|
Uzushi na uongo huu
haukupasa kujuzu hata kwa mwanamke duni tu hata awe mpumbavu kiasi gani
kuudhihirisha uchafu wake wazi wazi kiasi hicho. Na aje namna hivi katika
weupe wa mchana akiambatana na hawara yake huku watu wote wakishuhudia,
akayafichua maovu yake yaliyojificha! Na akaitangazia kadamnasi aliyoyatenda,
hata! Hili halikubaliwi na akili nyoofu; akili yenye mizani na chekeche lenye
kuchuja lenye kufaa na lisilofaa. Kwani maumbile ya mwanamke vyo vyote vile
awavyo ni kupondokea kujionyesha mzuri mbele za watu, na kujitokeza mbele yao
katika mandhari kamilifu kiasi awezavyo ili watu wasimpe mgongo. Basi je, kwa
maumbile haya ya mwanamke, inawezekana kweli kwa mama wa waumini; Aysha Bint
Sidiq aliye mfano kwa wanawake waumini kuudhihirisha uchafu huo?! Hivi ndio
kusema halikumtosha kemeo la Allah katika kauli yake iliyoelekezwa moja kwa
moja kwa wakeze Mtume: “ENYI WAKE WA MTUME! ATAKAYEFANYA MAOVU DHAHIRI
MIONGONI MWENU, ATAZIDISHIWA ADHABU MARA MBILI, NA HAYA NI SAHALI KWA ALLAH.
NA MIONGONI MWENU ATAKAYEMTII ALLAH NA MTUME WAKE NA KUTENDA MEMA TUTAMPA
MALIPO YAKE MARA MBILI NA KUMUANDALIA RIZIKI YENYE HISHIMA. ENYI WAKE WA
MTUME, NYINYI SI KAMA YE YOTE TU KATIKA WANAWAKE WENGINE (nyinyi ni wakeze
Mtume). KAMA MNATAKA (kufanya jambo la) KUMCHA ALLAH, BASI MSILEGEZE SAUTI
(zenu mnaposema na wanaume) ILI ASITAMANI MTU MWENYE UGONJWA MOYONI MWAKE
(kufanya mabaya nanyi) NA SEMENI MANENO MAZURI. NA KAENI MAJUMBANI MWENU, WALA
MSIONYESHE MAPAMBO YENU KAMA WALIVYO KUWA WAKIONYESHA MAPAMBO YAO WANAWAKE WA
ZAMA ZA UJAHILI. NA SIMAMISHENI SWALA NA TOENI ZAKAH NA MTIINI ALLAH NA MTUME
WAKE. ALLAH ANATAKA KUKUONDOLEENI UCHAFU, ENYI WATU WA NYUMBA (ya Mtume) NA
(anataka) KUKUTAKASENI KABISA KABISA. NA WATAJIENI (watu) YASOMWAYO MAJUMBANI
MWENU KATIKA AYA ZA ALLAH NA (maneno ya) HIKIMA (ya Mtume). KWA HAKIKA ALLAH
NI MJUZI WA MAMBO YA SIRI NA MJUZI WA MAMBO YA DHAHIRI”. [33:30-34]
Hivi baada ya kauli hii kali ya Allah, bado Bibi huyu mtukufu
hakuwa na khofu ya kushukiwa na adhabu ya Allah kwa kutenda tendo chafu hilo?!
Hivi ni kweli kuwa hakuchelea kuipomosha daraja na cheo hiki kitukufu
alichopewa na kukirimiwa na Allah, hata akajasiri kutenda uvundo huo?! Hivi
tunaweza kuamini kuwa hakuogopa kuichafua twahara ya nyumba hii ambamo wahyi
unashuka humo na kufunikwa na malaika?!
Ukweli unaoweza kusemwa juu ya hili ni kwamba huo ulikuwa ni
uzushi duni na ni uongo usiokubaliwa na akili, dini wala busara ya kawaida tu.
Wala haukubaliwi na mantiki ya kimazingira bali hata hali za jamii
zijapotolewa dalili alfu juu yake.
II.
QUR-ANI TUKUFU YAUBOMOA
UZUSHI HUU NA KUUFANYA KUWA NI MUHIMILI KATIKA KUWEKA SHERIA YA KULINDA
HESHIMA/HADHI YA MTU.
Kwa ajili hii Qur-ani
Tukufu haikutosheka tu na kuukadhibisha uzushi huo na kumkanushia tuhuma hizi
nzito Bibi Aysha. Bali uliyapatia dawa mazingira yake kwa pande zake zote;
tiba ya hikima pevu ambayo italinda na kuhifadhi heshima za watu. Na kuzikatia
njia ya kuongopa ndimi chafu zenye tabia hiyo chafu na kuilinda heshima na
utukufu wa jamii ya Kiislamu. Aya za Surat Nuur zimeanza kwa kuweka adhabu
kemezi kwa jarima ya zinaa na kuamuru kuitekeleza kwa wazinifu bila ya huruma.
