|
Kwa sababu zote hizi na kwa kuyazingatia yote yaliyojiri, Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-aliharakisha kuwazingira Baniy Quraydhwah siku ile ile
yaliyoondoka Madinah majeshi shirika (Ahzaab). Aliona ni wajibu wa mwanzo
kuwaendea ghafla kabla hawajakamilisha maandalizi yao ya vita na kuziimarisha
ngome zao. Kabla kidogo ya kuingia wakati wa swala ya Adhuhuri, Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Bilali-Allah amuwiye radhi-kuwanadia
watu: “Ye yote aliye msikivu na mtii kwa (Allah na Mtume wake), basi
asiiswali swala ya Laasiri ila kwa Baniy Quraydhwah”. Waislamu
waliousikia wito huu wa Mtume wa Allah, pale pale wakaanza kuchukua silaha zao
na kumiminikia kwenye ngome za Baniy Quraydhwah. Wako miongoni mwao
walioidiriki swala ya Laasiri katika kitongoji cha Baniy Quraydhwah kutokana
na wepesi wao na wengine iliwadiriki njiani, wakaiswali hapo hapo
ilipowadiriki. Pia wako walioichukulia amri ya Mtume kwa njia ya dhahiri, hawa
hawakuswali njiani, bali waliendelea kwenda
huku wakati wa Laasiri ukitoka na kuipisha Maghribi iingie. Wakaiswali
Laasiri nje ya wakati wake (Qadhaa) walipofika kitongojini kwa Baniy
Quraydhwah. Vyo vyote ilivyokuwa kila kundi lilikuwa na lengo la kuharakia
kuitekeleza amri ya Mtume wa Allah kwa namna ya uweza na uelewa wake. Basi
haukuingia wakati wa swala ya Ishaa ila waislamu wote tayari walikuwa
wamekusanyika nje ya ngome za Baniy Quraydhwah wakiwa katika maandalizi kamili
ya vita. Idadi yao ikiwa ni askari alfu tatu wa miguu na wapanda farasi
thelathini.
Mtume
wa Allah-Rahema na Amani zimshukie-alikuwa amempa bendera ya vita Sayyidina
Aliy Ibn Abiy Twaalib-Allah amuwiye radhi. Akampa bendera hiyo aliongoze kundi
la Muhajirina na Answari kwenda kwa Baniy Quraydhwah. Mayahudi walipowaona
Waislamu wakawapokea kwa matusi, wakimtukana Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-na wake zake, waislamu hawakuyajibu matusi haya zaidi ya kuwaambia:
“Leo ni upanga tu ndio utakaozungumza baina yenu nasi na wala sio matusi”.
Halafu Mtume-Rehema na Amani zimshukie-nae akampanda mnyama wake kwenda
kuungana na maswahaba wake waliotangulia kwa Baniy Quraydhwah. Baniy
Quraydhwah walipomuona Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amefika
kujiunga na maswahaba wake, wakaingia ngomeni mwao kwa kutambua kuwa sasa ni
vita tu na wala si maskhara. Mtume wa Allah na maswahaba wake wakawazingira
kwa kipindi kisichopungua majuma mawili, katika kipindi chote hiki ikawa
hakuna atokaye wala aingiaye. Kwa maana hii wakawa wanaitumia akiba ya maji na
chakula walicho nacho bila ya kupata ziada kutoka nje. Wakachoshwa na kukimwa
na mzingiro huu mrefu na Allah akatia khofu ndani ya nyoyo zao. Hili
likawapelekea kufikia uamuzi wa kutuma ujumbe maalumu kwa Mtume wa Allah. Ya
kwamba awaruhusu kuhama wao, wake na watoto wao pamoja na mali inayoweza
kubebwa na ngamia kama ilivyokuwa kwa watangulizi wao; Banin-Nadhwiyr. Mtume
akawakatalia ombi lao hilo, nao hawakuchoka wakatuma ujumbe mwingine wakiomba
waruhusiwe kutoka wao wenyewe tu bila ya kuchukua mali wala silaha. Ombi lao
hili pia likakataliwa na Mtume na wakataka airidhie hukumu atakayoitoa yeye tu
na si vinginevyo kama watakavyo wao.
