|
Mwanachuoni
mwenye kitabu AL-IMTAA-Allah amrehemu-amesema: [Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alipoichukua ngawira mali ya Banin-Nadhwiyr. Alimtuma Thabit Ibn
Qaysi kuwaita Answari wote (wenyeji wa Madinah). Walipoitika wito wake,
akasimama na akamuhimidi Allah na kumsifia, kisha akawataja Answari na mema
yote waliyowatendea ndugu zao Muhajirina (wakimbizi kutoka Makkah). Yakiwa ni
pamoja na kuwahifadhi majumbani mwao na kuwapendelea zaidi katika kila kitu
kuliko nafsi zao, kisha akasema: “Ikiwa mtapenda nitagawa baina yenu na
Muhajirina mali aliyonipa Allah kutoka kwa Banin-Nadhwiyr na wao wataendelea
kuishi majumbani mwenu na kupata hisa katika mali zenu. Na iwapo mtapenda,
niwape wao na watoke majumbani mwenu”. Sa’ad Ibn Ubaadah na Sa’ad Ibn
Muaadh wakasema: Bali tuigawe kwa Muhajirina na wabakie majumbani mwetu kama
walivyokuwa. Answari wote wakasema kwa sauti moja: Tumeridhia na tumesalimu
amri ewe Mtume wa Allah! Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:
“Ewe Mola wa haki wee! Warehemu Answari na watoto wa Answari”. Halafu
akaigawa mali aliyopewa na Allah baina ya Muhajirina bila ya kuwapa kitu
Answari. Isipokuwa watu wawili tu miongoni mwao waliokuwa wahitaji; Sahli Ibn
Hunayf na Abu Dujaanah, hawa aliwapa kwa sababu ya uhitaji mkubwa waliokuwa
nao. Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawagawia Muhajirina mafungu yenye
kukidhi haja katika mali ya Banin-Nadhwiyr]. Na wakasilimu watu wawili katika
Banin-Nadhwiyr kwa sharti ya kurejeshewa mali yao, wakasilimu na wakarudishiwa
mali yao.
Vita
hivi vya Banin-Nadhwiyr vilikuwa katika mwezi wa Mfunguo mosi (Shawwal), mwaka
wa nne wa Hijrah (June 625 A.D). Allah Taala akashusha Suratil-Hashri (59)
kufuatia vita hivi, akavitolea hoja ndani yake vitendo vilivyotendwa na
waislamu na kuonwa kuwa ni uhalifu wa kivita. Kuanzia kukata kwao mitende ya
mahasimu wao na kuwazingira mpaka wakaweza kuwatoa katika miji yao. Na Allah
akawakamia wanafiki waliowaunga mkono makafiri na kuwachochea watu dhidi ya
Allah, Mtume wake na waumini. Na Allah akamtakasia Mtume wake mali
aliyoichukua kutoka kwa maadui hawa. Kwa hivyo ikawa ni yake khasa, akawapa
aliowapa sehemu katika mali hiyo na akabakisha sehemu nyingine. Na akawa
anaendesha kilimo katika ardhi yao ya mitende ambayo sasa iko chini ya milki
yake. Akawa anajiwekea yeye na familia yake akiba ya chakula cha mwaka mzima
kutokana na shayiri na tende zinazovunwa katika ardhi hiyo. Na sehemu ya
mavuno iliyobaki baada ya kutoa chakula chake aliitenga kwa ajili ya farasi,
kununulia silaha na zana nyingine za vita. Pia sadaka alizokuwa akitoa kuwapa
mafakiri miongoni mwa maswahaba wake na wageni mbalimbali waliomfikia
zilitokana na mavuno ya ardhi hii.
IV/.
KUWAADABISHA WAASI.
Vita
vya Banin-Nadhwiyr vilikuwa ni hatua endelevu muafaka na pigo adabishi
lililowapata kwa pamoja mayahudi na wanafiki. Likaivunja nguvu yao na kuzijaza
nyoyo zao khofu na kuwafanya wanafiki kuacha kuwabeza waislamu na kueneza
uvumi na fitna baina yao. Na Baniy Quraydhwah wakabakia katika ardhi yao
wakiwa katika hali ya khofu na hadhari kubwa. Mji
wa Madinah ukawa shwari kwa kipindi ambacho Mtume-Rehema na Amani zimshukie-
na maswahaba wake wakaweza kuzielekeza juhudi zao zote katika kuyaadabisha
makabila mengine ya mabedui waliokuwa na choko choko dhidi yao.
SOMO
LA PILI-VITA VYA DHAATIR-RIQAA.
Katika
mwezi wa Jumaadal-Uula (Mfunguo nane) wa mwaka huu huu, Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-alitambua kuwa Baniy Muhaarib na Baniy Tha’alabah
wanajiandaa kuja kumpiga. Akawatokea na kikosi cha watu mia saba,
akamtawalisha Sayyidina Uthman Ibn Affaan kuendesha shughuli za utawala
Madinah. Mtume wa Allah huyoo akaenda mpaka akapiga kambi “Nakhla”-hili ni
eneo lililopo Najid katika ardhi ya Ghatwfaan. Hapo akakutana na kundi kubwa
miongoni mwa mahasimu wake, makundi mawili haya; waislamu na makafiri
yakakurubiana, lakini hayakuzuka mapambano baina yao. Yakaogopana kiasi cha
kumlazimisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuwaswalisha waislamu
swala ya khofu. Ikawa unapoingia wakati wa swala, huliswalisha kundi moja la
maswahaba wake na kundi jingine likabakia limesimama likiwalinda dhidi ya
shambulio la kushtukiza la adui. Hata likesha kuswali lile kundi la kwanza,
huja likasimama uelekeo wa adui na kumpa Mtume fursa ya kuliswalisha lile
kundi lililokuwa likilinda. Na vita hivi vimeitwa kwa jina hili la “Dhaatur-riqaa”,
kwa sababu mawe yaliyokuwepo eneo hili yaliidhoofisha miguu yao. Hali hii
ikawapelekea kufunga vitambara (Riqaa) miguuni mwao ili kuepuka kuumizwa na
mawe hayo.
