|
I.
Ushujaa wa Salamah Ibn Al-Akwaa:
Kwa hakika Salamah Ibn Al-Akwaa-Allah amuwiye
radhi-alidhihirisha ushujaa mkubwa katika vita hivi, ushujaa uliompelekea
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kummwagia sifa, akisema: “Bora
ya askari wapanda farasi wetu leo ni Abu Qataadah na bora ya askari wetu wa
miguu leo ni Salamah”. Na akampa mafungu yote mawili; fungu la mpanda
farasi na lile la mpiganaji wa miguu. Salamah mwenyewe anasimulia hali
ilivyokuwa: “Nilitoka kabla ya kuadhiniwa kwa adhana ya kwanza (ya swala ya
Alfajiri) na ngamia wa Mtume wa Allah walikuwa wakichunga Dhiy Qirdi. (Anaendelea
kusema): Njiani nikakutana na kijana (mtumishi) wa Abdirahmaan Ibn Auf,
akaniambia: Ngamia wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wameporwa.
Nikamuuliza: Ni nani aliyewachukua? Akajibu: Ghatwafaan. (Anaendelea kusema):
Nikapiga mayowe matatu yaliyowafikia watu wa Madinah. Kisha nika chapua mwendo
mpaka nikawakuta (waporaji) Dhiy Qirdi wakiwa wamepumzika wakinywa maji.
Nikaanza kuwarushia mishale huku nikiimba ubeti huu:
Mimi,
mimi ndiye Ibn Al-Akwaa *** Na leo hii ni siku ya mapambano tu.
Nikaendelea
kuimba na huku nikiwatupia mishale mpaka nikafanikiwa kuwaokoa ngamia na
kuchukua maguo yao thelathini waliyoyaacha kwa haraka ya kukimbizana. (Anaendelea):
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafika na kundi la watu, nikamwambia:
Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi nimewazuilia watu wale (waporaji) kunywa maji
nao wakiwa na kiu, basi waendee upesi sasa hivi. (Mtume) akasema: “Ewe Ibn
Al-Akwaa, tulia na fanya mambo taratibu”. (Akasema): Kisha tukaanza kurejea
na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akinipandisha nyuma yake juu ya
ngamia wake mpaka tukaingia Madinah). Bukhaariy & Muslim kutoka kwa Yazid
Ibn Abiy Ubeid-Allah awarehemu.
Ama
yule mwanamke, yeye alifanikiwa kuwapumbaza watekaji nyara wake na hatimaye
kuwatoroka akimtumia ngamia wa Mtume wa Allah, aliyekuwa miongoni mwa ngamia
waliokuwa wameporwa. Kabla waislamu hawajaanza kulijadili suala lake, tahamaki
huyoo anaingia Madinah na kuwaacha wakipigwa na butwaa. Alipofika kwa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamsimulia khabari yake ilivyokuwa hata
akaweza kutoroka na kufika Madinah salama. Halafu akasema: Ewe Mtume wa Allah,
hakika mimi niliweka nadhiri ya kumchinja ngamia huyu ikiwa Allah ataniokoa
juu yake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatabasamu na kusema:
“Malipo mabaya yaliyoje unayotaka kumlipa ni kumchinja baada ya Allah
kukubeba juu yake na kukuokoa! Hakika hapana nadhiri kwa ye yote katika
kumuasi Allah na wala mtu hawezi kuweka nadhiri kwa asichokimiliki. Hakika si
vinginevyo, huyo ni mmoja wa ngamia wangu (walioporwa), haya rejea kwenu kwa
baraka za Allah!”
Katika
mwezi huu huu wa Rabiul-Awwal, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alimtuma Ukaashah Ibn Mihswan kuliongoza kundi la askari wapandaji
kwenda “Ghamri”. Hili ni eneo lenye maji lililo kuwa likimilikwa na Baniy
Asad kwenye njia iendayo Najid. Akatoka shoti ili awashambulie watu hao kwa
kuwashtukiza, lakini wapi tayari walikwishapata khabari zake na wakakimbia
kabla hajawafikia. Alipofika mahala pao, akaanza kuulizia khabari zao mpaka
akaitokea mifugo yao akaiswaga na walikuwa jumla ya ngamia mia moja. Halafu
huyoo akarejea Madinah bila ya kukumbana na upinzani wo wote wala kupata
madhara.
II.
