|
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafunga bendera tatu. Akaitoa bendera ya
Ausi akampa Usaid Ibn Hudhwayri aibebe na kuipeperusha yeye. Bendera ya
khazraj akampa Al-Hubaab Ibn Al-Mundhir na ile ya Muhaajirina akampa Musw-ab
Ibn Umeir-Allah awaridhie wao na maswahaba wote
wa Mtume aliye kipenzi chake. Baada ya kukamilisha zoezi hili la
kukabidhi bendera za vita, Bwana Mtume akaagiza aletewe farasi wake, akampanda
na kutoka kuelekea uwanja wa mapambano. Akiwaongoza maswahaba wake alfu moja,
mia moja miongoni mwao wakiwa wamevaa diraya (nguo za chuma maalumu kwa ajili
ya vita). Akaenda huku kukiwa na kundi la maswahaba kuumeni na kushotoni kwake
na mbele yake kukiwa na walinzi wawili; Sa’ad Ibn Ubaadah na Sa’ad Ibn
Muaadh. Kutoka huku kwa Mtume wa Allah na jeshi lake kwenda katika vita hivi
vya Badri kulikuwa ni katika siku ya Ijumaa ya tarehe sita ya mwezi wa Shawwal
{mfnguo mosi} wa mwaka wa tatu wa Hijrah. Bwana Mtume kabla hajaondoka alimpa
uamiri wa kuwaswalisha watu wa Madinah swahaba wake Abdullah Ibn Ummu Maktuum.
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaenda mpaka akafika mahala panapoitwa
‘Shaykhayn’, akapiga kambi hapo. Kisha akalikagua jeshi na kuwaamuru
kurejea Madinah wale aliowaona kuwa hawajafikia umri wa kushiriki vitani
(wadogo). Miongoni mwa waliorudishwa na Mtume alikuwa ni kijana mdogo Raafii
Ibn Khadiij na samurah Ibn Jundub-Allah awawiye radhi. Bwana Mtume akaambiwa
hakika huyu Raafii unayemrudisha ni mlenga shabaha mzuri sana, ndipo alipompa
rukhsa ya kushiriki vitani, samurah alipoona mwenzake kapewa rukhsa na yeye
amekataliwa akalia sana na kusema: Bwana Mtume amemruhusu Raafii na
kunirudisha mimi na il-hali mimi ninamuangusha katika mieleka. Bwana Mtume
akayasikia maneno haya, ndipo
akaamrisha wapigane mieleka na mshindi akawa ni Samurah. Ushindi wake huu ndio
uliomshawishi Bwana Mtume amuidhinishe kushiriki vitani kama alivyomuidhinisha
Raafii.
ABDULLAH
IBN UBAYYI AMTUPA MKONO BWANA MTUME NA KUMEGA THELUTHI YA JESHI.
Usiku
ule Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie alilala pale pale Shaykhain mahala
alipopiga kambi. Akampa kazi ya kulinda jeshi (kufanya doria) Muhammad Ibn
Muslimah na Dhakwaan Ibn Qaysi akamfanya kuwa ni mlinzi wake yeye. Karibu na
kuchomoza kwa alfajiri Bwana
Mtume akaliamuru jeshi kuondoka, akaenda nalo mpaka akafika ‘Shautwa’, hii
ni bustani iliyo baina ya Madinah na Uhud. Hapa ndipo theluthi ya jeshi
ilipojitenga na Bwana Mtume, Abdullah Ibn Ubayyi akajitoa na wafuasi wake mia
tatu huku akisema: “Vijana wamemtii na kuniasi mimi, ni kwa lipi khasa
tuziue nafsi zetu hapa (kwa kupigana)? Abdullah Ibn Amrou Ibn Hiraam akajaribu
bila mafanikio kuwashawishi waache msimamo wao huu. Akawaomba kwa jina la
Allah wasiivunje fimbo ya umoja na wasiitupe mkono kaumu yao na Mtume wao
mbele ya adui. Yote haya hayakufaa kitu bali ndio yaliwachagiza kusema:
“Tungejua kuwa kuna kupigana bila ya shaka tusingelikufuateni”. Kitendo
hiki kibaya kilisababisha pengo kubwa sana katika muundo wa jeshi na mtikisiko
mkubwa katika nafsi za waislamu. Kitendo hiki kilikurubia kuleta ushawishi
mkubwa wa kujitenga kwa koo za Baniy Haarithah katika kabila la Khazraj na
Baniy Salamah katika kabila la Ausi. Lakini Allah akawahifadhi kwa sababu ya
imani yao, wakarudi katika safu za jamaa na wakaendelea kusonga mbele na
jeshi.
BWANA
MTUME ALIPANGA JESHI LAKE NA KUWAUSIA WATUPA MISHALE WASIONDOKE SEHEMU
WALIYOPANGIWA KWA HALI YO YOTE IWAYO.
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaendelea na safari yake Mpaka akafika
‘Uhud’. Uhud, hili ni jabali lenye vijia vingi na ambalo linakatwa kati na
mabonde kadhaa. Jabali hili linazunguka duara pana luelekea tambarare finyu
ambako ndiko makurayshi wamefanya kituo chao. Pindukopinduko za ardhi katika
kuporomoka kwake zilisababisha mianya katika ardhi iliyoshabihiana na mashimo.
