|
Mnamo mwezi wa Shaaban wa
mwaka huo huo wa tano Hijiria (Desemba 626 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-alitoka kuwaendea Banil-Muswtwalaq. Hawa ni katika ukoo wa
Khuzaa, kiongozi wao akiwa ni Al-Haarith Ibn Abiy Dhwiraar. Khabari ilimfikia
Bwana Mtume ya kwamba wao wanawakusanya watu kwenda kumpiga, kabla hawajatoka
yeye akawatokea na kundi kubwa la maswahaba wake. Kwa mshangao wa wengi, wengi
miongoni mwa wanafiki ambao hawakuwa na mazoea ya kutoka kwenda vitani nao pia
walitoka pamoja na jeshi hili wakisukumwa na tamaa ya kupata ngawira. Safari
hii Mtume alitoka na wakeze wawili; Bi. Aysha na Bi. Saudah-Allah awawiye
radhi wao na wote wakeze Mtume wa Allah. Bwana Mtume akaenda zake mpaka
akalifikia eneo lenye maji liitwalo “Al-Marsii”, hapo ndipo alipokutana na
Al-Haarith akiwa pamoja na watu wake. Makundi mawili haya; kundi la Mtume na
lile la Al-Haarith yakajipanga tayari kuanza mapambano. Makundi mawili haya
yalipoonana ana kwa ana, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamuamrisha
Sayyidina Umar kuwatolea wito watu wale ya kwamba: “Semeni: Laa Ilaaha
Illal-laahu {hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah}, mtazizuia nafsi na
mali zenu kwa tamko hilo”. Wakakataa kulitamka tamko hili litakalowafanya kuwa
waislamu, makundi mawili haya yakaanza kurushiana mishale kwa kitambo kidogo.
Halafu tena ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawaamrisha
maswahaba wake kuwashambulia, wakawa shambulia ushambulizi wa mtu mmoja.
Wakawaua watu kumi miongoni mwao na kuwateka wengine, hapana hata mmoja wao
aliyeweza kuponyoka na kukimbia. Waislamu wakapata ngawira ya ngamia alfu
moja, mbuzi alfu tano na kuwachukua mateka watu wa kaya mia mbili; wanamume,
wanawake na watoto.
Miongoni mwa mateka hawa alikuwemo Juwayriyah Bint Al-Haarith;
binti wa kiongozi wa Banil-Muswtwalaq. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akataka kulivutia kwenye Uislamu kabila la Juwayriyah, akamuacha
huru na kisha akamuoa. Kuolewa kwake bibi huyu na Mtume wa Allah kukawa ni
baraka, neema na faraja kwa ukoo wake mzima. Kwani waislamu waliwaachilia huru
mateka wao waliokuwa wakiwashikilia kwa ajili ya kuwatukuza na kuwaheshimu
wakweze Mtume. Na uachaji huru huu wa mateka ukawa ni sababu ya wengi wao
kusilimu.
II.
WANAFIKI WAJARIBU
KUCHOCHEA FITNA BAINA YA WAISLAMU.
Vita vya Banil-Muswtwalaq
vilikuwa ni vita vilivyopangwa barabara katika kila hatua yake na waislamu
walikuwa na ari na pupa ya kufurahikia kile walichoandikiwa na Allah katika
vita hivi. Yaani kuwezeshwa kupigana na kisha kuibuka na ushindi lau si
wanafiki kutaka kuitibua furaha hii. Wanafiki hawa waliitumia fursa ya matukio
mawili yaliyotokea baada ya vita hivi. Matukio ambayo yalistahiki kupishwa
yapite kama yanavyopita matukio mengine ya kawaida bila ya kuvuta hisia za mtu
ye yote au kumuacha akishangaa. Lakini kwa tabia ya wanafiki hawakuridhika
kuyaacha matukio haya kupita hivi hivi tu, wakaamua kulitumia tukio la mwanzo
kuchochea na kupalilia fitna. Fitna ambayo ilikurubia kuufagilia mbali umoja
baina ya Muhajirina na Answari. Na kulitumia tukio la pili kuinajisi na
kuichafua twahara ya nyumba ambayo ni toharifu na takatifu kuliko nyumba zote.
