|
I/.
MASHAHIDI HAWAFI.
Naam, ni kweli isiyo na shaka kwa kila muumini kwamba mashahidi wale
waliokufa katika vita vya Uhud kwa ajili ya kuipigania dini ya Allah. Na wale
wote watakaokufa kwa ajili hiyo tu, hawafi kama walivyodhania mushrikina wa
kikurayshi na wale wote wasioifahamu maana halisi ya mauti. Wasiojua katika
uhai huu ila picha na sura yake ya dhahiri tu. Dhana na fikra zao hizi
haziiondoshi hakika na ukweli kuhusu suala zima la mashahidi. Kwa yakini si
suala la kupingwa kwa kila mwenye imani hai na sahihi kwamba mashahidi wako
hai wanaruzukiwa mbele ya Bwana Mlezi wao waliyemsabilia maisha yao.
Wakizifurahia neema alizowapa Allah kwa fadhila zake, kutokana na maisha
mazuri waliyoandaliwa huko wanatamani kurudi tena duniani. Waje kuipigania
dini ya Mola wao na wauawe tena katika kuipigania dini ya Allah ili
warudufishiwe neema za Mola wao.
Imamu Ahmad-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa Ibn Abbas-Allah amuwiye
radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ndugu
zenu walipouliwa katika vita vya Uhud, Allah aliziweka roho zao ndani ya ndege
wa kijani. Zikaenda (roho hizo) katika mito ya peponi na kula katika matunda
yake na kwenda kupumzika katika kandili za dhahabu chini ya jivuli la Arshi.
Walipopata uzuri wa malaji yao, manywaji yao na malazi yao, wakasema: Ee laiti
ndugu zetu (walio hai) wangeliyajua aliyotufanyia Allah ili wasidhoofike
katika jihadi na wala wasikimbie vitani....! ndipo Allah Mtukufu akasema: Mimi
nitakufikishieni (salamu zenu hizi) kwao...ndipo Allah akateremsha aya hizi:
“WALA USIWADHANI WALE WALIOUAWA KATIKA NJIA YA ALLAH KUWA NI WAFU (maiti).
BALI WAHAI, WANARUZUKIWA KWA MOLA WAO WANAFURAHIA ALIYOWAPA ALLAH KWA FADHILA
ZAKE; NA WANAWASHANGILIA WALE AMBAO HAWAJAJIUNGA NAO, WALIO NYUMA YAO (wako
ulimwenguni, bado hawajafa); YA KWAMBA HAITAKUWA KHOFU JUU YAO WALA
HAWATAHUZUNIKA. WANASHANGILIA NEEMA NA FADHILA ZA ALLAH, NA KWAMBA ALLAH
HAPOTEZI UJIRA WA WANAOAMINI”. [3:169-171]
II/.
ATHARI ZA VITA VYA UHUD.
- MAYAHUDI
NA WANAFIKI WAFURAHIKIA MSIBA MKUU ULIOWASIBU WAISLAMU KATIKA VITA HIVI NA
KUITUMIA FURSA HIYO KUENEZA UVUMI MADINAH.
Ilikuwa
ni sehemu ya maumbile waislamu kuhuzunika kutokana na msiba uliowapata katika
vita vya Uhud na kujawa na majuto kwa kuwa yote yaliyowapata yalisababishwa na
wao wenyewe. Wakajutia yaliyowapata mashahidi wao kuuliwa na kukatwakatwa
viungo vyao na wakajuta kwa majeraha mabaya yaliyompata Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie. Na pia haikuacha kuwa ni sehemu ya maumbile maadui wa
waislamu Madinah na viungani mwake kuyaonea raha na furaha yaliyowasibu
waislamu. Nyoyo zao zikajawa na furaha kuu pale walipowaona waislamu wakiingia
Madinah hali ya kuwa wanyonge wakitawaliwa na kimya kikuu na unyong’onyevu.
Huku wakiwa wamefunikwa na wingu la huzuni na kukimwa na kufura kwa chuki na
ghadhabu kutokana na kitendo walichokifanya na kuwa wao ndio sababu ya yote
yaliyowasibu na kuwapa maadui kicheko cha ushindi.
Mayahudi na wanafiki hawakuona raha kukificha kicheko na furaha yao hiyo
kutokana na yaliyowapata waislamu. Kwa hivyo wakaanza kuidhihirisha bayana
furaha na kicheko chao na isitoshe wakaitumia fursa hiyo kuwatukana waislamu
na Uislamu. Wakaziachilia ndimi zao katika kumsema vibaya Mtume wa Allah,
da’awa (ulingano) yake na maswahaba wake. Mayahudi wakaanza kumtilia mashaka
na wasiwasi Mtume wa Allah na da’awa yake wakisema: “Lau angelikuwa Mtume
kweli, basi wasingelimshinda na wala asingepatwa na yaliyompata. Lakini yeye
anatafuta ufalme tu, dola iwe yake aitawale basi”. Wanafiki nao kwa upande
wao wakaanza kuchukua juhudi za makusudi kuwatenganisha watu na Mtume wa
Allah. Na kuwakumbushia waislamu huzuni ya mashahidi wao waliokufa vitani na
kuwalaumu na kuwashtumu vikali kwa kusababisha kufa kwa ndugu zao hao.
