Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SULUHU (MKATABA WA AMANI)YA HUDAYBIYA

 Faida

           Ilikuwa ni fursa na wakati muafaka wa kuizuru nyumba ya Allah (Al-Ka’abah), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaazimia kufanya ziara hiyo pamoja na wafanya ziara wengine miongoni mwa Waarabu. Ni katika mwaka huu wa sita pia, ndimo ilimofaradhishwa nguzo ya tano ya Uislamu; ibada ya Hijjah sambamba na ile ya Umrah. Usiku mmoja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliona ndotoni kwamba yeye na maswahaba wake wanaingia katika nyumba tukufu ya Allah. Wakiwa ni wenye amani, wamenyoa nywele na wengine kupunguza wakiwa hawamkhofu adui atakayewazuia wasiingie. Mtume akafurahishwa sana na ndoto yake hii na akawasimulia maswahaba wake, nao pia wakafurahi na kujawa na furaha. Wakaiyakinisha ndoto hiyo ya Mtume kuwa ni ukweli utakaotokea bila ya shaka, kwa sababu waliamini kuwa ndoto za mitume huwa ni kweli na haki. Ndoto hizo huwa ni ilhamu kutoka kwa Allah juu ya jambo litakalotokea kabla ya kudhihiri kwake katika ulimwengu wa maono. Kwa hivyo shauku ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na ile ya waumini katika kuizuru Al-Ka’abah ikarudufishwa na kuamshwa na ndoto hii. Ndipo Mtume alipotia azma ya kuizuru nyumba hii tukufu ya Allah katika mwaka huu. Fursa na mazingira yalikuwa muafaka yanayoruhusu kufanyika kwa ziara hii, kwani tayari amani imekwisharejea tena Madinah baada ya kutimuliwa kwa Mayahudi. Wanafiki wamevunjwa nguvu baada ya kuondoka kwa washirika na wafadhili wao wakuu  na mabedui huko majangwani wamekuwa si tishio tena kwa waislamu bali waislamu ndio wamekuwa tishio kwao. Wote hawa walitishwa na nguvu ya waislamu katika kuitetea, kuilinda na kuihami imani yao, kwa hivyo kitisho cha Uislamu kikazitamalaki nyoyo zao na kuzitetemesha nafsi zao. Msimu wa ibada ukawadia na Waarabu kutoka pande za mbali na zile za karibu wakaanza kujiandaa kwa ajili ya ziara hii tukufu. Kwa nini basi waislamu wasiitumie fursa hii, wakaikusudia nyuma tukufu pamoja na wakusudiaji wengine na wakaingia pamoja na wenye kuingia?! Laala (pengine) Makureishi zimelainika tabia zao na kupunguza uadui wao dhidi ya Uislamu na waislamu baada ya kushindwa kwa njia zote za nguvu walizojaribu kuzitumia. Kila walipojaribu kuudhoofisha Uislamu ndio ulikuwa ukizidi nguvu na kila jaribio la kuuzima ndio lilizidisha nuru yake. Kila walipofanya jaribio la kuutokomeza ndio watu walizidi kuujongelea na kuingia makundi kwa makundi. Kwa kuyazingatia yote haya haikupita katika dhana kwamba Makureishi watawazuilia waislamu peke yao kufanya ziara ya nyumba hii. Nyumba iliyofanywa sawa sawa kwa watu wote, kwa wakaao humo na wale wageni.

