Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

III) MTUME NA UCHUNGAJI KONDOO

Faida

Historia inatuambia kuwa kazi ya mwanzo kabisa iliyofanywa na Bwana Mtume ilikuwa ni uchungaji wa kondoo na mbuzi. Aliamua kufanya kazi hii ile aweze kupata pesa za kujikimu mwenyewe na kumpunguzia Ami yake Abdul Mutwalib ukali wa maisha. Hivyo Mtume – Rehma na Amani zimshukie – akaanza kuchunga kondoo na mbuzi wa watu wa Makkah kwa ujira mdogo aliokuwa akipewa. Kituo cha kazi yake hii ilikuwa ni "Ajyaad"; hii ni jangwa lililokuwa nje kidogo ya mji wa Makkah, hapo ndipo alipokuwa akiwachunga wanyama hao.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ana hekima kubwa sana katika kuifanya shughuli hii ya uchungaji kuwa ndio kazi ya mitume. Wanayaanza maisha yao kwa kuchunga wanyama na kuyahitimisha kwa kuwachunga binadamu wenziwao. Amesimulia swahaba Jaabir bin Abdillah –Allah amuwie Radhi – akisema : [Tulikuwa pamoja na Mtume – Rehma na Amani zimshukie – tukichuma matunda ya mabivu ya mpili mpili tawa, akasema "Chumeni (matunda) yaliyo meusi kwani ndiyo matamu zaidi, mimi nilikuwa nikiyachuma wakati nilipokuwa ninachunga kondoo na mbuzi". Tukamuuliza : Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ulikuwa ukichunga kondoo na mbuzi ? Akajibu "Ndio na hakuna mtume yeyote ila alichunga"]

Kwa hiyo uchungaji wa kondoo ni alama nyingine inayothibitisha utume wa Nabii Muhammad. Mwenyezi Mungu amejaalia uchungaji wa wanyama kuwa ni chuo cha kutoa mafunzo ya uchungaji na uongozi kwa mitume wake. Wakiweza kuwachunga kondoo na mbuzi ambao hawa ni wanyama wanyonge zaidi kuliko wengine, nyoyo zao zitatawaliwa na huruma na upole. Wakifuzu ma kuhitimu katika chuo hiki kinachotoa mafunzo ya uchungaji na uongozi, ndipo hupewa shahada zao kwa kukabidhiwa jukumu gumu na zito la kuwachunga binadamu wenziwao. Kama walivoweza kuwastahamilia wanyama ndivyo wanavyotakiwa kuwavumilia wanadamu wenzao wenye tabia ngumu zilizosheheni ukukutavu wa moyo. Tunasoma ndani ya Qurani Tukufu juu ya ugumu wa nyoyo : "KISHA NYOYO ZENU ZIKAWA NGUMU BAADA YA HAYO (yote); HATA ZIKAWA KAMA MAWE AU NGUMU ZAIDI (kuliko mawe) … [2:74]

Ni watu kama hawa ndio ambao Bwana Mtume anapewa jukumu la kuwalea na kuwachunga. Kwa kuwa alihitimu vema chuoni, alifaulu kuifanya kazi yake hii ngumu kwa ufanisi mkubwa, ingawa ilimgharimu subira ya hali ya juu. Mwenyezi Mungu anamtunukia Mtume wake shahada ya kufaulu, pale aliposema : "BASI KWA SABABU YA REHEMA ITOKAYO KWA ALLAH UMEKUWA LAINI KWAO (Ewe Muhammad) NA KAMA UNGEKUWA MKALI NA MWENYE MOYO MGUMU BILA SHAKA WANGALIKUKIMBIA (usingelimpata hata mtu mmoja) …." [3:159]

Hii ndiyo natija na matunda ya uchungaji wa wanyama na hiyo hekima yake kwa mukhtasari.

 

SOMO LA SITA :

i) SAFARI YA PILI YA SHAMU

Bi Khadijah binti Khuwaylid, Bibi mkureshi alikuwa ni mwanamke mwenye tabia njema, anayekubalika na kuheshimika katika jamii ya watu wa Makkah. Mbali na sifa hizi, Bibi huyu alikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa wa mji wa Makkah, alipenda sana kufanya biashara. Kutokana na kuona mbali na upevu wa akili yake alikuwa akiizalisha mali yake kwa kuwaajiri watu. Aliwapa mali wakaiuze kwa mkataba na kuwapa sehemu ya faida iliyopatikana.

Habari za tabia murua, uaminifu na ukweli wa Bwana Mtume – Rehma na Amani zimshukie – zilipoyagonga masikio ya Bi Khadija; akajawa na raghba ya kutaka kumuhusisha mtu huyu mwaminifu na mkweli katika biashara yake. Akamtumia salamu za kumuita naye Bwana Mtume akaitikia mwito. Bi Khadijah akamueleza alilomuitia ya kwamba amfanyie biashara naye atampa sehemu kubwa ya faida itakayopatikana. Bwana Mtume akakubali na mara moja akaianza kazi yake hii mpya ya biashara badala ya ya ile kazi yake ya kwanza ya uchungaji. Ikumbukwe wakati huo Mtume alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano. Akatoka kuelekea Shamu katika msafara wa biashara akiambatana na Bwana Maysarah, msaidizi aliyepewa na Bi Khadijah. Wakafika Shamu, wakafanya biashara wa kuuza na kununua, wakapata faida kubwa sana kuliko iliyokuwa ikipatikana huko nyuma. Bwana Maysarah alishuhudia katika safari yake na Bwana Mtume tabia njema, ukweli na uaminifu wa Mtume na hivi ndivyo vilivyokuwa vigezo vya ufanisi katika biashara yao. Kadhalika aliona miujiza mingi iliyoonyesha kwamba Muhammad ndiye Mtume mtarajiwa aliyebashiriwa katika vitabu vitakatifu. Miongoni mwa miujiza hiyo ni pale Bwana Mtume alipopumzika chini ya mti uliokuwa karibu na kibanda cha Padri Nestori. Padri huyu baada ya kumuona Mtume amepumzika chini ya mti ule akamuendea Maysarah na kumuuliza khabari za Mtume. Bwana Maysara akamueleza Padri Nestori kila alilolijua juu ya Mtume kwa kulisikia ama kulishuhudia yeye mwenyewe. Hapo ndipo Padri Nestori akamwambia Bwana Maysara : "Hajapumzika chini ya mti huu ila ni Mtume (Kwani huu ni mti wa mitume) basi (nakuusia) uhiifadhi siri hii (ili mayahudi wasimdhuru)". Pia Maysarah alikuona wakati wa jua kali la utosi kiwingu kikimfunika Bwana Mtume kumkinga na jua.

