|
Tukio
la kuuawa kwa hila kwa kiongozi wao lilikuwa kubwa sana katika nyoyo za watu
wa kabila la Hudhayl, wakaanza kutafuta mbinu za kulipa kisasi. Baadhi ya watu
wa makabila mawili ya Adhwal na Al-qaraah walimuendea Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-wakadai kwamba watu wao wana raghba na Uislamu. Kwa hivyo
wanaomba awape baadhi ya maswahaba wake wakawafundishe dini na kuwasomesha
Qur-ani. Bwana Mtume akawapa kundi la maswahaba wake bora likiongozwa na
Aaswim Ibn Thabit. Wakaondoka pamoja nao hata walipofika kwenye eneo la maji
la kabila la Hudhayl liitwalo “Rajii”. Wakawasaliti na kuomba msaada wa
kunusuriwa nao kutoka kwa kabila la Hudhayl, tahamaki waislamu wamezungukwa na
watupa mishale wa Hudhayl wapatao mia mbili hivi. Waislamu kuona hivyo, wakawa
hawana hila ila kupambana tu pamoja na uchache wao ukilinganisha na maadui zao
wenye uchu wa kulipa kisasi cha kiongozi wao. Wakatumia mbinu ya kujihifadhi
na jabali ili wasije kushambuliwa kutokea nyuma, ndipo wakaanza kupambana na
adui kufa kupona. Wakapigana kishujaa kweli kweli bila ya kusalimu amri mpaka
wakauawa wote ila watatu tu miongoni mwao. Hawa walihadaika na hila ya
kujisalimisha iliyotolewa na mahasimu wao, wakatekwa nao ni Khubaybu Ibn Adiy,
Zayd Ibn Duthunnah na Abdullah Ibn Twaariq. Ama Abdullah Ibn Twaariq yeye
aliona dalili za usaliti machoni mwa adui tangu walipojisalimisha kama
walivyowataka. Akachomoa mkono wake katika kamba waliyofungiwa, kisha akatwaa
upanga wake na kurudi kinyumenyume, wakampopoa kwa mawe mpaka wakamuua. Ama
wale wenzake wawili waliwachukua na kwenda kuwauza kwa Makurayshi Makkah.
Khubaybu alinunuliwa na Uqbah Ibn Al-Haarith ili amuue kulipiza kisasi cha
baba yake; Al-Haarith Ibn Aamir. Na Zayd akanunuliwa na Swafwaan Ibn Umayyah
ili amuue kwa ajili ya kulipa kisasi cha baba yake; Umayyah Ibn Khalaf
aliyeuawa na waislamu.
MAUAJI
YA MASHAHIDI; KHUBAYBU IBN ADIY NA ZAID IBN DUTHUNNAH YALIUTIKISA MJI WA
MADINAH.
Mauaji
ya maswahaba wawili hawa yalikuwa ni tukio kubwa lililoushtua mno mji wa
Makkah na kuzitetemesha nyoyo za wengi miongoni mwa makurayshi. Imepokelewa
kwamba maswahaba wawili hawa waliwekwa mahabusu
katika mojawapo ya majumba ya Makkah na kushikiliwa humo mpaka miezi mitukufu
imalizike ndipo wauawe. Miezi mitukufu ilipomalizika walitoka nao mpaka Tan-iym;
hili ni eneo la wazi lililokuwa umbali wa maili nne kutoka mjini Makkah.
Walifuatiwa na kundi la wanaume, wanawake na watoto ili kushuhudia mauaji ya
watu hawa. Zayd akauawa na mtumwa wa Swafwan Ibn Umayyah aitwaye Nistwaasi.
Alipoletwa tayari kwa kuuawa, Abuu Sufyaan alimwambia: “Ninakuuliza kwa jina
la Allah ewe Zayd, je ungependa Muhammad awe mahala pako hivi sasa uipige
upanga shingo yake na wewe uwe nyumbani kwako?”. Zayd akajibu: “Wallah,
nisingependelea Muhammad hapo alipo hivi sasa kuchomwa na mwiba na mimi nikiwa
nimekaa nyumbani kwangu (seuze huko kuwa hapa)!”. Abuu Sufyaan
akasema: “Sijapatapo kumuona ye yote katika watu akimpenda mtu kama
maswahaba wa Muhammad wampendavyo Muhammad!”.
