|
SOMO
LA KWANZA – VITA VYA AHZAABU (KHANDAQ).
I/.
Mapenzi ya kuangamiza ndiyo yaliyowasukuma Mayahudi
kukusanya makundi (Ahzaabu) ya Waarabu dhidi ya Mtume na maswahaba
wake.
Nafsini mwa
Banin-Nadhwiyr suala la kutolewa na kufukuzwa Madinah halikuwa ni jambo jepesi
hata kidogo kiasi cha kuachwa lipite hivi hivi tu. Wala halikuwa ni jambo
lenye kukoma athari zake kwa kumalizika kwake. Haikuwa hivyo kwa sababu
Madinah ndio palikuwa mahala pao na mahala pa wahenga wao kwa karne kadhaa.
Pamoja na mandhari ya ustahamilivu na furaha waliyoionyesha wakati walipokuwa
wakitoka, bado kusahau kwao halikuwa ni jambo rahisi. Kwani nyoyo zao zilikuwa
zikitokota chuki dhidi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na
maswahaba wake. Mbele za macho yao hawa walionekana kuwa ni wavamizi
waliowatoa kwa nguvu katika ardhi yao na kuwalazimisha kuyaacha makazi yao,
ngome, silaha, mashamba, biashara, mali na mifugo yao. Na isitoshe wavamizi
hawa hawa kuwaruhusu kuchukua katika mali zao hizo ila kiasi kidogo tu
kinachoweza kubebwa na ngamia wa kila mmoja wao. Kwa hali hii fikra zao zote
zikawa ni kutaka kujilipia kisasi na kuwaangamizilia mbali maadui na
wanyang’anyi hawa. Wawashushie pigo moja la kifo litakalo wasambaratishia
mbali kama si kuwafyeka kabisa.
Haya ndio yaliyozijaza nyoyo zao hasadi na chuki kwa Mtume huyu aliyekuja na
ulinganio wake katika mji wao. Ujaji uliowapokonya nafasi, cheo na hadhi ya
kidini waliyokuwa wakiishikilia na kuitumia kuwaongoza wazalendo waarabu
washirikina wa Madinah na makabila mengine ya Kiarabu katika miji mingine.
Mlingano huu uliendelea kukua na kuenea kwa kasi huku wafuasi wake
wakiongezeka siku hata siku na hivyo kuwafanya kuwa na nguvu kubwa ya kuweza
kujihami dhidi ya adui wa wito wa dini yao hiyo. Ni nguvu hii ndio
iliyowawezesha waislamu kuwatoa wao Mayahudi Madinah kikundi kikifuatiwa na
kingine na hali ya kuwa wao ni miongoni mwa wazalendo wa mahala hapo waliokuwa
na hadhi na sauti. Ni kwa ajili ya yote haya ndio mayahudi wakaziunganisha
nafsi zao na fikra ya kulipa kisasi. Wakaanza kutafuta fursa ya kummaliza
Mtume na maswahaba wake. Kwa kufanya hivyo, wote kwa pamoja Mayahudi na
Waarabu watakuwa wamepumzika na shari ya hii dini mpya. Na amani, salama na
utulivu utakuwa umerejea katika rasi (peninsula) hii kama ilivyokuwa kabla ya
kuingia kwa da’awah hii Madinah.
Makurayshi
waliitilia mashaka nia/dhamira ya Mayahudi, shaka hii ikawasukuma kuwauliza
swali hili: Dini yao (Makurayshi) na dini ya Muhammad ni ipi iliyo bora?