Na kwamba adhabu hiyo itekelezwe mbele ya hadhara ili iwe ni maonyo kwao kwa
sababu hiyo ni jarima iichafuayo jamii. Na ni jarima yenye athari yenye
kuendelea katika kuifisidi jamii na kuvunja heshima na hadhi yake. Hawajasiri
kuitenda jarima hii ila wale ambao zimekhabithika nafsi zao na waliofilisika
kiitikadi. Ama waumini, hawa kwa mujibu wa imani yao na ucha-Mungu wao ni watu
walio mbali mno na jarima hii chafu: “MZINIFU MWANAMKE NA MZINIFU MWANAMUME,
MPIGENI KILA MMOJA KATIKA WAO MIJELEDI (bakora) MIA. WALA ISIWASHIKENI KWA
AJILI YAO HURUMA KATIKA (kupitisha) HUKUMU HII YA ALLAH IKIWA NYINYI
MNAMUAMINI ALLAH NA SIKU YA MWISHO. NA LISHUHUDIE ADHABU YAO (hii) KUNDI LA
WAUMINI. MWANAMUME MZINIFU HAFUNGAMANI ILA NA MWANAMKE MZINIFU AU MWANAMKE
MSHIRIKINA, NA MWANAMKE MZINIFU HAFUNGAMANI NAYE ILA MWANAMUME MZINIFU AU
MSHRIKINA. NA HAYO YAMEHARIMISHWA KWA WAUMINI”. [24:2-3]
Kisha aya zikaendelea kuilinda jamii ya Kiislamu dhidi ya
shari za watu hao mafasiki ambao husema katika heshima/hadhi za watu bila ya
kuwa na ujuzi wa wayasemayo. Na wavunjao heshima za majumba ya watu wasio na
hatia, aya zikawalazimisha kusimamisha na kutoa ushahidi wa kutinda juu ya
tuhuma zao hizo. Walete hoja zisizokubali shaka kuthibitisha ukweli wa madai
yao wanayo wazushia watu. Na wakishindwa kuleta ushahidi huo, basi wanastahiki
kupata adhabu kemezi na kuvunjiwa heshima yao mpaka waache kuchezea heshima na
hadhi za watu. Hata wanandoa wenyewe pia sheria inawalazimisha kuleta ushahidi
pale watakapo watuhumu wenziwao na uchafu huu muovu (zinaa). Wakishindwa
kufanya hivyo, basi ni wajibu wao kuyakazia madai yao hayo kwa kuleta viapo
vizito, washuhudie ndani yake kwamba wao ni wakweli katika madai yao hayo na
wala hawasemi uongo: “NA WALE WANAO WASINGIZIA WANAWAKE WATOHARIFU (kuwa
wamezini), KISHA HAWALETI MASHAHIDI WANE, BASI WAPIGENI MIJELEDI (bakora)
THAMANINI NA MSIWAKUBALIE USHAHIDI WAO TENA, NA HAO NDIO MAFASIKI. ISIPOKUWA
WALE WENYE KUTUBU BAADA YA HAYO NA WAKATENGENEZA AMALI NZURI (hao Allah
atawasamehe kwani) BILA SHAKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA
KUREHEMU. NA WALE WANAOWASINGIZIA WAKE ZAO (kuwa wamezini) NA HAWANA MASHAHIDI
ILA NAFSI ZAO, BASI USHAHIDI WA MMOJA WAO UTAKUWA NI KUSHUHUDILIA MARA NNE KWA
KIAPO CHA ALLAH: YA KWAMBA BILA SHAKA YEYE NI MMOJA WA WANAOSEMA KWELI. NA
MARA YA TANO (aape) KWAMBA LAANA YA ALLAH IWE JUU YAKE IKIWA NI MIONGONI MWA
WAONGO. NA (mke) ITAMUONDOKEA ADHABU KWA KUTOA SHAHADA MARA NNE KWA KIAPO CHA
ALLAH: YA KWAMBA (huyu mume) NI MIONGONI MWA WAONGO. NA MARA YA TANO (aape) YA
KWAMBA HASIRA YA ALLAH IWE JUU YAKE KAMA (mumewe) YU MIONGONI MWA WANAOSEMA
KWELI (na yeye mke ndiye muongo)”. [24:4-9]
Baada ya hapo ndipo aya zilipoanza kulizungumzia tukio hili la
uzushi, zikalielezea kwamba ni uzushi wa kundi ongo lililokusudia kwa uzushi
huo kueneza shari kwa waislamu. Na Allah akataka kheri kwao kwa tukio hilo na
kwamba hapana budi Allah atawaadhibu waongo hawa kwa madhambi yao hayo:
“HAKIKA WALE WALIOLETA UWONGO HUO (wa kumsingizia Bibi Aysha-mkewe Mtume-kuwa
amezini) NI KUNDI MIONGONI MWENU (ni jamaa zenu). MSIFIKIRI NI SHARI KWENU,
BALI HAYO NI KHERI KWENU. KILA MTU KATIKA WAO ATAPATA ALIYOYACHUMA KATIKA
MADHAMBI HAYO. NA YULE ALIYEJITWIKA SEHEMU YAKE KUBWA MIONGONI MWAO, ATAPATA
ADHABU KUBWA (zaidi)”. [24:11]
|