|
Vita
vikaanza rasmi kwa ‘mubaraza’; mtu wa upande huu akipambana na yule wa
kule na waliobakia wakishuhudia. Akatoka mtu mmoja katika safu za washirikina
akitaka mtu wa kupigana nae kwa mubaraza. Swahaba Zubeir Ibn Al-awaam
akamtokea, akapambana nae na kumuua. Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-akafurahishwa na ushindi huu wa mwanzo dhidi ya adui, akapiga takbir
kuonyesha furaha yake hii. Waislamu wakaipokea takbir hii tukufu, anga
likarindima kwa takbir zao huku wakimvaa adui yao na ilhali wakipiga ukelele
wa vita: “Ua ua!” Sayyidina Aliy Ibn Abiy Twaalib-Allah amuwiye
radhi-akamshambulia mshika bendera wao; Twalhah Ibn Abiy Twalhah na kufanikiwa
kumuua. Baada ya kuuawa huyu adui wa Mungu; Twalhah bendera ya mushrikina
ikachukuliwa na kupeperushwa na nduguye; Uthmaan Ibn Abiy Twalhah. Sayyidina
Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib-Allah amuwiye radhi akamshmabulia na kumuua. Bendera
sasa ikawa inapeperushwa na ndugu yao akiitwa Abuu Said, Sayyidina Sa’ad Ibn
Abiy Waqaasw-Allah amuwiye radhi-akamlenga mshale na kumuacha akianguka maiti.
Alipouawa kafiri huyu, wakaanza kupokezana bendera watoto wanne wa Twalhah;
mshika bendera wa mwanzo, nao wote wakiuawa mmoja baada ya mwingine. Hatimaye
bendera ikaokotwa na kupeperushwa na kijana mtwana wao aliyeitwa Swuaab, nae
pia akauawa akiiacha bendera kuanguka chini bila ya kupata wa kuiokota na
kuipeperusha.
Mushrikina
wakaendeshwa puta, nguvu yao ikavunjika na safu zao zikameguka, waislamu
wakawashambulia shambulizi la kweli. Wakiwashushia dharuba za panga, chomo za
mikuki na tupo za mishale zilizowasambaratisha kabisa wasiweze kuhimili
mapigo. Wakawa hawana la kufanya ila kutimua mbio na kuwaacha wanawake wao
wakipiga mayowe ya mtu aombaye msaada wa dharura na kulia kilio cha huzuni.
Huku wakikimbizana kuepuka kuchukuliwa mateka. Waislamu nao kwa upande wao
wakawakimbiza maadui zao wakiwaua na wengine wakafanikiwa kukimbia mbali
kabisa na kambi yao. Waislamu wakaitumia fursa hii kwa kuanza kukusanya
ngawira huku wakiamini kuwa warusha mishale bado wanaendelea kuwalinda dhidi
ya shambulio lo lote kutokea nyuma.
WATUPA
MISHALE WAONDOKA MAHALA WALIKOWEKWA NA BWANA MTUME NA KUUGEUZA USHINDI KUWA
USHINDWA NA MAANGAMIVU.
Watupa
mishale waliokuwa jabalini wakadhania kwamba vita imemalizika na tayari
mushrikina wameshashindwa. Dhana hii isiyo na msingi wala mashiko,
ikawasahaulisha wasia wa Mtume na kuona kuwa hakuna sababu ya wao kuendelea
kubakia jabalini hapo. Wakachelea kupitwa na wenzao katika zoezi zima la
ukusanyaji wa ngawira, wakaambizana: “Kipi kinachotubakisha hapa na ilhali
Allah ameshamuangamiza adui kwa mikono yetu? Hao wenzenu wanachukua ngawira,
nanyi ingieni mkachukue ngawira pamoja nao”. Amiri wao; Abdullah Ibn Jubeir
alipoona uroho wa ngawira umewatambaa na kuwavaa watu aliopewa kuwaongoza.
Akaanza kuwakumbusha wasia waliopewa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.
Akawatahadharisha na matokeo mabaya ya kukhalifu amri ya Mtume wa Allah na
kumuasi. Lakini wapi sikio la kufa halisikii dawa, tahadhari na makumbusho
yote hayo ikawa ni mithili ya kumpigia mbuzi gitaa. Hao nao wakajitoma katika
kambi ya mahasimu wao wakikusanya ngawira, huku wakimuacha amiri wao jabalini
pale na watu wasiozidi kumi. Kuondoka kwao kukaifanya ngome iliyokuwa
ikiwalinda kwa nyuma waislamu kuwa wazi, inayoweza kupenywa na adui kirahisi
kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Kamanda
shupavu wa mushrikina Khaalid Ibn Al-Waleed alikuwa akikimbia kisengerenyuma
(kinyumenyume) huku akiyakazia macho yake jabalini. Alipoona watupa mishale
wakiziacha sehemu zao, akaamua kuitumia vema fursa hii ya kosa baya
lililofanywa na waislamu. Akapanua wigo wa vita akarejea kwa nyuma akiwaongoza
wapiganaji wake, akizitumia ardhi za uficho kama njia na chochoro zake.
