|
Ikawa katika jumla ya matunda ya suluhu hii, ni
kusitishwa kwa vita baina ya waislamu na Makureishi. Ni vema ikakumbukwa
kwamba hawa Makureishi ndio waliokuwa kikwazo kikubwa tangu kudhihiri kwa
Uislamu. Na uadui na chuki zao dhidi ya Uislamu na waislamu ukawa ndio
chemchem na shina la mabalaa yote yawafikayo waislamu. Na Waarabu wengine na
Mayahudi nao wakawa wanafuata nyayo za Makureishi katika kuhakikisha kuwa
Uislamu unakufa. Kama kwamba Makureishi ndio waliokuwa kijinga cha moto
kinachowasha moto wa uadui na chuki dhidi ya waislamu. Ilipotimia suluhu baina
yao na waislamu, kijinga hiki hatari kikawa kimezimika chenyewe. Na hivyo
kuufanya moto ukizungukao kugeuka na kuwa majivu yasiyomdhuru hata mdudu
chungu. Tumeona hukoo tulikoanzia kwamba mara tu Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-alipoanza kuitekeleza amri ya kufikisha ujumbe wa Allah kwa
waja wa Allah. Hapo hapo Makureishi nao wakaingia kazini na kutangaza vita
dhidi yake ikiwa hatoacha kuendelea kuitangaza imani hiyo ya Mungu mmoja.
Wakamuwekea vikwazo vya kila namna ili tu asiweze kufanikiwa kupata wafuasi.
Wakati mwingine wakatumia propaganda na kueleza kuwa yeye ni mchawi, mara
kuhani, mara mwendawazimu na mara nyingine wakisema kuwa ni muongo.
Wakiwatahadharisha watu katika misimu ya Hijah na Umrah dhidi ya shari na
uchawi wake ili wapate kumtenga. Mpaka wakafikia kumuweka yeye na watu wake
katika vikwazo na kuhakikisha kuwa hakuna kiingiacho wala kutoka kwao mpaka
wasalimu amri. Vikwazo hivi vilikaribia kuwaua kwa njaa na isitoshe
waliwabadilishia maswahaba wake anuwai za adhabu. Kiasi cha kufikia kuwatoa
kwa nguvu majumbani mwao na kuwanyang’anya mali zao. Na wakala njama za kumuua
Mtume mpaka wakamlazimisha kuhamia Madinah na huko bado wakaendelea kumfuata
na kumshambulia. Wakishirikiana na Mayahudi wa Madinah kufanya majaribio
kadhaa ya kumuua na wakimkusanyia majeshi shirika na kumuundia makundi ya
kumuangamiza. Matukio mfululizo muambatano haya yasiyokoma, ndiyo
yaliyoyafanya maisha ya Mtume na maswahaba wake kuwa ni jihadi endelevu na
mapambano ya nguvu.
Kisha tena hawa hawa Makureishi baada ya kibri na inadi yao,
baada ya upinzani wao usiochoka na uadui wao mkali. Sasa wamekuja kukaa na
mahasimu wao hawa katika meza moja ya mazungumzo wakitaka kusimamishwa vita na
kupatikana amani baina ya pande mbili hizi. Wakiikubali wenyewe amani baada ya
kuikataa huko nyuma na kumtuma mjumbe wao kwenda kujadiliana na Mtume juu ya
suala la suluhu. Kuna fursa gani nyingine iliyokuwa nzuri kuliko hii kutumiwa
na Mtume wa Allah kwa maslahi ya Uislamu na waislamu?! Fursa itakayofungua
ukurasa mpya kwa mlingano (da'awah) wa Uislamu ambao Mtume amekuwa akipigania
kusimama kwake. Kwa yakini, hii ilikuwa ni fursa adhimu na adimu ambayo ni
khasara tupu kuipoteza. Na ni fursa ambayo haikupaswa kuzuiwa na kupotezwa kwa
sababu ya mambo ya kipuuzi yaliyojitokeza. Khususan upande wa Makureishi
uliotia mkazo usio na maana zaidi ya kuonyesha jeuri yao iliyofurutu ada. Kwa
hakika Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliitumia vema fursa hii,
akaupitisha mkataba wa amani baina yake na Makureishi. Tena akaipitisha suluhu
kama walivyotaka Makureishi, bila ya kujali ghadhabu ya maswwahaba wake wala
ujinga/upuuzi wa Makureishi na tashdidi zao. Kwa kitendo chake hiki kitukufu
chenye kusifiwa na kufanywa kuwa ni ruwaza/kigezo chema kwa kila kiongozi wa
uma. Akawa amepiga na kusajili mfano bora kabisa katika medani ya siasa,
hekima na diplomasia. Na hapo hapo akawa ameonyesha uwezo wake mkubwa katika
kuyachunguza mambo na umahiri wake mpana katika kuangalia natija/matokeo ya
mambo.
