|
Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-akatuma wapelelezi wake
kupeleleza khabari za mahasimu wake. Wakarudi na kumpasha khabari kwamba
wamepiga kambi katika bonde la Uhud, wakamkadiria idadi yao na utayarifu wao.
Mushrikina hawa walikuwa wamewaachia farasi na ngamia wao kula katika
mashamba ya watu wa Madinah yaliyokuwa nje kidogo ya mji.
Walifanya hivyo makusudi kwa lengo la kuwadhoofisha waislamu kiuchumi
kwa siku za usoni. Mifugo hii ikafanya uharibifu mkubwa kutoka na kula mimea na
miti kwa kiasi kikubwa mpaka ikakaribia kuingia Madinah. Khatari ikawajongelea waislamu mpaka milangoni, ikalazimu
sasa zichukuliwe hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo ya hatari
bila ya kuchelewa. Ikawawajibikia waislamu kuchukua tahadhari na kujiandaa
kupambana na adui aliye milangoni mwao. Mji wote wa Madinah ukawekwa chini ya
doria kali usiku kucha, waislamu wengine wakakesha msikitini na silaha tayari
kwa lo lote wakimlinda Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie. Kulipopambazuka Bwana Mtume akawakusanya washauri wake na
kuanza kushauriana juu ya mahala pa kukutana/kupambana na adui huyu.
Al-Waaqidiy–Allah
amrehemu–amepokea kwamba: “Bwana Mtume– Rehema na Amani
zimshukie-aliwaambia maswahiba wake: “Nipeni ushauri”. Abdullah Ibn Ubayyi
akasimama na kusema: “Ewe Mtume wa Allah, sisi tulikuwa katika jahilia
tukipigana katika zama hizo tuliwaweka wanawake na watoto katika ngome na
tukawapa mawe. Tukauunganisha mji wa Madinah kwa majengo mpaka ukawa kama
ngome kwa kila upande. Kazi ya wanawake na watoto ikawa ni kuwapopoa maadui
kwa mawe kutokea juu ngomeni na vilimani, nasi tukawa tunapigana kwa panga
zetu katika njia zilizo wazi. Ewe Mtume wa Allah, kwa yakini
mji wetu huu wa Madinah katu haujawahi kuingiwa na adui, nasi
hatujapatapo kumtokea adui nje yake ila alitushinda. Na hajapatapo kutuingilia humu ndani ila tulimshinda tu.
Basi ewe Mtume wa Allh achana nao, kwani wakikaa huko nje watakuwa
wamejipa wenyewe kifungo kibaya. Na
kama wataamua kurudi Makah, watakuwa wamerejea patupu hali ya kushindwa bila
ya kupata la manufaa. Ewe Mtume
wa Allah, nakusihi unitii katika shauri hili na utambue kwamba mimi nimeirithi
rai hii kutoka kwa wazee wangu wenye busara ambao walikuwa na uoni na uzoefu
wa mambo”.
Rai
ya Mtume wa Allah–Rehema na amani zimshukie–ikasadifu kuwafikiana na rai
hii iliyotolewa na Ibn Ubayyi. Rai
hii ya Mtume ilitokana na ushauri wa maswahaba wake wakubwa kutoka pande zote
mbili; Muhajirina na Answaar. Mtume
wa Allah akasema: “Kaeni/bakieni Madinah na wawekeni wanawake na watoto
ngomeni, wakituingilia mjini mwetu tutapambana nao katika vijia ambavyo sisi
tunavijua zaidi kuliko wao (vichochoro).
Na wapopoeni kwa mawe na mishale kutokea juu ngomeni.
Vijana barobaro ambao hawakushiriki katika vita vya Badir kutokana na
umri wao kutowaruhusu. Vijana hawa walipandwa na mori na raghba ya kufa
mashahidi, wakapenda kukutana na adui ana kwa ana, wakasema: “Ewe Mtume wa
Allah, tutoe tukapambane na adui huyu.” Na watu wazima wenye dhamira njema
wakasema kwa nia njema kabisa: “Ewe Mtume wa Allah, sisi tunachelea adui
yetu kudhani kuwa sisi tumeogopa kumtokea kwa uoga wa kupambana nae.
Hili litawapa moyo wa ujasiri juu yetu.
Katika vita vya Badri ulikuwa na watu mia tatu tu na bado Allah akakupa
ushindi juu yao. Leo sisi tuko
wengi na tulikuwa tukiitamani siku hii na tukimuomba atufikishe, sasa leo
Allah ametuletea siku hii mipakani mwetu”. Maalik Ibn Sinaan nae akasema:
“Ewe Mtume wa Allah, sisi ni watu tulio baina ya (kupata) mojawapo ya mema
mawili. Ama Allah atupe ushindi
juu yao na hili ndilo tulitakalo. Na jingine ewe Mtume wa Allah, aturuzuku
Allah kufa shahidi kwa sababu yao. Wallah,
ewe Mtume wa Allah, sijali lo lote litakalokuwa kati ya mawili haya, kwani kwa
yakini kila moja lina kheri nasi”. Nae Sayyidna Hamzah akasimama na kusema:
“Naapa kumuapia yule ambaye aliyekuteremshia kitabu (Qur-ani), leo sitakula
chakula mpaka nipigane nao kwa upanga wangu huu nje ya Madinah”.
