|
SOMO LA KWANZA – MWAKA WA SITA WA HIJRAH.
I.
Mtazamo mpya kuelekea Da’awah:
Baada ya kushindwa kwa majeshi shirika (Ahzaab) na
kushindwa kwa Mayahudi wa Baniy Quraydhwah, Waarabu walianza kuwa na mtazamo
mpya kuielekea Da’awah. Ikawapitia fikra kwamba wimbi hili la Da’awah ya
Kiislamu lazima litakuwa na msukumo wa nguvu isiyo ya kibinadamu, hapana shaka
kwamba linapata msaada kutoka kwa Allah, kwa hivyo hawataweza kamwe kushindana
nalo wakalishinda. Na kwamba hapana shaka Muhammad na wafuasi wake watakuwa
katika haki, kwa hivyo ni dhahiri kuwa hatimaye ushindi na nusra vitakuwa
upande wao. Fikra hizi zilitokana na mkondo wa mambo yanavyojiri, ziliyafanya
baadhi ya makabila ya Waarabu kupunguza uadui wao kuwaelekea waislamu. Na
wakati huo huo makabila mengine yakaanza kujaribu kuwa karibu na waislamu.
Hali ya hewa ya utisho na utukufu wa waislamu na Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-ikazagaza anga na kuzijaza nyoyo za maadui. Mazungumzo katika
baraza za watu sasa yakawa ni kuizungumzia tu nguvu ya ajabu na inayokua kwa
kasi ya ajabu ya waislamu, mamlaka yao pamoja na cheo cha Mtume na nguvu tiifu
inayomzunguka.
Pamoja na hali kuwa hivyo, waislamu hawakubweteka, bali waliendelea
kuwa macho na silaha zao zikiwa mikononi tayari kukabiliana na adui
atakayejitokeza. Hii ni kwa sababu, walitambua fika kwamba wana maadui wengi
na kwamba bado maadui hawa wanasongwa na kiu ya kutaka kulipa kisasi na
kuwaangamiza. Nafsi zao zimejaa chuki dhidi ya Da’awah hii inayo endelea
kukua siku hata siku na dhidi ya kundi hili dogo linaloendelea kupata nguvu
kila kukicha. Kwa ajili hii waislamu wakawa hawana budi kuwa macho na harakati
za maadui zao na kujiandaa kukabiliana na lo lote linaloweza kujitokeza. Na
ulikuwa ni wajibu wao kuwathibitishia watu ya kwamba wao wanastahiki nusra
waliyopewa na Allah. Na wawatie maadui zako fikra ya kwamba wao wana nguvu ya
kupambana na ye yote miongoni mwao na wakaweza kumzuia adui pamoja na wingi na
nguvu zo zote atakazokuwa nazo. Ili lisifikirie kabila lo lote la Waarabu au
Mayahudi kuushambulia Uislamu au kuwa na tamaa ya kuwashinda waislamu baada ya
ushindi ule wa kishindo. Ushindi waliozawadia na Allah kutokana na ikhlasi na
juhudi yao katika dini ya Allah; ushindi wa Ahzaab na ule dhidi ya Baniy
Quraydhwah.
Kumtia khofu adui:
Ni kwa sababu zote hizo, ndipo waislamu
hawakuziweka pembeni silaha zao kwa kutambua kuwa mapambano ya haki dhidi ya
batili bado hayajaisha. Wala hawakulala usingizi mbele ya adui yao kwa
kutegemea kuwa Allah yu pamoja nao na atawasaidia kwa nguvu zake zisizoshindwa.
Walifanya hivi kwa sababu ya kutambua kwao kuwa daima Allah hayuko pamoja na
watu walioghafilika na wala hawapi msaada watu waliobweteka. Watu
wasioshughulika na sababu za ushindi kadiri/upeo wa uweza wao. Baada tu ya
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kumaliza kuwashughulikia Baniy
Quraydhwah mwishoni mwa mwaka wa tano. Akaanza kuwatia khofu maadui wa Uislamu
kila upande, mwanzoni tu mwa mwaka wa sita. Akaanza kupeleka vikosi vya askari
na wakati mwingine yeye mwenyewe akiongoza vita mashariki na magharibi,
kaskazini na kusini. Aliyafanya yote haya kwa lengo la kuwatia khofu maadui
zake wote; Waarabu wenzake na Mayahudi. Akitumia mbinu ya kuwasambaratisha kwa
mashambulizi ya kushtukiza kabla hawajajiandaa na kujikusanya.
III.
Mashambulizi ya Dhwariyah:
Tarehe 10 ya mwezi wa Muharram wa mwaka huu huu wa
sita {May 627 A.D.}, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma
Muhammad Ibn Maslamah. Akiongoze kikosi cha askari wapanda farasi kwenda kwa
Baniy Bakri Ibn Kilaab waliokuwa wamepiga kambi pande za “Dhwariyah”;
mahala palipokuwa umbali wa mwendo wa siku saba kutokea Madinah kupitia njia
ielekeayo Basrah. Akawaendea, akijificha mchana na kutembea usiku mpaka
akawafikia na kuwashambulia kwa ghafla. Akafanikiwa kuwaua kumi miongoni mwao
na wengine kufanikiwa kuponyoka na kukimbia. Akaichukua ngawira mifugo yao;
ngamia mia moja na khamsini, kondoo na mbuzi alfu tatu. Kisha akarejea Madinah
siku moja kabla ya kumalizika kwa mwezi wa Muharram baada ya kuwa nje kwa siku
kumi na tisa.
