|
Na tukio jingine miongoni mwa matukio yaliyoonyesha udhaifu katika safu za
waislamu, yaliyofichuliwa na kushindwa katika vita hivi. Ni kwamba adui
alipowazingira na kuwaweka kati, hawakuungana na kushikamana pamoja. Bali
walitapanyika kila upande kutokana na kizaizai kilichowakumba pasipo
kutarajia. Hata yasemekana kwamba baadhi yao walitimua mbio mpaka Madinah,
lakini wakashindwa kuingia kutokana na kuona haya. Suala la kila mtu kutaka
kuiokoa nafsi yake likawashughulisha mpaka wakamsahau Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie. Wakamuacha pekee katika uwanja wa vita akipatwa na jeuri
na kushukiwa na nguvu ya adui aliye na uchu wa kumfyekelea mbali.
Wakamuacha Bwana Mtume na pote la watu wachache mno ambao wasingemtosheleza
kwa cho chote lau si kupata ulinzi wa Allah. Katika kimtim hiki ambacho jeshi
liliwajibika kumzunguka kamanda na jemadari wao ndipo jeshi likamkimbia na
kumuacha, kila mmoja akitafuta kuiponya nafsi yake. Ni jambo la kushangaza mno
waislamu kumsahau Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika mshindo huu
mkuu uliokurubia kuyagharimu maisha yake matukufu. Wanamuacha pamoja na
kupaaza kwake sauti kuwaita, lakini wapi hao wanaendelea kukimbia mithili ya
watu walio katika mashindano ya mbio. Hivi ndivyo Allah anavyoielezea hali
ilivyokuwa: “(Kumbukeni) MLIPOKUWA MKIKIMBIA MBIO, WALA NYINYI HAMUMSIKILIZI
YO YOTE, HALI MTUME ALIKUWA ANAKUITENI, YUKO NYUMA YENU...” [3:153] Katika
ibara hii fupi, Qur-ani Tukufu inawachorea waumini mandhari kamili ya kukimbia
inayosawirisha “harakati hisia sambamba na harakati nafsi”.
Kosa na kunguwao hili lililofanywa na waislamu ni katika jumla ya makosa ya
udhaifu yaliyowapitikia waislamu katika kipindi hiki kigumu na kizito. Allah
Mola Mwenyezi akataka kuwafichulia waislamu kosa hili ili walione na waihisi
na kuionja athari yake ili waweze kulisahihisha na wasilirudie hapo baadaye:
“WALE WALIORUDI NYUMA (waliokimbia) MIONGONI MWENU SIKU AMBAYO MAJESHI
MAWILI YALIPOKUTANA (katika vita vya Uhud; jeshi la makafiri na la waislamu).
SHETANI NDIYE ALIYEWATELEZESHA KWA (sababu ya) BAADHI YA (makosa)
WALIYOYAFANYA, NA ALLAH (sasa) AMEWASAMEHE. HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE
(na) MPOLE SANA”. [3:155]
- BAADHI
YA WAISLAMU WALIACHA KUENDELEA KUPIGANA WALIPOSIKIA KHABARI YA UZUSHI KUWA
BWANA MTUME AMEUAWA.
Na
tukio jingine miongoni mwa matukio yaliyoonyesha udhaifu, lililofichuliwa na
tukio hili la vita. Ni pale zilipotangaa khabari za kifo cha Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie, hapo baadhi ya waislamu waliacha kuendelea
kupigana na kukubali kushindwa. Wakasema baadhi ya walioacha kupigana:
“Laiti tungelimpeleka mjumbe kwa Abdillah Ibn Ubayyi, akatuchukulia amani
kwa Abu Sufyaan! Enyi kaumu zetu, bila ya shaka Muhammad amekwishauawa, basi
rejeeni mkajiunge na jamaa zenu kabla hawajakujieni na kukueni”. Kana kwamba
kwa kauli yao hii walidhania kuwa wamefanya kosa kubwa kuja kushiriki vitani
na kwamba ushauri wa kutinda ni ule wa kurejea nyuma aliouchukua Ibn Ubayyi.
Na kana kwamba hawakuja vitani kwa ajili ya kuilinda itikadi na kufa kwa ajili
ya itikadi hiyo. Bali walikuja vitani kwa kufitinishwa na ama kwa kuitii amri
ya Bwana Mtume ya kwenda vitani na kuepuka kumkhalifu. Au kwa kutekeleza ile
ahadi ya kumlinda waliyompa wakati anahamia kwao. Basi maadam Bwana Mtume amekwishakufa, imekufa pamoja nae sababu
ya vita. Kwa mantiki hii, vita havina nafasi tena na wao hawana sababu ya
kujiangamiza kwa kuendelea kupigana.
Hili
lilikuwa ni kosa baya mno ambalo waislamu walikuwa hawana budi kuling’amua,
kwani lengo walililokuwa wakilipigania halikuwa ni Muhammad; Mtume wa Allah.