I/.
PICHA/SURA YA IKHLASWI YA KWELI.
Katika
vita hivi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipiga kambi kwenye
mojawapo ya njia za majabalini jangwani. Akasema: “Nani atakayeshika zamu ya
kutulinda katika usiku wetu huu?” Wakajitokeza watu wawili kuifanya kazi
hiyo, mmoja akiwa ni Muanswari na mwingine Muhajiri, wakasema: “Sisi ewe
Mtume wa Allah tutaifanya kazi hiyo”. Mtume akawaambia: “Basi kuweni
mlangoni mwa njia/bonde”. Watu wawili hawa walipotoka kuelekea mahala
walipoelekezwa na Mtume, yule Muanswari akamwambia mwenziwe Muhajiri: “Ni
sehemu ipi ya usiku unayopenda nikutoshelezee (nianze kushika zamu mimi); ya
mwanzo au ile ya mwisho?”. Mwenzake akamjibu: “Nitoshelezee sehemu ya
mwanzo ya usiku”. Yule Muhajiri mwenye zamu ya mwisho wa usiku akalala na
yule Muanswari mwenye zamu yake akainuka na kuanza kuswali suna za usiku.
Akiwa ndani ya swala akaja mushriki mmoja akifuatilia nyendo za waislamu,
alipomuona yule Muanswari akatambua kwamba yeye ni mmojawapo wa walinda doria
wa waislamu. Akamrushia mshale ukampata, yule Muanswari akauchomoa mshale ule
mwilini mwake na kuutupa chini na akaendelea na swala yake. Adui akatupa
mshale wa pili nao ukampata sawia kama ule wa kwanza, nae akauchomoa na
kuutupa na kuendelea kuswali. Adui akatupa mshale wa tatu nao vile vile
ukampata, akauchomoa na kuutupa chini, kisha akarukuu na kusujudu. Halafu
akamuamsha mwenzake na kumwambia: “Amka ushike zamu nimekwishapigwa sijiwezi”.
Yule Muhajiri akavumburuka na kusimama wima, adui alipowaona akatambua kuwa
sasa wamedhamiria kupambana nae, huyoo akatimua mbio. Muhajiri alipoona damu
inayomtoka nduguye Muanswari akasema: “Sub-haanallah! Kwa nini hukuniamsha
mwanzo tu alipoanza kukushambulia?” Akajibu: “Nilikuwa nikiisoma
sura fulani, kwa hivyo
sikuweza kuikata mpaka nimalize kuisoma, aliponifululizia ndipo nikarukuu na
kukuamsha. Na ninamuapia Allah lau si kupoteza doria aliyoniamrisha Mtume wa
Allah kulinda, adui angelizikata pumzi zangu (angeniua) kabla mimi sijaikata
sura niliyokuwa nikiisoma”. Pima mwenyewe mpendwa msomaji wetu ni ikhlaswi
ya namna gani waliyokuwa nayo maswahaba wa Mtume wa Allah-Allah awawiye radhi.
Ni jinsi gani walivyokuwa wakitaladhadhi wawapo ndani ya ibada kiasi cha
kutohisi machungu yawapatayo. Eeh tu wapi sisi leo na hali hiyo?!
II/.
SURA YA UAMINIFU NA UKWELI JUU YA ALLAH:
Na
katika vita hivi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikwenda kando peke
yake kujipumzisha chini ya mti kutokana na uchovu wa joto shadidi (kali) la
jangwani. Akautundika upanga wake kwenye mojawapo ya matawi ya mti ule,
mmojawapo wa maadui akajipenyeza bila ya kuonekana mpaka akamfikia Mtume akiwa
amelala. Akautwaa upanga wa Mtume wa Allah akauchomoa kutoka kwenye ala yake,
Mtume akazinduka kutoka usingizini, tahamaki huyo ni mtu amemsimamia kichwani,
upanga mkononi mwake akimwambia: “Ni nani atakayenizuia nisikuue?” Mtume
akasema: “Allah”, kwa kauli hiyo ya Mtume, upanga ukamuanguka adui yule na
kutwaliwa na Mtume. Upanga ulipotua mkononi mwake, Bwana Mtume akamuuliza
swali lile lile alilomuuliza yeye wakati akiumiliki upanga: “Ni nani
atakayenizuia nisikuue?” Akajibu: “Kuwa mchukuzi mwema (wa upanga huo)”.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamsamehe, kwa wema huu aliotendewa
na mtu ambaye yeye alitaka kumuua na kisha nae akapata nafasi ya kumuua na
akaamua kumsamehe. Mtu huyu akasilimu, kisha akawaendea jamaa zake na kuwataka
na wao wawe waislamu, akawaambia: “Nimekujieni kutoka kwa mbora wa watu”.
|