|
Kama
kwamba Allah Taala alitaka kupima upeo wa subira na nguvu ya imani ya waumini.
Akawapelekea Abu Jandal Ibn Suhail Ibn Amrou katika kitambo ambacho hata wino
wa mkataba wa amani haujakauka. Akawajia akikimbia kutoka Makah akiwa na pingu
za miguu na mikono. Huko Makah atokako alikuwa amefungwa katika nguzo ya chuma
na baba yake; Suhail ambaye ndiye yuko mbele ya Mtume akiandika mkataba kwa
niaba ya Makurayshi. Baba yake aliyetumwa kama mjumbe kwenda kuzungumza na
Mtume, ndipo yeye alipopata upenyo akatoroka mahabusu akiwa na pingu zake.
Akapita njia za uficho akipanda na kushuka majabali mpaka akafika Hudaybiyah.
Waislamu wakampokea kwa shagwe na furaha, wakamtaka hali na kumuweka mahala
apumzike kutokana na machofu ya safari ndefu. Suhail akainua kichwa chake
akatupa jicho, akamuona mwanawe; Abu Jandal aliyemuacha Makah akiwa kifungoni
kwa kosa la kusilimu na kuacha dini ya wazazi wake. Akamuinukia na kuanza
kumshushia kisago cha nguvu, akamkwida barabara, Abu Jandal akapaaza sauti
kutokana na kipigo kikali kilichokuwa kikimshukia: “Enyi kusanyiko la
waislamu, hivi ninarejeshwa kwa mushrikina wanifitinishe na dini yangu?!”,
kauli hii nzito inayogusa imani moja kwa moja ikawazidishia waislamu machungu
juu ya machungu waliyokuwa nayo yaliyotokana na mkataba ule wa upande mmoja
zaidi. Wakaanza kulia kutokana na maneno haya yenye hisia za imani
yaliyotamkwa na ndugu yao wa imani; Abu Jandal. Suhail Ibn Amrou akamwambia
Mtume wa Allah: “Hili ndilo suala la mwanzo nililo andikiana nawe mkataba,
haya mrudishe. Wallah sitaendelea na mkataba mpaka umrudishe kwanza”. Mtume
hakuwa na la kufanya ila kuutekeleza mkataba, akamrudisha huku akimsihi
amuachie. Lakini Suhail akaziba masikio, akayakataa maombi hayo ya Mtume na
pale pale mbele yake na maswahaba akaanza kumpiga usoni na tawi la mti wa
miiba. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia: “Nipe hiba kijana
wako huyu au muokoe na adhabu hii”, Suhail akajibu: “Wallah, hilo silifanyi!”
Baadhi ya wajumbe waliokuwemo katika ujumbe wa Suhail ndio waliomnusuru na
suluba hiyo kali. Halafu ndipo Mtume wa Allah alipopaaza sauti yake na kusema:
“Ewe Abu Jandal subiri na utarajie malipo (ya mateso haya) kutoka kwa Allah.
Kwani hapana shaka Allah atakupa wewe na wanyonge wote walio pamoja nawe (huko
Makah) faraja na muondokano wa dhiki zote hizi! Hakika sisi tumeshafunga
mkataba na watu hawa, sisi tumewapa na wao wametupa ahadi ya Allah nasi
hatuthubutu kuvunja tuliyokwisha yaridhia”.
Hamasa na
mori vikampanda Sayyidina Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-na
kumsukuma kwenda kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamuuliza tena
kama alivyomuuliza mwanzo. Kisha akamuendea Sayyidina Abu Bakri na kumuuliza
pia, halafu akachupia kwa Abu Jandal; mteswa wa imani akitembea pembeni yake
na kumwambia: “Subiri ewe Abu Jandal, hakika si vinginevyo hawa ni mushrikina
tu na vyo vyote iwavyo damu ya mmoja wao ni mithili ya damu ya mbwa tu!” Akawa
akimsogelea karibu na kumkurubishia mkono wa jambia akimtarajia auchukue na
kumpiga nao baba yake, lakini Abu Jandal hakuweza kumuua baba yake.