Mashimo haya yalifaa kutumika kwa vita vya kujihami ambamo mtu aliweza kurusha
mishale au mawe kutokea humo na kisha kuyafanya ngao ya kumkinga dhidi ya
mashambulizi ya adui. Hii ndio sura ya Uhud; uwanja wa mapambano ulivyokuwa.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaamua kupiga kambi katika miamba
iliyokuwa upande wao. Miamba iliyo upande wa kilima kirefu kilichoitwa
‘Jabal Aynain’. Hapa ndipo Bwana Mtume kama amiri jeshi mkuu alipoanza
kuwapanga safu maswahaba wake na kuwaanda kimapambano. Akawaelekeza kulipa
migongo jabali ili liwahami na mashambulizi yanayoweza kutokea kwa nyuma yao.
Huku wakizielekezea nyuso zao upande wa Madinah kwa sura itakayowawezesha kuwa
mkabala na bonde la Uhud, wakilichomozea kwa juu yake. Akawaweka watupa
mishale khamsini juu ya jabali Aynayn na akamfanya Abdullah Ibn Jubeir kuwa
ndio kiongozi wao, atakayeongoza mashambulizi kutokea hapo juu jabalini. Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawapa watupa mishale hawa dhima na jukumu la
kuwalinda wenzao wasishambuliwe kutokea nyuma wakati vita vitakapouma.
Akawaambia wasimpe adui hata mwanya mdogo wa kuipenya ngome yao hiyo na
wasiondoke mahala hapo waislamu wakishinda au wakishindwa. Kisha akawafundisha
namna ya kuwashambulia wapanda farasi kwa mishale kila watakapojaribu
kuwakaribia kwa lengo la kuisambaratisha ngome yao. Kisha akawasisitizia na
kuwausia tena wasiiache ngome yao hiyo hata kama wataona wenzao
wakisagwasagwa. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomaliza kuzipanga
safu na kukipangia kila kikosi mahala pake. Ndipo akalikhutubia jeshi la haki,
akiwahimiza maswahaba wake kupigana kwa ajili ya Allah na akiwausia kuwa na
subira. Na akawaamuru kuwa wasianze kushambulia mpaka atakapowapa idhini ya
kufanya hivyo. Wakati Bwana mtume alipokuwa ameshughulika na kupanga safu za
jeshi lake, wakatokeza makurayshi katika tambarare iliyotandawaa chini ya
jabali lile. Hapa majeshi mawili haya yakawa ana kwa ana, waislamu wako kwa
juu na makafiri kwa chini yao. Wanawake wa kikurayshi wakaonekana baina ya
safu wakipiga dufu na kuimba nyimbo za kuwahamasisha na kuwapandisha mori wa
vita wanaume wao.
MAKURAYSHI
WAJARIBU KUWASHAWISHI WAISLAMU WAACHE KUWA PAMOJA NA BWANA MTUME.
Yalipokutana
majeshi mawili haya na kabla ya kuanza kwa mapambano, Abuu Sufyaan alianza
kuchukua mkakati wa kuwashawishi Muhajirina na Answaari kujitoa katika vita
hivi. Akatoa wito akisema: “Enyi kusanyiko la Ausi na Khazraj, tuachieni
wazi njia baina yetu na binamu zetu tupambane wenyewe kwa wenyewe, nasi
tutakuondokeeni (hatutakupigeni)”. Sauti yake hii ya wito ikasambaa angani
na kusikiwa na waislamu, ikasindikizwa na Abuu Aamir aliyekuwa mtawa.
Akajitokeza baina ya safu akiwalingania jamaa zake Ausi: “Enyi Ausi, njooni
njooni kwangu (muacheni huyo Muhammad)”. Haikuwa jawabu ya jamaa zake ila
laana, kumfukuza na kumpopoa kwa mawe mpaka akakimbia akiwa kahizika na
kufedheheka, akiwaambia washirika wake; makurayshi: “Kwa yakini shari
imeisibu kaumu yangu baada ya kuondoka kwangu”. Mkakati huu wa kuwashawishi
waislamu kumtupa mkono Mtume ukashindwa kama ulivyoruka patupu ule mkakati wa
shambulizi la ghafla la kuparaganisha. Ikawa sasa mapambano ya ana kwa ana
hayakimbiliki, ni lazima kuingia mapambanoni.
Hapa
sasa makurayshi wakajaribu kuwaweka kati waislamu na kuwakusanyikia kwa pamoja
kwa kutumia harakati/mbinu ya mzinge (msonge)
wa haraka. Ikrimah Ibn Abu Jahli akaiongozea bendera yake upande wa
kushoto kwa lengo la kuizunguka kambi ya jeshi la haki, lakini wapi hakuweza.
Khalid Ibn Al-Waleed naye akajaribu kwa upande wa kulia, watupa mishale
wakamuachia mvua ya mishale, farasi wakarudi nyuma haraka. Baada ya kushindwa
kwa zoezi hili, mushrikina hawa wakarejea sehemu zao ili kujipanga upya na
kufikiri namna ya mashambulizi itakayowaibua washindi.
|