|
Baada
ya kurushiana maneno na waislamu, Abuu Sufyaan akageuza hatamu za farasi wake
na huyoo akashika njia kurejea kwa watu wake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akapendelea kujua Makurayshi wanaelekea wapi. Akamtuma Sayyidina
Aliy, akamwambia: “Wafuatilie watu hawa, chunguza wanafanya nini na
wanaelekea wapi. Angalia wakiwaweka kando farasi na kupanda ngamia, basi bila
ya shaka watakuwa wanaelekea Makah. Na iwapo watapanda farasi na kuwaswaga
ngamia, basi bila ya shaka watakuwa wanaelekea Madinah”. Sayyidina
Aliy-Allah amuwiye radhi-akaipokea amri hii ya Bwana Mtume kwa utii mkubwa,
huyoo akatoka na kuanza kuwafuatilia. Katika fuatilia yake hiyo, akawaona
Makurayshi wamewaweka kando farasi na kupanda ngamia wakielekea upande wa
Makah. Akarudi kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na kumpasha khabari,
Mtume akasema: “Namuapia yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, ikiwa
watakwenda Madinah, nitawaendea tu huko kisha nitapambana nao”.
Makurayshi
walipoondoka zao, maswahaba wa Mtume wa Allah-Allah awawiye radhi-wakamzunguka
Bwana Mtume na kuanza kumtibu majeraha yake. Abuu Ubeidah akainuka na
kuving’oa vile vijimsumari viwili vilivyokuwa vimekita usoni kwa Bwana Mtume
kwa kutumia meno yake. Kijimsumari cha kwanza kikang’oka na jino moja la
pembeni la Abuu Ubeidah, wakati kile cha pili nacho kikiondoka pamoja na jino
jingine. Ikawa Bwana Mtume kang’olewa vijimsumari viwili
na kubakia na majeraha ya kuuguza, huku Abuu Ubeidah akipoteza meno
yake mawili na kuwa mapengo kwa ajili ya Mtume wa Allah. Sayyidat Faatimah
Bint ya Mtume wa Allah akaja na kundi la wanawake kutoka Madinah, alipomuona
Mtume wa Allah (baba yake) akitokwa na damu usoni akambusu na kuangusha kilio.
Akamkosha damu na kuipangusa lakini haikukoma kutoka, akatwaa kipande cha
jamvi/mkeka akakiunguza moto mpaka kikawa majivu. Akayachukua majivu yale na
kumbandika nayo Bwana Mtume majerahani mwake, hapo ndipo damu ikakatika.
BWANA
MTUME APATWA NA SIMANZI (HUZUNI) KUU JUU YA MASHAHIDI.
Kisha
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akashuka kwenye medani ya vita
kuangalia waliouliwa miongoni mwa maswahaba wake. Alipomuona ami yake;
Hamzah-Allah amuwiye radhi-akiwa amepigwa
mueleka na mauti na kufanyiwa unyama aliofanyiwa wa kukatwakatwa na kupasuliwa
tumbo. Alishikwa na huzuni kuu juu yake na akapandwa na chuki na hasira kuu
kwa wale waliomfanyia ami yake unyama huo. Bwana Mtume akafikia kusema:
“Sijapatapo kushuhudia tukio litialo uchungu na simanzi kuliko tukio
hili”. Kisha akamtazama swahaba wake; Musw-ab Ibn Umeir-Allah amuwiye
radhi-amelala chini akiwa amevaa guo lake, akasema kwa huzuni: “Mtu
niliyekuona Makah na ilhali kukiwa hakuna mwenye kuvaa nguo nzuri kukushinda,
mwenye mkusanyiko mzuri wa nywele. Leo umelala chini na guo hili tena tim tim
wa nywele!”. Kisha akawaangalia mashahidi wengine wote na kusema: “Mimi
ni shahidi juu ya hawa, hakika ya hali ilivyo hapana majeruhi yo yote
aliyejeruhiwa kwa ajili ya Allah ila Allah atamfufua siku ya kiyama na ilhali
jeraha lake hilo likitoka damu. Rangi yake rangi ya damu na harufu yake ni
harufu ya miski”.
Handhwalah
Ibn Abiy Aamir-Allah amuwiye radhi alikuwa ndio kwanza katoka kufunga ndoa na
kuingia ndani. Aliposikia la mgambo la vita likilia, akatoka haraka kuelekea vitani
kabla hata ya kukoga janaba. Huyu hakurudi tena kwa Bi. harusi, akawa ni
miongoni mwa mashahidi-Allah awawiye radhi. Bwana Mtume alipomuona, akasema:
“Hakika mwenzenu huyu anakoshwa na malaika”. Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akaamrisha mashahidi wazikwe pale pale walipofia, akaagiza:
“Wazingirishieni pamoja na damu na majeraha yao, kisha muangalieni
aliyekusanya (aliyehifadhi) Qur-ani zaidi kuliko wenzake na mumuweke mbele ya
wenzake kaburini”. Wakawa wanazikwa na nguo zao zilizolowa damu bila ya
kukoshwa. Na walikuwa wakizikwa wawili wawili au watatu watatu katika kaburi
moja. Hili lilitokana na udhaifu na uchovu mkubwa waliokuwa nao maswahaba na
hivyo kushindwa kumchimbia kila shahidi kaburi la peke yake. Idadi ya
mashahidi haikupungua sabini, mashahidi wanne wakitoka kwa Muhajirina na
waliosalia walikuwa ni katika Maanswari. Kwa upande wa mushrikina waliuliwa
watu ishirini na nne.
