Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

III. UJUMBE WA URWAH IBN MASOUD

 Faida

           Akainuka Urwah Ibn Masoud; kiongozi wa kabila la Thaqiyf, huyu alikuwa ni mtu mwenye sauti na busara, akawaambia: “Bila ya shaka mtu huyu (Muhammad) amekupeni mipango ya uongofu, basi ikubalini, hebu niacheni nikazungumze nae”. Wakamwambia: “Nenda”, akamuendea Mtume na kumwambia: “Ewe Muhammad, hakika mimi nimewaacha huko watu (jamaa) wako wamewatolea wito watu kutoka kuja kupambana nawe. Nao wameapa kwa Allah kwamba hawatakuruhusu kuifikia Al-Ka’abah ila uwaue wote. Hakika si vinginevyo, mbele yako una mambo mawili tu ya kuchagua; ama uwasagesage na kuwaua watu wako upate kuifikia Al-Ka’abah, nasi hatujapatapo kumsikia mtu aliyewamaliza watu wake kabla yako. Au wakutupe na kukuacha peke yako hawa watu ulio nao, kwani mimi naona watu ulio nao ni watu hovyo hovyo tu wasio na muelekeo wala hazijulikani nasabu zao”. Sayyidina Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-akamshtumu na kumwambia maneno makali: “Ole wako wee! Hivi sisi tunaweza kumtupa mkono na kumuacha peke yake?”

   Wakati Urwah alipokuwa akiongea na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akizishikashika ndevu za Mtume. Alifanya hivyo ikiwa ni kufuata ada/desturi ya Waarabu wakati wanapokuwa na mazungumzo yenye nia ya kuunga udugu na kuleta mapatano. Wakati akifanya ada hiyo, Mugheerah Ibn Shu’ubah ambaye ni mwana wa kaka yake Urwah, alikuwa amesimama karibu kabisa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Akiwa amevaa kofia ya chuma na kushika upanga, kila mara Urwah alipokuwa akiunyoosha mkono wake kuzishika ndevu za Mtume, Mugheerah aliugonga mkono wake kwa ubapa wa upanga huku akimwambia: “Ondosha mkono wako usoni kwa Mtume wa Allah kabla sijaukata”. Urwah  nae akamjibu akiwa hamjui (kuwa ni mwana wa nduguye): “Ole wako! Ukali na ugumu wa moyo ulioje uliokuvaa!”, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akitabasamu (kutokana na majibizano hayo baina ya mwana na ami yake).

   Urwah akaondoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa ameguswa mno na jinsi maswahaba wanavyo mpenda na kumuadhimisha Mtume wao. Na namna wanavyo shindana kumtii na kutekeleza amri yake, akarejea kwa Makureishi na kuwaambia: “Enyi kusanyiko la Makureishi! Hakika mimi nilimtembelea Kisra katika ufalme wake, nikamtembelea Qayswar katika ufalme wake na Najaashi katika ufalme wake. Hakika wallah, mimi sijapatapo kumuona mfalme kwa watu wake kama alivyo Muhammad kwa maswahaba wake! Wallah, hawamkazii macho, hawainui sauti zao mbele yake na kunamtoshea yeye kuashiria tu jambo na likatendwa. Na nimewajaribu watu hao (waislamu), nikagundua ni watu wasiojali kitawapata nini katika kumlinda mtu wao (Mtume), haya basi ifikirieni upya rai yenu. Yeye amekwisha kuelezeni mipango yake, basi enyi watu nyie wekeni muda wa amani baina yake nanyi na muukubali mpango aliokuja nao kwenu. Hakika mimi ni mtoa ushauri nasaha kwenu pamoja na kuchelea kwangu kuwa huenda msiushike na kuufuata!”. Makureishi hawakuisikiliza rai na ushauri mzuri wa Urwah na wala hawakuiitika suluhu aliyo waraghibishia. Urwah hakuwa na la kufanya kwa vichwa maji hawa ila kurejea Twayf na kundi (ujumbe) lake.