Akalazimika kukubaliana na matokeo ya imani yake mpaka pale Allah
atakaposhusha faraja yake. Akarudi Makah vile vile akichechemea na pingu zake
na huku waislamu wakimsindikiza kwa macho ya huzuni na masikitiko makubwa.
Macho yao yakafurika na kububujika machozi ya huruma kwa kutokuwa na njia ya
kumuokoa.
V.
Waislamu wagubikwa na
huzuni kiasi cha kukurubia kuuana wao kwa wao:
Suhail na ujumbe wake
walipomaliza kuandika mkataba na kushika njia wakaondoka, Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-akawaambia maswahaba wake: “Inukeni, mchinje, mnyoe na
mfungukane na ihramu yenu”. Hapana hata mtu mmoja aliyeiitikia amri yake hiyo,
akayakariri tena maneno yake hayo mara tatu, lakini wapi bado hakuna
aliyeinuka kutekeleza. Mtume akaingia hemani kwa mkewe; Ummu Salamah akiwa
amewiva kwa ghadhabu, mkewe akamuuliza: “Kulikoni ewe Mtume wa Allah?”, Mtume
akamjibu: “Waislamu wameangamia, nimewaamrisha hawakuamrika!”, halafu
akamtajia hali aliyokutana nayo kwa maswahaba wake. Mkewe akamwambia: “Ewe
Mtume wa Allah! Usiwalamumu, kwani hakika wao wamefikwa na jambo kubwa mno
kutokana na mashaka uliyo jitumbukiza katika suluhu hii, na suala hili la
kurejea bila ya kupata walilolijia limewahemeza”. Halafu ndipo mama huyu wa
waumini alipomshauri atoke bila ya kuzungumza na ye yote, amchinje ngamia wake
wa sadaka na anyoe nywele. Basi Mtume akatoka bila ya kuzungumza na mtu kama
alivyoshauriwa, akamchinja ngamia wake na akamuita kinyozi wake akamnyoa. Watu
walipomuona Mtume akifanya hivyo, nao haoo wakainuka wakachinja na wakaanza
kunyoana mpaka wakafikia kukurubia kuuana wenyewe kwa wenyewe kutokana na
huzuni kuu.
Abdullah Ibn Umar na Abdullah Ibn Abbas-Allah awawiye
radhi-wamesema: “Watu walinyoa siku ile ya Hudaybiyah na wengine walipunguza
tu, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Allah awarehemu
walionyoa”, maswahaba wakasema: Ewe Mtume wa Allah na waliopunguza je?
Akasema: “Allah awarehemu walionyoa”, wakasema tena: Ewe Mtume wa Allah na
waliopunguza je? Akasema tena (kwa mara ya tatu): “Allah awarehemu walionyoa”,
wakasema maswahaba (mara ya tatu): Ewe Mtume wa Allah na walio punguza je?
Mtume akasema: “Na waliopunguza (Allah awarehemu pia)”. Wakauliza: Ewe Mtume
wa Allah wee! Ni kwa nini umewakhusu walionyoa kwa rehema na kuwaacha nyuma
waliopunguza? Akajibu: “Kwa sababu wao hawakuitilia shaka amri yangu”.