 

middle east

ii) MTUME AMUOA BIBI KHADIJAH :

Mara tu baada ya Mtume kurudi kutoka Shamu aliiwasilisha mara moja faida kubwa iliyopatikana kutokana na biashara kwa Bi Khadijah. Bi Khadijah aliifurahia sana faida hiyo ambayo hakuwahi kuipata kutoka kwa watu wengine aliowaajiri kabla ya Mtume Muhammad. Kwa kigezo hiki Bi Khadijah akazidi kuthibitisha khabari zilizomfikia juu ya uaminifu na ukweli wa Nabii Muhammad, ukiachilia mbali yale aliyoelezwa na mtumishi wake Maysarah ambaye alikuwa msaidizi wa Mtume katika safari yao ya Shamu. Sifa zote hizi njema zikamteka Bi Khadijah na kujikuta akimpenda Mtume na kutamani awe na mume mwenye sifa njema kama Nabii Muhammad. Akamtuma mshenga kwa Mtume amuelezee nia yake ya kutaka kuolewa naye. Ni vema ikakumbukwa kwamba wakati huo Bi Khadijah alikuwa ana umri wa miaka arobaini na Bwana Mtume alikuwa amefikia umri wa miaka ishirini na tano. Bwana Mtume kwa kuzingatia utukufu, heshima na tabia njema za Bi Khadijah bila ya kusita akakubali kumuoa bibi huyu. Ndipo tena mipango na taratibu za harusi zikaanza na hatimaye wawili hawa wakawa ni mke na mume. Ndoa hii ilifungwa miezi miwili tangu Mtume kurejea kutoka Shamu. Bibi huyu ameishi na Mtume kwa karibu robo karne yaani kipindi kisichopungua miaka ishirini tano. Kwa kipindi hiki chote Mtume hakumuolea Bibi huyu mke mwenza, naye ndiye mkewe wa kwanza. Bi Khadijah alimzalia Bwana Mtume watoto sita, wawili wa kiume nao ni Kasim na Abdallah na wanne wa kike nao ni Zainabu, Rukia, Ummu Kulthum na Fatimah. Ama Ibrahimu, huyu alizaliwa na Bi Mariah Mqibtwi wa Misri. Ni vema tukakumbuka kuwa Bi Khadijah kabla ya kuolewa na Mtume alikuwa ameolewa na Bwana Abu Haalah ambaye alimfia. Hivi ndivyo Bwana Mtume alivomuoa Bi Khadijah – Allah amuwie Radhi mama yetu huyu-.

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI : kuwa kama ambavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu alikuwa akiwaandaa mitume wake kubeba jukumu la kuuongoza ummah, ni kama hivi na sisi tuna jukumu kubwa la kuwalea na kuwaandaa watoto wetu. Tuwaandae watoto wetu kubeba jukumu zito la kuulinda na kuutetea uislamu. Tuwaandae kuwa masheikh/viongozi watakaochukuwa dhima na dhamana ya kuhakikisha Uislamu unatawala ulimwengu huu. Tuwaandae kuwa askari watakaokuwa tayari kuulinda na kuutetea Uislamu kwa gharama yeyote ile iwayo, hata ikibidi roho zao zitoke, basi wawe tayari kujitoa muhanga. Bwana Mtume – Rehma na Amani zimshukie – anatuagiza : "Wafundisheni watoto wenu kuogelea na kutupa mishale/mikuki na kasi bora na kwa mwanamke muumini nyumbani kwake ni kufuma"

TUJIFUNZE NA TUKUBALI : kuwa ukweli na uaminifu ndio siri kubwa ya mafanikio katika biashara bali katika kila kitu. Bwana Mtume – Rehma na Amani zimshukie – anatuambia "Mfanyabiashara muaminifu mkweli mwislamu atakuwa pamoja na mashahidi siku ya kiyama" Ibn Majah na Al-Hakim kutoka kwa Ibn Umar. Ewe mfanyabiashara mche Mwenyezi Mungu katika biashara yako, usipunje wala usidhulumu.

TUJIFUNZE NA TUKUBALI Kuwa tabia njema ni silaha njema maishani. TABIA NJEMA ni urimbo umnasao kila ndege. Ni kwa sababu hiyo ndiyo Bwana Mtume – Rehma na Amani zimshukie – anatuambia "Mkamilifu zaidi wa waumini ni yule (aliye) mzuri wao kitabia" Ahmad, Abu Dawood, Ibn Hibban na Al-Haakim kutoka kwa Abu Hurayrah


Forum | Guestbook | Tuandikie |