra waliyokuwa wakiifanyia kazi makurayshi tangu kumalizika kwa vita
vya Badri. Ilikuwa ni kukusanya
nguvu zake zote, kwa lengo la kuelekeza pigo la kuvunjavunja litakalommalizia mbali Bwana Mtume na maswahaba wake. Kwa
pigo hili takatifu watakuwa wameifagilia mbali na kuitokemeza kabisa dini yake
hii mpya inayotishia utukufu na maslahi yao. Wakaanza kufanya maandalizi
motomoto kwa ajili ya kuitimiza fikra yao hii. Wakaaza kuchanga pesa,
kukusanya zana za vita na kuyapelekea wajumbe wake makabila ya waarabu yaliyo
pembezoni mwao kuomba ushirikiano wao ili kuufanikisha mkakati wao huu.
Miongoni mwa wajumbe (mabalozi) hawa alikuwa Abuu Azah; mshairi aliyetendewa
wema na Mtume kwa kumuacha huru bila ya fidia katika vita vya Badri. Nae kwa
kuonyesha shukrani zake kutokana na ukarimu aliotendewa akachukua ahadi ya
kutokumsaidia ye yote dhidi ya Mtume wala kuwa miongoni mwa adui zake. Akavunja ahadi aliyoiweka mwenyewe akaenda pamoja na wajumbe
wengine sehemu za Kinaanah na Tihaamah, kuwahamisha watu wa sehemu hizo
kujiunga nao katika vita hii dhidi ya Mtume.
Katika kipindi cha takribani mwaka mzima Makurayshi waliendelea
kukusanya mali, washirika na kutayarisha chakula kitakachokidhi mahitaji ya
jeshi. Mpaka vikafikia kiwango walichokikusudia
katika tathmini yao, wakaridhika na maandalizi hayo na kuona kuwa yamekamilika
na kutimia. Na kwamba yanaweza kuwafikisha katika lengo lao na kuwahakikishia
ushindi. Karibu na kumalizika kwa mwaka wakatoka na jeshi linalotoa mvumo wa
sauti ya kutisha kutokana na wingi wa idadi yake. Walitoka pamoja na washirika wao wa Tihaamah na Kinaanah,
pamoja na ndugu zao wa yamini; Wahabeshi wa Banil-Mustwaliq na Banil-Huun Ibn
Khuzaymah. Wakaelekea Madinah wakiwa na hamasa iendeshwayo na ukali wa
ghadhabu ya kutoa pigo la kuvunjavunja na kuhilikisha.
Wanawake wa Kikurayshi nao hawakubakia nyuma, walikuwa bega kwa bega na
waume, baba na kaka zao wakiwahamasisha na kuwatia mori na ari. Kongozi wa
wanawake hawa alikuwa ni Hindu Bint Utbah; mkewe Abuu Sufyaan Ibn Harb.
Miongoni
mwa waliotika wito wa makurayshi dhidi ya Bwana Mtume na kujiunga na jeshi
lao, alikuwa ni Abuu Aamir Al-Ausiy. Huyu ni mtu wa kabila la Ausi (Ausi na
Khazraji ni makabila makuu ya waarabu wa Madinah), alikuwa mpinzani wa Mtume
na akiukanusha utume wake. Huko nyuma alijitia utawa akidai kumgonjea Mtume
atakayeletwa katika zama hizo. Akiwatajia watu sifa za Mtume huyo na akiwaambia: Hakika
zimekurudia zama za kuja kwake. Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–alipohamia Madinah na sifa zake
kuwadhihirikia maanswaari kama walivyoambiwa wakamfuata na kumuamini. Abuu
Aamir kuona hivyo, akamfanyia husuda Mtume na kuukanusha utume wake. Alikuwa
ni kiongozi wa Ausi kama alivyokuwa Abdullah Ibn Ubayyi kwa Khazraj; wawili
hawa wote walimfanyia hasadi Mtume. Lakini Abdullah Ibn Ubayyi aliingia katika
Uislamu kinafiki na huyu alijitenga kabisa na Uislamu na kuendelea kuwa
kafiri. Akatoka na kundi lake la watu khamsini miongoni mwa vijana wa kiausi,
akakaa Makah akiwaunga mkono makurayshi na kuwahimiza kupigana na Mtume.
Makurayshi walipoazimia kutoka kwenda Uhud, Abuu Aamir aliwaahidi Makurayshi
kuwashawishi jamaa zake Ausi kumtupa mkono Bwana Mtume.
Watoke katika safu ya waislamu wajiunge na safu ya mushrikina
yatakapokutana vitani makundi mawili hayo.
Alitegemea kuyafikia haya kutokana na nafasi/cheo alichokuwa nacho huko
nyuma kwa kabila lake. Akiamini
kabisa kwa cheo chake hicho ataweza kuigawa safu ya waislamu.
MAKURAYSHI
ALFU TATU WAELEKEA UHUD.
Mwanzoni mwa mwezi wa Shawwaal (Mfunguo mosi) wa mwaka wa pili wa
Hijrah, lilitoka Makah kuelekea Uhud jeshi lenye kila alama ya maangamizi.
Jeshi hili lenye imani ya ushindi kwa asilimia mia moja liliongozwa na Sufyaan
Ibn Harb. Bendera ya jeshi
ikibebwa na Twalhah Ibn Abuu Twalhah, kuliani mwa jeshi alikuweko kamanda
Khaalid Ibn Al-Waleed na kushotoni Ikrimah Ibn Abuu Jahli.