Ushindi bayana:
Pamoja na kwamba waislamu
waliuitikia wito wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakawachinja
wanyama wao wa sadaka na wakafungukana na ihramu zao. Lakini bado wao walikuwa
katika muhemezo kulielekea suala hili la suluhu aliyoipitisha Mtume bila ya
ridhaa/kinyume na matakwa yao. Akaipitisha pamoja na dhulma na punjo la wazi
lililokuwemo humo, mpaka wakafikia kumuuliza Mtume juu ya ile bishara ya
kuingia msikiti mtukufu aliyowapa. Kisha isitimie, kwani wanarudi Madinah bila
ya kutufu Al-Ka’abah, nae Mtume akiwauliza: “Kwani mimi nilikuambieni kuwa
mtaingia mwaka huu (au nilisema tu mtaingia)?”, nao wakijibu: “Hapana
(hukusema mwaka huu)”. Ndipo alipowaambia: “Basi bila ya shaka mtaingia (humo)
na mtafanya twawafu, inshallah”, nao wakizidi kumuuliza: “Na jinsi gani
tumrudishe kwa makafiri mtu aliyetujia hali ya kuwa muislamu na wala wao
wasilazimike kuturudishia mtu aliyewaendea hali ya kuwa murtadi?”, Mtume
akiwaambia: “Ye yote miongoni mwetu atakayekwenda kwao, basi Allah asimrejeshe
na atakayetujia kutoka kwao nasi tukamrejesha (kwa ajili ya kutekeleza
mkataba). Basi hapana shaka kuwa Allah atamjaalia faraja na mapito ya kutokana
na dhiki (ya makafiri)”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akakaa
Hudaybiyah kiasi cha siku kumi na kitu. Halafu tena huyoo akashika njia kurudi
Madinah, wakati akiwa njiani ndipo Allah alipomteremshia Suratil-Fat-hi [48].
Watu wakaja wangu wangu mpaka wakamkusanyikia, akawasomea: “BILA SHAKA
TUMEKWISHAKUPA KUSHINDA KULIKO DHAHIRI”. [48:01]. Umar akauliza: “Hivi huu
ndio ushindi ewe Mtume wa Allah?!”, (Mtume) akajibu: “Naam, namuapia yule
ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, hakika huo ni ushindi”. Mmoja wa
maswahaba akarukia na kusema: “Huu sio ushindi kitu, watu tumezuiliwa na
nyumba ya Allah na wanyama wetu pia wamezuiliwa. Na kisha tena Mtume wa Allah
amewarejesha kwa makafiri waumini waliomjia (huu ndio ushindi huu)?”. Kauli ya
mtu huyu ikamfikia Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Ni maneno mabaya
yaliyoje hayo! Basi huu ni ushindi mkubwa kuwahi kutokea, hakika mushrikina
wameridhia kukuzuilieni kwa kutoingia mjini kwao (bila ya kutumia njia ya
vita). Tena wamekujilieni kujadiliana nanyi juu ya suala la suluhu na
kukuraghibishieni amani ilhali wameyaona kwenu yawachukizayo. Nae Allah
akakushindisheni juu yao na akakurejesheni mkiwa salama na ilhali mmepata
ujira (wa nia yenu ya Umrah), basi huu ndio ushindi mkuu nyinyi kuwahi
kuupata. Hivi mmekwisha sahau siku ile ya vita vya Uhud mlipokuwa mkikimbia
mbio, wala hamumsikilizi ye yote ilhali mimi nikukuiteni nikiwa nyuma yenu?!
Hivi mmekwisha sahau pia siku ya vita vya Ahzaab pale walipokujieni
kukushambulieni kutokea juu yenu na kutoka chini yenu. Na macho yalipokodoka
na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkaanza kumdhania Allah dhana mbali mbali?”.
Waislamu wakasema: “Amesema kweli Allah na Mtume wake! Huu wallah ndio ushindi
mkuu kuliko yote, ewe Mtume wa Allah. Sisi hatukuyafikiria kamwe
uliyoyafikiria, wallah wewe unamjua mno Allah na mambo yake kuliko sisi”.
Naam, hivi ndivyo waislamu walivyorejea kutoka Hudaybiyah, nyoyo zao zikiwa
zimetua na kukwatuka na wakayakinisha kuwa Allah amewatakia kheri katika suala
hili la suluhu. Lakini bado walikuwa hawajui kheri hii itatoka wapi, lini na
vipi.
|