III.
Waislamu wakawa na uwezo
wa kuwasiliana na watu katika vitongoji vyao na kuwafikishia ujumbe wa Allah
bila ya bughudha.
Katika jumla ya matunda bivu ya suluhu hii ni
kufunguka uwanja wa kazi ya da'awah kwa waislamu na hivyo kuwafagilia njia ya
kuzifikia nyoyo za walengwa. Kwani baada ya kuwa waislamu wamefungika Madinah
peke yake, hawana fursa ya kufikisha ujumbe nje ila kwa uficho mkubwa. Wakiwa
wamekatiwa mawasiliano na makabila ya Kiarabu yale yaishiyo mjini na yale ya
mashambani. Kwa kupita na kuridhiwa suluhu na pande mbili hizi hasimu, sasa
kukawamkinikia waislamu kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na watu katika
vitongoji vyao. Na wakaweza kukutana na kuchanganyika na watu katika
sehemu/makazi yao na kuwafikishia ujumbe wa Allah. Wakiwafafanulia misingi ya
dini hii ya haki na ukweli na hakika ya wito wake na kuwaonyesha misingi ya
utu na tabia njema zinazolinganiwa na dini hii. Watu kutokana na hali na
matendo ya waislamu wanayoyashuhudia na mwenendo wa Mtume wanaousikia na
kuuona kwa macho yao wenyewe. Wakaanza kuujongelea, kuukubali na hatimaye
kuukumbatia Uislamu baada ya kuona uzuri wa misingi na mafundisho yake kupitia
kauli na amali za waislamu na Mtume wa Uislamu. Kwa njia hii, Uislamu
ukatangaa na kuenea kwa kasi katika makabila ya waarabu na watu wengi
wakaupokea kama njia ya maisha yao na imani yao ya uwokovu. Mzingo na wigo wa
Uislamu ukazidi kutanuka siku hata siku mpaka Makah yote ikawa imesilimu na
kuikubali haki. Nayo idadi ya waislamu ikazidi kuongezeka na kurudufika, kiasi
haikupita miaka miwili tangu kumalizika kwa tukio la Hudaybiyah. Mpaka Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaingia Makah akiwa na kundi la maswahaba
wasiopungua elfu kumi. Wakati ambapo siku ile ya Hudaybiyah jeshi lake
halikuwa na askari zaidi ya elfu moja na mia sita.
Kama alivyojishughulisha Mtume na jukumu la kuutangaza na
kuueneza Uislamu katika miji ya Waarabu. Ndivyo hivyo hivyo alivyochukua
juhudi ya kuueneza katika falme na nchi zilizomzunguka. Akawaandikia ujumbe
rasmi viongozi na wafalme wa nchi hizo, akiwalingania Uislamu. Akawateua na
kuwakabidhi kazi hii ya kufikisha ujumbe kwa wafalme na viongozi hawa watu
mahiri miongoni mwa maswahaba wake. Akawatuma mtu mmoja, barua moja kwa mfalme
mmoja, pamoja na ukweli kwamba wengi wa wafalme na viongozi walengwa hawa
kutozipokea vema barua za Mtume wa Allah bali hata hao wajumbe wa Mjumbe wa
Allah. Bado sauti ya uislamu ilifika na kurindima katika nchi hizo mpaka Allah
akazitiisha na kuupokkea Uislamu katika kipindi kisichozidi miaka thelathini.
|