|
Handaki
hili likawa ni kikwazo kikubwa kwa majeshi shirika (Ahzaabu):
Waislamu wakaifanya
kazi ya uchimbaji wa handaki mpaka waka ikamilisha kwa ufanisi mkubwa.
Wakalipanua, wakaliendesha kina mpaka likafikia mahala pa kumshinda farasi
aliye hodari kulivuka. Wakaweka
kizuizi imara na mawe katika njia ielekeayo Madinah ili viwe ni kingamizi
baina yao na adui yao na viwasaidie katika kupambana na adui pindi
itakapojitokeza haja ya kufanya hivyo. Wakaupachanisha mji wa Madinah kwa
majengo, wanawake na watoto wakawekwa katika ngome. Baada ya kuyafanya yote
hayo ndipo Mtume na maswahaba wake wakapiga kambi kwenye sehemu ya chini ya
mlima, migongo yao ikilielekea jabali. Huku wakimuelekea adui kwa nyuso zao
kutokea upande wa handaki na katikati yao kukiwa na ardhi yenye majimaji ya
chumvi. Waislamu walikuwa ni alfu tatu; wapiganaji wapanda farasi miongoni
mwao wakiwa ni thelathini na sita tu, hii ikimaanisha kuwa wengine wote
waliosalia ni askari wa miguu.
Wakati bado Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akiwa amefa dhaishwa na
suala la handaki, kikajitokeza kikosi cha mwanzo cha jeshi shirika kikija
Madinah kutokea upande wa Uhud. Walipokaribia milango ya kuingilia Madinah,
tahamaki hilo ni handaki kubwa mbele yao limeizuilia njia yao wasiweze kusonga
mbele. Hili likawa ni jambo la ghafla mno kwao, ambalo hawakulitarajia kabisa
mpaka wakaambizana: Hiki ni kitimbi ambacho Waarabu hawakuwahi kukitumia.
Handaki hili likayalazimisha majeshi shirika kusimama mbele ya kizuizi hiki
cha ajabu. Wakasita kidogo hapo ili kulitafakari hilo na kupanga upya mikakati
yao. Makureishi, Wahabeshi na washirika wao wa Kinaanah na Tihaamah wakapiga
kambi katika makutano ya mumbwi (torrential stream) mkabala na handaki.
Ghatwfaani na washirika wao katika makabila ya Najid wakapiga kambi katika
eneo lililojulikana kama “Dhanabu Naqamaa”, kwa upande wa Uhud.
Wakawaachilia ngamia na farasi wao kula katika mashamba ya Madinah kwa lengo
la kuwadhoofisha waislamu kiuchumi. Lakini wapi, watu tayari walikuwa
wameshavuna mazao yao mwezi mmoja kabla ya kuja kwa Ahzaabu.
Vikosi
vya majeshi shirika vyasimama muda mrefu mbele ya handaki vikiizengea fursa ya
kulivaa na kuvukia ng’ambo ya pili:
Vikosi vya majeshi
shirika vikasimama mbele ya handaki vikiwa vimehemewa visijue nini cha kufanya.
Vilikuja na dhana kuwa vita hiyo itachukua siku moja tu au chini ya hapo,
haitakuwa ila makundi haya ya muungano yatamzunguka Muhammad na maswahaba wake
na kuwateketeza mara moja tu. Kisha warejee makwao wakiwa na ngawira maridhawa
huku wakiwa wameufyekelea mbali mzizi wa fitina ya dini hii mpya. Dini
iliyoteteresha hali yao ya amani, ikawagawa na kuyachafua mapokeo ya wahenga
wao. Lakini ikaja kuwabainikia kuwa vita hii haitakuwa nyepesi kama
walivyofikiria mwanzo na kwamba itawalazimu kusimama mbele ya handaki hili kwa
muda mrefu kabla ya kupata njia na mbinu ya kulivuka.
Kama hivi makundi mawili haya; waislamu kwa upande mmoja na majeshi shirika
kwa upande wa pili yakawa ana kwa ana mbele ya handaki. Waislamu wakiwa
wachache wenye silaha duni na mushrikina wakiwa katika muungano wao na
maandalizi kabambe ya kutisha. Lakini eeh tofauti iliyoje baina ya nguvu
shikamana yenye imani na lengo moja na baina ya watu tapanyi wasio na lengo
moja linaloziunganisha pamoja nyoyo zao! Ama kwa upande wa kimaada majeshi
shirika yalikuwa na wingi wa watu na zana, lakini havikuwepo viunganishi
vinavyowapelekea kuwa na ikhlaswi na kusaidiana katika mapambano. Mwanzoni
ilionekana kuwa Abu Sufyaani ndiye kamanda na amiri jeshi mkuu wa majeshi
shirika kwa jina si hakika. Hii ni kwa sababu kila kundi lililotoka lilikuwa
chini ya uongozi ambao linaona kuwa unafaa kuwaongoza na kwamba ndio
unaostahiki kuyaongoza makundi mengine yote.
Majeshi mawili haya yakakaa siku kadhaa huku kila moja likizichunguza kwa
makini nyendo za mwenzake na majeshi shirika yakilizunguka handaki mchana
kutwa na usiku kucha. Yalifanya hivyo yakitarajia kuwa huenda yakapata upenyo
utakaowavusha ng’ambo ya pili au wakaitumia fursa ya kughafilika kwa
waislamu kuvuka. Lakini wapi waislamu nao walikuwa hadhiri wakihakikisha kuwa
hawatoi hata chembe ya mwanya itakayompatia ushindi adui yao. Kila
kilipojaribu kikundi cha adui kulijongelea handaki walikinyeshea mvua ya
mishale na mawe na kukilazimisha kurejea kinyumenyume kule kilipotokea.
Muhammad Ibn Maslamah anasimulia: “Usiku wetu katika handaki ulikuwa ni
mchana na mushrikina wao walikuwa wakishikiana zamu. Siku moja akidamka Abu
Sufyaan na kundi lake kujaribu kuvuka handaki. Siku nyingine akidamka Khaleed
Ibn Al-Waleed, siku nyingine Amrou Ibn Al-Aaswi, siku nyingine Hubayrah Ibn
Ubayyi, siku nyingine Ikrimah Ibn Abu Jahli na siku nyingine Dhwiraari Ibn Al-Katwaab.
Majaribio haya yakaendelea mpaka balaa likawa kubwa na khofu kuu ikazitambaa
nyoyo za waislamu. Walipokuwa wakidamka waliwatanguliza mbele yao warusha
mishale, wakavurumisha mvua ya mishale kuelekea kwa Mtume kwa kitambo. Wakati
wote huo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa juu ya farasi wake
akiwaelekeza maswahaba wake namna ya kujibu mashambulizi hayo ya nguvu.
|