|
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika vita hivi aliwapatia maswahaba wake
bali uma mzima wa kiislamu masomo ya juu kabisa katika nyanja za:-
ü
Kuheshimu shura
(ushauri na maoni ya uma).
ü
Kuwa na azma ya
kweli.
ü
Kuwa na moyo
thabiti, na
ü
Kustahamili maudhi
na kumsamehe mkosaji.
Imekwishafahamika huko nyuma kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alitoka kwenda katika vita hivi bila ya khiari yake, alilazimishwa.
Lakini Bwana Mtume alilazimika kutoka wakati ambapo alikuwa na mamlaka ya
kupinga kwa ajili ya kuchunga na kuheshimu shura ya maswahaba wake. Na pale
maswahaba wake walipohisi kuwa wamemshurutisha walitaka kuwafikiana na rai
yake ya kutokwenda vitani. Bwana Mtume akakataa kubadilisha uamuzi wa kutoka
uliofikiwa na wengi baada ya kuwa amekwishafunga azma hiyo ya kutoka.
Na katika kule kuthibiti kwake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-mbele
ya adui katika wakati huu wa chinjachinja na uaua. Na katika kupambana kwake
na adui katika wakati ambao waislamu waliomzunguka wanakimbia kuziokoa nafsi
zao na mauti. Katika kipindi ambacho anapaaza sauti yake kuwaita waislamu
wanaokimbia warudi kuthibiti pamoja nae. Akiwashajiisha na kuzitia nguvu nyoyo
zao, nao kutokana na mshindo mkuu uliowapata hawasikii na wala hawaoni. Na
katika kule kujizatiti kwake na ilhali khatari imemzunguka kila upande, hana
makimbilio hata finyu, maadui wamemkusanyikia na kumzonga wakiwa na dhamira na
lengo moja tu. Nalo ni kuponya chuki zao kwa kumuua. Kwa yakini mna ndani ya
yote haya kila dalili juu ya upeo wa ushujaa wa moyo aliopewa Bwana Mtume na
Allah Bwana Mlezi wake. Mna maono na ufanyajikazi haraka wa akili na nguvu ya
yakini kwa Allah Mshindi Mtukuka.
Na hakika katika sura na picha hii ambayo Qur-ani imemchora Mtume na
waislamu (maswahaba wake) na miongoni mwao wakiwemo mashujaa, mabwana wakubwa
na mabwana wa vita. Wote hawa wakiwa katika mfadhaiko wao na kushindwa
kukabiliana na hali iliyowakumba, wakikimbia mbio hawasikilizi lo lote. Wao
wakiwa katika hali hiyo, Bwana
Mtume akiwa katika uthabiti na yakini yake akiwaitia akhera yao na
akiwaogofyesha na kukimbia kwao. Hakika katika hili mna tofauti ya upeo wa
mbali kabisa baina ya ushujaa wa maswahaba ukiulinganisha na ule wa Mtume wa
Allah. Na baina ya nguvu ya maswahaba ukiipima na ile ya Bwana Mtume na baina
ya yakini ya maswahaba kwa Allah ukiimithilisha na ile ya Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie.
Pamoja na yote yaliyomsibu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-miongoni
mwa majeraha na maumivu kwa sababu ya kukimbiwa na waislamu na kumuacha
akipambana peke yake na waislamu wachache tu. Bwana Mtume hakumkaripia wala
kumlaumu ye yote miongoni mwao kama ambavyo angelifanya ye yote miongoni mwetu
sisi kama angekuwa katika nafasi yake. Na pengine asingekomelea kukaripia na
kulaumu tu, bali angeliadhibu vikali kabisa. Lakini je, Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-alifanya nini? Hakufanya kingine cho chote zaidi ya kuwasamehe
kutokana na uzembe na udhaifu wao wa kiimani waliouonyesha. Na isitoshe akawa
anawaliwaza na kuziunganisha na kuzifungamanisha pamoja azma zao, akiwaambia: “Hawatoweza
kamwe kututia madhara kama haya tena mpaka tulishike hajarul-aswad”. Na
Allah Mtukufu anamsifia Mtume wake kwa hilo pale aliposema: “ BASI KWA
SABABU YA REHEMA ITOKAYO KWA ALLAH UMEKUWA LAINI KWAO (ewe
Muhammad). NA KAMA UNGEKUWA MKALI NA MWENYE MOYO MGUMU BILA
SHAKA WANGALIKUKIMBIA. BASI WASAMEHE WEWE NA UWAOMBEE MSAMAHA (kwa Allah) NA
USHAURIANE NAO KATIKA MAMBO...” [3:159]
VITA
HIVI VILIKUWA NI JARIBIO GUMU LILILOTOA MAFUNZO MENGI YENYE MANUFAA MAKUBWA
KWA UMA MZIMA WA KIISLAMU.
