Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA SITA

 Faida

       I.          Kiapo cha utii (baia) cha Ridhwaan.

          Hapa ndipo hali ya hewa ilipobadilika na kuwa si shwari tena na ikawa hapana budi sasa tatizo hili lipatiwe ufumbuzi mwingine baada ya juhudi za kidiplomasia kushindwa. Kwani tayari Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa amekwisha itangaza wazi nia yake ya amani. Na akalidhihirisha hilo kwa kauli sambamba na matendo yake tangu alipopiga hatua ya kwanza akitoka Madinah kuelekea Makah. Na akawaitia Makureishi kwenye njia zisizo na matumizi ya nguvu ili kuzuia umwagikaji wa damu usio wa lazima. Na ili kubakisha mafungamano ya kidugu na kuhifadhi utukufu wa nyumba tukufu ya Allah na kuchunga heshima ya mwezi mtukufu. Lakini wapi, njia zote hizi hazikusaidia kuwalainisha Makureishi na kuwafanya wabadili msimamo wao shupavu. Mpaka subira ikafikilia ukomo wake, hali ya hewa sasa ikawa haihitaji subira tena na wala haiwezi kutengenea kwa subira aslani. Ikawa sasa matumizi ya nguvu yakabiliwe na matumizi ya nguvu mfano wake, hapo ndipo Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliposema: “Hatutaendelea tena na hali hii ila kupambana na watu hawa”. Na akawatolea waislamu wito wa kumbai (kula kiapo cha utii) juu ya vita dhidi ya Makureishi. Watu wakaanza kuharakia kumbai huku wakipigana vikumbo na kukanyaga vifaa/mizigo yao. Zoezi hili la baia lilipomalizika, wakachukua silaha zao na kuwa tayari kwa vita. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akambaia Uthman, akasema: “Hakika Uthman amekwenda kuitekeleza haja ya Allah na haja ya Mtume wake, basi mimi ninafanya baia kwa niaba yake”. Akakipiga kiganja chake cha kushoto kwa kile cha kulia na kusema: “Huu ni mkono wa Uthman”.

     Tukumbuke kwamba maswahaba-Allah awawiye radhi-hawakuwa wamechukua silaha zaidi ya majambia yao. Na wala hakukuwa na mizania ya idadi yao na ile ya Makureishi hata kidogo. Pia hawakuwa na mavazi ya vita yatakayo wakinga na mapigo ya adui katika medani ya vita. Na walikuwa wanajua kwa yakini kwamba kuingia vitani katika mazingira hayo ni kuyahatarisha maisha yao. Lakini pamoja na yote hayo, bado walimbai Mtume juu ya kuingia vitani kwa hamasa, ari, mori na nguvu kubwa. Wakaziuza nafsi zao kwa Allah kwa ajili tu ya kupata radhi zake-Allah awawiye radhi na awatakabalie baia yao hiyo takatifu. Baia yao hiyo ikawa ndio sababu ya ushindi dhahiri wa kishindo ambao kwao Allah aliwafungulia waja wake milango ya nusra na kheri. Na baada yake Uislamu ukawa katika mkondo wa ushindi na nguvu mpaka ukazishinda dola zote zilizouzunguka: “KWA HAKIKA ALLAH AMEWAPA RADHI WAISLAMU WALIPOFUNGAMANA NAWE CHINI YA MTI; NA ALIJUA YALIYOMO NYOYONI MWAO. BASI AKATEREMSHA UTULIVU JUU YAO, NA AKAWAPA KUSHINDA KWA ZAMA ZA KARIBU. NA NGAWIRA (nyara) NYINGI WATAKAZO ZICHUKUA, NA ALLAH NI MWENYE NGUVU (na) MWENYE HIKIMA”. [48:18-19]

 

    II.          Makureishi walegeza msimamo wao na kuamua kukaa katika meza ya suluhu.

          Khabari za baia hii tukufu zikagonga ngoma za masikio ya Makureishi na kitendo hiki chenye kuonesha upeo wa imani kikawaweka sawa na kuwarudishia busara pevu. Wakaanza kuufikiria upya msimamo wao mkali na kulitazama suala hili kwa uoni wa mbali. Wakaangalia nyuma, sasa na mustakbali (hali yao ya baadae) wao na jamaa yao huyu Muhammad, mustakbali majuhuli (usiojulikana utakuwaje). Na pengine walitafakari katika waliyo tafakari, kwamba hawa walioziuza nafsi zao kwa Allah na kuyaendea mauti kwa mori na hamasa hii kubwa. Wakafanya hivyo wakiwa katika hali ya udhaifu wa silaha/maandalizi na uchache wa idadi. Hawakuyafanya yote haya ila wakiwa na yakini ya kupata nusra na ushindi kutoka kwa Allah kwa kuwa wako juu ya haki. Na Makureishi walikuwa wanakiri kuwa waislamu wana haki na hili walitakalo, yaani kuizuru nyumba ya Allah. Na kwamba wao wako katika batili kwa kuwanyima haki yao hiyo, pia hawakupuuzia hata kidogo kwamba siku zote Allah huinusuru haki na kuitupa mkono batili. Kwa hivyo basi lau wao watapambana na waislamu, mapambano yakaisha kwa waislamu kuibuka na ushindi. Basi huo ndio ungekuwa mwisho wa uongozi na utukufu wao miongoni mwa Waarabu wenzao. Hali kadhalika Makureishi waliuona msimamo thabiti usiotetereka wa waislamu na jinsi walivyokuwa tayari kuilinda imani yao hata kwa gharama ya nafsi zao. Kwa hivyo ikawa ni lazima wawaidhike na kunasihika na hali halisi waishuhudiayo na kuihisi kwa milango yao yote ya fahamu/hisia. Na waache kiburi, jeuri, dhulma na upasito wao utokanao na kujiona.

Huenda Makureishi waliyafikiria yote haya, wakaupima mwenendo na mtiririko wa mambo/matukio kwa kugeuka nyuma kuangalia huko walikotoka. Hapa walipo hivi sasa na huko waelekeako ambako hakuna akujuaye wala kubashiri kukoje. Na wakalinganisha baina ya haki na batili katika msimamo wao na baina ya kheri (wema) na shari (uovu) katika suala hili. Baada ya tafakari hizi za kina, ndipo ilipo wadhihirikia kuwa suluhu ni bora zaidi kuliko kuendelea katika dhulma na uadui usio na natija njema. Na kwamba kurudi katika haki ni bora zaidi kuliko kuendelea kushikilia batili. Na kwamba kumili kwenye amani kutaibakisha haiba na utisho wao kuliko vita ambavyo matokeo yake hayajulikani wala kutabirika. Khususan pale walipoiona nia ya Wahabeshi na watu wa Thaqiyf kutaka kujitoa katika ushirika wao. Kwa sababu ya kutokukubaliana kwao na msimamo wao huu wa upasito kumuelekea Muhammad na maswahaba wake. Kwa kuyazingatia yote haya, Makureishi wakaona ni kheri kuiitika mito ya amani itolewayo hata na washirika wao wa karibu. Wakamtuma Suhail Ibn Amrou kuuongoza ujumbe wa watu kadhaa kwenda kuongea na Muhammad juu ya suala zima la suluhu. Huku sharti kuu la mazungumzo haya likiwa ni kumtaka Mtume arudi Madinah bila ya kuingia Makah mwaka huu, ili kulinda heshima na kubakisha heba yao baina ya Waarabu.

 

 



 | Tuandikie |