|
Bwana Mtume Rehma na Amani zimshukie- alijulikana miongoni mwa
jamii yake kwa sifa na tabia zake njema kama vile ukweli, uaminifu, haya, unyenyekevu na
upole. Jamii yake ilimkubali na ikampa jina la MKWELI MUAMINIFU. Huu ulikuwa ndio umaarufu
wake pale mjini Makkah na kwingineko. Jamaa zake na jamii nzima walimuheshimu na kumpenda
kwa kuwa alikuwa ni mtu mwepesi kuzoeleka na alishirikiana katika kazi mbali mbali za
maendeleo katika jamii yao. Kutokana na tabia njema hizi alizopambika nazo Bwana Mtume,
watu walikuwa wakienda kuweka amana zao kwake. Waliamini kuwa nyumbani kwa Mtume ndio
mahala salama pa kuweka amana zao ambapo wanaweza kuzipata wakati wowote wakizihitajia
hata kama ni usiku.
Lakini pamoja na mapenzi na heshima aliyoivuna Mtume kutoka kwa jamii
yake, ikiwa ni jazaa ya tuzo na tabia zake njema kwao bado alihisi dhiki ndani ya nafsi
yake. Bwana Mtume hakuichukia jamii yake kama watu bali alikerwa na tabia zao mbaya na
itikadi yao potofu ya ushirikina. Hili ndilo lililomsumbua na ili kuonyesha chuki yake
dhidi ya tabia na itikadi potofu ya jamii yake, hakupata kushirikiana nao katika kunywa
pombe hata mara moja kiasi cha kuwashangaza walio wengi kwani ulevi lilikuwa ni jambo la
kawaida kwa jamii ile mbali ya kuwa ni fakhri. Kadhalika hakuhudhuria hata mara moja
sherehe na ibada za miungu sanamu japokuwa jamii yake ilimsihi sana ashirikiane nao lakini
alikataa. Haya yote hayakuwa ila ni kwa fadhila zake Mwenyezi Mungu ambaye ndiye
aliyemuhifadhi Mtume wake kutokana na uchafu ule wa kijahili. Kwa mukhtasari hivyo ndivyo
Mtume alivyoishi na jamii yake kabla hajakabidhiwa rasmi dhamana ya Utume.
SOMO LA SABA
i) UFUMBUZI WA MTUME KATIKA MZOZO WA UWEKAJI
WA HAJAR ASWAD
Watu wa Makkah walipoona kwamba jengo la nyumba ya Mwenyezi Mungu
Al-Kaaba limeanza kuonyesha nyufa na kubomoka, viongozi wao waliona kuna
umuhimu wa kuibomoa nyumba hiyo na kuijenga upya. Hivyo basi likapitishwa azimio la ujenzi
wa Al-Kaaba katika kikao chao na ndipo mikakati ya ujenzi ilipoanza. Kila
kabila likapewa jukumu lake katika kazi ile tukufu ya ujenzi wa nyumba tukufu ya Mtukufu
Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume nae hakubakia nyuma bali alishirikiana bega kwa bega na jamaa
zake katika kazi ile tukufu ya ujenzi akibeba mawe mabegani pamoja nao.
Jengo lilipomalizika na kufikia hatua ya kuliweka Hajar
Aswad {Jiwe Jeusi} mahala pake hapo ndipo ulipoanza mzozo wa nani apewe heshima na
nafasi ya kuliweka jiwe lile tukufu mahala pake huku kila kabila likigombea nafasi hiyo na
kujiona lina haki zaidi kuliko kabila jingine. Mzozo huu ulikuwa mkubwa sana kiasi cha
kuhatarisha hali ya amani na utulivu waliyokuwa nayo kwa kukurubia kulipuka vita baina
yao. Viongozi wao wenye busara waliona ni vema wakaketi chini kuutafutia ufumbuzi mzozo
ule mbaya. Ni vema ikumbukwe kwamba kikao kile kilifanyika ndani ya Al-Kaaba,
baada ya kipindi kirefu cha kuchangia fikra na mawazo ndipo wakakubaliana kwa kauli moja
kuwa wamfanye kuwa ni hakimu mtu yeyote atakayekuwa wa mwanzo kuingia mle kupitia
Baniy Shaybah, mlango huu leo unajulikana kama Babus-Salaam. Hivyo
wote wakayakazia na kuyakodolea macho yao upande wa mlango ule, kwa hekima anazozijua
mwenyewe Mwenyezi Mungu akajaalia wa mwanzo kuingia baada ya muafaka ule awe ni Bwana
Mtume Rehma na Amani zimshukie -. Alipoingia tu wote wakamfurahikia na kumpokea kwa
shangwe huku wakisema Huyu ni mtu mwaminifu na sote tunamkubali na kumridhia.