Naam,
ni kweli kabisa kwamba vita hivi vilikuwa ni jaribio gumu na zito kwa
waislamu. Na bila shaka vilikuwa ni mtihani wenye mshindo mkuu uliozifichua
siri za nyoyo na unafiki ukapambanuka na imani. Wakatambulika wale ambao
walioipiga teke dunia na wala
hawavutwi na tamaa za kidunia na wale walioielekea dunia na tamaa zao mbaya
zikaanzisha kutokana na cheche ndogo moto mkubwa (maafa) wa kutisha. Allah
Taala anabainisha sababu ya kuwapa waislamu mtihani huu mgumu: “NA MSIBA
ULIOKUFIKENI SIKU YA MKUTANO WA MAJESHI MAWILI (la waislamu na makafiri) ULIKUWA
KWA IDHINI YA ALLAH, NA KUWAPAMBANUA WALIOAMINI. NA KUWAPAMBANUA
WALE WALIOKUWA WANAFIKI. NAO WALIAMBIWA: NJOONI MPIGANE KATIKA NJIA YA
ALLAH AU MZUIE (maadui pamoja na sisi). WAKASEMA: TUNGEJUA KUWA KUNA KUPIGANA
BILA SHAKA TUNGELIKUFUATENI. WAO SIKU ILE WALIKUWA KARIBU NA UKAFIRI
KULIKO NA UISLAMU (japokuwa siku zote wakidhihirisha Uislamu wa
uwongo). WANASEMA KWA MIDOMO YAO YASIYOKUWA NYOYONI MWAO. NA
ALLAH ANAJUA VYEMA (yote) WANAYOYAFICHA” [3:166-167]
Waislamu kwa upande mwingine walifaidika sana na vita hivi kutokana na
masomo/mafunzo waliyoyapata, mafunzo ambayo yalikuwa ni dira na sukani ya
maisha yao yote baada ya vita hivi. Wakatambua maeneo ya udhaifu wao na nguvu
zao na wakajifunza kwa vitendo
anavyotakiwa kuwa mpiganaji katika njia ya Allah. Ya kwamba:-
ü
Awe na imani ya
kweli kuielekea akida (itikadi) anayoiamini na afanye matendo yake yote kwa
ajili ya Allah pekee bila ya kuchanganya na tamaa za kidunia.
ü
Awe na ustahamilivu
na uthabiti wakati apambanapo na adui na kutokuonyesha udhaifu na kukata tamaa
ya kupata nusra wakati vita vinapopamba moto.
ü
Amuelekee Allah
pekee na kumtegemea katika kupata msaada, nguvu na nusra.
Na Allah Taala amewapigia mithali aina hii ya Mujahidina wa kweli katika
kauli yake: “NA MANABII WANGAPI WALIPIGANA NA MAADUI, NA PAMOJA NAO KULIKUWA
NA WATAKATIFU WENGI. HAWAKULEGEA KWA YALE YALIYOWASIBU KATIKA NJIA YA
ALLAH, WALA HAWAKUDHOOFIKA WALA HAWAKUDHALILIKA. NA ALLAH ANAWAPENDA
WAFANYAO SUBIRA. WALA HAIKUWA KAULI YAO (watakatifu hao) ILA NI KUSEMA: MOLA
WETU! TUGHUFIRIE MADHAMBI YETU NA ITHIBITISHE MIGUU YETU NA UTUSAIDIE JUU YA
WATU MAKAFIRI. ALLAH AKAWAPA MALIPO YA DUNIA NA MALIPO MAZURI YA AKHERA, NA
ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO MEMA”. [3:146-148]
AYA
ZA QUR-ANI ZILIZOSHUKA KATIKA VITA VYA UHUD ZILIKUWA NI FARAJA NA FUNDISHO KWA
WAUMINI.
