|
- KUSHINDWA
KATIKA VITA VYA UHUD KULIKUWA NI DARASA (FUNDISHO/SOMO) MUHIMU KWA
WAISLAMU WOTE KWA UJUMLA WAO.
Mtu
atakayetafakari kwa kina hali ya mambo ilivyokuwa katika vita vya Uhud, na
akayachunguza kwa makini matukio na picha za mambo zilivyokuwa. Bila ya shaka
ataamini kwamba vita hivi na matokeo yake vilikuwa ni jambo ambalo hapana budi
kutokea kwake. Isitoshe vita hivi vilikuwa ni somo/fundisho ambalo ni lazima
waislamu walipate katika kipindi hiki cha uchanga wa Uislamu kwa ajili ya
ustawi wake katika siku za usoni. Kushindwa katika vita vya Uhud ndio lilikuwa
pigo zito la kwanza lililowapata waislamu wengi ambao Allah aliwanusuru katika
vita vya Badri na ilhali walikuwa ni wachache ukiwalinganisha na hasimu wao.
Baada ya nusra hii ya Allah katika vita vya Badri, ilijengeka dhana katika
nafsi za waislamu kwamba ushindi katika vita vyo vyote ni suala la kimaumbile
tu ambalo huja lenyewe. Ni suala lisilo na uhusiano hata kidogo na hali na
mazingira halisi. Ni suala lisilotegemea mwenendo na sababu halisi za ushindi,
halisuhubiani wala kuambatana na kuyashinda matamanio na tamaa za nafsi. Ni
suala lisilohitaji kuthibiti na kuwa imara mbele ya shida na hali ngumu na
kuelekea na kujitupa mikononi mwa Allah Mshindi Mtoa ushindi. Hii ndio dhana
iliyokuwa imekita mizizi ndani ya nyoyo za waislamu, dhana iliyokurubia kuwa
imani. Ndipo Allah Mola Mtukufu akataka kuwafundisha waja wake kwamba haupati
ushindi ila yule mwenye kujitwalia sababu na akaandaa mazingira ya ushindi.
Bila ya kusahau kwamba hashindwi ila yule mwenye kuandaa mazingira na mwanya
wa kushindwa. Pia akataka waja wake wafahamu kwamba kamwe Allah hatawatupa
waja wake waumini maadam wanamtakasia yeye tu nia na amali zao.
Likiwashughulisha naye jambo miongoni mwa vitu vya kilimwengu hata wakamsahau,
nae atawaacha kwa kadri ya kushughulika kwao na hilo lililowashughulisha nae.
Wala hatakuwa pamoja nao mpaka wao wawe pamoja nae kwa nyoyo, hisia (fikra),
dhahiri na batini yao.
- WAISLAMU
WALIKWENDA UHUD BILA YA KUWA NA MSHIKAMNO NA MAFUNGAMANO YA KWELI.
Ni
ukweli unaodhihirika wazi kwamba katika vita hivi zilikuwepo
sura na rangi mbali mbali. Matukio yakapunga kufuatana na mawimbi
(mpungo) ya nyoyo na nia za watu zilivyokuwa. Waislamu walivitokea vita hivi
na ilhali kidhahiri wakionekana ni watu wamoja, wenye dhamira na nia moja.
Watu wanaolipukwa na mori wa kukutana na adui, wenye kuchemkwa na shauku ya
kufa kwa ajili ya dini ya Allah. Watu hawa hawakwenda masafa marefu, khilafu
ikadhihiri baina yao na ukinzani ukazitambaa safu zao. Abdullah Ibn Ubayyi
akajitoa na kumega theluthi ya jeshi, hili likalifanya jengo lililokamatana
kuanza kuvunjika. Nguzo za jengo hili zikalegalega kiasi cha kukurubia
kuanguka upande wake mmoja lau si Allah kuwadiriki waumini kwa rehema zake.
