|
Katika jumla ya misaada ambayo Allah aliwapa waislamu ni kwamba kabila la
“Khuzaah” lilikuwa limeandikiana mkataba wa amani na ushirikiano na Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Ma’abad Mkhuzai alimpitia Bwana Mtume na
kumwambia: “Ewe Muhammad, hakika yametuhuzunisha mno yaliyokusibu wewe na
maswahaba wako, tungelipendelea kwamba Allah angelikitukuza cheo chako na
kwamba msiba huo ungeliwasibu mahasimu wako!” Alipokwishaliwakilisha kabila
lake katika kuelezea huzuni na masikitiko yao juu ya janga lililowapata
waislamu; washirika wao. Alishika njia akaenda zake mpaka akakutana na Abuu
Sufyaan akiwa pamoja na makurayshi pande za “Rauhaa”. Hili ni eneo lililo
baina ya Makkah na Madinah, liko kiasi cha umbali wa maili thelathini na sita
(36) kutokea mjini Madinah. Aliwakuta wakitupiana lawama na kujuta kwa nini
hawakufyekelea mbali Bwana Mtume na maswahaba wake, wakafikia kuambizana:
“Hamkufanya lo lote, mmeupata mzizi wa watu wale (waislamu) kisha mkawaachia
waende zao hivi hivi tu na wala msiukatilie mbali! Haya sasa wamebakia
viongozi wao wanajikusanya kuja kupigana nanyi. Hamkumuua Muhammad na wala
hamkuwachukua wanawake mateka, eeh ubaya ulioje wa mliyoyafanya!” Baada ya
kulaumiana na kushutumiana vikali kabisa wakakongamana kwa kauli moja kurejea
tena Uhud kwenda kuwasagasaga waislamu waliobakia ili kuukata kabisa mzizi wa
fitina.
Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anasema: “Abuu Sufyaan alipomuona Ma’abad
akamuuliza: Kuna khabari gani huko utokako ewe Ma’abad? Akamjibu: Khabari
zilizopo ni kwamba tayari Muhammad amekwisha toka na maswahaba wake
kukufuatieni katika kundi ambalo katu sijapatapo kuuona mfano wake. Wanajihisi
kuungua nyoyo zao kwa shauku ya kukutana nanyi, tena wamejiunga nae wale wote
waliobakia nyuma katika siku yenu (ya jana mliyowashinda) ilhali wanajuta kwa
kitendo walichokifanya. Wana hasira na ghadhabu kali juu yenu sijapatapo kamwe
kuuona mshabaha wake. Akasema Abuu Sufyaan: Eeh ole wako wee, unasemaje?
Akasema (Ma’abad): Wallah, mimi sioni kama mtaanza kwenda zenuni kabla
hamjaziona tosi za ngamia wao. Akasema (Abuu Sufyaan): Sisi tumepitisha
azimio la pamoja kufanya hujuma kali ya kuwamaliza kabisa waliobakia (jana).
Akasema (Ma’abad): Kwa hakika mimi ninakuonya juu ya azimio lenu hilo. Hapo
ndipo Abuu Sufyaan na watu wake wakanyong’onyea na kuishiwa nguvu”. Mwisho
wa kunukuu.
Abuu Sufyaan akabadilisha mawazo, sasa badala ya kwenda kutoa pigo la
kuwafagia waislamu, akatishika asijefikwa na yale ya mtu apambanaye na chui
mjeruhiwa. Badala yake akaamua kuchukua hatua mbadala, nayo ni kuwatisha
waislamu na kuwakatisha tamaa kuwa hawana ubavu wa kuhimili nguvu na ukali wa
jeshi lake. Na kwamba uamuzi wa busara kwao ni kukubali kushindwa na kurudi
Madinah kukusanya nguvu mpya. Akaitumia vema fursa ya msafara wa biashara
uliopita mahala walipopiga kambi ukielekea Madinah. Akawaagiza wafanyabiashara
hao wamzuie Muhammad asije na wamkhofishe dhidi ya shambulizi la kufagia na
hujuma za nguvu za makurayshi dhidi yao na akawaahidi ujira kwa kuitekeleza na
kuifanikisha kazi yake hiyo. Msafara huu wa biashara ulipompitia Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-pale Hamraaul-Asad, wakamueleza yale
waliyoagizwa na Abuu Sufyaan kama propaganda za kumtisha na kumvunja nguvu.
Lakini Mtume wa Allah hakuathiriwa hata kidogo na vitisho hivyo vya
wafanyabiashara na akasema: “Allah anatutosha, nae ni Mlinzi bora kabisa”.
