|
I/.
HIMA YA MAKURAYSHI KATIKA VITA HIVI ILIKUWA NI KUMUUA
BWANA MTUME.
Makurayshi
wanne walifunga ahadi ya kumuua Mtume wa Allah katika vita hivi na mushrikina
wenzao walilitambua hilo. Hawa walikuwa ni Abdullah Ibn Shihaab, Utbah Ibn
Abuu Waqaasw, Amrou Ibn Qamiah na Ubayyi Ibn Khalaf. Huyu Abdullah Ibn Shihaab
alimpasua Bwana Mtume katika paji lake la uso, damu zikamchuruzika kiasi cha
kuzilovya ndevu zake. Utbah Ibn Abuu Waqaasw katika harakati zake za
kutekeleza ahadi aliyofunga na wenzake, yeye alimpiga Mtume wa Allah katika
mdomo wake wa chini. Pigo la shetani huyu lilivunja jino la mbele la upande wa
kulia la Mtukufu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Amrou Ibn Qamiah, yeye
alijaribu kuifungua ahadi aliyoifunga na wenzake kwa kumpiga tayani Mtume wa
Allah. Pigo hili lilimsababishia Bwana Mtume kuchomwa na vijimsumari viwili
vilivyokuwa vimeshikilia kifuniko cha chuma alichokuwa amekivaa usoni. Muovu
huyu hakukomea hapo, bali alimpiga Bwana Mtume upanga wa bega, pigo
lililomuacha akiangukia shimoni na kuchubuka magoti yake na uvumi kuenea kuwa
Mtume kauawa. Sayyidina Aliy Ibn Abuu Twaalib akamshika mkono na Sayyidina
Twalhah Ibn Ubeidillah akamuinua mpaka akasimama na kulingana sawa. Maumivu ya
pigo la shetani huyu begani kwa Mtume yalimchukua mwezi mzima. Ubayyi Ibn
Khalaf, yeye alimsukumiza Mtume wa Allah huku akimwambia: “Ewe muongo
utakimbilia wapi?” Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akajihami dhidi ya
shetani huyu kwa kumchoma mkuki wa shingo. Akayumbayumba juu ya farasi wake
akitoa mlio mithili ya ule wa ng’ombe dume, akafia njiani wakati makafiri
walipokuwa wakirejea Makah.
Uvumi
wa kuuawa kwa Mtume wa Allah ukamalizika baada ya waislamu kuyakinisha kuwa
yungali hai. Hapo ndipo waislamu wakamzunguka na kumuondoshea kiwingu cha
maadui waliojizatiti kumuua. Mtu wa mwanzo kumtambua Bwana Mtume alikuwa ni
Ka’ab Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-kama anavyosimulia mwenyewe:
“Niliyatambua macho yake yaliyokuwa yaking’ara nyuma ya kifuniko cha chuma
alichovaa usoni. Nikaita kwa sauti ya juu: Enyi kusanyiko la waislamu!
Furahini, Mtume wa Allah huyu hapa. Mtume wa Allah akaniashiria kunyamaza”.
Kundi la waislamu likamkusanyikia Bwana Mtume, wakamchukua na kumpeleka katika
uchochoro ulio baina ya miamba ya jabali Uhud. Bwana Mtume akajificha hapo na
baadhi ya maswahaba waliojeruhiwa vibaya. Akiwa hapo alijaribu kupanda juu ya
mwamba kushuhudia mapambano yanavyoendelea, lakini hakuweza kutokana na
kuishiwa nguvu kutokana na kutokwa na damu nyingi. Twalhah Ibn
Ubeidillah-Allah amuwiye radhi-akambeba na kumpandisha mwambani hapo.
WANAWAKE
WA KIKURAYSHI WAZIKATAKATA MAITI ZA WAISLAMU.
Kwa
kipigo hiki kilichowashukia waislamu katika vita hivi vya Uhud, mushrikina
waliona kuwa wamejilipia kisasi kutokana na kipigo kilichowapata katika vita
vya Badri. Wakaviponya vidonda vya nafsi zao kwa kuuawa Mtume wa Allah kama
walivyodhania na hili likawaridhi kuwa ni ngawira tosha. Vita vikaanza kupoa
makali yake na kuzimika harara lake. Hao mushrikina wakaanza kuondoka katika
uwanja wa mapambano kurejea kambini kwao na kuanza kujishughulisha na mazishi
ya watu wao waliouliwa vitani. Wakati wanarejea kambini ndipo wanawake wao
wakaitumbua nyongo ya chuki iliyomo vifuani mwao kwa kuzikatakata maiti za
mashahidi. Wakazikata pua na masikio ya mashahidi hawa-Allah awawiye radhi.