Kikosi (Sariya) cha vita cha Dhil-Qiswah:
Mnamo mwezi wa Rabiul-Aakhir wa mwaka huu huu wa
sita (Agosti 627 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma
Muhammad Ibn Maslamah pamoja na watu kumi kuwaendea Baniy Tha’alabah upande
wa “Dhil-Qiswah”. Hili ni eneo lililokuwa umbali wa maili ishirini na nne
kutoka Madinah kwa upande wa Hijaaz. Mushrikina wakapata khabari ya kutoka
kwao, wakajificha watu mia moja miongoni mwao, wakawangojea waislamu mpaka
walipolala. Ndipo walipowatokea na kuwashambulia kwa ghafla na kwa nguvu na
kufanikiwa kuwaua wote isipokuwa Muhammad Ibn Maslamah waliyemdhania amekufa
baada ya kuanguka akiwa kajeruhiwa vibaya sana. Wakamuacha hapo, mmoja wa
waislamu aliyekuwa akipita hapo akamuona na kumchukua mpaka Madinah. Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akajua yaliyotokea, akamtuma Abu Ubeidah Ibn
Al-Jaraah na watu arobaini. Hao wakatoka hata walipofika kwenye makazi ya watu
wale, hawakuwakuta ila baadhi ya wanawake, mifugo na samani chakavu.
Wakavichukua ngawira hivyo walivyovikuta bila ya kuwapata mushrikina wale.
III.
Sariya (kikosi) ya Al-Jumuum:
Katika mwezi huu wa Rabiul-Aakhir, pia Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimpeleka Zaid Ibn Haarithah kwenda kwa Baniy
Suleim pande za “Al-Jumuum”, akiwa na kundi la waislamu. Mahala palipokuwa
umbali wa maili nne kutokea Madinah kwenye njia ielekeayo Basrah. Walipofika
kwenye maboma yao, walikuwa tayari wamekwisha tawanyika, wakamkuta mwanamke
mmoja wa kabila la Muzeinah wakamchukua. Huyu ndiye aliye wafahamisha na
kuwaonesha baadhi ya maboma ya Baniy Suleim, humo wakawapata ngamia, kondoo na
mbuzi. Wakawakuta na baadhi ya wanamume wakawachukua mateka, miongoni mwa
mateka hawa alikuwemo mume wa mwanamke huyu. Zayd aliporejea Madinah na
ngawira aliyoipata kutoka kwa maadui wale, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akamuacha huru mwanamke yule na mumewe.
IV.
Sariya ya Al-Iyswi:
Mnamo mwezi wa Jumadaal-Uula wa mwaka huu (Septemba
627 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma tena Zayd Ibn
Haarithah kuliongoza kundi la askari wapanda wanyama mia moja na sabini.
Alimtuma kwenda “Al-Iyswi”, mahala palipokuwa umbali wa mwendo wa siku nne
kutoka Madinah, ili kuuzuia msafara wa biashara wa Makureishi uliokuwa
ukitokea Shamu kuelekea Makkah. Zayd akafanikiwa kuukata njiani na kuuteka,
ndani ya msafara huo kulikuwa na madini mengi ya fedha ya Swafwaan Ibn Umayyah.
Na katika waliowachukua mateka alikuwemo Abul-Aaswi Ibn Ar-rabee; mumewe Bi.
Zaynab Bint ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Walipofika Madinah,
Abul-Aaswi (mkwewe Mtume) akaomba dhamana kwa kumtumia Bi. Zaynab, nae
akamchukulia dhamana mumewe huyo. Akawatangazia watu wakati Mtume alipokwisha
kuswali swala ya Alfajiri, akisema: “Hakika mimi nimemdhamini Abul-Aaswi”.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akauliza: “Enyi watu, je
mumeyaelewa mliyoyasikia?”, wakajibu: Naam. Mtume akasema: “Namuapia yule
ambaye nafsi ya Muhammad i mikononi mwake, sikujua cho chote katika khabari
hii mpaka niliposikia niliyoyasikia. Waumini wote ni mkono (kitu) mmoja, mmoja
wao huzungumza kwa niaba yao na wote wakayaheshimu maneno yake na kuipitisha
dhamana yake. Nasi tumemkubalia dhamana ya aliyechukua dhamana na kutoa
hifadhi”.
Kisha Mtume akaingia nyumbani mwake, Bi. Zaynab akamfuata na kumuomba
amrudishie Abul-Aaswi mali yake iliyochukuliwa. Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-akawaambia maswahaba wake: “Bila ya shaka mnamjua vema mtu huyu (Abul-Aaswi)
alivyo kwetu na mmemchukulia mali. Iwapo mtafanya ihsani na mkamrejeshea mali
yake, hakika sisi tunalipenda hilo na ikiwa mtakataa, basi mali hiyo ni mali
mliyopewa na Allah nanyi mnaistahiki kuliko yeye”. Wakasema: Ewe Mtume wa
Allah, tumekhitari kumrudishia mali yake. Wakaanza kurudisha walivyovichukua
mpaka ikafikia mtu analeta hata ndoo na mwingine analeta chombo cha
kujitwahirishia. Mpaka wakamrejeshea mali yake yote bila ya kubakisha hata
chembe ya kitu”.
|