Huyu
ndiye Nu’umaan Ibn Maalik anainuka na kusema: “Ewe Mtume wa Allah, kwa
nini unatunyima pepo? Namuapia yule ambaye hapana Mola ila yeye nitawavaa
nitawavaa”. Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–akamuuliza: “Kwa
nini/kivipi?” Akamjibu: “Mimi ni mtu nimpendaye sana Allah na Mtume wake
na wala sitimui mbio siku ya vita”. Yule pale Iyaas Ibn Ausi nae anasema:
“Mimi sipendi makurayshi warudi kwao na kusema: Tumemzingira Muhammad katika
ngome za Yathrib, huu utakuwa ni ujasiri wa makurayshi kwetu angalia tayari
wameikanyagakanyaga mitende yetu, kama hatukuwafukuza mashamba hayalimiki”.
Abuu Sa’ad Ibn Khaythamah nae akasema: “Nilivikosa vita vya Badir ambavyo
nilivikamia, pupa yangu katika vita hivyo ilinifikisha kumtoa mwanangu
ashiriki. Akapata fungu lake kwa
kufa shahidi, nami niliuwania mno ushahidi.
Jana nilimuona mwanangu usingizini akiwa katika hali nzuri sana,
akivinjari katika matunda ya peponi na mito yake, nae akisema ungana nasi
usuhubiane nasi peponi, kwa yakini nimeyakuta aliyoniahidi Mola wangu kuwa ni
haki (kweli). Wallah, ewe Mtume
wa Allah nimepambazukiwa nikiwa na shauku ya kusuhubiana nae peponi. Umri
wangu umekuwa mkubwa na mifupa yangu imelegea nami napenda kukutana na Mola
wangu. Basi ewe Mtume wa Allah,
niombee kwa Allah aniruzuku kufa shahidi na kuungana na mwanangu Sa’ad
peponi”.
BWANA
MTUME ASALIMU RAI YA KUTOKA KWENDA KUPIGANA:
Bwana
Mtume–Rehema na Amani zimshukie–akaona kwamba kutoka ndio mapenzi na
matakwa ya walio wengi. Akawaswalisha mashwahaba wake Ijumaa, kisha
akawawaidhi na kuwaamrisha kufanya jitihada na bidii na akawaambia kwamba
watapata ushindi maadam watasubiri. Watu
wakafurahia mno kwenda kukabiliana na adui yao ana kwa ana.
Lakini miongoni mwao hawakupendezwa na utokaji huo kutokana na kuona
kwao katika uso wa Bwana Mtume dalili ya uchukivu.
Watu wakaanza kujiandaa kwa vita, wakavaa deraya zao na kuchukua silaha
zao wakaanza kujikusanya msikitini kwa Mtume wa Allah, ulipofika wakati wa
Alasiri watu walikuwa wameshajikusanya. Mtume akawaswalisha swala ya Alasiri,
baada ya kumalizika swala akaamrisha wanawake na watoto wawekwe katika ngome.
Kisha akaingia nyumbani mwake kujitayarisha huku akiwaacha watu
wakijadiliana juu ya suala la vita. Bado
lilikuwepo kundi miongoni mwao likiona kuwa rai ya kubakia Madinah ndio ya
sawa na kwamba watu wamemkalifisha Mtume kutoka wakati yeye hakutaka. Sa’ad
Ibn Muaadh na Usayd Ibn Hudhwayr wakasema kuwaambia wenzao: “Mmemwambia
Mtume wa Allah mliyomwambia na kumlazimisha kutoka na il-hali yeye anashushiwa
wahyi kutoka mbinguni. Basi lirudisheni suala hili kwake kwa uamuzi,
atakalokuamrisheni ndilo mlifuate. Lile
mtakaloona ana mapenzi nalo, basi mtiini”.
Wakati
wakiwa katika majadiliano hayo, Bwana Mtume–Rehema na Amani
zimshukie-akawatokea akiwa tayari amechukua zana zake za vita.
Wale waliokuwa wakishikilia kutoka wakasema: “Ewe Mtume wa
Allah,haitufalii sisi kukukhalifu, tenda likudhihirikialo”. Bwana Mtume
akawaambia: “Nilikwisha kuitieni shauri hili la kutotoka mkalikataa.
Na wala haimpasii Mtume ye yote (sio mimi tu) aliyekwisha vaa zana zake
za vita kuzivua mpaka Allah ahukumu baina yake na adui zake kwa vita. Basi kwa
hivyo liangalieni nililokuamrisheni ndio mlifuate na enendeni kwa jina la
Allah, ushindi ni wenu mkisubiri”.
|