|
Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani zimshukie
alipokaribia umri wa miaka arobaini alipenda kukaa peke yake faraghani na kujitenga na
jamii yake; jamii ya watu wa Makkah. Jamii iliyozama katika kiza cha ushirikina na tabia
mbaya zisizo na chembe ya utu. Kujitenga huku hakukuwa ni kwa sababu alikuwa anaichukia
jamii yake, la hasha. Bali ni kwa ajili ya kuyachukia maovu yaliyokuwa yakitendwa na jamii
yake. Kwa hivyo akaonelea ni vema akae faraghani atafakari ni jinsi gani atakavyoweza
kuinusuru na kuitoa jamii yake katika itikadi ile potofu ya ushirikina, itikadi ya
kuyaabudia masanamu yaliyotengenezwa na mikono yao wenyewe.
Baada ya kufikiri kwa kina, ni wapi katika mji wa Makkah
ambapo anaweza kupata nafasi ya faragha, hakupapata. Hapo ndipo akaamua atoke nje kabisa
ya mji wa Makkah. Akaamua ajitenge kwa kukaa ndani ya pango la Hiraa.
Hiraa ni pango dogo lililopo juu ya jabali Nuur. Jabali hili liko kiasi cha
umbali wa wa maili tatu kutoka mji wa Makkah, mahala pasipo na nyumba wala mashamba. Pango
la Hiraa lilikuwa linatisha na lenye upweke mkubwa, upweke ambao ulizidishwa
na kiza kilichotanda mahala pale. Hapa ndipo Mtume aliona patamfaa kutafakari jinsi ya
kuikomboa jamii yake kutokana na utumwa wa ushirikina. Akawa anachukua chakula cha kutosha
kutoka kwa mkewe Bi Khadija na kwenda zake faraghani katika pango la Hiraa. Huko alikaa
kiasi cha siku kumi na mara nyingi akitimiza mwezi kamili. Kazi kubwa aliyokuwa akiifanya
huko ilikuwa ni kumuabudu Mola wa haki kupitia mafundisho sahihi yaliyoachwa na babu yake,
Nabii Ibrahim Rehema na Amani ziwashukie wote -. Athari ya mafundisho ya Nabii
Ibrahim alikuwa ingali hai miongoni mwa makurayshi wachache ambao waliendelea kufanya
ibada kwa mujibu wa mafundisho hayo. Naye Mtume akawa anafanya ibada kwa kuufuata muongozo
huo huo.
SURA YA PILI
SOMO LA KWANZA
i)
KUPEWA UTUME
Mtume Muhammad Rehema na Amani zimshukie
alipofikia umri wa ukamilifu, umri ambao akili ya mwanadamu huwa imepevuka na kukomaa,
umri wa miaka arobaini. Huu ukawa ndio wakati muafaka wa kupewa kazi nzito, ngumu na yenye
kuhitaji subira ya kutosha. Kazi ya kuinusuru jamii yake na kiza totoro cha ushirikina.
Hapo ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akamkabidhi dhamana ya utume, awabashirie watu wema
kupata pepo ya milele kwa kumfuata na awakhofishe na adhabu kali ya moto wa milele wale
wote watakaomkadhibisha na kuacha kumfuata. Awalinganie watu kuwatoa katika viza vya
ushirikina kuwapelekea katika nuru ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu asiye na mshirika.
