|
Ama Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisimama imara mbele ya adui akipambana
nae mpambano wa kufa na kupona. Akamnyeshea adui mvua ya mishale mpaka
ikamuishia na upinde wake ukakatika kutokana na wingi wa kutumiwa. Alipoishiwa
mishale akaanza kuvurumisha mvua ya mawe mpaka akaanguka chini. Katika
kizaizai hiki na katikati ya kundi la maadui, Bwana Mtume alikuwa pamoja na
maswahaba wake wachache. Inaaminiwa kwamba mswahaba waliothibiti pamoja na
Mtume wa Allah mbele ya adui hawakuzidi kumi. Baada ya wengi wao kusambaratika
huko na huko kutokana na shambulizi kali, kubwa, la nguvu na la kushtukiza
likitokea kusikotazamiwa. Hawa walikula kiapo cha utii kwa Mtume kwamba
watakuwa pamoja nae mpaka kufa au ipatikane nusura ya Allah. Baada ya Mtume wa
Allah kuanguka chini, wakamzunguka na kuwa mithili ya ngome imara inayomuhami
dhidi ya hujuma za adui mwenye uchu na roho yake. Wakweli hawa waliyatoa
maisha yao hidaya njema katika kumlinda Mtume wa Allah. Huyu hapa Sayyidina
Twalhah Ibn Ubeidillah-Allah amuwiye radhi-anampigania Mtume wake kwa kuyatoa
muhanga maisha yake asalimike Mtume wa Allah. Akawa anamlinda mbele yake,
nyuma, kuliani na kushotoni kwake kwa upanga wake uliokuwa ukizivuna shingo za
maadui. Kwa kuwa hivi ni vita, unapiga na kupigwa, Twalhah nae alifunikwa na
wingu la panga za maadui huku mvua ya mishale ikimjia kutokea kila upande.
Pamoja na hali hii ngumu ya hatari, Twalhah aliendelea kuwa ni ngome imara ya
Mtume wa Allah mpaka kikamuondokea kiwingu cha mushrikina hawa. Siku hii
Twalhah ndiye aliyekuwa nyota katika kumuhami Mtume wa Allah, mpaka Bwana
Mtume akawa anasema: “Kwa yakini amejiwajibishia Twalhah!” Yaani
ameiwajibishia nafsi yake kuingia peponi kwa sababu ya kumlinda kwa dhati
Bwana Mtume.
Huyu
hapa Sayyidina Shamaas Ibn Uthman-Allah amuwiye radhi-hakuwa nyuma katika
kumuhami Mtume wa Allah. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa hatupi
jicho lake kuliani wala kushotoni ila alimuona bwana huyu upande huo akimlinda
kwa upanga wake. Pale Mtume alipozungukwa na kutiwa kati na adui, Shamaas
akageuka ngao madhubuti iyazuiliayo mashambulizi makali ya adui
yaliyoelekezwa kwa Mtume wa Allah kwa lengo la kumtokomezelea mbali.
Mashambulizi yakamlemea na kumuacha chini maiti hali ya kuwa shahidi-Allah
amrehemu yeye na maswahaba wote wa Mtume wa Allah. Akasindikizwa Shamaas na
kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Simpatii Shamaas badali
ila pepo”. Abuu Twalhah-Allah amuwiye radhi-alikuwa mlenga shabaha
hodari sana, akaumwaga mfuko wa mishale yake mbele ya Bwana Mtume. Akaanza
kutupa mishale kumlinda Mtume wa Allah, nae Bwana Mtume akawa anamwambia
ye yote anayepita miongoni mwa maswahaba wake: “Mmwagie mishale yako
Abuu Twalhah”. Kauli hii ya Bwana Mtume ilitokana na umahiri mkubwa
aliouonyesha Sayyidina Abuu Twalhah katika kurusha mishale iliyowarudisha
nyuma maadui. Kila Abuu Twalhah alipokuwa akirusha mishale, Bwana Mtume
alikuwa akiangalia kwa nyuma yake ili apate kuona matuko (mahala ulipoangukia)
ya mshale. Abuu Twalhah akawa anamwambia: “Ewe Mtume wa Allah, nakufidia
mama na baba yangu! Usiangalie, usije kupatwa na mishale ya watu hawa. Niuawe
mimi kabla yako na uso wangu uwe ni fidia ya uso wako”.