Baada
ya maombi yao yote mawili kukataliwa, kiongozi wao; Ka’ab Ibn Asad
akawashauri waingie katika Uislamu huku akiwa kumbushia ufahamu (elimu)
walionao juu ya utume wa Muhammad kutoka katika vitabu vyao, hawakuukubali
ushauri wake huu. Akawaambia ikiwa hamlitaki shauri hili la kusilimu, basi
waueni wake na watoto wenu, kisha nyinyi tokeni mkapigane na waislamu mpaka
mshinde au muuawe nyote. Ushauri huu pia wakaukataa, ndipo akawashauri
wawatokee ghafla waislamu usiku wa kuamkia siku ya Sabato (Jumamosi) na
kuwafyekelea mbali. Wakamwambia kiongozi wao: “Hatuwezi kuvunja utukufu/heshima
ya Sabato”, wakakhitilafiana na kujuta kwa yote waliyowatendea jirani zao
wema (waislamu).
- Ishara
ya Abu Lubaabah:
Mzingiro ulipowazidia na kuwachosha, wakapeleka ujumbe kwa Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-ya kwamba tunaomba umruhusu Abu Lubaabah aje tushauriane
nae katika suala letu hili. Ombi lao hili likakubaliwa, Mtume akawapelekea Abu
Lubaabah Ibn Al-Mundhir Al-Answaariy Al-Ausiy ambaye alikuwa mshauri mkuu wa
Baniy Quraydhwah na mali na familia yake ilikuwa kwao. Walipomuona, wanamume
wakamuinukia na wanawake na watoto wakaangusha kilio, kwa hali aliyoiona
huruma ikamuingia Abu Lubaabah. Baniy Quraydhwah wakamzunguka wakimuuliza:
“Unaonaje shauri hili ewe Abu Lubaabah, hakika Muhammad hasikii wala
kukubali lo lote ila tuiridhie hukumu yake”. Abu Lubaabah akawajibu kwa
kuashiria kooni kwake na akasema: “Shukeni katika hukumu hiyo”,
akimaanisha kuwa hukumu inayowasubiri ni kuchinjwa tu ikiwa mtajisalimisha.
Abu
Lubaabah akadiriki kuwa kwa ishara yake hii aliyoitoa amekwishaifichua siri
ambayo adui hakupaswa kuijua na kwamba kwa kitendo chake hicho tayari
amekwishamkhini Allah na Mtume wake. Akashindwa kuonana uso kwa uso na Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaamua kwenda msikitini, humo akajifunga
kamba barabara kwenye mojawapo ya nguzo. Akaapa ya kwamba hataonja chakula
wala maji mpaka afe au Allah amkubalie toba yake kutokana na aliyoyatenda. Na
akachukua ahadi kwa Allah ya kwamba kamwe hatoikanyaga ardhi ya Baniy
Quraydhwah; ardhi ambamo amemkhini ndani yake Allah na Mtume wake. Khabari ya
Abu Lubaabah ilipozigonga ngoma za masikio ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akasema: “Ama lau yeye angenijia ningelimuombea maghufira, lakini
maadam amefikia uamuzi alioufikia basi mimi siye nitakayemuacha huru mpaka
Allah amkubalie toba yake”. Abu Lubaabah akakaa hapo nguzoni siku sita bila
ya kula chakula wala kunywa japo funda ya maji. Mkewe akawa anamjia katika
kila wakati wa swala akimfungua ili apate kuswali, akimaliza kuswali humfunga
tena na kuendelea na kifungo chake hicho alichojihukumu yeye mwenyewe. Hali
yake ikawa taabani mpaka akazimia, hapo ndipo Allah Taala alipomkubalia toba
yake na akaishusha kwa Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-kauli yake tukufu:
“NA (wako) WENGINE WAMEKIRI DHAMBI ZAO (wametubia kwa Allah, wakapokelewa).
WAMECHANGANYA VITENDO VIZURI NA VINGINE VIBAYA. ASAA ALLAH AKAPOKEA TOBA ZAO,
HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU”. [9:102] Allah
alipompokelea toba yake, Abu Lubaabah akakataa kufunguliwa ila na Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomfungua akasema: “Ewe Mtume wa Allah,
hakika katika jumla ya toba yangu ni mimi kukihama kitongoji cha kaumu yangu
ambamo humo ndimo nilimotenda dhambi na niitasadaki mali yangu yote”. Mtume
akamwambia: “Inakutosha kutoa sadaka theluthi ya mali yako na sio mali yote”.
|