Ikiwa watawazuia watakuwa wameudhihirishia ulimwengu udhalimu na uadui wao. Ili Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-awakatie Makureishi hoja zote na kuwahakikishia wao na watu wote. Kwamba yeye hakika si vinginevyo amekuja katika nyumba ya Allah kufanya ziara kwa amani na kwamba hakuja kwa vita. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anahadithia: “Alitoka katika mwezi wa Dhul-Qa’adah kwa ajili ya kufanya Umrah akiwa hataki vita. Akawatolea wito wa kutoka pamoja nae majirani zake miongoni mwa watu wa vitongoji vilivyoizunguka Madinah. Alifanya hivyo huku akichelea Makureishi wasije kumtangazia vita au kumzuia kuingia Makah”. Lakini Mabedui (wakazi wa vitongojini) aliowataka kutoka pamoja nae, walidhania kwamba lazima tu vitazuka vita baina ya Mtume na Makureishi. Na kwamba Mtume na maswahaba wake watahiliki tu katika vita hivi, kwa ajili hii wakakataa kuambatana na Mtume katika safari hii ya hatari, wakichelea kujitia maangamivuni wao wenyewe. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anaendelea kuhadithia: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatoka na Muhajirina na Answari na baadhi ya Waarabu waliojiunga pamoja nao. Akawaswaga pamoja nao wanyama wa sadaka; ngamia sabini na akahirimia Umrah ili kuwatoa watu wasiwasi wa vita. Na ili watambue kwamba yeye hakika si vinginevyo ametoka kwa ajili ya ziara ya nyumba tukufu ya Allah na kuiadhimisha”.

 

  IV.          Mtume atoka na maswahaba wake bila ya silaha:

          Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamuachia ukhalifa wa Madinah, Abdullah Ibn Ummu Maktuum, swahaba wake aliyekuwa kipofu. Katika safari yake hii akaambatana na mkewe Ummu Salamah, akatoka Madinah mwezi mwandamo wa Dhul-Qa’adah (Februari 628 A.D.). Akatoka akiwa na waislamu wapatao alfu moja na mia tano wakiwa hawakuchukua silaha zaidi ya majambia yao yaliyofutikwa kwenye ala zake. Hizi zilikuwa ni silaha za kawaida ambazo kila msafiri hana budi kuchukua katika Bara Arabu wakati huo. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akampanda ngamia wake aliyekuwa akiitwa “Al-Qaswaa”, akaenda na maswahaba wake mpaka wakafika “Dhul-Hulayfah’. Hapa ni mahala palipokuwa kiasi cha umbali wa maili sita kutoka Madinah, wakaswali Adhuhuri hapo. Baada ya kumaliza kuswali akaamuru waletwe ngamia, wakavishwa vitambaa, wakatiwa alama zioneshazo kuwa ni wanyama wa sadaka na kuvikwa shingoni mwao kitu mithili ya vidani. Hii ndio ilikuwa ada na desturi ya Waarabu kwa wanyama wanao wachukua kuwachinja na kuwatoa sadaka katika msimu wa Hijjah. Kisha ndipo akahirimia Umrah na kufuatiwa na maswahaba, halafu ndipo msafara wa kuelekea Makkah ulipoanza. Wakiwa wamevaa mavazi ya Ihraamu wakileta Talbiyah: “LABBAYKA ALLAAHUMMA LABBAYKA, LABBAYKA LAA SHARIYKA LAKA LABBAYKA, INNAL–HAMDAH WAN-NI’IMATA LAKA WAL-MULKU, LAA SHARIYKA LAKA”. Maana: “Labeika (nakuitika) ewe Mola wa haki labeika, labeika huna mshirika labeika. Hakika himda njema, neema (zote) na ufalme ni wako, huna mshirika”. Ikawa kila anayewaona katika mandhari hii nzuri ya kupendeza, hana shaka kwamba wao wanakuja kwa amani, hawakusudii ila kutekeleza ibada zao tu basi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamtanguliza mbele yao Ubbaad Ibn Bishri pamoja na wapanda wanyama ishirini. Ili wawe watangulizi wao wa kuangalia usalama wa njia na akamtuma Bishri Ibn Sufyaan kama mpelelezi wake kwa Makureishi. Akapeleleze dhamira na maoni yao juu ya ziara yake hii aliyoikusudia na kisha aje kumpasha khabari kabla ya kuingia Makkah.

 



 | Tuandikie |