Wakijionyesha kwamba wao walichukua uamuzi wa busara pale
walipoamua kurudi nyuma njiani wasiende vitani. Na kwamba lau waislamu
wangeliwatii na kuwasikiliza pale walipowatolea wito wa kurudi, basi
yasingeliwapata yaliyowapata. Kwa hivyo basi yote yaliyowapata ni matokeo ya
ukaidi na upasito wao. Allah Mtukufu ametusajilia maneno ya wanafiki hawa,
haya na tuyasome huku tukichukua mazingatio: “WALE WALIOSEMA JUU YA NDUGU
ZAO-NA (wao wenyewe) WAMEKATAA KWENDA VITANI: WANGALITUTII WASINGEUAWA.
SEMA: JIONDOLEENI MAUTI (nyinyi wenyewe msife maisha) IKIWA MNASEMA KWELI”.
[3:168]
Mayahudi na wanafiki wakakithirisha kumsema vibaya Bwana Mtume na waislamu,
mpaka Madinah nzima ikachemka kwa uvumi mithili ya mchemko wa sufuria kubwa la
maji. Kiasi kwamba uvumi huo ulikurubia kulipua fitna kubwa, Bwana Mtume
akachelea waislamu wasijemilikiwa na udhaifu na uvumi huu usijefikia lengo
lake katika nafsi zao. Propaganda hizi zikifanikiwa kama walivyokusudia
wapikaji na wasambazaji wake zitasababisha kuporomoka kwa haiba na kitisho cha
Uislamu ndani ya Madinah na nje ya mipaka yake. Kadhalika Bwana Mtume
alichelea tamaa isijewasukuma makurayshi kuwashambulia waislamu shambulizi la
kumaliza nao wakiwa katika hali hii ya kizaizai.
LAZIMA
ICHUKULIWE HATUA YA MAKUSUDI NA YA HARAKA ITAKAYOWAREJESHEA WAISLAMU KUJIAMINI
KWAO NA KURUDISHA TISHO LAO KATIKA NAFSI ZA MAADUI ZAO. HILI LIKAZAA VITA VYA
HAMRAAUL-ASADI.
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaona kwamba hapana budi ichukuliwe hatua
ya haraka itakayoufagilia mbali unyonge uliozalishwa na maadui katika nyoyo za
waislamu. Na lazima ipatikane
tiba muafaka itakayowarejeshea waislamu kujiamini kwao na kuwarudishia tisho
lao walilolipoteza katika nafsi za maadui zao. Ndipo Bwana Mtume akaazimia
kutoka na maswahaba wake kuwafuatia makurayshi bila ya kubali (kujali) wala
kuyaangalia majeraha, machungu, maumivu na uchovu waliokuwa nao. Ilikuwa ni
lazima achukue hatua hiyo ya makusudi na ya haraka bila ya kungojea ili
kuondosha hatari kubwa iliyokuwa inawakabili waislamu na Uislamu kwa ujumla.
Katika kuchukua kwake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hatua hii alikuwa
akilenga mambo mawili ya msingi:-
MOSI: Kuwakatia njia na uwanja hawa wapika na waenezaji uvumi huu
hatari kuliko silaha kali. Ahakikishe kuwa haupi uvumi huu hata
mwanya wa tundu ya sindano kufanya kazi yake katika nafsi za
maswahaba wake.
PILI: Kuwaonyesha na
kuwathibitishia makurayshi na washirika wao
kwamba waislamu bado wana nguvu yao ile ile pamoja na yote
yaliyowasibu. Bado wanayo nguvu inayowawezesha kuwaogope
sha maadui wa Allah na maadui zao.
