|
SOMO
LA KWANZA-VITA VYA BANIN-NADHWIYR.
I/.
BWANA MTUME ACHELEA USALITI WA MAYAHUDI NA AWAJARIBU ILI KUJUA DHAMIRA YAO.
Vita
hivi vya Banin-Nadhwiyr ni miongoni mwa athari zilizotokana na vita vya Uhud.
Vita hivi vilitokea katika kile kipindi kigumu ambacho waislamu bado walikuwa
wakipatwa na machungu yaliyotokana na kushindwa katika vita hivyo. Bado
walikuwa katika hali ya kutapanyika kifikra wakiwa wamezungukwa na visasi.
Mayahudi na wanafiki ambao wanaishi pamoja nao Madinah, mabedui waishio katika
vitongoji jirani yao na mushrikina wa Makkah. Wote hawa walikuwa
wakishirikiana katika hisia; hisia ya bughudha na uadui dhidi ya waislamu. Na
wakisaidiana katika fikra moja, nayo ni kumfagilia mbalini Bwana Mtume na
maswahaba wake wote. Na wakilenga lengo moja, nalo si lingine bali ni kuua
Uislamu na da’awa (mahubiri) yake. Katika mazingira kama haya, adui aliye
karibu anakuwa ni khatari zaidi kuliko yule aliye mbali. Na khatari ya ndani
inakuwa na athari mbaya na ya kina zaidi kuliko ile itokayo nje. Na hali ya
hewa inakuwa imesheheni vitimbi, hila, kuaibishana na kuviziana baina ya
mahasimu. Bila ya shaka mayahudi na wanafiki ndio waliokuwa adui wa karibu kwa
waislamu. Alama za uadui zilikuwa zikichemka nafsini mwao na kutamkwa na ndimi
zao na haikuwa muhali kwao kusubiri fursa ya kuwachoma waislamu kwa nyuma yao.
Kwa hakika katika kipindi hiki waislamu walikuwa wakitazamia khiyana na
usaliti kutoka kwa maadui zao.
Kwa mazingira haya na hali hii ya hewa iliyochafuka, utaona kuwa Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakuwa na muamana na usaliti na khiana ya
mayahudi na wanafiki wa Madinah. Na hakuwa na imani tena na ukweli na
utekelezaji wao wa makubaliano baina yao na waislamu. Ama wanafiki, hawa
walijificha nyuma ya pazia la Uislamu na haikuwaelea maswahaba wala Bwana
Mtume kuwafunulia pazia hili la Uislamu walilolifanya kama kichaka chao cha
kujifichia. Na kwa upande wa mayahudi, hawa walikuwa wamefunga ahadi na Mtume
wa Allah kwamba yeye Mtume asiwaingilie katika dini yao na hali kadhalika wao
wasimbughudhi na dini yake. Na kwamba wasiwaunge mkono na kuwasaidia maadui wa
kila upande. Lakini pamoja na ahadi yao hii, bado mayahudi hawakuwa ni watu wa
kuaminiwa katika utekelezaji wa ahadi. Hii ni kwa sababu tayari ulikuwa
umekwishadhihiri usaliti na khiana yao katika matukio mengi huko nyuma. Na
kundi moja miongoni mwa makundi yanayounda jamii ya mayahudi Madinah
lilidhihirisha uadui wao waziwazi kiasi cha kumlazimisha Bwana Mtume
kulifukuza na kulitoa Madinah. Haya yalitokea wakati waislamu wakiwa katika
kile kipindi cha nguvu nyingi na ustawi uliotokana na ushindi wa kishindo
walioupata katika vita vya Badri. Haya hali sasa itakuwaje katika kipindi hiki
cha kizaizai cha kushindwa katika vita vya Uhud? Je, usaliti na khiana katika
hali kama hii si unatarajiwa zaidi, jambo hili kwa mayahudi haliko mbali.
Kwani kama walithubutu bila ya uoga katika kile kipindi cha nguvu ni lipi
litakalowazuia katika kipindi hiki cha kitatange cha kushindwa?! Katika
kipindi hiki ambacho ndugu zao Baniy Qayunqaa wametolewa na kufukuzwa Madinah
na waislamu na isitoshe wamemuua kiongozi na mshairi wao Ka’ab Ibn Al-Ashraf.
QUR-ANI
TUKUFU YAWATAHADHARISHA WAISLAMU NA KHIANA YA MAYAHUDI.
Allah
akawakashifia waislamu siri za mayahudi katika kipindi hiki na
akawatahadharisha kutowaamini, akasema-utakatifu ni wake: “ENYI MLIOAMINI!
MSIWAFANYE WASIRI WENU WATU WASIOKUWA KATIKA NYINYI, HAO HAWATAACHA
KUKUFANYIENI UBAYA. WANAYAPENDA YALE YANAYOKUDHURUNI. BUGHUDHA (yao juu yenu)
INADHIHIRIKA KATIKA MIDOMO YAO NA YANAYOFICHWA NA VIFUA VYAO NI MAKUBWA ZAIDI.