Katika usiku wa mwezi kumi na saba (17) Ramadhan mwaka wa
kumi na tatu kabla ya hijra sawa na Mwezi Julai mwaka mia sita na kumi na moja (611)
Miladia Mtume akiabudu faraghani ndani ya pango la Hiraa hapo ndipo ulipomshukia
wahyi/ufunuo kwa mara ya kwanza. Jibriil Amani imshukie malaika mwaminifu wa
wahyi alimtokezea na kumwambia Soma Mtume akamjibu Mimi si mwenye
kusoma Jibril akamshika Mtume na kumgandamizia kifuani kwake kama vile anamkaba,
kisha akamuachia na kumwambia tena Soma Mtume akamjibu kama alivomjibu mwanzo
Mimi si mwenye kusoma Jibril akamkamata tena na kumgandamiza na kumwambia
Soma hii ikiwa ni mara ya tatu, Mtume akauliza Nisome nini ? Hapo
sasa Jibril ndipo akamwambia : SOMA KWA JINA LA MOLA WAKO ALIYEUMBA, AMEUMBA MWANADAMU KWA
PANDE LA DAMU. SOMA NA MOLA WAKO NI KARIMU SANA. AMBAYE AMEMFUNDISHA (Binadamu elimu zote
hizi) KWA WASITA (msaada) WA KALAMU (zilizoandika vitabu, watu wakapata elimu)
AMEMFUNDISHA MWANADAMU (chungu ya) MAMBO ALIYOKUWA HAYAJUI [96:1-5]
Kisha Jibriil akashika njia akaenda zake, naye Mtume kwa wepesi
akarejea kwa mkewe Bi Khadija akiwa amejawa na khofu kubwa kutokana na kiumbe mgeni,
malaika kwa mara ya kwanza. Akasema Nifunikeni ! Nifunikeni! Mkewe akamfunika
maguo kutokana na alivyokuwa akitetemeka kama mtu mwenye homa kali kabisa. Alipotulizana
ndipo akamuuliza kulikoni, mbona yuko katika hali hiyo? Mtume akamuhadithia mkewe hali
ilivyokuwa mwanzo hadi mwisho na kusema Ninaichelea nafsi yangu na shetani/pepo
mbaya mkewe akamtuliza na kumwambia Sivyo hivyo ! Wallah Mwenyezi Mungu kamwe
hatokufedhehesha. Kwani unaunga udugu, unasema kweli, unasaidia mnyoge, unamkirimu mgeni,
unawapa sadaka masikini na unasaidia katika majanga
Halafu ndipo Bi Khadijah alipoamua kumpeleka Mtume kwa mwana wa
ammi yake Waraqah ibn Naufal, huyu alikuwa ni mwanachuoni mwenye elimu ya vitabu
vitakatifu kabla ya Qur-ani {Taurati, Zaburi na Injili}. Bi Khadijah akamuhadithia binamu
yake yote yaliyomtokea Mtume kama alivomueleza mwenyewe. Waraqah kutokana na elimu
aliyokuwa nayo akamtoa wasiwasi Mtume na kumwambia Huyu ndiye Naamus {Jibril}
aliyekuwa akimshukia Issa bin Maryam, basi furahi kwani wewe ndiye Mtume wa umati
huu
Baada ya hapo wahyi ulikatika kwa kipindi kirefu, kukawa hakuna
mawasiliano yoyote baina ya mbinguni na ardhini. Kukatika huku kwa wahyi hakukuja kwa
bahati mbaya tu, bali hekima yake ilikuwa ni kuizidisha shauku na kiu ya Mtume kwa wahyi.
Mtume akapatwa na huzuni kuu na akawa akienda na kurudi pangoni Hiraa, huenda pengine
Jibril atamjia tena, lakini wapi hakumuona. Hali ilikuwa hivyo mpaka Mtume akadhania kuwa
Mola wake amemkasirikia na kumtupa. Baada ya kipindi hicho kigumu ndipo Wahyi ulipoanza
kushuka tena na Mola wake akamtuliza kwa kumwambia : HAKUKUACHA MOLA WAKO WALA
HAKUKASIRIKA (nawe Ewe Nabii Muhammad) NA BILA SHAKA (kila) WAKATI UJAO (utakuwa) NI BORA
KWAKO KULIKO WAKATI ULIOTAGULIA [93:3-4]
Kisha tena ikamshukia kauli yake Mola : EWE ULIYEJIFUNIKA
MAGUO. SIMAMA UONYE (viumbe) [74:1-2].
Huu ndio ukawa ndio mwanzo wa kazi na safari ndefu yenye taabu
na misukosuko mikubwa ya kufikisha ujumbe wa Mola wake Mtukufu kwa watu wote.
|