|
I.
Hujuma kuu na mzingiro mkali:
Mushrikina wakaja siku iliyofuatia wakiwa wamewakusanya watu wao na
kuvitapanyia vikosi vyao kila upande. Upande aliokuwa Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-wakapeleka kikosi kikali ndani yake akiwemo shujaa wao Khalid
Ibn Al-Waleed. Waislamu wakapambana nao na kutoa upinzani mkali, mapambano
yakaendelea mpaka usiku mwingi. Ukali wa mapambano ukamlazimisha Mtume wa
Allah na maswahaba wake kutoondoka hata kwa dakika chache sehemu zao za
mapambano. Wala hapana hata mmoja aliyepata mwanya wa kuswali Adhuhuri,
Laasiri, Maghribi wala Ishaa. Haki iliendelea hivyo mpaka pale Allah
alipowafunua mushrikina na kila kundi likarejea kambini kwake tayari kwa
mapambano ya siku ya pili. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipofika
kambini kwake akamuamuru Bilali kuadhini na kisha akakimu kwa ajili ya swala
ya Adhuhuri. Baada ya kuswaliwa Adhuhuri kukakimiwa kwa ajili ya swala
nyingine zote zilizosalia bila ya kuadhiniwa. Mtume na maswahaba wake
wakazikidhi swala zote zilizowafutu katika
kitaanani cha vita.
Baniy
Quraydhwah wakapanga kuivamia Madinah usiku, khabari hizo zikamfikia Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie. Akampeleka Salamah Ibn Aslama pamoja na watu
mia mbili na Zayd Ibn Haarithah pamoja na kundi la watu mia tatu kuulinda mji
wa Madinah. Khofu ya kuwachelea Baniy Quraydhwah dhidi ya wanawake na watoto
wa Kiislamu Madinah ilipewa nafasi kubwa na Mtume kuliko hao Makurayshi na
Ghatwfaani walioko mbele yao. Mushrikina wakawazingira na kuwatia kati
waislamu kiasi cha kuwafanya wachanganyikiwe wasijue la kufanya. Hali ikawa
mbaya sana, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza kumuomba Mola
wake akisema: “Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba kwa ahadi na miadi yako!
Ewe Mola wa haki wee! Ukitaka hutoabudiwa. Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba
utukinge na shari yao, utunusuru nao na asikushinde asiye wewe”. Waislamu
wakamjia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na kumuuliza: Je, iko dua yo
yote tuombe kwani tayari nyoyo zimeshapanda kooni (kutokana na mshindo mkuu wa
vita)? Mtume akawajibu: “Naam, semeni: Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba
uzisitiri aibu zetu na uziaminishe khofu zetu”.
Ibn
Sa’ad-Allah amrehemu-anasema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na
maswahaba wake wakawekwa mzingironi kwa kadiri ya siku kumi na kitu. Mpaka
kila mmoja wao akapatwa na msongo wa moyo, Mtume wa Allah akataka kuituliza
hali hiyo kwa kufanya suluhu na Ghatwfaani. Aandikiane nao mkataba wa kuwapa
theluthi moja ya mavuno ya tende za Madinah ili wajitoe katika majeshi shirika
na washike njia kurudi makwao. Answari wakaipinga azma hii ya Mtume kwa kuwa
itawadhalilisha na kuwatia unyonge wa milele mbele ya macho ya walimwengu.
Mtume wa Allah akakubaliana na shauri lao hilo na kuitupilia mbali azma yake.
Bishara
za faraja:
Mpaka dakika hii Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake-Allah awawiye
radhi-walikuwa wameshafanya kila waliwezalo. Na wamemaliza juhudi zao zote
katika kuitetea na kuilinda imani yao na mji wao kiasi cha kutobakisha kitu
katika nguvu/uwezo wa kibinadamu. Hapo ndipo ulipoingilia kati uwezo na nguvu
za ki-Mungu ili kuwasaidia waumini hawa walioipigania dini ya Allah haki ya
kuipigania. Ghafla mwenendo wa vita ukageuka na kubadili mwelekeo wake kiasi
cha kuwashangaza watu namna yake: “...WALA HAPANA YE YOTE AYAJUAYE MAJESHI
YA MOLA WAKO ILA YEYE TU...” [74:31]
II.
