|
I.
NI WAJIBU WA WAUMINI KUWA NA DHANA NJEMA KUWAELEKEA WAUMINI WENZAO NA
WASIWE NYUMA YA UZUSHI NA UVUMI.
Hapo
ndio aya zikawapa waumini somo yenye kwenda mbali mno mafundisho yake katika
namna waliyotakiwa kuwa katika
mfano wa matuko haya yenye khatari. Ilikuwa ni wajibu wa waumini kuwadhania
vema waumini wenzao; wanaume na wanawake. Na wala wasingeliwasadiki waongo
hawa walioueneza uvumi huu mpaka walete usahidi wa kutinda katika kuthibitisha
madai yao hayo. Na wala wasingeliwasaidia wapumbavu hawa katika kueneza uwongo
wao huo mkubwa na wakazihifadhi ndimi zao kujiingiza katika hilo. Halafu aya
zikawatahadharisha kutorudia kosa kama hilo kamwe na wasiende nyendo za
kueneza uovu/machafu katika jamii yao. Kwani yote hayo ni katika jumla ya
matendo ya shetani na aya zikawakumbusha neema ya imani waliyopewa na Allah
kwa fadhila zake, neema ambayo inawapa kinga dhidi ya kunguwao. Na namna
ambavyo Allah amewasamehe makosa yao hayo na akawataka wale wenye mwendo mzuri
na hali jema kimaisha wawasamehe wale walioleta uovu kwa njia hii. Na kwamba
wasiwanyime misaada waliyokuwa wakiwapa eti kwa sababu tu ya makosa yao hayo.
“HAKIKA WALE WALIOLETA UWONGO HUO (wa kumsingizia Bibi Aysha-mkewe
Mtume-kuwa amezini) NI KUNDI MIONGONI MWENU (ni jamaa zenu). MSIFIKIRI NI
SHARI KWENU, BALI HIYO NI KHERI KWENU. KILA MTU KATIKA WAO ATAPATA
ALIYOYACHUMA KATIKA MADHAMBI HAYO. NA YULE ALIYEJITWIKA SEHEMU KUBWA MIONGONI
MWAO, ATAPATA ADHABU KUBWA (zaidi). MBONA MLIPOSIKIA (khabari) HII, WAUMINI
WANAUME NA WAUMINI WANAWAKE HAWAKUWA DHANIA WENZAO MEMA, NA KUSEMA: HUU NI
UZUSHI DHAHIRI? MBONA HAWAKULETA MASHAHIDI WANE? NA WALIPOKOSA KULETA
MASHAHIDI, BASI HAO MBELE YA ALLAH NI WAONGO. NA KAMA ISINGELIKUWA JUU YENU
FADHILA YA ALLAH NA REHEMA YAKE KATIKA DUNIA NA AKHERA, BILA SHAKA
INGELIKUPATENI ADHABU KUBWA KWA SABABU YA YALE MLIYOYASHUGHULIKIA. MLIPOUPOKEA
(uwongo huo mkawa mnautangaza) KWA NDIMI ZENU NA MKASEMA KWA VINYWA VYENU
MSIYOYAJUA NA MLIFIKIRI NI JAMBO DOGO, KUMBE MBELE YA ALLAH NI KUBWA. NA MBONA,
MLIPOSIKIA HAMKUSEMA: HAITUJUZII KUSEMA HAYA, UTAKASIFU NI WAKO (Mola wetu!)