Banu Sulaym na Banu Haarithah wakazuia ukinzani ambao ulikurubia kujitokeza: “(Kumbuka)
MAKUNDI MAWILI MIONGONI MWENU YALIPODHAMIRIA KUFANYA WOGA (na kwenda zake kama
walivyokwenda zao wale wanafiki). NA ALLAH AKAWA MLINZI WA YOTE MAWILI HAYO
(Kwa hivyo yakahifadhika, hayakufanya mabaya hayo). NA WAISLAMU WAMTEGEMEE
ALLAH (tu basi)”. [3:122]
Kwa
hivyo basi, utawaona waislamu wanakwenda katika vita hivi wakiwa katika hali
inayoshabihiana kwa karibu kabisa na ile hali waliyokuwa nayo Makurayshi
wakati wakienda katika vita vya Badri. Naam, kwa kushindwa huku Allah
aliwakashifia (aliwafichulia) waumini nyoyo zenye maradhi ya unafiki
zilizojificha miongoni mwa jamii yao. Na kwa ushindwa huu Allah akawa
amewalinda waislamu na shari nyingi ambazo zingeliwapata kutokana na kuwa
pamoja na wanafiki hawa. Lakini pamoja na yote haya, bado tunalazimika kukiri
kwamba kitendo hiki cha kushindwa kwa dhati yake kilisababishwa na udhaifu
fulani uliokuwepo upande wa waislamu. Ambukizo la udhaifu huu lilikurubia
kutambaa katika safu za waislamu, lakini Allah akaleta salama yake.
- WARUSHA
(WATUPA) MISHALE WALIIKHALIFU AMRI YA MTUME WA ALLAH.
Vita
vilipouma ukajitokeza udhaifu mwingine uliosababisha mzozo au ugomvi baina ya
watupa mishale wao kwa wao. Wakapapatikia ngawira na kuikhalifu amri
ya Bwana Mtume pamoja na kuwatahadharisha kwake kutoondoka mahala
alipowapangia. Ni jambo lisilo na shaka kwamba utii ndio msingi/uti wa mgongo
wa nidhamu ya jeshi na ni anuani ya unyoofu (Ikhlasi) ya mwanajeshi. Ni juu ya
msingi huu wa utii ndio amiri/kamanda jeshi mkuu huchora/hupanga mikakati yake
na huainisha mahala pake pa kupigania. Kwa mantiki hii basi, ni dhahiri kuwa pasipo na utii hapana mikakati, hii ni
kwa sababu kamanda mkuu huweka mikakati yake baada ya kuyakadiria mazingira
yote yanayomzunguka katika uwanja wa mapambano. Ni juu ya makadirio haya ndio
huchora mikakati ya kufuata ili kuziba mianya yote inayoweza kutumiwa na adui
kwa namna moja au nyingine kuleta madhara. Kwa mikakati hii anakuwa
amejidhaminia ushindi na nusra dhidi ya adui yake. Na tukumbuke kwamba wakati
kamanda anapoweka mikakati yake na kuchora hatua za kupita katika vita, huwa
ana yakini kwamba kila hatua itafikia lengo lake. Sasa katika hali hii
unapokosekana utii bila ya shaka mikakati yote itakuwa imefisidika na kuacha
mambo kwenda shaghlabaghla ambapo mwisho wake huwa ni mbaya kama tulivyoona.
Haya ndio yaliyojiri/yaliyotokea katika vita vya Uhud, tunawaona watupa
mishale wakiikhalifu amri ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ambaye
ndiye kamanda mkuu. Wakamuasi amiri wao; Abdullah Ibn Jubeir ambaye ndiye
aliyekuwa kamanda wa kamandi (kikosi) yao. Wakaondoka mahala walipopangiwa na
kwenda kuhodhi ngawira kwa mapenzi na raghba yao. Kwa kitendo chao hiki cha
uasi, mikakati iliyowekwa na kamanda mkuu ikafisidika. Maasi haya ya kamandi
hii ikawa ni sababu tosha ya kufisidika kwa mikakati mizima ya vita. Na huku
kufisidika kwa mikakati kukawa ni sababu ya mgongano ndani ya jeshi, mgongano
ambao ukawa ni sababu ya ushindi kugeuka ushindwa. Tena ushindwa uliokurubia
kuwa ni kusagwasagwa lau si ulinzi na wema wa Allah.