Khadaa ya Nuaim Ibn Masoud:
Miongoni
mwa mambo ambayo Allah alimfanyia Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-na
waumini katika vita hivi ni kuwaletea Nuaim Ibn Masoud Al-Ashjaiy akiwa
muislamu tayari. Akasema: “Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi nimekwishasilimu
na hakuna ye yote katka watu wangu anayejua juu ya huku kusilimu kwangu, basi
niamuru ulitakalo”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia:
“Hakika si vinginevyo, wewe ni mtu mmoja tu katika Ghatwfaani, basi lau
ungetoka ukenda kuwakatisha tamaa nasi kama unaweza. Ingelikuwa ni bora zaidi
kuliko kubakia pamoja nasi hapa, basi haya toka kwani vita ni khadaa”. Huyoo
Nuaim Ibn Masoud akatoka mpaka kwa Baniy Quraydhwah na alikuwa akinywa pamoja
nao katika zama za Jahilia, akawaambia: “Enyi Baniy Quraydhwah! Kwa yakini
mnayajua vema mapenzi yangu kwenu na khususan urafiki ulio baina yangu nanyi”.
Wakamjibu: “Wewe sema tu, kwani wewe kwetu si mwenye kutuhumiwa kwa ubaya”.
Hapo ndipo akaanza kuwaambia: “Hakika Makurayshi na Ghatwfaani si kama
nyinyi, huu mji (Madinah) ni mji wenu ambao ndani yake kuna mali, watoto na
wake zenu. Na hakika hawa Makurayshi na Ghatwfaani wamekuja tu kumpiga vita
Muhammad na watu wake (hawana kitu hapa), nanyi mmekwishachukua uamuzi wa
kuwasaidia (katika vita yao hii). Wao wakiiona fursa wataitumia (kufikia
malengo yao) na mambo yakiwa kinyume na matarajio yao, haoo watashika njia na
kurudi makwao na kukuacheni peke yenu na mtu huyu (Mtume). Nanyi hamna ubavu
wa kupambana nae peke yenu, kwa ajili hii mimi ninakushaurini msiingie vitani
pamoja na watu hawa mpaka muwachukue rehani watukufu wao”. Kisha kuwaambia
hivyo, huyoo akatoka mguu mosi mguu pili kuwaendea Makurayshi, nao akawaambia:
“Bila shaka enyi kusanyiko la Makurayshi mnayajua vema mapenzi yangu kwenu
na kumuacha kwangu Muhammad. Hakika limenifikia jambo ambalo naona ni haki
yangu kukufikishieni kama ushauri nasaha kwenu, basi tafadhalini nifichieni
siri”. Wakasema: “Tutakufichia”. Akawaaambia: “Mnajua, Mayahudi
wamekwishajuta kumsaliti kwao Muhammad na wamempelekea ujumbe: Ya kwamba sisi
tume shayajutia tuliyoyatenda, basi je yakuridhi wewe sisi tuwachukue watu
katika Makurayshi na Ghatwfaani, tuwasalimishe kwako uzikatilie mbali shingo
zao. Kisha sisi tusimame nawe mpaka tuwamalize waliosalia?” Halafu
akawaendea Ghatwfaani na kuwa ambia maneno hayo hayo.
Ulipofika
usiku wa kuamkia Jumamosi na hili lilikuwa katika jumla ya mambo ambayo Allah
alimfanyia Mtume wake na waumini. Abu Sufyaan alimtuma Ikrimah Ibn Abu Jahli
kwenda kwa Baniy Quraydhwah akiliongoza kundi katika Makurayshi na Ghatwfaan,
awaambie: “Hakika sisi hatutaendelea kukaa hapa, ngamia na farasi wetu
wanaangamia kwa njaa, kwa ajili hii jiandaeni kwa vita kesho asubuhi tummalize
Muhammad”. Baniy Quraydhwah nao wakasema: “”Hakika siku hiyo (Jumamosi)
ni siku ya Sabato ambayo sisi hatufanyi kazi yo yote ndani yake nanyi nyote
mnayajua vema yaliyowafika walioikhalifu amri hii miongoni mwetu. Pamoja na
yote haya sisi hatutapigana upande wenu mpaka mtupe rehani watu wenu wawe
mikononi mwetu ili iwe ni uthibitisho kwetu. Kwani sisi tunachelea vita
ikikuelemeeni mtashika njia na kurudi makwenu na kutuacha sisi na mtu huyu
katika mji wetu nasi hatuna ubavu juu yake”.
Wajumbe
waliporejea na majibu hayo ya Baniy Quraydhwah, wakasema: “Wallah,
ametuambia kweli Nuaim Ibn Masoud”. Wakapeleka tena wajumbe kuwaambia:
“Wallah, hatutakupeni rehani aslani, mkitaka tokeni pamoja nasi tukapigane
na kama hamkufanya hivyo, basi makubaliano yetu yamevunjika”. Baniy
Quraydhwah wakasema: “Wallah, amesema kweli Nuaim Ibn Masoud!” Kwa mbinu
na hila hii ya Ibn Masoud, Allah akawa ameuvunja umoja na nguvu yao na
kuwatapanya.
|