Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

V. MAKUREISHI WASHIKILIA MSIMAMO WAO WA KUTOMRUHUSU MTUME KUINGIA MAKKAH NA WAJIANDAA KWA VITA :

 Faida

           Makureishi walipandwa na mori/hamasa za kijahilia pale zilipogonga ngoma za masikio yao khabari za ujio wa Mtume wa Allah. Wakashika msimamo wa kutokumruhusu Mtume kuingia Makah kwa namna yo yote iwayo na wakaanza kujiandaa kwa vita ikiwa atang’ang’ania kuingia bila ya ridhaa yao. Wakamtuma Khaled Ibn Al-Waleed na Ikrimah Ibn Abu Jahli kuliongoza kundi la mashujaa wao mia mbili, kwenda “Kuraail-Ghamiym” kuwazuia waislamu wasiingie Makah. Wakawatolea wito wa kutoka pamoja nao washirika wao katika Wahabeshi na watu wa Thaqiyf. Wakatoka wakaenda mpaka wakafika mahala paitwapo “Baldahi”, nje kidogo ya Makah wakapiga kambi hapo. Wakasimika mahema na kujenga vibanda vya muda, wakakaa na wake na watoto wao na wakaweka wapelelezi juu ya majabali kuchunguza harakati zote za adui yao. Kisha wapelelezi hawa wakawa wakipashana khabari kwa sauti, wakisema: “Muhammad amefanya kadha wa kadha”, wakipokezana hivyo mpaka khabari zikifika kambini kwao.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipofika mahala panapoitwa “Usfaani” na akawa umbali wa mwendo wa siku mbili kutokea Madinah. Akakutana na Bishri Ibn Sufyaan, huyu akampasha khabari za Makureishi, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipozisikia khabari hizi akasema: “Ee ole wao Makureishi, wameshaliwa na vita! Wangelipatwa na nini lau kama wangeliniachia njia pamoja na watu wengine. Ikiwa watanigusa, kitakuwa hicho wakitakacho na iwapo Allah atanipa ushindi wataingia Uislamuni kwa makundi? Wallah, sitaacha kuendelea kupigana nao kwa ajili ya hiki alichonituma kwacho Allah, mpaka Allah aipe ushindi dini hii au mimi nife!”

 

SOMO LA TANO.

 

       I.          Mtume ajitahidi kwa jitihada zote kuepusha vita:

           Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakupendelea kabisa kuzuka kwa vita na alijitahidi sana kuonesha kuwa safari yake hii ni safari yenye malengo ya amani. Safari iliyojitenga na sababu zote zinazoweza kuitia dosari na imeepukana na mambo yote yanayo pingana na malengo yake. Pamoja na jitihada zote hizi za makusudi katika kuepusha vita, alipoona Makureishi wamejiandaa kwa vita na wametuma vikosi tangulizi ili kumzuia asiingie Makah. Na wanatumia nguvu kumzuia kufikia lengo la safari yake hii ambalo si jingine zaidi ya kuizuru nyumba tukufu ya Allah. Akaonelea ni vema abadili muelekeo na njia ya safari yake, badala ya kupita njia ambayo tayari ina kizuizi cha Makureishi walio tayari kwa vita, apite njia nyingine ili kuepusha vita. Kwani kama atashikilia tu kupita njia hiyo hiyo ya kawaida ni lazima tu atakutana na Makureishi. Ambao huenda watamlazimisha kuingia katika matumizi ya nguvu ambayo hakuyapendelea, hapo ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipowaambia maswahaba wake: “Nani atakayeweza kutupitisha njia nyingine isiyo hii?”. Akaja mtu mmoja kutoka katika kabila la Aslama, akawaongoza katika njia ngumu sana iliyowawia uzito waislamu kuipita. Kisha akawapitisha katika ardhi tambarare kwenye bonde la ufa, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaamuru wapite upande wa kulia. Wakaenda mpaka wakafika kwenye maporomoko ya Hudeibiyah kwa chini ya Makah umbali wa mwendo wa siku moja mpaka kuingia Makah.

Walipofika mahala hapo, ghafla ngamia wa Mtume aliyekuwa akiitwa “Al-Qaswaa” akakita magoti na kugoma kuendelea na safari. Watu wakaanza kumpigia kelele ili ainuke na kuendelea na safari, makelele yao hayo hayakusaidia kitu kwani Al-Qaswaa hakuinuka. Watu wakashangazwa mno na tukio hili, wakasema: “Al-Qaswaa amegoma kufuata amri (ameasi)”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawajibu: “Hajagoma na wala hana tabia hiyo, lakini kilichomzuia kusonga mbele ni kile kile kilichowazuia watu wa ndovu kuingia Makah. Namuapia yule ambaye nafsi ya Muhammad i mkononi mwake, leo Makureishi hawataniitia hatua ambazo wataniomba ndani yake kuunga udugu na kuyaadhimisha matukufu ya Allah, ila nitawaitika”. Halafu akawaamuru watu kupiga kambi hapo hapo walipo. Na mahala hapo palikuwa ni bonde kame lisilo na maji zaidi ya maji kiduchu tu yaliyokuwa katika shimo moja tu. Watu wakaanza kuyatumia maji yale kidogo kidogo na kwa uangalifu mkubwa mpaka yakaisha. Walipoyamaliza na pakawa hapana tena tone la maji, wakamshtakia Mtume wa Allah kiu chao. Nae Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaja akakaa kwenye ukingo wa kisima (shimo) kile, akaomba aletewe ndoo yenye maji ya kisima hicho. Akaletewa, akachota choto moja akasukutua na kuomba Mungu, kisha akayatemea kisimani mle na kuwaambia: “Kiacheni kisima hiki kwa muda”, wakakiacha kwa kitambo kidogo tu, basi haukupita muda ila maji yake yalijaa na kufurika. Watu wakanywa, wakanywa hata kikakatika kiu na wakajitwaharisha na kuwanywesha wanyama wao. Wakaendelea kuyatumia maji yale bila ya kwisha mpaka wakaondoka.

 

    II.          Mtume atangaza nia yake ya amani kwa wajumbe wa Makureishi:

          Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipotuama hapo Hudeibiyah, alijiwa na Budeil Ibn Warqaa pamoja na kundi la watu wa kabila la Khuzaa. Wamekuja kumuuuliza madhumuni ya msafara wake huu na ikumbukwe kwamba hawa Khuzaa walikuwa ni washirika wa Mtume tangu zamani. Budeil alipofika kwa Mtume alimpasha khabari za maazimio ya Makureishi na akamuuliza Mtume sababu/nia ya majaji yake haya. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamjibu: “Hakika sisi hatukuja kupigana na mtu, sisi tumekuja kufanya Umrah tu. Ikiwa Makureishi watataka tutawapa muda na watuachie njia tuingie Makah pamoja na watu wengine. Na iwapo watakataa, basi naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad i mkononi mwake, wallah nitapambana nao hadi kufa”. Budeil na ujumbe wake wakarejea kwa Makureishi na kuwaambia: “Hakika nyinyi mnamfanyia haraka Muhammad, kwani yeye hakujia vita, hakika si vinginevyo amekuja kuizuru Al-Ka’abah”. Wakasema: “Hata kama hakuja kwa vita, basi wallah kamwe hataingia Makah kwa nguvu bila sisi kupenda wala Waarabu hawatatuzungumza kwa unyonge huo katu”.

 

 



 | Tuandikie |