Naam,
ni lipi khasa lililowapelekea warusha mishale hawa kuikhalifu amri ya Bwana
Mtume? Je, ulikuwa ni uasi tu na kujitoa katika twaa ya kamanda mkuu? Au
ilikuwa ni pupa ya kugombea ngawira? Riwaya zote zilizopokewa katika kulitaja
tukio hili zinakongamana kwamba watupa mishale hawa waliasi amri ya amiri wao;
Abdullah Ibn Jubeir. Na kwamba amiri wao huyu aliwahadharisha na matokeo ya
kukhalifu amri na isitoshe akawakumbusha wasia na maonyo waliyopewa na Mtume
wa Allah. Halafu zinawafikiana riwaya kwamba wao watupa mishale hawakuacha
malindo yao ila mpaka walipoona adui kesha endeshwa mbio na wakawaona wenzao
wakikusanya ngawira katika hali ya amani. Vyo vyote itakavyokuwa katika suala
hili, marejeo yetu sote ni katika Qur-ani Tukufu iliyolisifu tukio hili kuwa
ni maasi. Na kwamba ni udhaifu wa kibinadamu uliozivaa nyoyo
hizi zilizoamini, udhaifu uliowapondoa na lengo kuu walilokuja kupigana kwa
ajili yake. Ukawapeleka katika lengo duni la kujipatia vitu vya kilimwengu
vipitavyo na kusababisha wapate jazaa kwa jinsi ya amali yao: “...AKAKUPENI
(Allah) HUZUNI JUU YA HUZUNI. (Amekusameheni hivyo) ILI MSISIKITIKE (sana) KWA
YALE YALIYOKUPOTEENI WALA KWA (misiba) ILIYOKUSIBUNI. NA ALLAH ANA KHABARI ZA
YOTE MNAYOYATENDA”. [3:153]
Hivi
ndivyo waislamu walivyojua kawaida/kanuni za Allah zinazopita kwa viumbe
vyake. Wakatambua kwamba ushindi haupatikani ila kwa kuwepo sababu za
ushindi. Na wakafahamu kwamba kushindwa si suala la sadfa tu bali
husababishwa na sababu zake. Wakajua kuwa Allah yu pamoja na waumini
muda wa kuwa wao wako pamoja nae kwa hali zao zote. Na huwatupa mkono
pindi wakimsahau kwa kushughulishwa na mambo ya kidunia. Wakaona namna
Allah alivyowanusuru juu ya adui wao wakati nia yao ilikuwa ni kuipigania dini
yake. Nia yao hii ilipogeuka kukusanya ngawira, Allah akawaacha na ushindi
walioupata ukageuka kuwa ushindwa mbaya kabisa: “NA ALLAH
ALIKUKAMILISHIENI MIADI YAKE (ya kuwa mtawashinda). BASI MKAWAUA KWA IDHINI
YAKE. MPAKA MLIPOREGEA NA MKAGOMBANA KATIKA SHAURI LILE NA MKAASI BAADA YA
YEYE KUKUONYESHENI MLIYOYAPENDA (hapo ndipo alipoacha kukunusuruni). WAKO
MIONGONI MWENU WANAOPENDA DUNIA, NA WAKO MIONGONI MWENU WANAOPENDA AKHERA.
KISHA (Allah) AKAKUEKENI MBALI NAO (hao makafiri, msiweze kuwashinda) ILI
AKUTIENI ADABU. NAYE SASA AMEKUSAMEHENI. NA ALLAH NI MWENYE IHSANI NYINGI JUU
YA WANAOAMINI”. [3:152]
|