Kama ambavyo Allah Mtukufu alivyoteremsha Suratil-Anfaal (9) katika kadhia
ya vita vya Badri, akiwafundisha waislamu ndani yake misingi ya vita na adabu
(taratibu) zake. Na yawapasayo wakati wa kukutana na adui miongoni mwa
uthabiti, uvumilivu na kukithirisha kumdhukuru Allah na kumtii Mtume wake. Na
wanayotakiwa kutahadhari nayo miongoni mwa kugombana, kutofautina, kufanyiana
khiana, udanganyifu na kukimbia vitani. Ndivyo hivyo hivyo Allah akashusha
katika kadhia hii ya vita vya Uhud kadiri ya aya sitini katika Surat Aali
Imraan (3). Akawabainishia waumini ndani yake makosa yao katika kuitekeleza
kivitendo ile misingi aliyowafundisha katika vita vya Badri.
Na akawaonyesha natija ya makosa yao hayo muono wa macho, lakini
hakuwaacha katika msiba wa kukata tamaa. Msiba ambao huziua nyoyo na kulegeza
hamasa, bali akazipangusa na kuzifuta huzuni zao kwa upole na rehema. Na
akazichanganya zile lawama nyepesi na darasa lenye manufaa. Na akawabainishia
kwamba kushindwa hakulichafui lile lengo wanalopigana kwa ajili yake wala
utukufu wa misingi wanayoilinda na kuitetea. Na hakukuwa kushinda na kushindwa
ila ni vizuka viwili wanavyobadilishana na kupokezana watu; akishinda huyu leo
huwa ameshindwa mwingine ambaye kesho anaweza kuwa mshindi vile vile. Na ni
katika jumla ya kawaida (kanuni) miongoni mwa kawaida za Allah kwa viumbe
wake.
Kisha akawabainishia kwamba kushindwa huku hakukuwa ni shari iliyolengwa
kwao, bali kulikuwa ni mtihani. Mtihani ambao Allah alitaka kuwadhihirishia
kupitia mtihani huo waumini wakweli na kuwafichua wanafiki wafanyao khadaa.
Kwa hiyo basi, wale mashahidi (waliokufa kwa ajili ya Allah) ndio chaguo
halisi alichagualo Allah miongoni mwa wenye kuipigania dini yake ili alienezee
fadhila zake: “NA MSILEGEE WALA MSIHUZUNIKE, MAANA NYINYI NDIO MTAKAOKUWA
JUU IKIWA MNAAMINI KWELI. KAMA YAMEKUPATENI MAJARAHA, BASI NA WATU HAO
YAMEWAPATA MAJARAHA KAMA HAYA. NA SIKU ZA NAMNA HII TUNAWALETEA WATU KWA ZAMU.
(Amefanya haya) ILI ALLAH APAMBANUE WALIOAMINI (kweli, kwa hivyo
hawakukimbia) NA AFANYE MIONGONI MWENU MASHAHIDI (waliouawa katika hivyo vita
wapate daraja ya ushahidi). NA ALLAH HAWAPENDI MADHALIMU. NA ILI
ALLAH AWASAFISHE WALIOAMINI NA KUWAFUTA (waondoke ulimwenguni wale)
WALIOKUFURU. JE! MNADHANI MTAINGIA PEPONI, HALI ALLAH HAJAWAPAMBANUA
WALE WALIOIPIGANIA DINI YA ALLAH MIONGONI MWENU NA KUWAPAMBANUA WALIOFANYA
SUBIRA? (sharti yaonekane kwanza haya hapa ulimwenguni). NA NYINYI MLIKUWA
MKITAMANI MAUTI (kuwa shahidi), KABLA HAMJAKUTANA NAYO. BASI MMEKWISHAYAONA NA
HUKU MNAYATAZAMA”. [3:139-143]
Hivi ndivyo Allah Taala alivyokuwa akiwaliwaza waumini
katika mtihani wao huu mgumu na kuwafariji katika msiba huu mkuu
uliowasibu. Na akiwavumbulia pande za mazingatio katika matukio na msimamo wa
vita hivi. Na akiwatahadharisha kutokuusalimisha uongozi wao kwa makafiri na
wanafiki au kusikiliza uvumi uenezwao na makafiri juu ya mashahidi waliouawa
katika njia ya Allah. Kwani yawatoshea mashahidi kile alichowaandalia Allah;
yaani thawabu maridhawa kabisa: “NA KAMA MKIUAWA KATIKA NJIA YA ALLAH AU
MKIFA (si khasara kwenu) KWANI MSAMAHA NA REHEMA ZINAZOTOKA KWA ALLAH
(kukujieni) NI BORA KULIKO VILE WANAVYOKUSANYA (hapa ulimwenguni). NA
KAMA MKIFA AU MKIUAWA (ni sawasawa). (Nyote) MTAKUSANYWA KWA ALLAH”.
[3:157-158]
|