IV.
Vita vya Baniy Lahyaan:
Mwanzoni mwa mwezi wa Rabiul-Awwal {Mfunguo sita
– Julai 627 A.D.}, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka na kundi
la maswahaba wake mia mbili akiwakusudia Baniy Lahyaan. Hawa ndio wale
wasaliti wa watu wa Rajii; Khubaib na wenzake. Hawa walikuwa wamepiga kambi
katika mojawapo ya mabonde ya Hijaazi, upande wa Makkah, bonde hilo likiitwa
“Fazzaan”. Mtume akidhihirisha kuwa anaelekea Shamu ili Baniy Lahyaan
wasijue makusudio yake, wakakimbia. Akatoka Madinah akielekea upande wa
Kaskazini, akakaza mwendo kuelekea njia ya upande wa Buraidi. Hata
alipokwishakuwa mbali na kudhaniwa kuwa kweli anaelekea Shamu, ndipo
alipochepukia upande wa kushoto na kukaa sawa katika njia ya Makkah. Halafu
akaanza kushuka bonde na kuanza kuelekea upande wa Kusini, akiharakia Fazzaan.
Pamoja na jitihada yake yote hii ya kuficha muelekeo wake, bado Baniy Lahyaan
walikuwa katika hali ya tahadhari na khofu. Walikuwa wakimchunga chunga Mtume
wa Allah na kuzifuatilia kwa karibu nyendo zake. Mtume alipofika mahala pale
walipouliwa maswahaba wake, tayari Baniy Lahyaan walishajua kuwa anawafuata
wao kulipa kisasi cha maswahaba wake. Haoo wakatimua mbio na kwenda kujificha
majabalini, kwa hivyo hakumkuta hata mtu mmoja. Mtume akaamua kupiga kambi
hapo siku moja au mbili na akavituma vikosi vyake kila upande kwenda kuwasaka
wasaliti hao. Lakini wapi hakufanikiwa kumkamata hata mtu mmoja, akafunga azma
kurejea Madinah. Lakini kabla ya kuondoka akalituma kundi dogo la maswahaba
wake kuelekea upande wa njia ya Makkah chini ya uongozi wa Sayyidina Abu Bakri.
Aliwatuma kwa lengo la kuwatia khofu Makurayshi na kuwajulisha kuwa yuko
njiani, wakaenda mpaka wakafika sehemu iitwayo “Kuraai-Ghamiym”. Hapa ni
mahala palipo kuwa umbali wa mwendo wa siku mbili kutokea Madinah, walipofika
hapo wakageuza kurudi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawa nje ya
Madinah kwa kipindi kisichopungua siku kumi na nne. Halafu akarejea katika
siku iliyokuwa na joto kali sana na alikuwa akisema: “Tumerudi tukiwa ni
wenye kutubia na Mola wetu tunamuhimidi. Ninajilinda kwa Allah kutokana na
uchovu wa safari, huzuni ya marejeo na mandhari mbaya kwa watoto na mali”.
V.
Vita vya Dhiy Qirdi:
Baada ya siku kadhaa tangu kurejea kwake Madinah,
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka na maswahaba wake mia tano
kuelekea “Dhiy Qirdi”. Hili ni eneo lenye maji lililokuwa umbali wa mwendo
wa siku moja kutoka Madinah, lilikuwa katikati ya Madinah na Khaibar. Aliamua
kwenda huko kwa ajili ya kujibu mashambulizi yaliyofanywa na Uyainah Ibn
Hiswni dhidi ya mifugo ya Madinah iliyokuwa ikichunga sehemu za “Al-Ghaabah”.
Miongoni mwa mifugo hiyo, alikuwemo ngamia wa Mtume. Usiku mmoja Uyainah
akisaidiana na watu wa kabila la Ghatwfaani walilivamia kundi hilo la mifugo.
Wakamuua mchungaji na kumchukua mkewe na ngamia, khabari ya uchokozi ule dhidi
ya waislamu ikamfikia Salamah Ibn Al-Akwaa; mmoja wa maswahaba wa Mtume. Yeye
akachukua hatua ya kupanda juu ya jabali “Sal-i”, akaanza kupiga yowe la
kuomba msaada. Mayowe yake hayo yakapasua ngoma za masikio ya watu wa Madinah,
hapo hapo ikapigwa mbiu kwa waislamu: “Ewe farasi wa Allah panda!” Kusikia
mbiu hiyo, watu wakaanza kushindana kuiitikia mbiu ya Mtume wa Allah, Bwana
Mtume akampa Al-Miqdaad Ibn Al-Aswad uamiri-jeshi wa kundi lililofika mwanzo.
Akamwambia: “Toka nenda kawafuatilie watu hao mpaka niungane nawe pamoja na
watu wengine”. Wakaenda shoti wakizifuatia nyayo za wachokozi wale,
wakafanikiwa kuwadiriki wa mwisho mwisho, wakawaua watatu miongoni mwao.
Wakafanikiwa kuwaokoa ngamia kumi wenye mimba na wengine kumi wakaponyoka na
adui. Huku nyuma, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatoka na
maswahaba wake mia tano na kuungana na lile kundi tangulizi. Wakakusanyika
Dhiy Qirdi, lakini tayari wachokozi wale walikuwa wameshaponyoka na
kujichanganya kwenye makazi ya kabila la Ghatwfaani. Mtume wa Allah akaamua
kutowafuata huko, akapiga kambi hapo siku moja, kisha huyoo akarejea Madinah
baada ya siku tano.
|