Khubaybu nae aliwaambia wakati walipotaka kumuua: “Ikiwa mnaona vema
kuniacha nikaswali rakaa mbili kwanza, basi fanyeni hivyo”. Wakamwambia:
“Swali tafadhali”. Akaswali rakaa mbili kwa uzuri na kwa kuzitimiza, kisha
akawaelekea wauaji wake na kuwaambia: “Ama wallah, lau isingekuwa kudhania
kwenu kwamba nimerefusha swala kwa sababu ya kuogopa kufa, basi
ningekithirisha kuswali”. Kisha akawaendea mwenyewe, wakamnyanyua juu kwa
juu na kumuweka katika ubao ili wamsulubu. Walipokwishamfunga barabara juu ya
ubao ule, akaunyanyua uso wake kuuelekeza
mbinguni na kusema: “Ewe Mola wa haki wee! Hakika sisi tumekwishafikisha
ujumbe wa Mtume wako, basi na wewe nakuomba umfikishie khabari za haya
tufanyiwayo asubuhi ya leo”. Kisha akawatupia jicho watu wale na kusema:
“Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba uwadhibiti kwa idadi, uwauwe kwa mtapanyo
na usimbakishe ye yote miongoni mwao”. Watu wale wakaenda pembeni kidogo kwa
kuchelea kupatilizwa na dua yake hiyo. Al-Waaqidiy anasema: “Kwamba
walimkusanyia watoto wa wale aliowaua katika vita vya Badri na kumshakizia,
nao wakawa wanamchoma kidogo kidogo kwa mikuki mpaka wakamuua-Allah amuwiye
radhi”.
Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-amepokea kwamba Sayyidina Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah
amuwiye radhi-alimpa Said Ibn Aamir Al-Jamhiy uliwali wa baadhi ya miji ya
Shamu. Akawa anapatwa na maradhi ya kuanguka mbele za watu, khabari zikaenda
kwa Amirul-Muuminina. Nae akachukua khatua za kumuita, alipokuja akamuuliza:
“Ewe Said, hebu nambie ni kitu gani hiki kinachokusibu?” Akajibu:
“Wallah, ewe Amirul-Muuminina mimi sina tatizo lo lote. Isipokuwa tatizo
langu ni kwamba mimi nilikuwa ni miongoni mwa walioshuhudia mauaji ya Khubaybu
Ibn Adiy na nikaisikia dua yake. Basi wallah, haijapatapo kunipitikia moyoni
nami nikiwa katika baraza ila huanguka mweleka!”
Mauaji ya mashahidi hawa yalikuwa katika mwezi wa Swafar (mfunguo tano)
mwaka wa nne Hijiria. Machungu ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa
mauaji yao yalikuwa makubwa sana, kwa sababu walikuwa ni katika jumla ya
wasomaji bora wa Qur-ani katika maswahaba wake. Na kwa sababu ya khiana,
usaliti na kukatwakatwa walikofanyiwa-Allah awawiye radhi wote.
MASHAHIDI
WA BI’IRI MAUUNAH.
Kabla nafsi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na nafsi za maswahaba
wake-Allah awawiye radhi-hazijapata kutulizana kutokana na uchungu wa tukio
hili. Likawapata tukio jingine lenye kutia uchungu zaidi katika sura nyingine
ya usaliti mbaya kabisa. Tukio zima linaanzia pale alipokuja mbele ya Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-mmojawapo wa viongozi wa kabila la Baniy Aamir,
aitwaye “Abuu Baraai”. Bwana Mtume akamkunjulia maelezo juu ya Uislamu
lakini hakusilimu na wala hakuwa mbali na kusilimu na akasema: “Ewe
Muhammad, unaonaje lau ungeliwapeleka baadhi ya maswahaba wako kwa watu wa
Najid wakawalingania jambo lako hili, mimi ninataraji watakuitika”. Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamjibu: “Mimi ninawachelea juu yao watu wa
Najid kuwadhuru”, Abuu Baraai akamwambia: “Mimi ninawachukulia dhamana,
basi wewe watume tu wakawalinganie watu katika jambo lako hili”.
Baada ya ahadi hiyo ya dhamana, Bwana Mtume hakuwa tena na sababu ya
kuukataa wito wa bwana huyu. Akampeleka Al-Mundhir Ibn Amrou kuliongoza kundi
la maswahaba arobaini katika waislamu bora bora kama ilivyotajwa katika riwaya
ya Ibn Is-haaq-Allah amrehemu. Wakaenda zao mpaka “Bi’iri Mauunah”,
wakapiga kambi hapo. Hiki ni kipande cha ardhi kilicho baina ya eneo la kabila
Baniy Aamir na ardhi yenye mawe iliyokuwa ikimilikiwa na ukoo wa Baniy Sulaym.
