|
Ama tukio la pili ni lile
tukio la uzushi na uwongo dhidi ya Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-kwa jambo
ambalo Allah alimtakasa nalo. Tukio hili linaanzia pale ambapo Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa njiani kurejea Madinah akitokea kwenye
vita vya Banil-Muswtwalaq. Mtume alipiga kambi njiani usiku ili watu wapumzike
na kisha kuendelea na safari baada ya mapumziko hayo mafupi. Bi. Aysha akatoka
nje ya kambi kwenda kukidhi haja yake akiwa peke yake, njiani kikamuanguka
kidani chake. Akarudi tena kule alikotoka kukitafuta, akakitafuta mpaka
akachelewa kurudi kambini. Ikumbukwe kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alikuwa na haraka ya kufika Madinah, kwa ajili hii akaamuru kambi
ivunjwe na safari iendelee. Alitoa amri hii bila ya yeye wala ye yote
miongoni mwa maswahaba kujua kuwa Bi. Aysha hayupo. Wakakibeba kibanda chake
na kukipakia juu ya ngamia wake wakidhania kuwa yumo ndani yake na haraka
haraka wakaondoka, huku wakimuacha nyuma bila ya kujua.
Bi. Aysha baada ya
kukitafuta kidani chake kwa kitambo na kukipata, akarejea kambini na hapo
hakumkuta hata mtu mmoja. Basi akaamua kubakia hapo hapo akiwa na yakini
kwamba hapana budi watamrudia tu pale watakapotambua kuwa hayupo. Akakaa hapo
mpaka usingizi ukamshinda, akalala. Nyuma kabisa ya msafara alikuwepo mtu
mmoja aitwaye Swafwaan Ibn Muatwali, huyu alikuwa akiufuatia msafara kwa nyuma
kwa ajili ya kuokota kitu/mzigo uliosahauliwa na msafara. Akiwa katika
harakati zake hizi akamuona Bi. Aysha na kusema: “Innaa Lillaahi wa Inna
Ilayhi Raajiuun” – hakika sisi sote ni milki ya Allah na kwake yeye
tutarejea”. Akaendelea kusema maneno hayo mpaka Bi. Aysha akazinduka kutoka
usingizini, alipoamka akampelekea ngamia wake nae akampanda. Akaondoka
Swafwaan akimvuta ngamia aliyembeba Bi. Aysha mpaka akaingia nae Madinah
majira ya mchana wa jua kali. Abdullah Ibn Ubayyi alipomuona akauliza: “Huyo
ni nani?”, akaambiwa: “Ni Bi. Aysha huyo”. Kusikia hivyo akasema: “Loh! Mke wa
Mtume wenu amelala na mwanaume mpaka asubuhi, halafu tena hawara yake huyo
akaja akimkokota juu ya ngamia wake!” Hapo tena midomo ya wanafiki ikapata la
kubwabwaja, wakawa hawana la kuzungumza ila suala lile la uzushi dhidi ya Bi.
Aysha mkewe Mtume kwa upande mmoja na Swafwaan kwa upande wa pili. Mji mzima
wa Madinah ukazizima kwa khabari hii ya uongo na uzushi mtupu mpaka pale wahyi
uliposhuka kumtakasa na uchafu aliosingiziwa. Wahyi ukawakadhibisha hawa
waliouzua uzushi huu, ukawafedhehesha na kuwakamia kupata adhabu kali kama
jazaa ya uovu wao huo.
III.
MAZINGIRA YA TUKIO HILI
LA UZUSHI.
Kwa kweli, tukio hili kwa
dhati yake lilikuwa ni suala/jambo la kawaida tu ambalo halikustahili kuamsha
hisia za tuhuma au shaka. Kwani halikuzidi katika mazingira yake juu ya kwamba
mwanamke mwenye heshima ameachwa na msafara bila yeye wala wao kujua. Akakutwa
njiani na mtu anayeufuatia msafara kwa nyuma kama ilivyokuwa ada, huyu
akamuweka katika hifadhi yake mpaka akamrejesha kwake. Kitendo hiki
alichomtendea mwanamke huyu ni kitendo cha mtu anayetekeleza wajibu wake kwa
kutambua kuwa ni wajibu wake kufanya hivyo. Na kama haikuwa ni wajibu basi
haipungui kuwa ni murua unaomsukuma mtu karimu kutoka ndani ya uvungu wa moyo
wake kuutenda. Na katika hali zote mbili hizi, hakukustahiki kuwepo na
ukumbi/jukwaa la shaka katika kadhia hii ya mwanamume karimu mwenye murua na
mwanamke mtukufu mwenye staha. Kwa sababu hili ni suala la kimaumbile
linalosukumwa na mazingira ya utu wa kibinadamu katika suala zima la
kusaidiana katika shida.