Wakamuhadithia tatizo lao nae aliwasikiliza kwa makini kabisa. Walipomaliza akaikunjua
shuka yake ya kujitanda na kuitandika chini, kisha akalichukua Hajar Aswad na
kuliweka katikati ya shuka ile, hapo ndipo alipomtaka kila kongozi wa kabila kuliwakilisha
kabila lake kwa kunyanyua ncha ya shuka ile. Wakalibeba Hajar Aswad wote kwa
pamoja mpaka mahala linapotakiwa liwekwe. Hapo sasa ndipo Bwana Mtume akalichukua kwa
mkono wake mtukufu na kuliweka mahala pake. Kwa hekima yake hiyo, mzozo ule ukaisha na
makurayshi wakashangazwa sana na upeo wa kufikiri na uelekevu wa akili ya Bwana Mtume,
kijana mwenye umri usiopindukia miaka thalathini na tano akaweza kufanya walichoshindwa
kukifanya watu wazima na akawa ameinusuru jamii yake na janga la balaa ya vita vya wenyewe
kwa wenyewe lililokuwa linawojongolea kutokana na mzozo wa uwekaji Hajar
Aswad.
ii) VITA VYA FUJJAAR NA VIAPO
VYA NUSRA
Bwana Mtume Rehma na Amani zimshukie alijenga moyo wa
kushirikiana na jamii yake katika kazi zote za ujenzi wa jamii yake kama tulivyoona namna
alivoshiriki katika ujenzi wa Al-Kaaba. Kwa upande mwingine alikuwa akichukia sana
kushirikiana nao katika zile ada na desturi mbaya japokuwa jamaa zake walitamani
ashirikiane nao lakini mara zote alikuwa akiwakatalia. Vita vya Fujjaar ni
ushahidi tosha uonyeshao jinsi Mtume Muhammad alivyoshirikiana na jamii yake. Alipofikia
umri wa miaka kumi na tano au ishirini alijiunga na jamii yake katika vita vya Fujjaar.
Sababu ya vita hivi ilikuwa ni kulinda na kuhifadhi heshima na utukufu wa ile miezi minne
mitukufu iliyotajwa ndani ya Qurani ambamo vita vimeharamishwa. Mojawapo la makabila ya
Hijazi ilivunja utukufu wa miezi ile kwa kulishambulia kabila jingine ndani ya miezi ile
mitukufu, ndipo makabila mengine yakajiunga pamoja kuliadabisha kabila lile chokozi. Kazi
ya Bwana Mtume katika vita hivi ilikuwa ni kuwakusanyia silaha wapiganaji na wakati
mwingine ilimbidi kushiriki moja kwa moja katika medani ya vita. Vita hivi vilidumu kwa
kipindi kisichopungua miaka minne, vikaisha kwa kuwekeana mkataba wa suluhu na amani baina
ya zile pande mbili husika huku upande wa uliopoteza idadi kubwa ya watu ukilipwa fidia na
upande mwingine.
Viapo vya Nusura : hili ni tukio lililotokea wakati Mtume Muhammad
akiwa na umri wa miaka ishirini. Viapo vya nusra ilikuwa ni mojawapo ya maazimio ya
kikundi cha kutetea haki ambacho kimsingi ilikuwa ni kumtetea mtu mnyonge asidhulumiwe,
kumpatia haki kila mwenye kuistahiki na kumsaidia kila mwenye haja na matatizo. Maazimio
ya kikundi hiki yalipitishwa ndani ya nyumba ya Bwana Abdillah bin Jadaan
Al-Tamiymi, huyu alikuwa miongoni mwa viongozi wa makurayshi . Mtume Muhammad aliona hii
ndio fursa aliyoitamani na kuingojea kwa muda mrefu ili aweze kushirikiana na jamii yake
katika kuyapiga vita maovu na dhuluma iliyoitawala jamii yake. Hivyo basi kutokana na azma
hiyo alishiriki kikamilifu na ami zake katika kikao kile na kuwa miongoni mwa walioshiriki
kuyapitisha maazimio yale matukufu.
|