Walipokwishakupiga kambi hapo wakamtuma Hiraam Ibn Mal-haan kumpelekea Aamir
Ibn Twufail; kiongozi wa kabila la Baniy Aamir, barua ya Mtume wa Allah.
Alipofika na kumpa barua, hakuwa na muda wa kuisoma zaidi ya kumrukia na
kumuua mjumbe huyu. Kwa kitendo chake hiki kiovu akawa ameivunja kanuni na
utaratibu waliojiwekea wao wenyewe na kujilazimisha kuufuata, hii ni ile
kanuni isemayo: (Mjumbe hauawi). Baada ya kumuua mjumbe yule, akawapigia mbiu
Baniy Aamir waende wakawaue wale maswahaba wengine waliopiga kambi Bi’iri
Mauunah. Baniy Aamir wakakataa kumtii kwa sababu ya kuheshimu dhima na dhamana
aliyoichukua Abuu Baraai kwa Mtume wa Allah. Alipoona hakuitikiwa na watu
wake, akayapigia mbiu ya mgambo makabila ya Baniy Sulaym, hawa wakamuitika.
Wakatoka na silaha zao na kuja kuwazingira walinganiaji dini wale katika kambi
yao. Maswahaba walipowaona wakaanza kuchomoa panga zao na kuanza kupambana nao,
wakiua na kuuliwa. Mpaka wakauliwa wote-Allah awarehemu-ila Ka’ab Ibn Zayd,
huyu walimuacha akiwa anapumua pumzi za mwisho mwisho.
Katika msafara wa wanyama wa watu wale walikuwepo Amrou Ibn Umayyah na
Muanswari mmoja, hawa walipowaona ndege wakiambaambaa angani juu ya kambi ile.
Wakajongea kuja kuangalia kulikoni hata ndege wakawepo pale. Walipofika
wakawakuta wajumbe wa mjumbe wa Allah wamelala maiti katika dimbwi la damu zao
na wabaya wao wangali pale pale wakijipongeza kwa uovu wao huo. Yule Muanswari
hakuweza kujimudu kuona mandhari ile ya ukatili uliokithiri, akauchomoa upanga
wake na kuanza kuzivuna shingo za makhabithi wale kwa ushujaa mkubwa mpaka
alipozidiwa na kuuawa. Akabakia Amrou Ibn Umayyah, yeye akachukuliwa mateka,
walipomsaili kuwa yeye ni mtu wa kabila gani, akawaambia kuwa yeye ni mtu wa
kabila la Mudhwar, wakamuachia huru. Akaondoka kurudi Madinah hata alipofika
“Baqarqaratul-Kudri”-hili ni eneo lenye maji linalomilikiwa na Baniy
Sulaym, kiasi cha maili 96 kutoka Madinah. Akaamua kupiga kambi hapo kupumzika
na wakaja kujumuika nae watu wawili wa kabila la Baniy Aamir. Watu wawili hawa
walikuwa na makubaliano ya amani na dhamana ya siri na Bwana Mtume ambayo
Amrou hakuijua. Alipowatambua kuwa ni watu wa kabila la Baniy Aamir,
akawavizia hata walipolala akawaua na kuona kuwa amelipa kisasi kwa Baniy
Aamir kutokana na mauaji ya maswahaba wa Mtume waliyoyafanya. Akaondoka na
kwenda zake kwa Bwana Mtume na kumpasha khabari za yote yaliyojiri huko
atokako. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia: “Hakika
umewaua watu wawili wenye mapatano nasi, nitalipa nitalipa fidia yao!”
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawahuzunikia sana maswahaba wake
hata akafikia kusema: “Hii ni kazi ya Abuu Baraai”. Akawa mwezi mzima
katika kila swala anaomba dua (Qunuut) dhidi ya wauaji wa maswahaba wake
katika Bi’iri Mauunah na Rajiy’i mpaka Allah Taala akamshushia kauli yake:
“WEWE HUNA LAKO KATIKA SHAURI HILI-AU (Allah) AWAONEE HURUMA AU AWAADHIBU,
MAANA WAO NI MADHALIMU (atafanya anavyoona yeye mwenyewe)”. [3:128] Hapo
ndipo nafsi yake ikatulizana, huzuni ikamuondoka na akaacha kuwaapiza waovu
hawa waliowaua maswahaba wake. Hii ndio athari iliyoachwa na vita vya Uhud kwa
waislamu.
|