|
I.
Ausi wawaombea shafaa Baniy Quraydhwah:
Naam, hivyo ndivyo
ilivyomalizika kadhia ya Abuu Lubaabah. Ama Baniy Quraydhwah baada ya
kukataliwa maombi yao yote, hawakuwa na uchaguzi tena ila kujisalimisha kwa
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Mtume akaamuru wanaume wafungwe
kamba na kuwekwa kando, wanawake na watoto nao wawekwe upande mwingine. Hapo
ndipo wakatoka wazee wa Kiausi wakamuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-kuwaombea msamaha ndugu zao hawa wa yamini. Wakamuomba Bwana Mtume
awatendee Baniy Quraydhwah; washirika wao kama alivyowatendea Baniy Qayunqaa;
washirika wa Khazraji. Wakataraji Mtume awaachie Baniy Quraydhwah kutoka kama
alivyowaachia Baniy Qayunqaa na kwamba atawakubalia uombezi wao huo kwa
washirika wao kama alivyowakubalia Khazraji kwa washirika wao. Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-akawaambia: “Je, nyinyi kusanyiko la Ausi hamridhii mimi
kuweka mtu miongoni mwenu (Muasi mwenzenu) baina yangu na washirika wenu?”,
wakajibu: “Kwa nini tusiridhie!”. Mtume akawaambia: “Basi waambieni hao
washirika wenu wamteue ye yote wamtakaye”. Mayahudi wakamchagua Sa’ad Ibn
Muaadh; kiongozi wa Ausi kuwa ndio msuluhishi baina yao kwa upande mmoja na
Mtume wa Allah kwa upande wa pili.
Sa’ad
Ibn Muaadh alikuwa ni majeruhi kutokana na mshale aliopigwa katika vita vya
Khandaq na alikuwa akipata matibabu katika hema la mwanamke mmoja aliyeitwa
Rufaydah. Huyu ni mwanamke aliyekuwa na hema msikitini akitoa humo huduma kwa
majeruhi wa vita. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ndiye aliyewaomba
jamaa za Sa’ad wampeleke katika hema hilo la matibabu la Bi. Rufaydah.
Aliwaomba hivyo ili apate kuwa karibu nae na hivyo kupata fursa ya kumjulia
hali mara kwa mara. Mtume wa Allah alipompa Sa’ad dhima ya hukumu kama
walivyoomba Mayahudi, jamaa zake walimuendea na kumbeba juu ya punda. Wakawa
wanakuja nae njiani na huku wanamwambia: “Ewe Aba Amrou, watendee wema
washirika wako, kwani hakika si vinginevyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-amekutawalisha suala lao ili upate kuwatendea wema. Nawe uliona
namna Ibn Ubayyi alivyowatendea nduguze wa yamini (washirika wao)”.
Wakamshikilia na kumkariria maneno hayo, nae akiwasikiliza tu bila ya kuwajibu
japo kwa kipande cha neno. Walipozidi nae akawa amekereka na maneno yao hayo,
ndipo alipowaambia: “Bila shaka umemfikia Sa’ad wakati wa kutoogopa
kulaumiwa kwa ajili ya Allah”.
II.
Hukumu ya Sa’ad Ibn Muaadh:
Sa’ad alipofika
kwenye baraza ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie-Mtume aliwaambia maswahaba
wake muinukieni Bwana wenu. Wakasimama na kujipanga safu mbili, akipita kati
yao na kila mtu akimuamkua mpaka akafika mahala alipokuwa amekaa Mtume. Mtume
akamwambia: “Wahukumu ewe Sa’ad”, akamjibu: “Allah na Mtume wake ndio
wenye haki zaidi ya kuhukumu”. Mtume akamwambia: “Allah ndiye aliyekuamuru
kuwahukumu”. Kwa kauli hii ya Mtume, ndipo Sa’ad alipougeukia upande wa
waislamu na kuwaambia: “Je, mnachukua ahadi kwa Allah kwamba hukumu yao
itakuwa ni ile nitakayohukumu mimi”, wakajibu: “Naam”. Akasema: “Na
hapa pia nimepata ahadi hiyo hiyo? – huku akiashiria upande alioko Mtume wa
Allah huku akiwa amefumba macho kwa ajili ya kumuheshimu Bwana Mtume. Mtume wa
Allah akamjibu: “Naam”. Halafu tena ndipo Sa’ad alipowaambia Baniy
Quraydhwah: “Je, mtairidhia hukumu yangu?”, wakajibu: “Naam”.
Akachukua kwao ahadi ya Allah ya kwamba hukumu itakuwa ni ile itakayotolewa
nae, halafu ndipo aliposema: “Basi hakika mimi ninahukumu wanaume wauawe,
mali zao zigawanwe na wanawake na watoto wachukuliwe mateka”. Alipomaliza
kutoa hukumu yake hii, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:
“Kwa yakini kabisa umewahukumu kwa hukumu ya Allah kutoka juu ya mbingu ya
saba”.