Nyumba yenye heshima, daraja na cheo kitukufu katika nyoyo za waislamu.
Ama tukio la mwanzo lilisababishwa na kugombea maji baina ya
kibarua wa Sayyidina Umar Ibn Al-Khatwaab na mshirika wa Khazraj. Wakazozana
kwa ajili ya maji na hatimaye kupigana, yula mshirika wa Khazraji akapiga
ukelele kuomba msaada kutoka kwa washirika wake: “Enyi kusanyiko la Answari!”
Kibarua kusikia hivyo nae akapiga ukelele kuomba msaada, akaita: “Enyi
kusanyiko la Muhajirina!” Washirika wa kila mmoja wa wagomvi hawa wakauitika
ule wito wa msaada uliotolewa, wakatoka walio wepesi miongoni mwao kuja
kuangalia kulikoni na kutoa msaada ulioombwa. Makundi yote mawili yakakutana
na kukurubia kuzuka mapigano baina yao na kuamka fitna baina ya Muhajirina;
washirika wa kibarua, na Answari; washirika wa mshirika wa kabila la Khazraji.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliposikia zogo hilo akatoka nje
haraka akisema: “Ni ya nini hii miito ya Kijahilia?” Wakampasha khabari nzima
inayojiri hata kusababisha zogo hilo alilolisikia, Mtume akapiga ukelele wa
ghadhabu: “Hebu liacheni neno hili (la ukabila), kwani linanuka na kutoa
harufu ya uvundo”. Kwa kauli yake hii, Bwana Mtume akaweza kuyatuliza
makundi mawili yale ya waislamu na hali ikarejea kuwa shwari. Mtume wa Allah
akamgeukia yule mtu aliyepigwa katika ule mzozo wa maji, akazungumza nae mpaka
akakubali kusamehe, kwa njia hii moto wa fitna ulioanza kuwaka ukazimika na
kuashiria kuhizika, kufedheheka na kushindwa kwa maadui; wapikaji wa fitna
hii. Kuzimika na kuruka patupu kwa fitna hii hakukumfurahisha mpishi mkuu wa
fitna hii; Abdullah Ibn Ubayyi. Kuzimika kwa cheche za moto huu kabla ya
kulipua moto mkubwa kama alivyotarajia na kufa kwa fitna hii kabla ya
kuusambaratishia mbali umoja na mshikamano wa waislamu kama alivyotamani.
Jambo hili lilimkera na kumuudhi upeo Ibn Ubayyi, khasa pale ilipomfikia
khabari ya namna suala la kibarua na mshirika lilivyomalizwa na Mtume wa Allah
kwa amani na salama. Akaanza kuwaambia wafuasi wake: “Wallah, sijapatapo
kuuona udhalili kama huu wa leo! Wametukimbiza na kutuzonga katika mji wetu na
wamekosa hata shukrani kwa wema wetu tuliowatendea! Wallah, mimi sijioni na
hii mikanzu ya Makurayshi ila kama vile alivyosema msemaji: Mnenepeshe mbwa
wako akule! Tukirudi Madinah, mwenye utukufu (Ibn Ubayyi) atamfukuza mnyonge
(Mtume)”. Kisha akawaelekea jamaa zake waliohudhuria pale akiwalaumu na
kuwatupia maneno makali: “Haya ndio mliojitakia wenyewe, mmewahalalishia mji
wenu, mkawakaribisha majumbani mwenu na mkawasaidia katika mali zenu mpaka
wakajikwasia (wakawa matajiri). Wallah, lau mngeliwazuilia vilivyomo mikononi
mwenu, bila ya shaka wangelihama. Basi msitoe mali kuwapa wafuasi wake ili
waondokelee mbali”.
|