Huku askari wa miguu wakiongozwa na Swafwaan Ibn Umayyah. Hili ndilo
jeshi la askari alfu tatu, jeshi lenye maandalizi makubwa na kamili, miongoni
mwao wakiwemo wapanda farasi mahiri mia mbili, mia saba wenye vifuniko vya
chuma kama kinga ya mwili (armoured) dhidi ya shambulizi za panga, mikuki,
mishale na kadhalika. Wengi wa
askari wakiwa wamepanda wanyama, wakifuatiwa na kundi kubwa la watumwa wa
kuwasaidia na kuchunga mizigo yao. Miongoni mwa watumwa hawa alikuwemo mmoja
Muhabeshi aitwaye “Wahshiy”, huyu alikuwa na umahiri mkubwa wa kihabeshi
wa kurusha mikuki. Bwana wake Jubayr Ibn Mutw-im akamshakizia kumuua Sayyidna
Hamzah Ibn Abdul–Mutwalib; ami yake Mtume, na akamwambia: “Ukimuua Hamzah
utakuwa huru”. Kadhalika Hindu Bint Utbah alimuahidi kwa kumuua Hamzah kumpa
mali mengi. Haya yalikuwa ni kutaka kulipa kisasi kutokana na Sayyidna Hamzah
kuwauwa katika vita vya Badri, Twuaimah Ibn Adiy; ami yake Jubayr na Utbah Ibn
Rabeei; baba yake Hindu.
MIKAKATI
YA MAKURAYSHI.
Mwenendo na mpangilio wa vita wa Makurayshi ulidhihirisha kuwa
walipanga mikakati maalum ili kujihakikishia ushindi mkubwa katika vita hivi.
Mkakati wao ulikuwa ni kuwashambulia waislamu ndani ya Madinah kwa mtindo wa
kushtukiza, kabla hawajajiandaa na hivyo kukosa nafasi ya kutoa upinzani.
Mkakati huu ukishindwa kutokana na kuvuja kwa khabari ya kutoka kwao
ikawafikia waislamu wakajiandaa. Basi
utumike mkakati wa kuzigawa safu zao katika medani ya vita. Huu ukishindwa,
basi utumike mkakati wa kumuua Mtume wa Allah, kisha wauawe maswahaba wakubwa
(viongozi) katika muhajirina (wa Makah wenzao). Mauaji ya watu hawa yatawaacha
waislamu wakiwa wamesambaratika hawana kiongozi wa kuongoza mapambano.
Jambo hili litawapa ushindi usio na gharama kubwa. Mikakati hii ndio
iliyowapelekea makurayshi kutoka kwa siri ili wasiwashtue waislamu. Wakaenda
kwa uficho mpaka wakapiga kambi katika bonde la Uhud lililo kiasi cha umbali
wa maili tano kutoka Madinah. Lau si kuwa Sayyidina Abbas Ibn Abdul-Mutwalib
kumuandikia barua Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie- kumjuza juu ya
kutoka kwa Makurayshi. Jeshi hili
lingeingia mjini Madinah wakati wenyeji wake wakiwa katika mghafala. Kwa
mujibu wapokezi wa Sira ni kwamba Sayyidina Abbas alimuandikia barua
Mtume wa Allah kumfahamisha khabari ya makurayshi na maandalizi yao
yote; watu, zana na namna
walivyopania. Akamtuma kupeleka barua hii mtu mmoja kutoka katika ukoo wa
Baniy Ghifaar. Tarishi huyu akaunga mwendo mchana na usiku mpaka akafika
Madinah baada ya siku tatu. Alipofika Madinah akang’amua kuwa mtume hayupo
hapo, yupo Qubaa nje kidogo ya Madinah mjini.
Akamfuata huko na kumkabidhi barua, Bwana Mtume akaipokea na kumpa
Ubayyi Ibn Ka’ab kumsomea. Baada
ya kumsomea, Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–akamtaka asiitangaze
khabari hiyo. Halafu Mtume akamuendea Sa’ad Ibn Rabeei akamjuza khabari ya
barua. Sa’ad akamwambia Mtume: “Wallah mimi ninatarajia kuna kheri katika
jambo hili”. Mayahudi na wanafiki wakaivumisha khabari ya barua, ikatangaa
kwa watu jambo ambalo makuryshi walilichelea kutokea.
Al-Waaqidiy amepokea kutoka kwa Abdullah Ibn Amrou Ibn Abiy Hakiymah
Al-Aslamiy–amesema: “Abuu Sufyaan alipopambazukiwa akasema: Ninaapa kwa
Allh kwamba wamempelekea Muhammad khabari za kwenda kwetu na wamemtahadharisha
na kumjuvya idadi yetu. Kwa hiyo,
wao sasa wanalazimikiana na ngome zao, sidhani kama tutakabiliana nao ana kwa
ana. Swafwaan akamwambia: Wakitotoka kupambana nasi katika mbuga hii jangwani,
tutaviendea viunga vya mitende vya Ausi na Khazraji na na kuifyekelea mbali
yote. Hivyo tutawaacha wakiwa hawana mali na hawataweza kuuzuia ufakiri
abadan. Na iwapo watatutokea basi
idadi yetu ni kubwa mno kuliko yao na tuna silaha nyingi kuliko wao. Isitoshe
sisi tuna farasi wao hawana, tena sisi tunapigana kwa ajili ya kisasi na wao
hawana kisasi nasi”.
|