TUMEKUBAINISHIENI DALILI (zote) IKIWA NYINYI NI WATU WA KUFAHAMU. OH! NYINYI
MNAWAPENDA (maadui zenu hao), HALI WAO HAWAKUPENDENI! NANYI MNAAMINI VITABU
VYOTE (chenu na vyao) NA WANAPOKUTANA NANYI HUSEMA, TUMEAMINI. LAKINI
WANAPOKUWA PEKE YAO WANAKUUMIENI VYANDA KWA UCHUNGU (wa kukuchukieni). SEMA:
KUFENI KWA UCHUNGU WENU (huo); HAKIKA ALLAH ANAYAJUA (hata) YALIYOMO VIFUANI.
IKIKUPATENI KHERI HUWASIKITISHA NA IKIKUPATENI SHARI WANAIFURAHIA. NA KAMA
NYINYI MKISUBIRI NA MKAMCHA ALLAH HILA ZAO HAZITAKUDHURUNI KITU. HAKIKA ALLAH
ANAYAJUA VIZURI YOTE WANAYOYATENDA”. [3:118-120]
Katika kipindi hiki waumini wakawa na hadhari kuu juu ya mayahudi na ilikuwa
hapana budi Bwana Mtume apate fursa ya kuwatahini ukweli wao. Ili apate
kuzifichua dhamira zao katika hali na mazingira haya magumu. Bwana Mtume
akaamua kuitumia fursa ya wale watu wawili wa ukoo wa Baniy Aamir waliouawa na
swahaba wake Amrou Ibn Umayah. Akawaendea mayahudi wa Banin-Nadhwiyr kuwaomba
msaada katika kulipa fidia ya wauliwa wawili hawa. Na ni vema ikaeleweka
kwamba Baniy Aamir ambao waliuliwa watu wao walikuwa ni washirika na ndugu wa
yamini wa Banni-Nadhwiyr.
II/.
BANINI-NADHWIYR WAFANYA JARIBIO LA KUMUUA MTUME WA ALLAH.
Ibn Is-haq-Allah
amrehemu-amesema katika kulielezea jaribio hilo: “Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-alitoka kuwaendea Banin-Nadhwiyr kuwaomba wamsaidie kulipa
fidia ya wauliwa wawili hawa wa Baniy Aamir. Mtume wa Allah aliwaendea kwa
mujibu wa mafungamano aliyofunga nao na baina ya Banin-Nadhwiyr na Baniy Aamir
kulikuwa na mafungamano na udugu wa yamini. Mtume wa Allah alipowaendea
kuwataka msaada, walimwambia: “Naam, ewe Abul-Qaasim, tutakusaidia
ukitakacho katika ombi lako hili kwetu”. Kisha wakakaa faraghani wao kwa wao
wakaambizana: “Kwa yakini nyinyi hamtaweza tena kumpata mtu huyu katika hali
kama hii”. Na wakati huo Mtume alikuwa amekaa pembezoni mwa kiambaza cha
nyumba zao. Wakaendelea kuambizana: “Basi ni nani atakayepanda juu ya nyumba
hii akamuangushia mwamba (jiwe kubwa), akatupumzisha nae?” Amrou Ibn Hijaash
akajipasishia jukumu hilo, akasema: “Mimi ni tayari kwa hilo”. Akapanda
juu ili amuangushie Bwana Mtume mwamba kama alivyoahidi na wakati huo Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa amekuja pamoja na kundi la maswahaba
wake. Miongoni mwao alikuwemo Sayyidina Abuu Bakri, Umar na Aliy-Allah awawiye
radhi. Khabari za dhamira mbaya ya watu hawa zikamjia Mtume kutoka mbinguni,
akainuka na kuondoka kurudi Madinah. Maswahaba wake walipomsubiri kwa muda
bila ya kurudi, wakaanza kumtafuta. Katika kumtafuta kwao huku wakakutana na
mtu ajaye kutoka Madinah wakamuuliza juu ya Bwana Mtume, akawajibu: Nimemuona
akiingia Madinah. Maswahaba wa Mtume wa Allah wakaenda mpaka alipokuwepo, naye
akawapasha khabari za dhamira ya mayahudi kutaka kumuua. Kisha akaamrisha
yafanyike maandalizi ya kwenda kupigana nao”.
Hivi ndivyo anavyosema Ibn Is-haq na waandishi wengine wa Sira ya Bwana
Mtume hawakutofautiana nae sana. Kwani wote wamekongamana kwamba
Banin-Nadhwiyr walidhamiria kumuua Bwana Mtume katika fursa hii. Bwana Mtume
akazitambua njama zao hizo dhidi yake, akawaonya na kuwaamuru waondoke Madinah
wenyewe kwa khiari yao, wakakataa. Baada ya kugoma kutoka Madinah, ndipo
akatangaza vita dhidi yao, akawazingira katika makazi yao kwa siku kadhaa,
mpaka akafanikiwa kuwatoa Madinah. Na hivi ndivyo Ibn Sa’ad anavyolisimulia
tukio hilo kwa ukamilifu wake: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akawapelekea mjumbe; Muhammad Ibn Maslamah kuwaambia: (Tokeni katika
mji wangu, hamtaishi nami humo na ilhali mlikusudia kufanya usaliti.
