Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SURA YA TISA-USHINDI BAYANA

 Faida

SOMO LA KWANZA.

       I.          Huenda mkalichukia jambo na Allah akajaalia kheri nyingi ndani ya jambo hilo.

Waislamu hawakupata katu kuwa na msimamo dhidi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kama waliokuwa nao katika suluhu ya Hudaybiyah. Na wala hawakutokea kumpinga kwa lo lote kama walivyompinga katika suluhu hii waliyoiona kuwa imeegemea zaidi upande mmoja. Na Mtume kwa upande wake hakupata kushika msimamo uliowaudhi na kuwakera kuliko huu, kwani aliipitisha suluhu kinyume kabisa na matakwa yao. Na akaacha kuwataka ushauri katika suala hili tete kama alivyo wazoesha ikiwa ni amri kutoka kwa Mola wake. Na akaukabili ushindani na upasito wa Makureishi kwa upeo wa wepesi na ulaini. Isitoshe akamrejesha adhabuni na fitinani  Abu Jandal wakati ambapo mkataba wa amani ulikuwa haujasainiwa bado kuashiria kuwa umepitishwa na kuridhiwa na pande zote mbili.

Waislamu katika siku hii wakawa na hisia za unyonge na kudhalilishwa, nafsi zao zikachemka kwa hisia kali za utukufu wa imani na nguvu ya mshikamano wa haki. Mpaka Umar Ibn             Al-Khatwab-Allah amuwiye radhi-akafikia kujadiliana na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akionyesha upinzani na chuki ya wazi. Akiuliza kwa mshangao sababu iliyompelekea Mtume wa Allah kuukubali unyonge na uduni huu. Nae Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akimjibu kwa utulivu uliosheheni kujiamini na kuelewa asemacho, akimwambia: “Mimi ni mja na mjumbe wa Allah, sitaikhalifu amri yake na wala yeye hatanitupa na kuniacha”. Hapa sasa ndipo ulipo muhimili unaozungukia kadhia yote hii, kwani ni wazi kuwa maamuzi yote aliyoyachukua Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ulikuwa ni wahyi (ufunuo) kutoka kwa Allah Mola Muumba wake. Kwa lugha nyepesi tunaweza kusema aliyafanya yote aliyoyafanya na katu hakuyafanya kwa matashi ya nafsi yake. Kwa ajili hii basi, hakukumfalia wala kumpasia yeye kwenda kinyume na amri ya Mola wake ambaye aliyemnusuru na kumuunganishia nyoyo za waumini. Na wala hakupaswa kuwataka ushauri maswahaba wake au kufuata maono na fikra zao katika hili na ilhali tayari amekwisha pewa amri kutoka kwa aliye juu ya kila kitu na mwenye busara. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alilihisi hili tangu mwanzoni kabisa pale ngamia wake alipokita magoti kwenye maporomoko ya bonde la Hudaybiyah na maswahaba wake wakasema: “Ameasi/amefanya ukorofi”. Nae akawaambia: “Hajaasi, lakini kilichomzuia ni kile kile kilichomzuia kuingia Makah ndovu (wa Aburahah)”. Na tangia hapo ndipo Mtume akaiandaa nafsi yake kukubali kila hatua inayopelekea kwenye amani na suluhu. Muda wa kuwa msingi wake ni kuyaadhimisha matukufu ya Allah na akaitangaza nia hii njema wazi wazi pale aliposema: “Namuapia yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, leo Makureishi hawataniitia hatua ambazo watayaadhimisha ndani yake matukufu ya Allah. Na ndani yake kuna kuunga udugu ila nitawaitikia”. Sasa pale ilipo mdhihirikia nia ya Makureishi kutaka suluhu, hakusita kuipokea na kuikubali nia yao hiyo na kuanza kuifanyia kazi mara moja. Na akafanya nia yake ni kulifikia lengo hili hata kama kufanya kwake hivyo kutamtumbukiza miibani. Na kwa mtazamo wake lengo hili lilikuwa tukufu na thamani mno kuliko kupotea kwa sababu tu ya maneno ya uchokozi/kukirihisha na mandhari ya ukavu na ugumu wa nyoyo. Ni kwa ajili hii ndio hakuupatiliza upuuzi wa Makureishi katika kadhia hii ya amani. Na akamchukulia mjumbe wao upeo wa kumchukulia kiasi cha kuonwa na maswahaba amekuwa laini mno na kuyakubali matakwa yote ya mahasimu wao. Wala hakuangaishwa na kushughulishwa na mori wa hasira uliowapanda maswahaba wake kutokana na kuridhia kwake kwa kifua kikunjufu ugumu na inadi ya mahasimu wao. Akaendelea na kadhia hii, akiishughulikia kwa hekima/busara na siasa yake makini. Mpaka ikafikilia tamati yake njema akitaraji kwayo kheri kwa Uislamu na waislamu. Kama kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiangalia kwa jicho la ghaibu kilichoko upande wa pili/nyuma ya suluhu hii. Suluhu ambayo ilitazamwa na maswahaba kuwa ni kukubali unyonge na kudunishwa katika imani yao ya kweli.

Kwa kweli suluhu hii ilitoa matunda yake haraka mno kuliko ilivyo tazamiwa na waislamu. Na ilileta natija ya kushangaza mno kuliko ilivyo sawirishwa katika fikra na maono yao. Na matunda yake yalikuwa mazuri mpaka Allah Taala mwenyewe akayaita kuwa ni: “USHINDI ILIO DHAHIRI (bayana)”, kama kwamba ushindi huu bayana ulikuwa ni mlango ulioficha kheri nyuma yake au ni kizuizi kinachozuia mafuriko. Mlango/kizuizi hiki kilipofunguka kheri ilichimbuka mchimbuko wa kasi na enevu. Hivi ndivyo Allah Taala anavyolizungumzia tukio zima la suluhu hii ya Hudaybiyah: “BILA SHAKA TUMEKWISHAKUPA KUSHINDA KULIKO DHAHIRI. ILI ALLAH AKUSAMEHE MAKOSA YAKO YALIYOTANGULIA NA YANAYOKUJA, NA KUTIMIZA NEEMA ZAKE NA KUKUONGOA KATIKA NJIA ILIYO NYOOKA. NA AKUNUSURU ALLAH NUSURA YENYE NGUVU KABISA... ALLAH ANAKUAHIDINI NGAWIRA (nyara) NYINGI MTAKAZO ZICHUKUA; KISHA AMEKULETEENI HAYA KWANZA (kabla ya hayo) NA AKAIZUIA MIKONO YA WATU ISIKUFIKIENI, NA ILI IWE DALILI (ya kheri) KWA WAUMINI NA KUKUONGOZENI NJIA ILIYO NYOOKA. NA (atakupeni ngawira) NYINGINE, HAMJAWEZA KUZIPATA BADO, (ambazo) ALLAH AMEKWISHA ZIZINGIA, NA ALLAH NI MUWEZA WA KILA KITU”. [48:1-3, 20 & 21]

 



 | Tuandikie |