Hakika si vinginevyo walipaswa kuelewa kuwa lengo la mwanzo na la mwisho
lilikuwa ni kuinusuru dini ya Allah na kuliinua neno lake. Na hiyo ndiyo akida
(itikadi) waliyoiamini na wakatoka kwenda kupigana kwa ajili ya kuilinda kwa
kuutoa muhanga uhai wao. Kwa hivyo basi, haikustahiki kabisa kwa waumini
kusalimu amri na kukubali kushindwa kwa vyo vyote vile itakavyokuwa. Bali
walilotakiwa kulifanya ni kuipigania akida yao mpaka wajipatie udhuru mbele ya
Allah. Kwani kwa yakini walitakiwa kuelewa kuwa wanaitetea na kulinda akida ya
dini ya Allah na wala hawapigani kwa ajili ya dhati ya Bwana Mtume. Basi iwapo
Mtume amekufa, hakika Allah yu hai milele hafi: “NA HAKUWA MUHAMMAD ILA NI
MTUME TU. WAMEPITA KABLA YAKE MITUME (wengi kabisa). AKIFA AU AKIUAWA NDIO
MTARUDI NYUMA (kwa visigino vyenu), MUWE MAKAFIRI KAMA ZAMANI? NA ATAKAYERUDI
NYUMA KWA VISIGINO VYAKE HATAMDHURU ALLAH CHO CHOTE. NA ALLAH ATAWALIPA
WANAOMSHUKURU”. [3:144]
- NA
KUNDI JINGINE LILISHUGHULISHWA NA SUALA LA KUZINUSURU NAFSI ZAO.
Na
tukio jingine miongoni mwa matukio yaliyoonyesha udhaifu, tukio lililosajiliwa
na vita vya Uhud. Ni kwamba lilikuwepo kundi la waislamu ambalo halijaamini
misingi ya kujitoa muhanga kwa ajili ya kuilinda itikadi (akida). Na
bado walikuwa hawajazijua kanuni za Allah
ziendeshazo ulimwengu, kana kwamba wao walikuwa wakipima uzuri (kufaa)
na ubaya (kutofaa) wa itikadi kwa ushindi au ushindwa unaowafika wafuasi wa
itikadi husika. Au walikuwa wakidhania kwamba kufaa kwa itikadi pekee
kunatosha kuinusuru na kuipa ushindi itikadi husika, hata kama waumini
wake hawakufuata sababu zipelekeazo katika ushindi na nusra. Sasa basi
waliposhindwa katika vita hivi wakawa wanajiuliza: “...AH! TUNA AMRI SISI
KATIKA JAMBO HILI?...” Kana kwamba wanaeleza kwa ibara hii wasiwasi na
mashaka yanayojiri ndani ya nafsi zao kuhusiana na suala la akida (itikadi)
hii; je akida hii yafaa na dini hii ni ya haki kweli?! Iwapo hii ni akida
ifaayo na dini ya haki, kwa nini basi kumepatikana kuuliwa na kushindwa huku?!
Allah Mtukufu ameisawirisha hali ya pote (kundi) hili na kulisahihishia kosa
lao hili kwa kauli yake tukufu: “...NA KULIKUWA NA KUNDI JINGINE NAFSI ZAO
ZIMEWASHUGHULISHA (hawajijui hawajitambui); WAKIMDHANIA ALLAH DHANA ZISIZOKUWA
NDIZO, DHANA ZA UJINGA; WAKISEMA: AH! TUNA AMRI SISI KATIKA JAMBO HILI? SEMA:
MAMBO YOTE NI YA ALLAH. WANAFICHA KATIKA ROHO ZAO (hao wanafiki)
WASIYOKUBAINISHIA. WANASEMA: TUNGEKUWA NA CHO CHOTE KATIKA JAMBO HILI
TUSINGEUAWA HAPA. SEMA: HATA MNGALIKUWA MAJUMBANI MWENU, BASI WANGALITOKA WALE
WALIOANDIKIWA KUFA, WAKENDA MAHALI PAO PA KUANGUKIA WAFE. (Amefanya haya Allah
ili) AYADHIHIRISHE YALIYO NYOYONI MWENU. NA ALLAH ANAYAJUA (hata) YALIYOMO
VIFUANI”. [3:154]
Kwa kauli hii, Allah Mtukufu akafichua waliyoyaficha nyoyoni mwao na
akawafundisha kwamba kushinda ama kushindwa hakuna uhusiano wala mafungamano
yo yote na kufaa au kutokufaa kwa akida. Na kwamba mauti na uhai havina
uhusiano na vita au amani, bali huo uhai na hayo mauti ni kanuni maalum
iliyowekwa na vina muda maalumu vilivyokadiriwa. Kwa hivyo basi, atakayeandaa
na kufuata sababu za ushindi ndiye atakayestahiki kupata ushindi. Na
utakayemfikia muda wake wa kuondoka ulimwenguni, atakwenda mwenyewe katika
mahala pake pa kuangukia, ili afie pale alipoandikiwa na Allah kufia.
|