MTUME
WA ALLAH AWAFARIJI JAMAA ZA MASHAHIDI.
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomaliza shughuli nzima ya mazishi ya
maswahaba wake. Akapanda farasi wake na kuanza safari ya kurudi Madinah akiwa
kazungukwa na maswahaba wake, wengi wao wakiwa ni majeruhi. Maswahaba wanarudi
Madinah huku kila alama ya machovu ikidhihiri kutokana na kuendeshwa mbio na
makafiri kulikowapata. Wakenda njiani wakitupiana lawama kutokana na
kuikhalifu kwao amri ya Bwana Mtume. Wakawa hawana la kufanya kwa yote
yaliyotokea ila kutaraji maghfira ya Allah na awasamehe kuteleza kwao huku.
Bwana Mtume alipowasili Madinah aliwakuta wanawake mlangoni kwake wakiwalilia
jamaa, waume na ndugu zao waliokufa mashahidi. Wanawake hawa walipomuona Mtume
wa Allah akija wakasahau huzuni ya ndugu zao, wakaharakia kutaka kujua kama
Mtume hakufikwa na dhara. Walipomuona yu salama, msiba wao ukawepesika na Ummu
Aamir Al-Ash-haliyah-Allah amuwiye radhi-akamwambia Mtume: “Kila msiba baada
yako ni mwepesi”. Ummu Sa’ad Ibn Muaadh-Allah amuwiye radhi-akaja mbio
kuelekea aliko Mtume kukagua hali yake. Hata aliposhusha pumzi baada ya
kumuona amesalimika, akasema: “Ama nilipokuona umesalimika, bila ya shaka
kila msiba ni mwepesi”. Bwana Mtume akayapokea maneno haya yaliyobeba imani
ya kweli ya mama huyu kwa kumfariji kutokana na kufiliwa na mwanawe; Amrou Ibn
Muaadh-Allah amuwiye radhi-katika vita hivi. Kisha akamwambia: “Ewe Ummu
Sa’ad, furahi! Na wape bishara njema jamaa zao (mashahidi) kwamba wauliwa
wao wanafuatana peponi”. Ummu Sa’ad akasema: “Tumemridhia Mtume wa Allah
na ni nani atakayewalilia baada ya bishara hii?” Kisha akamwambia Mtume:
“Ewe Mtume wa Allah! Waombee Mungu waliowaacha (wafiwa)”. Bwana Mtume
akalipokea ombi lake hili kwa mikono miwili na akawaombea dua kwa kusema:
“Ewe Mola wa Haki wee! Ninakuomba uondoshe huzuni ya nyoyo zao, uunge msiba
wao na uwape badali njema”.
Kisha
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akapitisha azimio kwamba maswahaba
wake wote waliojeruhiwa wabakie majumbani mwao kwa siku kadhaa ili kuganga
majeraha waliyoyapata. Majeruhi wote wakalipokea azimio hili la Bwana Mtume,
wakakesha kwenye mioto wakiyabandika dawa majeraha yao. Bwana Mtume nae
akashika njia kuelekea nyumbani kwake, alipofika hakuweza kushuka kutoka
kwenye farasi wake mpaka aliposaidiwa. Alisaidiwa kushuka na kuingia ndani na
maswahaba wake wawili; Sa’ad Ibn Ubaadah na Sa’ad Ibn Muaadh-Allah awawiye
radhi. Sayyidina Bilali-Allah amuwiye radhi-alipotoa adhana ya Maghribi, Bwana
Mtume alitoka kwenda kuswalisha kwa msaada wa watu wawili waliomshika upande
huu na huu. Baada ya swala kumalizika akarudi nyumbani mwake. Viongozi wa
makabila ya Ausi na Khazraj wakakesha mlangoni kwa Mtume wakimlinda kwa
kuchelea asije kushambuliwa ghafla na Makurayshi. Bwana Mtume alitoa idhini ya
kuwalilia mashahidi kwa sababu ya falsafa ya machozi. Bwana Mtume alitambua
kuwa mbubujiko wa machozi huiosha huzuni iliyomo moyoni na kuondosha machungu
ya huzuni ya kuondokewa na kipenzi chake mtu. Pamoja na rukhsa hii ya kulia
aliyoitoa, Bwana Mtume alikataza kulia kwa kunyoa nywele, kupara nyuso
makucha, kuchana nguo na kuomboleza.
|