HUU NI UWONGO MKUBWA. ALLAH ANAKUNASIHINI MSIRUDI KABISA KUFANYA MFANO WA HAYA,
IKIWA NYINYI NI WAUMINI KWELI. NA ALLAH ANAKUBAINISHIENI AYA (zake) NA ALLAH
NDIYE AJUAYE, MWENYE HIKIMA. KWA YAKINI WALE WANAOPENDA UENEE UOVU KWA WALE
WALIOAMINI, WATAPATA ADHABU IUMIZAYO KATIKA DUNIA NA AKHERA NA ALLAH NDIYE
ANAYEJUA (ya maslaha yenu) NA NYINYI HAMJUI. NA (yangetokea machafuko makubwa)
ISINGELIKUWA FADHILA YA ALLAH JUU YENU NA REHEMA YAKE NA KUWA ALLAH NI MPOLE,
MWENYE HURUMA. ENYI MLIOAMINI! MSIFUATE NYAYO ZA SHETANI, NA ATAKAYEFUATA
NYAYO ZA SHETANI (atapotea) KWANI YEYE HUAMRISHA MAMBO YA AIBU NA MAOVU. NA
LAU KUWA SI FADHILA ZA ALLAH NA REHEMA YAKE JUU YENU ASINGALI TAKASIKA
MIONGONI MWENU HATA MMOJA, LAKINI ALLAH HUMTAKASA AMTAKAYE, NA ALLAH NI MWENYE
KUSIKIA (na) MWENYE KUJUA. NA WASIAPE WALE WENYE MWENDO MZURI (wa dini) NA
WENYE WASAA (katika maisha yao) MIONGONI MWENU (wasiape kujizuia) KUWAPA WALIO
JAMAA NA MASIKINI NA WALIOHAMA KWA NJIA YA ALLAH. NA WASAMEHE NA WAACHILIE
MBALI (wapuze yaliyopita). JE, NYINYI HAMPENDI ALLAH AKUSAMEHENI? NA ALLAH NI
MWINGI WA MSAMAHA (na) MWINGI WA REHEMA (basi na nyinyi sifikeni kwa sifa hizi)”.
[24:11-22]
II.
UTAKASIFU WA HESHIMA/HADHI YA MTU:
Heshima/hadhi
ya mtu ni miongoni mwa vitu vitukufu kabisa anavyostahiki mwanadamu kutoka kwa
jamii inayomzunguka. Kwa hivyo basi ni kitu kinachohitajia mno kulindwa na
kuhifadhiwa ili kisichafuliwe na kuvunjwa hovyo. Kwa kulitambua hili, ndipo
aya tukufu zikatahadharisha kwa ukali kabisa kuvunja heshima ya mtu kwa kuzua
uzushi au kuleta utesi. Na zikawalaani wale wanao wasingizia machafu wanawake
waumini, laana ya Allah iwashukie duniani na akhera na kuwakamia kupata adhabu
kubwa mno siku ya kiyama: “BILA SHAKA WALE WANAOWASINGIZIA WANAWAKE
WALIOTAKASIKA WASIOJUA (maovu), WAUMINI (wenye kuwasingizia watu hawa)
WAMELAANIWA KATIKA DUNIA NA AKHERA; NAO WATAPATA ADHABU KUBWA. SIKU AMBAYO
ZITAWASHUHUDIA NDIMI ZAO NA MIKONO YAO NA MIGUU YAO, KWA YALE WALIYOKUWA
WAKIYAFANYA. SIKU HIYO ALLAH ATAWAPA SAWA SAWA MALIPO YAO YA HAKI, NA WATAJUA
KWAMBA ALLAH NDIYE (Mwenye kulipa kwa) HAKI ILIYO DHAHIRI”. [24:23-25]
Halafu
tena ndipo maudhui haya yakakhitimishwa kwa kuwekwa
kanuni jamii enevu yenye dhima ya kuvunja tuhuma kwenye msingi na mzizi
wake. Kanuni ambayo inasilihi (inafaa) kuwa ni mizani ya kutolea hukumu kwa
mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla wake katika kila zama na kila mahala:
“WANAWAKE WABAYA NI WA WANAUME WABAYA, NA WANAUME WABAYA NI WA WANAWAKE
WABAYA. NA WANAWAKE WEMA NI WA WANAUME WEMA, NA WANAUME WEMA NI WA WANAWAKE
WEMA; HAO WAO WAMEEPUSHWA NA HAYO WANAYOYASEMA, WAO WATAPATA MSAMAHA NA RIZIKI
ILIYO NA HISHIMA (peponi)”. [24:26]
Ni
kama hivi kila mmoja atafuata njia yake aliyoichagua na kila chombo hukiivisha
kilichomo ndani yake. Hivi ndio kusema wanawake wachafu (wazinifu) ni stahiki
ya wanaume wachafu wenziwao, kama ambavyo wanawake wazuri (wasiofanya machafu)
walivyo stahiki ya wanaume wazuri mithili yao.