Tukirudi nyuma tunamkuta
Bibi huyu mtukufu wakati anahama Makah kwenda zake Madinah, hakuambatana na ye
yote zaidi ya mwanawe mchanga wa kiume. Uthman Ibn Twalhah - ambaye hakuwa
muislamu bali mushriki – murua haukumpa hata kidogo kumuacha mwanamke na mtoto
mchanga peke yao jangwani. Akasuhubiana nae katika kipando (mnyama) chake
mpaka akamfikisha Madinah, halafu ndipo akageuza na kuelekea Makkah alikokuwa
akienda wakati anakutana na Bibi huyu. Katika hili hapana hata mtu mmoja
katika wakazi wa Madinah aliyethubutu kufungua kinywa chake kusema pamoja na
ukweli kwamba Uthman bado alikuwa ni mushriki na adui wa waislamu. Na pia
pamoja na ukweli kwamba safari hii ilikuwa ni ya masafa marefu na hivyo kutoa
mwanya na fursa ya kutosha kwa mwenye kutaka kuutumia mwanya/fursa hiyo
kufanya alitakalo. Kwa hakika na ukweli haya yote yalijiri kutokana na ule
ukarimu na silka ya Kiarabu ambayo inamuwajibishia mwanamume ye yote kumuhami,
kumuhifadhi na kumlinda mwanamke anapokuwa hana wa kumuhami hata kama mwanamke
huyo ni katika watu duni madhalili. Haya ni vipi basi itakuwa na ilhali Bi.
Aysha ni mke wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na isitoshe ni mzawa
wa nyumba ya Abu Bakri yule msadikishaji! Hiyo ni nyumba ambayo haikujulikana
kwa machafu katika zama za Jahilia, vipi unafikiri ndugu msomaji itakuwa
nyumba hiyo katika kipindi hiki cha nuru ya Uislamu! Ni vipi utafanyika uchafu
na ilhali Swafwaan ni mtu mwenye imani thabiti kwa Allah na Mtume wake na
anaifuata kikamilifu misingi ya Uislamu ambayo inakataza maovu na machafu?! Na
vipi itakuwa na ilhali zaidi ya yote hayo, yeye ni Muarabu mwenye damu ya
silka na ukarimu wa Kiarabu na murua wao?! Na je, haikutoshi kuwa yeye ni
muumini anayeamini kwa mujibu wa imani yake kuwa wake za Mtume wake ni mama
zake?!
IV.
MFUNDO WA IBN UBAYYI NDIO
ULIOKUWA SABABU KHASA YA UZUSHI NA URONGO HUU.
Lakini hali ilivyo, ni
mfundo, hasadi na chuki vilivyoula moyo wa Abdillah Ibn Ubayyi na kuujaza
ghadhabu dhidi ya Uislamu na Mtume wake ndivyo vilivyomsukuma kutunga na
kuzua uzushi na uongo huu duni. Ibn Ubayyi alirudi katika safari hii akiwa
ameghadhibika na kuungua moyo kwa sababu ya kuruka patupu vitimbi vyake na
kumpelekea kupatwa na udhalili na unyonge. Akaingia Madinah na ilhali nafsi
yake ikichemka na kutokota ghadhabu na chuki dhidi ya Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie. Akawa anaizengea fursa itakayomtua mzigo thakili (mzito) wa
chuki na ghadhabu iliyomo nafsini mwake. Alipowaona Bi. Aysha na Swafwaan
wakirejea peke yao Madinah, akaona hakuna fursa nzuri zaidi ya kuzusha uzushi
na uvumi kuliko hiyo. Na kuwasha moto wa fitna ambao alishindwa kuuwasha baina
ya Muhajirina na Answari katika lile tukio la kibarua na mshirika wa Khazraji.
Akaanza kuuachilia ulimi wake katika kumsingizia Bi. Aysha machafu ili kutia
chuki baina ya Mtume na mtu wake wa karibu zaidi; Abu Bakri. Au pengine
atafanikiwa kuwatia shaka waislamu kuelekea utukufu wa Mtume wao au kuzusha
ghasia na magomvi baina ya jamaa zake Khazraji na waislamu wengine. Kwa kweli
matukio na mazingira ya msafara huu yalikuwa yakihitajia haraka na ndio maana
mwendo wa jeshi hili wakati wa kurudi ulikuwa una mshindo mkuu. Kwa sababu ya
kuenea na kutangaa fitna baina ya waislamu na wafuasi wa Abdillah Ibn Ubayyi.
Na Mtume alifanya haraka ili awashughulishe watu na suala la fitna hii mpaka
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawa anamchapa mnyama wake na mjeledi ili
ampeleke mbio. Kwa hali hii, si ajabu kwa msafara kumacha Bi. Aysha katika
safari hii ya haraka ya kurejea bila ya mtu ye yote kujua kuwa hayumo ndani ya
msafara. Lakini lengo duni na uhasama mtwefu vilimpomosha Ibn Ubayyi mpaka
daraja ya chini kabisa, ndipo akaufyatua uzushi huu ambao mbele za watu wenye
uzingativu yakinifu si lo lote ila ni upuuzi mtupu tu usio na maana hata
chembe. Wakaunyakua na kuupokea uzushi na uongo huu watu wa sampuli yake;
wanafiki wenziwe na wakautapanya na kuueneza kila mahala. Mpaka masikio
yakashehenezwa nao, ndimi zikayapokea na akayazungumza asiyejua kilichojificha
nyuma ya uzushi huo.
|