Hivi ndivyo
walivyofikiri Banin-Nadhwiyr, na wakakongamana juu ya dhamira hii ya kulipa
kisasi. Akatoka Huyay Ibn Akhtwab na Sallaam Ibn A-Haqiyq pamoja na kundi la
watukufu wao kwenda kuyakusanya makundi dhidi ya Mtume na waislamu. Ujumbe huu
wa viongozi wa Mayahudi ukafika Makkah kwa Makurayshi na kuwataka waungane nao
katika kumpiga Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Wakawaambia: Sisi
tutakuwa pamoja nanyi mpaka tumng’oe na kumfagilia mbali”. Makurayshi
walipoisikia kauli hii ya Mayahudi, wakaingiwa na shaka kuelekea dhamira/nia
ya Mayahudi. Shaka yao hii ikawafanya kusita kutoa ushirikiano kwa Mayahudi
dhidi ya Muhammad ambaye ni mkurayshi mwenzao. Pia waliitilia mashaka dini yao
na wakataka kupata uhakika na kupima baina yake na dini aliyokuja nayo
Muhammad. Dini inayolingania kumuabudu Allah pekee, dini inayolingania tabia
njema na adabu murua. Hivi ndivyo walivyofikiria Makurayshi na kuona vyo vyote
ilivyokuwa Mayahudi ndio walioanza uadui na uchokozi. Na kwamba Muhammad na
maswahaba wake hawakuwa na uchaguzi ila kujilinda nafsi zao, itikadi yao na
haki yao ya kuitangaza itikadi yao hii kwa watu. Na kisha kuwaachia watu uhuru
wa ama kuiamini au kuikufuru. Naam, huenda ni fikra kama hizi ndizo
zilizowasukuma Makurayshi kuwaambia wajumbe wa Banin-Nadhwiyr waliowajia:
“Enyi kusanyiko la Mayahudi! Bila shaka nyinyi ndio watu wa kitabu cha
mwanzo na mna ujuzi/elimu ya kile tunachokhitilafiana sisi na Muhammad. Basi
hebu tuambieni dini yetu ndio bora au dini yake (Muhammad)?” Kwa kuwa
Mayahudi walikuwa wakitafuta kuungwa mkono na Makurayshi katika vita vyao
dhidi ya Mtume, hawakukawia ila walijibu: “Dini yenu ndio bora kuliko dini
yake, kwa hivyo basi nyinyi ndio mnaoistahiki haki kuliko yeye”.
Hivi ndivyo mfundo, hasadi na uadui dhidi ya Mtume na da’wah yake
ulivyowasukuma Mayahudi kutokuogopa kushuhudia uovu. Ya kwamba shirki ni bora
zaidi kuliko tauhidi na kwamba miungu ya mushirikina ni bora kuliko mungu wa
Muhammad; Bwana Mlezi wa viumbe wote. Na kwamba desturi na mapokeo
wanayoyafuata mushrikina ni maongofu zaidi kuliko itikadi na mila
anayoilingania Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Hivi ndivyo walivyojasiri
kuukanusha msingi wa dini yao wenyewe ambao ni kumuamini Allah peke yake bila
ya kumshirikisha na cho chote. Wakayafanya yote hayo kwa ajili tu kumpiga vita
Mtume mwenye kuilingania imani iliyo sawa kabisa na yao na mwenye kuikemea
shirki, madhambi na machafu. Hapo ndipo Allah Taala akaishusha kauli yake
tukufu: “HUWAONI WALE WALIOPEWA SEHEMU YA (kufahamu) KITABU (cha Allah)?
WANAAMINI MASANAMU NA UPOTOFU NA HUSEMA JUU YA WALE WALIOKUFURU KUWA WAO
WAMEONGOKA ZAIDI KATIKA NJIA (ya haki) KULIKO WALE WALIO AMINI. HAO NDIO ALLAH
ALIOWALANI NA AMBAYE ALLAH AMEMLANI BASI HUTAMUONA KUWA NA MWENYE KUMNUSURU”.
[4:51-52]
Kauli hiyo ya Mayahudi iliwafurahisha mno Makurayshi na kuwafanya
waichangamkie na kuipokea propaganda ya kumpiga vita Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie. Kwa hivyo wakaanza kujiandaa na suala hili.
Mayahudi
walikusanya makundi ya mushrikina mpaka ikafikia idadi yao watu alfu kumi:
Baada ya kupata
waliloliendea kwa Makurayshi, huoo ujumbe wa Makurayshi ukaondoka kuipeleka
propaganda yao kwa Ghatwfaani. Huko nako wakatoa wito wa kumpiga vita Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-na kuwafahamisha kwamba Makurayshi wamesha
kubali kushirikiana nao katika azma yao hii. Wakainogesha propaganda yao hii
chafu kwa kuwaahidi Ghatwfaani donge nono la kupata mavuno ya tende za Khaybar
kwa kipindi cha mwaka mmoja. Donge hili watalipata mara tu baada ya kumshinda
Muhammad, kwa tamaa ya donge nono hili koo zote za Ghatwfaani zikawaitika
Mayahudi katika ombi lao hilo. Hivi ndivyo Mayahudi walivyopata washirika wa
kuwasaidia katika dhamira yao hii, makundi kwa makundi na kuyachochea makabila
dhidi ya Mtume. Wakawakusanya wale wote wenye kisasi kwa Mtume wa Allah katika
makabila ya Kurayshi, Ghatwfaani, Asadi, Suleim na washirika wao katika
makabila ya Waarabu. Idadi yao ikafikia kiasi cha watu alfu kumi, jeshi hili
kubwa likaondoka kuelekea Madinah kwa kishindo kikubwa chini ya ukamanda wa
Abu Sufyaani Ibn Harbi. Hiyo ilikuwa ni katika mwezi wa Shawwal mwaka wa tano
(5) Hijiria (Februari 627 A.D.).
|