Ninakupeni muda wa siku kumi mtoke kwa khiari zenu wenyewe, atakayeonekana
baada ya kumalizika muda huo, itapigwa shingo yake {atauawa}). Mayahudi
wakaendelea kukaa kwa siku kadhaa wakijiandaa, Ibn Ubayyi akawatumia ujumbe
akiwaambia: “Msitoke katika majumba yenu na bakieni katika ngome zenu, kwani
mimi ninao jamaa zangu alfu mbili na makabila mengine ya Kiarabu. Wote hawa
wataingia pamoja nanyi katika ngome zenu na watapigana pamoja nanyi na kufa
mpaka wa mwisho wao. Na Baniy Quraydhwah na washirika wao wa Ghatwfaan
watakusaidieni”. Hubayyu Ibn Akhtwab akayatumai maneno yaliyomo ndani ya
ujumbe wa Ibn Ubayyi, akampelekea ujumbe Bwana Mtume akimwambia: “Kwa hakika
sisi hatutakoka majumbani mwetu na wewe fanya utakavyo”. Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-akapiga takbira na waislamu wakaipokea takbira yake hiyo na
akasema: “Mayahudi wametangaza vita”. Akawaendea na maswahaba wake,
akaswalia Alasiri katika uwanda (mbuga) ya Banin-Nadhwiyr. Na Sayyidina Aliy-Allah
amuwiye radhi-akibeba bendera yake na akamtawaza Ibn Ummu Maktuum kukaimu
Madinah. Walipomuona Mtume wa Allah, wakajitoma ngomeni mwao wakiwa na mishale
na mawe. Baniy Quraydhwah wakawatupa mkono wasiwasaidie (kama walivyoahidi),
na Ibn Ubayyi na washirika wao wa Ghatwfaan wakaacha kuwanusuru. Hapo wakakata
tamaa ya kunusurika, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawazingira na
kukata mitende yao. Wakasema (baada ya kuona kuwa hawana hila): Sisi sasa
tunatoka katika mji wako. (Bwana Mtume) akawaambia: “Leo siikubali kauli
yenu hiyo, lakini tokeni mkiwa na damu zenu na mali inayoweza kubebwa na
ngamia ila silaha”. Mayahudi wakatoka kwa sharti hilo, wakawabeba wanawake,
watoto na kujipakia katika ngamia mia sita]. Mwisho wa kunukuu.
Ibn Is-haq-Allah amrehemu-anasema: “Akawa mtu miongoni mwao akiibomoa
nyumba yake na kung’oa kizingiti cha mlango wake na kukipakia juu ya ngamia
wake na kuondoka nacho. Wakatoka kuelekea “Khaybar” na wengine wakaelekea
Shamu, wakamuachia mali Mtume wa Allah. Mali yote iliyoachwa ikawa ni ya Mtume
wa Allah, akawagawia Muhajirina bila ya kuwapa Answari”. Allah Taala
amelisajili tukio hili ndani ya Qur-ani Tukufu, tusome na tuzingatie: “YEYE
NDIYE ALIYEWATOA WALIOKUFURU MIONGONI MWA WATU WA KITABU (Mayahudi wa
Kibanin-Nadhwiyr) KATIKA NYUMBA ZAO (huko Madinah) WAKATI WA UHAMISHO (wao) WA
KWANZA. HAMKUDHANI YA KUWA WATATOKA (kwa nguvu zao walizokuwa nazo Madinah),
NAO WALIDHANI YA KUWA NGOME ZAO ZITAWALINDA NA (kufikwa na amri ya) ALLAH.
LAKINI ALLAH ALIWAJIA KWA MAHALI WASIPOPATAZAMIA NA AKATIA WOGA KATIKA NYOYO
ZAO (wasiweze kupigana na waislamu walipokuja kupigana nao). WAKAWA
WANAZIVUNJA NYUMBA ZAO KWA MIKONO YAO NA KWA MIKONO YA WAISLAMU, BASI ENYI
WENYE MACHO (maoni) ZINGATIENI. NA LAU KAMA ALLAH ASINGALI WAANDIKIA UHAMISHO
ANGALIWAADHIBU HAPA DUNIANI (adhabu kubwa zaidi kuliko hii), NA KATIKA AKHERA
WATAPATA ADHABU YA MOTO. HAYO NI KWA SABABU WALIMKHALIFU ALLAH NA MTUME WAKE.
NA ANAYEMKHALIFU ALLAH (Allah humtesa tu), KWANI ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU.
MTENDE WO WOTE MLIOUKATA (katika hicho kiambo cha Mayahudi) AU MLIOUACHA
UMESIMAMA VILE VILE KATIKA MASHINA YAKE. YOTE HAYA NI KWA IDHINI YA ALLAH (hapana
lawama juu yenu) NA KWA KUWADHALILISHA WAVUNJAO SHARIA”. [59:1-5]
|