III.
Machinjwaji ya Baniy Quraydhwah:
Baada ya kutolewa
hukumu hiyo kwa wasaliti hawa wasiouheshimu hata mkataba waliouandika na
kuuridhia wenyewe, hukumu iliyopata baraka zote za Allah na Mtume wake. Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaamuru mateka wote wapelekwe Madinah;
makao makuu ya dola ya Kiislamu. Wakapelekwa na kuwekwa katika boma la Usamah
Ibn Zayd, wanawake na watoto wakawekwa katika boma la Kaysah Bint
Al-Haarith. Na akaamrisha silaha, samani na mali yote itwaliwe, ngamia,
kondoo na mbuzi waachwe kwenye malisho yao huko huko. Kisha akaamuru Baniy
Quraydhwah wamwagiwe magunia ya tende, nao wakakesha wakizila kwa midomo yao
kama walavyo ngamia. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akadamkia kwenye
soko la Madinah na kuamuru lichimbwe hapo handaki kubwa. Baada ya handaki
kuchimbwa, akatoa amri waletwe wanaume wa Kibaniy Quraydhwah, wakawa wanaletwa
makundi makundi zikipigwa panga shingo zao na kutupwa handakini.
Huyay
Ibn Akhtwab alikuwa amejitia ngomeni pamoja na Baniy Quraydhwah mara tu baada
ya kuondoka kwa majeshi shirika. Alifanya hivyo kwa ajili ya kuitekeleza ahadi
yake aliyoitoa kwa Ka’ab Ibn Asad. Alipoletwa ili auawe, Mtume wa Allah
alimuangalia na kusema: “Je, Allah hajakutia mikononi mwetu ewe adui ya
Allah?”, akajibu: “Khasaa, Allah amekataa ila kunitia mikononi mwako!
Wallah, nafsi yangu bado haijaacha uadui nawe hata sasa, lakini ni kwamba
mwenye kuacha kumnusuru Allah nae huachwa kunusuriwa”. Alipokwisha kusema
maneno yake haya, akawageukia Mayahudi na kuwaambia: “Enyi watu! Hakika amri
ya Allah haina ubaya, ni hukumu na qadari iliyopitishwa na ni malanyama
waliyoandikiwa Baniy Israil na Allah”. Alipomaliza kusema akakaa, ikapigwa
shingo yake na kutumbukizwa handakini.
IV.
Kuokoka kwa waliosilimu:
Wakasilimu watatu
miongoni mwa Baniy Quraydhwah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akawapa amani ya nafsi, watu wao (wake na watoto) na mali zao.
Mwenzao Amrou Ibn Sa’ad hakuwa amewafikiana na fikra ya Baniy Quraydhwah ya
kutengua mkataba wao na waislamu. Huyu akaachiwa, akaenda kusikojulikana,
Mtume wa Allah akasema: “Huyo ni mtu aliyeokolewa na Allah kwa sababu ya
kutekeleza kwake ahadi yake”. Bwana mwingine Rifaa Ibn Samuel alikuwa
ameomba hifadhi kwa Ummul-Mundhir Al-Answaariyyah, Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akampa hiba mtu wake huyo, nae akasilimu kwa sababu hiyo.
Thabit Ibn Qaysi Al-Answaariy nae akataka kumlipa Zubeir Ibn Baatwaa kwa wema
aliopata kutendewa nae. Akamuomba Mtume ampe hiba mtu huyu, nae akamkubalia,
akampa yeye, familia na mali yake. Lakini Myahudi huyu; Zubeir akaikataa
ihsani na jazaa aliyopewa na kutaka aambatishwe na wapendwa wake miongoni mwa
mayahudi wenzake, ikapigwa shingo yake.
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiwachukulia upole mateka wao na
akiusia watendewe wema. Mara moja alipata kumuona mmoja wa mateka akiwa
kapigwa usoni na kuvuja damu za pua, Mtume akamwabia mlinzi wake: “Kwa nini
umemtendea hivi? Kwani panga halikutosha?”. Halafu akasema: “Wafanyieni
wema uteka wao, wapeni muda wa kulala na wapeni maji na wala msiwakusanyie
joto la jua na joto la silaha”. Na siku hiyo ilikuwa na joto kali mno,
wakawapa mapumziko, wakawapa maji na chakula. Jua lilipopungia, Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaenda na kuamuru kuuawa waliobakia. Mauaji
yakaendelea mpaka usiku hadi walipouliwa wote na walikuwa baina ya mia sita na
mia saba. Kauli nyingine inasema walikuwa ni baina ya mia nane na mia tisa na
nyingine walikuwa ni mia nne tu. Hakuuliwa katika wanawake wao ila mwanamke
mmoja tu, huyu aliwaangushia jiwe la kusagia nafaka waislamu waliokuwa
wamepumzika chini ya ngome zao. Akamuua Khalaad Ibn Suweid-Allah amuwiye radhi.
|