|
Ni katika wakati huu
ambamo mafungamano yalichangukana, ukweli/uaminifu baina ya majeshi shirika na
nafsi zikakimwa kwa kukaa muda mrefu. Ndimo Allah Taala aliyapelekea majeshi
shirika upepo mkali katika usiku unyeshao mvua, wenye baridi kali na giza
totoro. Majungu ya vyakula yakaanza kupinduliwa na upepo, vyombo vikarushwa
mbali, mioto ikazimika na mahema yakabomoka. Nyoyo zao zikatambaliwa na khofu
na fazaa iliyowapelekea kuchelea kushambuliwa ghafla na waislamu katika
kipindi hicho kigumu. Khofu na fazaa hii ikawafikisha kuchukua aumuzi wa
kuacha vita na kurudi mwakwao. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anasema: “Khabari
za kukhitilafiana kwao zilipomfikia Mtume wa Allah-Rahama na Amani
zimshukie-na jinsi Allah alivyouvunja umoja wao. Alimuita swahaba wake;
Hudhayfah Ibn Al-Yamaan-Allah amuwiye radhi-akamtuma kwenda kuchunguza
mahasimu wao wamefanya nini usiku. (Hudhayfah anahadithia): Nilijikuta
handakini pamoja na Mtume wa Allah, akaswali kidogo usiku ule, kisha
akatugeukia na kusema: “Nani atakayeenda kutuchunguzia mahasimu wetu
wamefanya nini, kisha arudi na kutujuza khabari? Nitamuomba Allah mtu huyo awe
rafiki yangu peponi”. Basi hapana hata mtu mmojaa aliyethubutu kujitokeza
kutokana na khofu kuu, njaa na baridi kali. Mtume kuona kuwa hakuna
aliyejitokeza, ndipo aliponiita nami sikuwa na budi ila kumuitika, akaniambia:
“Ewe Hudhayfah! Nenda kajichanganye na watu wale uchunguze wanafanya nini na
usifanye wala kusema cho chote mpaka utakaporudi hapa”. (Hudhayfah
anaendelea kusimulia): Basi nikaenda na kujichanganya na watu wale na ilhali
upepo ule mkali na majeshi ya Allah yakiendelea kuwashughulikia. Hali ikawa
mbaya kiasi cha kufikia hakuna chungu kilichothibiti bila ya kupinduka, moto
uliowaka bila ya kuzimika, wala hema lililosimama bila ya kung’oka. Abu
Sufyaan akainuka na kusema: “Enyi kusanyiko la Makurayshai! Kila mtu
aangalie amekaa na nani. (Hudhayfah akasema): Nikamshika mkono mtu aliyekuwa
ubavuni mwangu nikamuuliza: Wewe nani? Akajibu: Fulani Ibn fulani. Abu Sufyaan
akaendela kusema: Enyi kusanyiko la Makurayshi, wallah hakika nyinyi hamjapata
makazi mazuri hapa, farasi na ngamia wetu wanakurubia kuhiliki kwa njaa, Baniy
Quraydhwah nao wametutupa mkono. Na imetupata shida ya upepo mkali kama
mnavyoona hakuna jungu linalothibiti ila hupinduliwa, wala moto uwakao ila
huzimwa, tena hakuna hema linalosimama ila huezuliwa. Kwa hali hii fungeni
safari turudi Makkah, hakika mimi ninaondoka. Alipokwisha kusema maneno yake
hayo, akamuendea ngamia wake na kumpanda. Lau kuwa si ule usia wa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alioniambia: “Usifanye wala kusema lo lote
mpaka utakaporudi hapa”, ningelimuua kwa mshale. (Hudhayfah anaendelea
kusema): Nikarudi kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nae akiwa
amesimama anaswali, akiwa kajitanda guo la mmojawapo wa wakeze. Aliponiona
akaniingiza miguuni mwake na kunitupia ncha ya guo lile, halafu akarukuu na
kusujudu nami nikiwa humo humo ndani ya guo lile. Alipotoa salamu nikampasha
khabari za niliyoyaona na kuyasikia huko. Ghatwfaan wakapata khabari ya uamuzi
uliofikiwa na Makuryashi wa kuondoka na kurudi makwao, nao haoo wakaondoka
kurudi makwao.