Akaenda akifuatiwa nyuma na Ikrimah Ibn Abiy Jahli akiipeperusha bendera ya
batili dhidi ya haki. Wakafanikiwa kupenya na kufika jabalini penye ngome ya
waislamu inayowalinda kwa nyuma yao. Wakawafagia na kuwaondosha kirahisi mno
watupa mishale wachache waliokuwa wamethibiti katika lindo lao baada ya wenzao
wengi kuondoka kwenda kukusanya ngawira. Fagiafagia hii ikawawezesha kuzivaa
safu za waislamu kwa kutokea nyuma kwa ghafla isiyotazamiwa wala kutegemewa.
Mushrikina wakasonga mbele kwa kasi ya nguvu baada ya mkimbizano wa nguvu,
wakiwashambulia waislamu kwa mori mkuu. Amrah Bint Alqamah akaitwaa bendera
iliyokuwa imetupwa chini na kuinyanyua juu kuwaita wote waliokuwa wamekimbia
baada ya kipigo cha awali. Waislamu wakajikuta wamezingirwa na adui yao kiasi
cha kushindwa kutoa upinzani utakaomrejesha adui nyuma. Wakauliwa waislamu
wengi takriban sabini na kuwaacha wengi wakiwa wameumizwa vibaya sana. Safu za
waislamu zikachangukana, wakagongana na kupelekea kushambulia bila ya mpango
maalumu kiasi cha kuuana wenyewe kwa wenyewe bila ya kujua.
KIYOWE
CHENYE MVUTO CHAWADHOOFISHA WAISLAMU MARA DUFU.
Katikati
ya kizaizai na kitatange hiki kikuu ukasikika uyowe uliosikiwa barabara na
watu ukisema: “Muhammad tayari amekwishauawa”. Waislamu wakachanganyikiwa
na uyowe huu na kutikiswa nao sana na kuwaacha wakitambaliwa na hisia za woga
mkubwa. Nafsi zao zikaingiwa na fikra ya kujitoa na kuona kuwa hakuna sababu
ya kuendelea na vita. Hisia za woga na fikra za kujitoa ikawa ni sababu ya
kugawika waislamu makundi mengi. Wako miongoni mwao walioona kwamba kukimbia
ndio suluhisho pekee na wako walioamua kuthibiti na hima yao yote ikiwa ni
kuzilinda nafsi zao au kupigana mpaka wauawe. Kadhalika lilikuwepo kundi
ambalo mashambulizi yale ya ghafla na ya nguvu yaliwaondoshea kabisa matumaini
ya kunusurika, wakaamua kusalimu amri. Pia wako waliohemewa wasijue cha
kufanya.
Wakati
yote haya yakijiri, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa nyuma ya
maswahaba wake akiwaita: “Njooni kwangu enyi waja wa Allah! Njooni kwangu
enyi waja wa Allah! Njoo kwangu ewe fulani! Njoo kwangu ewe fulani! Mimi ndiye
Mtume wa Allah!”. Lakini wapi watu wamehamanika na kivangaito kilichowapata
bila ya kutazamia, litapatikana wapi katika hali hiyo sikio la usikivu? Tim
haooo watu wanatimka mbio, hawausikii wito wa Mtume wa Allah ila sauti na
kelele tu. Hivi ndivyo Qur-ani Tukufu inavyoeleza hali ilivyokuwa:
“(Kumbukeni) MLIPOKUWA MKIKIMBIA MBIO, WALA NYINYI HAMUMSIKILIZI YO YOTE,
HALI MTUME ALIKUWA ANAKUITENI, YUKO NYUMA YENU. AKAKUPENI (Allah) HUZUNI JUU
YA HUZUNI. (Amekusameheni hivyo) ILI MSISIKITIKE (sana) KWA YALE
YALIYOKUPOTEENI WALA KWA (misiba) ILIYOKUSIBUNI...” [3:153] Shetani mlaaniwa
akaitumia vema fursa hii ya kupapatika na kuhemewa kwa waislamu, akaanza
kuzitia maradhi ya wasiwasi nyoyo nyonge na kuzitelezesha nafsi dhaifu. Naam,
maradhi haya mabaya yakawasibu waislamu kama alivyolenga shetani, baadhi ya
waislamu wakafikia kusema: “Kwa nini tuendelee kupigana ikiwa Muhammad
amekwisha uawa? Rejeeni kwa jamaa zenu nao watakupeni amani”. Kuhusina na
hali hii tunasoma: “WALE WALIORUDI NYUMA (waliokimbia) MIONGONI MWENU SIKU
AMBAYO MAJESHI MAWILI YALIPOKUTANA (katika vita vya Uhud-jeshi la makafiri na
la waislamu),SHETANI NDIYE ALIYEWATELEZESHA KWA (sababu ya) BAADHI YA (makosa)
WALIYOYAFANYA. NA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MPOLE SANA”. [3:155]
Maswahaba
wengine walidhania kwamba huo ndio mwisho wao na ndio mwisho wa Uislamu kwani
hakuna atakayesalimika kutokana na nguvu ya makafiri. Hivi ndivyo walivyosema
kama walivyonukuliwa na Qur-ani Tukufu: “...TUNGEKUWA NA CHO CHOTE KATIKA
JAMBO HILI TUSINGEUAWA HAPA...” [3:154]
|