Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA TANO

 

i) MALEZI YA MTUME NA KIFO CHA MAMA YAKE :

Mtume alifiwa na baba yake kabla hajazaliwa na hakumuachia mali ya kutosha. Mtume alipofikia umri wa miaka minne, mlezi wake na mnyonyeshaji wake Bi Haliymah alimrejesha kwa mama yake Bi Aaminah akamlea mwanawe mpaka alipofikia umri wa miaka sita akampeleka kuwazuru wajomba zake Madinah. Bi Aminah alifia njiani wakati akirejea Makkah wakati akirejea na mwanawe baada ya ziara yake ya Madinah na akazikwa ABUWAI, kitongoji kilichoko baina ya Makkah na Madinah. Baada ya maziko ya mama yake Mtume, Mtume alichukuliwa na kupelekwa Makkah UMMU AYMANA muhabeshi. Huyu alikuwa ni mtumishi aliyeachwa na baba yake na ndiye aliyefuatana na mama yake Mtume safarini.

Baada ya kufiwa na mama yake, Mtume alilelewa na babu yake mzaa baba Mzee Abdul Mutwalib kwa kipindi kisichopungua miaka miwili. Babu yake alimpenda sana mjukuu wake huyu kiasi cha kumtanguliza kuliko wanawe (ami zake Mtume) na alikuwa akimketisha mahala anapokaa yeye kwa kumtukuza. Mtume alipofikisha umri wa miaka minane, babu yake alifariki dunia. Kabla hajafariki, alimuusia mwanawe Abuu Twalib kumlea mjukuu wake, hivyo Mtume akawa chini ya uangalizi na ulezi wa Ammi yake Bwana Abuu Twalib. Abuu Twalib alikuwa na mzigo wa familia kubwa na alikuwa na mali kidogo tu ambayo haikumtosha kuihudumia familia, lakini MwenyeziMungu akamkunjulia riziki yake kutokana na kumlea mtoto huyu yatima. Mtume aliishi nyumbani kwa ammi yake kama mmoja wa watoto wa familia ile na alikuwa akitosheka na alichopewa; hakuwa akililia na kupupia kila alichokiona kama ilivyo tabia na ada ya watoto.

ii) SAFARI YA MTUME NA AMMI YAKE KUELEKEA SHAMU

Bwana Mtume –Allah amshushie rehema na amani- alipofikia umri wa miaka kumi na nane alisafiri pamoja na ammi yake Abu Twalib kuelekea Shamu. Hii ilikuwa ni safari ya kibiashara. Walipofika katika HUURAANA wakiwa njiani kuelekea BASRAH nchini Shamu, hapo padri wa kiyahudi jina lake Bahiyrah alimuona Mtume akifunikwa na kiwingu kutokana na jua kali la jangwani wakati msafara wao ulipokuwa unakaribia hapo. Msafara ukaja ukapumzika chini ya mti uliokuwa jirani na kibanda cha padri yule, padri akakiona kiwingu kimefunika mti ule waliopumzika chini yake Mtume na watu wengine waliokuwemo katika msafara ule wa kibiashara, akayaona matawi ya mti ule yamemuinamia kijana mmoja aliyekuwemo katika msafara ule. Bahiyrah alikuwa mwanachuoni wa kiyahudi na alikuwa amesoma katika TAURATI na INJILI juu ya Mtume atakayetokea Bara Arabu. Bahiyrah akaandaa chakula na kuualika msafara mzima katika karamu nyumbani kwake kinyume na ada yake, kwani hakuwa na tabia ya kuwaalika chakula watu nyumbani kwake. Msafara ulipohudhuria karamu, Bahiyrah akawa anamkazia sana macho Bwana Mtume na akiziangalia alama alizokuwa nazo Mtume mwilini mpaka akafanikiwa kuuona muhuri wa utume ulokuwa baina ya mabega yake. Hapo ndipo padri Bahiyrah akamuuliza Bwana Mtume juu ya hali na mambo yanayomtokea akiwa yu macho au usingizini. Bwana Mtume akamueleza yote yanayomtokea bila ya kuficha hata jambo moja, Bahiyrah akaona aliyoelezwa na Mtume ndio sifa za Mtume aliyebashiriwa katika kitabu alichonacho yeye yaani Taurati. Bahiyrah akatambua kijana huyu ndiye Mtume angojewaye, ndipo akauliza wageni wake waalikwa khabari za kijana yule na amefuatana na nani katika msafara ule. Wakamuelekeza kwa ammi yake Bwana Abuu Twalib akamwambia : "Mrejeshe mwanao huyu Makkah usiende naye Shamu kwani mayahudi watakapomuona na kumtambua ndiye Mtume angojewaye watamuua kutokana na chuki ya kuhama utume kwao na kwenda kwa waarabu." Abuu Twalib akazisikiliza nasaha za Bahiyrah na akarudi naye haraka Makkah

 



Forum | Guestbook | Tuandikie |