Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA NNE

 Faida

            I.          Mauaji ya Abu Raafii:

         Katika mwezi wa Ramadhani (Desemba 627 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Abdullah Ibn Atiyk kwenda Khaybar pamoja na watu wanne wa kabila la Khazraj. Aliwatuma kwenda kumuua mmoja wa viongozi wa Khaybar; Abu Raafii Salaam Ibn Abil-Haqiyq. Huyu alikuwa ni mmojawapo wa viongozi wa Mayahudi Banin-Nadhwiyr waliohamia Khaybar baada ya kufukuzwa Madinah na kuchukua uongozi wa hapo Khaybar. Alikuwa ni mfanyabiashara maarufu tajiri anayemiliki biashara nyingi mpaka akawa anaitwa “Tajiri wa Hijaazi”. Na alikuwa ni miongoni mwa waliochangia kwa ari na mali kuyakusanya majeshi shirika dhidi ya Mtume wa Allah katika vita vya Khandaq. Akawasaidia mushrikina katika vita hivi kwa kuwapa mali nyingi mno, vita hivi vilipotamatia kwa kushindwa majeshi shirika na kuuawa kwa Baniy Quraydhwah. Hakukubali kushindwa, akaenda kuwashawishi Ghatwfaani na mushrikina wengine wa Kiarabu waliomzunguka kujiunga upande wake kwa pamoja waunde jeshi kubwa litakalo weza kumsagasaga Mtume na maswahaba wake.

Ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamtumia watu watano hawa wa kabila la Khazraj kumuua mtu huyu mwenye dhamira mbaya kuwaelekea waislamu na Mtume wao. Na akawakataza kuua mtoto au mwanamke, wakatoka mpaka wakafika Khaybar, wakajificha mpaka zilipotulia harakati za mchana kutwa. Ndipo wakamuendea muovu huyu nyumbani kwake usiku wakiongozwa na Abdullah Ibn Abiy Atiyk kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiongea Kiyahudi. Walipofika, akabisha hodi na kusema: Nimemletea zawadi Abu Raafii, mkewe akamfungulia mlango. Mwanamke yule alipoziona silaha akataka kupiga kelele, wakamnyooshea mapanga akafunga domo lake. Wakaingia alipo kuwa mumewe; Abu Raafii na kuanza kumshambulia kwa mapanga yao bila ya kumpa nafasi ya kujitetea, Abdullah Ibn Unaysi akamrukia na kumshindilia panga la tumbo likatokeza upande wa pili na kumuua. Walipokwishamuua wakateremka chini na kuondoka zao, hapo ndipo mkewe alipoweza kupiga kelele za kuomba msaada na kupokewa na watu wengine.

Abdullah Ibn Abiy Atiyk alikuwa na matatizo ya macho; haoni vizuri, akaanguka ngazini walipokuwa wakishuka. Akaumia vibaya mguu wake, wenzake wakambeba na kwenda nae mpaka katika dampo (mahala pa kutupia taka) la mji, wakajificha hapo. Huku nyuma watu wakatoka kuitika kelele zile za msaada na kuanza kuwatafuta wakiwa na vijinga vya moto, lakini hawakufanikiwa kuwaona. Wakaendelea kujificha mahala hapo mpaka zilipotulia harakati za kuwasaka. Wenyewe wanasimulia: Tukambeba mwenzetu na kufika kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-tukampasha khabari ya kuuawa kwa adui wa Allah huku kila mmoja wetu akidai kumuua yeye. Mtume akasema: “Hebu leteni panga zenu”, kila mmoja akawa anampa panga lake akiliangalia, akasema alipolishika panga la Abdullah Ibn Unaysi: “Huu ndio upanga uliomuua, ninauona una athari ya chakula”.

 

         II.          Kujilinda dhidi ya hujuma:

         Hivi ndivyo ulivyomalizika mwaka huu wa sita tangu kuhamia Madinah kwa mapambano mepesi mepesi kama haya. Mapambano yaliyoendeshwa kwa njia ya kumshtukiza na kummaliza adui kabla hajaanza kushambulia. Na lengo la mashambulizi haya halikuwa ni kuanza uchokozi na uadui, kwa sababu kuanza uchokozi na uadui ni msingi na sera isiyokubaliwa na Uislamu. Hakika si vinginevyo, lengo lilikuwa ni kujilinda dhidi ya hujuma tarajiwa iliyothibiti na wala si vinginevyo. Allah Taala anawaambia waislamu: “NA PIGANENI KATIKA NJIA YA ALLAH NA WALE WANAOKUPIGENI, WALA MSIPINDUKIE MIPAKA (mkawapiga wasiokupigeni). KWANI ALLAH HAWAPENDI WARUKAO MIPAKA”. [2:190]

   Kwa hivyo basi, mapambano haya mepesi mepesi yaliyotokea, hakika si vinginevyo yalikuwa ni kwa ajili ya kujibu na kuurudi uadui na uchokozi aliouanza adui. Au yalikuwa na nia ya kumkho fisha adui aliyekuwa na dhamira ya kufanya uchokozi. Na bila shaka mapambano na mashambulizi haya yalifanikiwa kufikia malengo yake kwa kiasi kikubwa kabisa. Kwani mwaka wa sita haukumalizika ila na haiba ya waislamu ikawa imeshaziingia nafsi za makabila ya Kiarabu yaliyokuwa majirani na Madinah. Na hali ya hewa ikaanza kuwa ya utulivu na amani baina ya waislamu na majirani zao. Na ikawa inamkinika kuanzisha mafungamano na mahusiano ya ujirani mwema baina yao kwa kuyapisha yapite yaliyokwishapita na kuzizika tofauti zao. Na kuanzisha ukurasa mpya wa ushirikiano chini ya anga la amani na utulivu.

 



 | Tuandikie |