Ngao
nyingine ya Mtume wa Allah katika wakati huu mgumu, ilikuwa ni Sayyidina Abuu
Dujaanah-Allah amuwiye radhi. Huyu aliipa mgongo wake mishale ya adui itue juu
yake isimpate kipenzi chake; Mtume wa Allah. Aliinamia mpaka akashindwa
kuhimili uzito wa mashambulizi huku mgongo wake ukiwa hauna mahala
pasipochomwa na mshale-Allah amuwiye radhi. Sayyidina Sa’ad Ibn Abiy
Waqaasw-Allah amuwiye radhi-nae hakuwa nyuma katika kuonyesha ushujaa wake
katika kumlinda Bwana Mtume. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawa
anamsaidia kwa kumpa mishale huku akimwambia: “Tupa nakufidia baba na mama
yangu”. Historia itakuwa haikutenda haki kama haitamtaja mwanamke
aliyesimama kidete katika kumuhami Mtume wake. Huyu si mwingine bali ni Ummu
Umaarah; Nasiybah Bint Ka’ab-Allah amuwiye radhi. Mchango wake ulikuwa ni
kuhakikisha kuwa jeshi la haki linapata maji ya kutosha ya kunywa katika
kipindi chote cha vita hivi. Mama huyu alipoona Bwana Mtume amezingirwa na
maswahaba wanakimbizana hovyo wakimuacha mtume wao katikati ya kundi la
maadui. Chini akaitupa ndoo yake ya kuchotea maji, akautwaa upanga na kuingia
mapambanoni akiwa amejifunga kibwebwe. Akapambana katikati ya kundi la maadui
wanamume kwa ajili tu ya kumuhami na kumnusuru Mtume wa Allah. Akapigana mpaka
akapatwa na majeraha yasiyopungua kumi na tatu, moja likiwa ni jeraha kubwa
lililoacha shimo kubwa begani kwake. Hapo ndipo mahala alipopigwa na Ibn
Qamiah. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alisikika siku hiyo akisema:
“Sikupata kugeuka kuliani wala kushotoni ila nilimuona akinilinda”.
Sayyidina
Hubaab Ibn Mundhir-Allah amuwiye radhi-yeye alikuwa akiwakusanya mushrikina
hawa kama mchungaji anavyowakusanya kondoo au mbuzi wake. Wakamkusanyikia kwa
wingi mpaka pakavumishwa kuwa kauawa, walipomtawanyikia hapo ndipo
alipowainukia na upanga wake mkononi. Akaanza kuliendesha mbio mojawapo la
makundi yao, huku wengine wakitimua mbio. Haya huyu hapa Ziyaad Ibn Sakan na
kundi la maanswari-Allah awawiye radhi-walipigana kumuhami Mtume wa Allah.
Wakiua na kuuawa mmoja baada ya mwingine kwa ajili ya kumnusuru Bwana Mtume.
Wa mwisho kuuawa katika kundi hili alikuwa ni Sayyidina Ziyaad, alipigana
mpaka majeraha yakamuhemeza. Mtume wa Allah akamtandikia miguu yake
mitukufu iwe ni mto wake wa kupumzikia kutokana na kazi nzito aliyoifanya.
Mauti yakamjia-Allah amuwiye radhi na wote swahaba wa Mtume-akiwa miguuni mwa
Bwana Mtume, eeh bakhti iliyoje! Musw’ab Ibn Umeir-Allah amuwiye
radhi-anakufa katika kumnusuru Mtume wa Allah. Huyu alikuwa akiyazuia kwa
mwili wake mapigo ya panga za mushrikina yaliyoelekezwa kummaliza Bwana Mtume.
Aliuawa na Ibn Qamiah kwa kumdhania kuwa ni Bwana Mtume, kisha akakimbia
akitangaza baina ya mushrikina wenzake kuwa amemuua Mtume wa Allah.
Siku
hii ndugu muislamu waliuawa maswahaba wengi katika kumnusuru Mtume wa Allah,
kila mmoja akiitoa nafsi yake fidia kwa Bwana Mtume. Akiwa ni ngome na ngao
baina ya Mtume na adui aliye mithili ya mbwa mwitu katika kundi la wanakondoo.
|