 

  IV.          Ujumbe wa Hulaysi; kiongozi wa Wahabeshi.

          Hulaysi Ibn Alqamah; kiongozi wa Wahabeshi akasema: “Hebu niacheni nami nimuendee”, wakamwambia: “Haya muendee”. Hulaysi alipochomoza kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-(Mtume) akasema: “Huyo ni fulani, nae ni katika watu wanaowatukuza wanyama wa sadaka (hadyu), basi wawekeni wanyama hao mbele yake”. Wakafanya kama alivyoagiza Mtume na wakampokea kwa mripuko wa Talbiyah. Hulaysi alipowaona wanyama wa sadaka wakimiminika bondeni wakiwa wamepambwa na akawaona waislamu wakiwa wamehirimia. Wakiwa wamechoka na nywele timtim kutokana na uchovu wa safari ndefu. Hulaysi akaamua kurejea bila ya kufika kwa Mtume kwa ajili ya kutukuza aliyoyaona na akawaambia Makureishi: “Wallah sisi hatukufanya ushirika nanyi ili mumzuilie na nyumba ya Allah mtu aliyeijia akiutukuza utukufu wake na kuitekeleza haki yake. Namuapia yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, mumuachie ayatekeleze aliyoyajia  au nitawatolea wito Wahabeshi waondoke wote (na kukuacheni peke yenu)!”. Makureishi wakamwambia: “Ewe Hulaysi wee! Yote uliyoyaona ni vitimbi na hila za Muhammad na maswahaba wake, hebu tuache tukate shauri tutakaloliridhia sisi wenyewe”.

 

     V.          Ujumbe wa Mtume kwa Makureishi:

          Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaona ni vema sasa yeye apeleke ujumbe wake rasmi kwa Makureishi. Ili awathibitishie kwamba ni hakika yeye amekuja kuizuru nyumba ya Allah na wala hakujia vita. Akamtuma Kharaash Ibn Umayyah Al-Khuzaaiy kuwafikishia ujumbe wake huo, lakini wapi Makureishi wakaendelea kutia pamba za masikio. Isitoshe wakamchinja ngamia wa mjumbe aliyetumwa kwao na Mtume na tena wakataka kufika mbali zaidi kwa kumuua na mjumbe mwenyewe kama si kuzuiliwa kufanya hivyo na Hulaysi; kiongozi wa Wahabeshi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akalistahamilia hilo na kuliona si kitu, ijapokuwa kuwadhalilisha wajumbe ni jambo lisilostahamilika wala kusamehewa miongoni mwa Waarabu. Ndipo tena Mtume alipoazimia kuwapelekea mtu wa karibu mno nao, akamtuma Sayyidina Uthman Ibn Affaan. Mjumbe huyu wa pili wa Mtume wa Allah, hakuweza kuingia Makkah mpaka alipochukuliwa dhamana na Abaana Ibn Sa’ad Ibn Al-Aaswiy ambaye alikuwa ni binamu yake. Uthman akakutana na viongozi wa Makureishi na kuwafikishia ujumbe wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Akawahakikishia ukweli wa nia ya majaji ya Mtume kuwa ni kutaka kuizuru nyumba ya Allah. Lakini wapi bado Makureishi wakaendelea kuwa ni viziwi wasiotaka kuisikiliza sauti ya haki wala kuitikia wito wa amani. Uthmaan akajaribu kuwakinahisha kadri alivyoweza, lakini hawakukinahika na badala yake wakaamua kumzuilia na kumshikilia kwa siku tatu. Kambini kwa waislamu ikatangaa khabari kwamba Uthman ameuliwa, uvumi huu ukasambaa mpaka ukamfikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kama kwamba ni kweli na hakika isiyo na shaka.

 

 



 | Tuandikie |