Allah Taala ametusajilia tukio hili ndani ya Qur-ani ili tuwaidhike: “WALE
AMBAO WATU (waliokodiwa na Makurayshi) WALIWAAMBIA (waislamu): WATU (yaani
Makurayshi) WAMEKUKU SANYIKIENI, KWA HIVYO WAOGOPENI. LAKINI (maneno hayo)
YAKAWAZIDISHIA IMANI (waislamu), WAKASEMA: ALLAH ANATUTOSHA (atatukifia), NAYE
NI MLINZI BORA KABISA”.[3:173]
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake-Allah
awaridhie-waliendelea kubakia katika kambi yao hapo Rauhaa kwa muda wa siku
tatu. Mpaka walipojua kwamba makurayshi wameondoka kuelekea Makah ndipo nao
wakaamua kurudi na kuingia Madinah kwa heshima. Wakati wa kurudi kwake, njiani
Bwana Mtume alikwaana (alikutana ghafla) na Abuu Azzah Al-Jumahiy, yule
mshairi aliyeivunja ahadi yake aliyoichukua kwa Mtume wa Allah. Bwana Mtume
akamuweka katikati ya maswahaba, akasema khaini huyu: Ewe Mtume wa Allah!
Nisamehe. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia: “Wallah, baada
ya leo hutazipangusa sharafa zako mara mbili! Muumini hagongwi na nyoka mara
mbili!” Kisha Bwana Mtume akaamrisha auawe kwa kukatwa shingo yake.
IV/.
MAKABILA MENGI YALIJIKUSANYA ILI KUWASHAMBULIA WAISLAMU, BWANA MTUME AKAWA
ANAWASAMBARATISHA KWA MASHAMBULIZI YA KUSHTUKIZA.
Hatua za haraka na za makusudi zilizochukuliwa na Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-kwa lengo la kuzima athari za Uhud. Hazikuweza kufuta athari
hizo kwa asilimia mia moja, kwani
makabila mengi yalianza kujikusanya dhidi ya waislamu. Mabedui waliokuwa
wakiishi kuzunguka mji wa Madinah walidhania kwamba sasa wanaweza kabisa
kuushambulia na kuuteka mji wa Madinah bila ya upinzani wa haja kutoka kwa
waislamu. Iliwasawirikia akilini mwao kwamba baada ya kushindwa huko Uhud,
waislamu sasa hawana tena uwezo wa
kujilinda dhidi ya mahasimu wao. Kabila
la mwanzo kujikusanya kwa lengo la kuwashambulia waislamu, lilikuwa ni kabila
la Baniy Asad. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoitambua azma yao
hiyo ya kuishambulia Madinah, alifanya haraka kuwavamia kabla hawajajiandaa
vema. Akawapelekea Abuu Salamah akikiongoza kikosi cha maswahaba wapatao mia
moja na khamsini. Wakawashambulia kwa mbinu ya kushtukiza na wakafanikiwa
kuwasambaratisha kwa kuwa walikuwa hawajajiandaa na wala hawakutarajia kabisa
kushambuliwa na waislamu. Waislamu wakawaswaga wanyama wao ngawira, kisha
wakarudi Madinah baada ya kutekeleza jukumu la kujilinda walilopewa na
Amirijeshi mkuu na kamanda mahiri; Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.
Wakarudi Madinah na ilhali hapana hata mmoja wao aliyejeruhiwa hata ukucha ila
amiri wao; Abuu Salamah alitonesha jeraha lake lililompata Uhud. Abuu Salamah
hakukaa muda mrefu akaaga dunia kutokana na jeraha hilo-Allah amuwiye radhi.
Baada ya tukio hili, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaletewa
khabari kwamba Khalid Ibn Sufyaan Al-Hadhaliy anakusanya jeshi kuja
kushambulia Madinah. Bwana Mtume akamteua Abdullah Ibn Unays miongoni mwa
maswahaba wake kwenda kumshughulikia muovu huyu. Akamuendea kwa uficho katika
sura ya mtu anayetaka kuungana nae katika kumpiga Muhammad. Hata
alipokwishayakinisha kwamba ni kweli anakusanya jeshi dhidi ya Mtume wa Allah.
Akaanza kumperemba kidogo kidogo mpaka akafanikiwa kumuua na kuliacha jeshi
aliloanza kulikusanya likiwa halina tena kamanda wa kuliongoza. Kitendo hiki
cha kuuawa kwa kiongozi wao kililifanya jeshi kusambaratika kwa khofu na
kuwafanya waislamu kuepuka shari lao.
|