Kulipopambazuka
asubuhi, waislamu hawakumuona hata mtu mmoja katika kambi ya majeshi shirika.
Hapo wakayakinisha ya kuwa msaada wa Allah u pamoja nao na kwamba jicho la
Allah linawahifadhi na kuwalinda. Imani yao ikazidi kwamba wao wako katika
haki na kwamba Allah atawapa nusra dhidi ya maadui zao siku zote. Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawaangalia maswahaba wake kwa jicho
lililojaa matumaini na ukweli kwa Allah, akasema: “Sasa tutawapiga na wala
hawatatupiga”, halafu akatamka kwa sauti kubwa na kufuatiwa na maswahaba
wake: Hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah pekee, amemnusuru mja
wake, amelipa nguvu jeshi lake na ameyashinda makundi (ya majeshi shirika)
peke yake, basi hapana kitu baada yake!”
IV.
Mazingira ya vita hivi:
Vita
hivi vya Ahzaab havikuwa ni vita vya medani ambamo huonekana ushujaa kwa
kushambulia na kurudi nyuma. Bali hivi vilikuwa ni vita vya kutahini azma na
nyoyo, ni kwa ajili hii ndio wanafiki wakashindwa mtihani na waumini kufaulu.
Wakati ambapo wanafiki na wale wote wenye maradhi ya nyoyo walidhihirisha
kupapatika, shaka na udhaifu wa nafsi. Waumini wao walionyesha ustahamilivu na
subira iliyoonyesha uimara wa imani yao na yakini yao kwa Allah. Na yakini yao
kwamba nyuma ya shida hii kuna faraja iliyo karibu na kwamba hakika si
vinginevyo Allah Taala ametaka kuwapa majaribu na kuwatahini imani zao kupitia
shida na dhiki hii iliyowasibu. Walipofaulu mtihani huu kwa kiwango hiki cha
juu kabisa ndipo Allah alipowakunjulia mkono wake wa rehema na kuwaokoa kwa
neema zake kutoka kwenye makucha makali ya adui yao: “NA WAUMINI WALIPOYAONA
MAJESHI (ya makafiri yamewashambuli hivyo) WALISEMA HAYA NDIO ALIYOTUAHIDI
ALLAH NA MTUME WAKE (kuwa tutapata misukosuko, kisha tutashinda). ALLAH NA
MTUME WAKE WAMESEMA KWELI, NA (jambo hili) HALIKUWAZIDISHIA ILA IMANI NA UTII.
WAPO WATU MIONGONI MWA WALIOAMINI WALIOTIMIZA AHADI WALIYO AHIDIANA NA ALLAH.
BAADHI YAO WAMEKWISHAMALIZA UMRI WAO (wamekwisha kufa) NA BAADHI YAO WANANGOJA
(siku yao kufika), WALA HAWAKUBADILISHA (ahadi yao) HATA KIDOGO. ILI ALLAH
AWALIPE WAKWELI KWA SABABU YA UKWELI WAO NA KUWAADHIBU WANAFIKI AKIPENDA (kwa
kuwa hawakurejea) AU KUWAGEUKIA (kwa rehema kama wakitubia). BILA SHAKA ALLAH
NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU. NA WALE WALIOKUFURU ALLAH
ALIWARUDISHA NA GHADHABU YAO, HAWAKUPATA CHO CHOTE KATIKA KHERI NA ALLAH
AKAWAKIFIA WAISLAMU MAPIGANO NA ALLAH NI MWENYE NGUVU MBORA”. [33:22-25].
|