Hind Bint Utbah ndiye aliyefanya unyama mkubwa kuliko wanawake wale wote. Yeye
hakuridhika na kukata pua na masikio ya
Ami yake Mtume; Sayyidina Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib-Allah amuwiye radhi. Huyu
alijasiri kulitumbua tumbo la Sayyidina Hamzah, akalitoa ini lake na kuanza
kulitafuna kwa meno yake, huku akionekana kufura kwa hasira na chuki. Abuu
Sufyaan; mumewe Hind akapita baina ya mashahidi akijaribu kuwatambua.
Alipomkuta Sayyidina Hamzah amelala chini akiwa ni miongoni mwa mashahidi,
akampigapiga mfupa wa taya lake kwa kitako cha mkuki wake huku akimsimanga kwa
kusema: “Onja jazaa ya kuwakata pande jamaa zako (kuwatupa mkono)”.
Al-Hulaysi; kiongozi wa Wahabeshi alimuona akifanya kitendo hiki, akamkemea
asifanye kitendo hicho cha kinyama kwa mwana wa ami yake akiwa maiti. Abuu
Sufyaan akaona amefedheheka kutokana na kitendo chake hicho cha aibu. Akamsihi
Al-Hulaysi amsitiri asiitangaze khabari hiyo mbaya inayoweza kushusha
hadhi yake mbele ya watu.
ABUU
SUFYAAN AMTAFUTA BWANA MTUME.
Hima
ya Abuu Sufyaan ilikuwa ni kumkuta Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akiwa ni miongoni mwa waislamu waliouliwa. Alipomkosa akaanza
kuingiwa na shaka ni kweli wamefanikiwa kumuua kama ilivyotangaa masikioni mwa
wengi wao kama si wote. Akaelekea upande alikojificha Bwana Mtume na baadhi ya
maswahaba wake na akaanza kupaaza sauti: “Je, Muhammad yuko kwenu? Je, Ibn
Abiy Quhaafah (Abuu Bakri) yuko huko? Je, mnaye Ibn Al-Khatwaab?”
Bwana Mtume akawakataza maswahaba wake wasimjibu, alipokosa jawabu akawaendea
mushrikina wenzake na kuwaambia: “Ama watu hawa kwa yakini mmetoshewa”.
Sayyidina Umar-Allah amuwiye radhi-kusikia kauli hiyo akashindwa kujizuia na
kuamua kumjibu, akamwabia: “Wallah umeongopa, ewe adui wa Allah! Kwa yakini
Allah amekubakishia likuudhilo (likukeralo)”. Abuu Sufyaan akiwa kama mtu
anayetaka kuomba radhi kutokana na kitendo kichafu kilichofanywa na wanawake
wao, akasema: “Mtawakuta watu wenu waliouliwa wamekatwakatwa viungo, mimi
sikuliamuru hilo lakini pia silioni kuwa ni baya”. Kisha akajikosoa mwenyewe
kutokana na kauli yake hii ambayo aliiona kama ni kuwanyenyekea mahasimu wake,
kwa kusema: “Ee kitendo kizuri kilioje! Hakika vita ni mghalaba (ushindani),
mtukuzeni hubal{1}”.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema kuwaambia maswahaba wake:
“Mwambieni Allah ndiye aliye Mtukufu kuliko vyote”. Abuu Sufyaan
akaendelea kutamba: “Utukufu ni wetu, nyie hamna utukufu”. Bwana Mtume
akasema: “Mwambieni Allah ndiye Mola na Mlinzi wetu, nanyi hamna Mola wala
Mlinzi”. Abuu Sufyaan akaendelea kusema: “Siku ya leo ni fidia ya siku ya
Badri”. Mtume wa Allah akasema: “Mwambieni hazilingani (siku mbili hizo),
wauliwa wetu wako peponi na wauliwa wenu wako motoni”. Abuu Sufyaan akapiga
mayowe: “Bila shaka miadi yenu ni Badri mwaka ujao (tukutane hapo muone kazi
yetu)”. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Mwambieni, hiyo ni
miadi baina yetu nasi (haina shaka)”.
________________________________________________________
{1}
Huyu ni mungu-sanamu aliyekuwa ndani ya Al-Ka’aba wakimuabudu.
|