Mwanasira; Ibn Is-haaq-Allah marehemu-anasema: “Ilipofika kesho ya siku ya
Uhud ya mwezi kumi na sita Shawwal {Mfunguo mosi}. Muadhini wa Mtume wa Allah
aliwaadhinia watu kumfuata adui, akatangaza: “Asitoke asitoke pamoja nasi ye
yote ila yule aliyekuwa pamoja nasi jana”. Jaabir Ibn Abdillah Ibn Amrou Ibn
Hiraam akamzungumza Bwana Mtume, akamwambia: “Ewe Mtume wa Allah! Hakika
baba yangu alikuwa amenipa uangalizi wa dada zangu saba na akaniambia: Ewe
kijana changu wee, kwa yakini hainipasii mimi wala wewe kuwaacha watoto hawa
wa kike peke yao bila ya kuwa na mwanamume wa kuwaangalia. Na sikuwa mimi ni
mwenye kukufadhilishia kupigana jihadi pamoja na Mtume wa Allah kuliko nafsi
yangu, basi wewe bakia uwaangalie dada zako (mimi nakwenda kupigana). Basi
nikabakia kuwaangalia”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-(akaukubali
udhuru wake huu uliomzuia kutoka nae ile siku ya kwanza) akampa idhini ya
kutoka pamoja nae (leo). Na hakika si vinginevyo, Mtume wa Allah alitoka kwa
ajili tu ya kuwaogopesha na kuwatisha maadui. Na ili iwafikilie khabari kwamba
yeye ametoka kuwafuatilia ili watambue kuwa bado ana nguvu, na kwamba
yaliyowasibu hayakuwadhoofisha katika kupambana na adui yao”. Mwisho wa
kunukuu.
Muadhini wa Mtume wa Allah alipotoa adhana ya vita, watu wakaanza kuziendea
haraka silaha zao na kuzivaa, kisha wakamiminika na kukusanyika msikitini.
Hakubakia nyuma majeruhi wala mzima bila ya kuangalia majeraha na maumivu
yaliyotokana na majeraha hayo ambayo kila mmoja alikuwa ameshughulishwa na
kuyaganga. Wito wa Bwana Mtume uliwafanya wayasahu yote hayo kama kwamba
halikuwepo lililotokea. Hapana ye yote miongoni mwao ila aliyasahau kabisa
majeraha na maumivu yake na akajiona mzima na mwenye nguvu mpya na ari ya
kusahihisha makosa aliyoyafanya. Mpaka ikafikia wanyonge kuzibebesha nafsi zao
zisiyoyaweza kwa ajili tu ya kumuitikia Mtume wa Allah kama walivyoamrishwa:
“ENYI MLIOAMINI! MUITIKIENI ALLAH NA MTUME WAKE ANAPOKUITENI KATIKA YALE
YATAKAYOKUPENI UHAI MZURI (wa duniani na akhera)...” [8:24]
Imepokelewa kwamba: Abdullah Ibn Sahmi Al-Answariy na nduguye Raafii Ibn
Sahmi Al-Answaariy, walikuwa wamerejea kutoka Uhud wakiwa wamejeruhiwa vibaya
sana. Wakatoka wakijikokota kwenda kuungana na Mtume wa Allah na Raafii ndiye
aliyekuwa amejeruhiwa vibaya sana kuliko nduguye, akashindwa kutembea. Nduguye
Abdullah akawa anambeba mgongoni kwake masaa kadhaa mpaka anapopumzika
anamuacha atembee kwa kitambo kidogo. Wakaenda
hivyo hivyo mpaka wakafika kwa Mtume wa Allah, Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alipowaona aliwaombea dua njema. Watu wengine ambao hawakwenda
vitani jana yake walimuomba Bwana Mtume idhini ya kutoka, akawakatalia ombi
lao hilo. Kwa hivyo hakutoka ye yote miongoni mwa ambao hawakwenda vitani siku
iliyotangulia ila Jaabir Ibn Abdillah-Allah amuwiye radhi-kwa sababu ya udhuru
mzito aliokuwa nao na nia yake ya kweli.
Watu walipokwishakusanyika, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akaswali rakaa mbili msikitini, kisha akaagiza aletewe farasi wake
akampanda akiwa amevaa nguo na kofia ya chuma. Akaagizia bendera yake ambayo
ilikuwa bado haijateremshwa tangu jana, akamkabidhi Sayyidina Aliy Ibn Abiy
Twaalib na kauli nyingine inasema kuwa alimpa Sayyidina Abuu Bakri. Na akampa
ukhalifa wa Madinah Sayyidina Abdullah Ibn Ummu Maktuum na akamfanya Abbaad
Ibn Bishri kuwa mlinzi wake. Kisha huyoo Bwana Mtume akatoka na maswahaba wake
wakaenda mpaka wakapiga kambi Hamraaul-Asad; hii ni sehemu iliyo umbali wa
maili nane kutoka mjini Madinah. Akakaa hapo siku tatu; Jumatatu, Jumanne na
Jumatano. Wakati wa mchana Bwana Mtume alikuwa anawaamrisha maswahaba wake
kukusanya kuni, usiku unapoingia alimuamrisha kila mmoja wao kuwasha moto.
Ikawa mianga ya moto ikionekana umbali mrefu kabisa na kuzagaza pande zote.
Mng’aro wa mioto hii ukawakhadaa maadui na kuwafanya wahisi kuwa waislamu
wako maelfu kwa maelfu. Ibn Is-haq-Allah amrehemu-anasema: “Khabari za
kupiga kwao kambi na mioto yao zikasambaa na kuenea kila mahala, hili likawa
ndio alililowadhalilishia maadui wao”.
|