Kisha
tena hakumuelei muumini kuyasadikisha au kuyakadhibisha anayoyasikia kutoka
kwa nduguye muumini ila baada ya kuyasoma mazingira ya hayo aliyoambiwa. Na
achunguze sababu na natija na azitafiti tabia za mtoa khabari wake, chimbuko
lake na mazingira aliyokulia. Si hayo tu, bali anapaswa kuchunguza ni mambo
gani yaliyomsukuma huyo fulani kutenda alilolitenda au kuacha kulitenda. Haya
huo ni kwa upande wa muumini mwenziwe, seuze kwa kafiri! Ama kuufuata uvumi tu,
kufanya hivyo si busara wala hekima na hili ndilo Allah Taala
alilowatahadharisha waumini wasilirudie tena, katika kauli yake tukufu:
“ALLAH ANAKUNASIHINI MSIRUDIE KABISA KUFANYA MFANO WA HAYA, IKIWA NYINYI NI
WAUMINI KWELI. NA ALLAH ANAKUBAINISHIENI AYA (zake) NA ALLAH NDIYE AJUAYE,
MWENYE HIKIMA”. [24:17-18]
III.
QUR-ANI ILIKUWA KALI KATIKA KULIELEKEA SUALA LA UZUSHI HUU:
Tukio
hili la uzushi kama lilivyosawirishwa na Qur-ani Tukufu, Allah Taala akaweka
sheria chini ya mazingira yake ili kuilinda jamii ya Kiislamu dhidi ya jarima
ya zinaa. Na kuilinda dhidi ya jarima ya kuchafua na kuvunja hadhi/heshima ya
wanawake waumini. Na ikatia mkazo mkata katika kuithibitisha jarima hii ili
watu wasio na hatia wasihukumiwe na kuadhibiwa kutokana na uzushi wa mtu tu.
Mtu anaweza kusema/kuuliza:
Þ
Hivi kweli ni jambo
linalowezekana mtu kuleta mashahidi wane ili kuthibitisha hali ya jarima ya
zinaa kwa mwanamume na mwanamke?
Þ
Je, hili
linamkinika katika hali zote?
Þ
Je, ni jambo
linaloingia akilini kwamba jarima ya zinaa haiwezi kuthibiti ila kwa ushahidi
wa kuona wa mashahidi wanne?
Þ
Na je, huku si
kumfanya mtu ashindwe kabisa kuithibitisha jarima hii chafu yenye kufedhehesha?
Naam, ni kweli
kabisa kwamba hilo linaweza kuwa gumu kupatikana kwake na pengine kushindikana
kabisa. Lakini Muweka sheria hiyo (Allah) ameyazingatia kwa upande huo mambo
kadhaa yenye umuhimu mkubwa sana. Alichoangalia na kuzingatia ni kule
kufungamana kwa jambo hili na heshima/hadhi za watu. Na kwamba hili ni suala
hisia lenye athari kubwa mno kwa kila mwenye kuguswa na maneno hayo ya watu,
yawe ni ya kweli au uongo. Na akazingatia kwamba tabia/maumbile ya watu ni
wepesi mno wa kupokea uvumi na kuusadiki na kisha kuueneza haraka. Kwa kuwa
hayo ndiyo maneno yapendezayo nafsini mwao na ndio mazungumzo ya baraza zao
kwa ghalibu. Na akazingatia kwamba hili ni suala linalofungamana na heshima/sifa
ya jamii ya Kiislamu, jamii inayopaswa kuwa mfano/kigezo cha kuigwa na jamii
nyingine katika utoharifu (utakasifu), unadhifu (usafi) na sifa yake njema. Ni
kwa ajili ya kuyazingatia yote haya ndio Muweka sheria akaweka vizuizi hivi
vigumu na akaweka ngome hizi imara ambazo ni kugumu mno kuzivuka. Ili alinde
na kuhifadhi heshima na hadhi ya waumini wake kwa waume na kukata ndimi za
watu wazushi waenezao uvumi kwa lengo la kuuchafua utu wa watu wasio na hatia.
Na ili awawekee waislamu desturi shadidi itakayowasukuma kutafakari na kuwa
makini wakati wa kusikiliza khabari za uzushi kama hizi. Desturi
itakayowalazimisha kutaka kubaini na kuthibitisha yote yasemwayo na kuweka
kizuizi baina yao na wasio waumini katika suala zima la kukubali na kusadiki
uvumi uwongo bila ya kuwa na ujuzi wa lisemwalo. “ENYI MLIOAMINI! KAMA
FASIKI (asiye wa kutegemewa) AKIKUJIENI NA KHABARI (yo yote ile msimkubalie tu)
BALI PELELEZENI (kwanza), MSIJE MKAWADHURU WATU KWA UJAHILI NA MKAWA WENYE
KUJUTA JUU YA YALE MLIYOYATENDA”. [49:06]
|