Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

IV. SULUHU YA HUDAYBIYAH YAWAKASIRISHA MAYAHUDI

 Faida

 

 IV.          Suluhu ya Hudaybiyah yawakasirisha Mayahudi na kuamua kuvunja ushirika wao na Makureishi.

          Miongoni mwa matunda matamu yaliyopatikana kutokana na kuupanda mti wa amani wa Hudaybiyah. Ni kule Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuutua mabegani mwake mzigo wa kuwafikiria Makureishi. Na badala yake akazielekezea nguvu zake zote kwa Mayahudi ambao ndio waliokuwa adui nambari mbili nyuma ya Makureishi. Hawa waliendelea kutumia njia zao za hila na vitimbi na mbinu chafu kuzidhoofisha nguvu za Uislamu na kuzivunja nguzo zake. Mpaka dola ya Kiislamu isisimame na wala waislamu wasiwe na sauti/nguvu. Tegemeo lao la kwanza katika kuzitekeleza dhamira zao chafu hizi na kuyafikia malengo duni yao haya, lilikuwa ni Makureishi. Na la pili yalikuwa ni makabila ya Waarabu waliokuwa jirani nao. Sasa basi, ilipofikiwa na kuridhiwa suluhu baina ya Waislamu kwa upande mmoja na Makureishi kwa upande wa pili. Na miongoni matokeo ya suluhu hii ikawa ni kusitishwa kwa vita baina ya pande mbili hizi kwa  kipindi maalumu. Ambacho hicho kitakuwa ni kipindi mpito cha amani, hili likayavuta makabila mengine ya Waarabu kutaka amani. Mayahudi wakawa kama kwamba wametengwa na washirika wao (Waarabu) dhidi ya hasimu wao mkubwa Muhammad. Mtandao wao dhidi ya Mtume na waislamu ukawa finyu kuweza kutoa upinzani wa haja. Hapa ndipo waislamu walipoamua kutoipoteza fursa hii adimu, wakajiandaa kuitumia vema fursa hii ya dhahabu kwa maslahi ya Uislamu na Waislamu. Wakafanya maandalizi ya kutosha kumfagilia mbali adui huyu msaliti mwenye vitimbi. Adui isiyoaminiwa shari yake iwezayo kuripuka na kuhatarisha usalama wao wakati wo wote. Adui isiyotarajiwa kheri yake kuwa iko siku atakuwa na matangamano na mahusiano mema na jirani zake. Hapo ndipo yalipofuatana matukio kama yale ya Khaybar, Fadaka, Taymaa na kwingineko. Kupitia matukio hayo, Allah akautia nguvu na kuupa ushindi Uislamu na kumdhalilisha na kumtenza nguvu adui huyu muovu.

 

SOMO LA PILI.

 

       I.          Makureishi waikiri haki ya waumini kuizuru nyumba ya Allah.

          Katika jumla ya natija njema zilizotokana na suluhu hii, ni Makureishi kuikiri haki ya waislamu kufanya ziara katika nyumba ya Allah. Na kwamba hili lifanyike na kutimia chini ya mazingira ya amani bila ya vita. Huku kukawa ni kufuzu kukubwa kwa Waislamu Madinah na kheri na baraka kwa waislamu wanyonge waliokuwa Makah. Kwani huko Makah walikuweko waislamu wake kwa waume wasiotambuliwa na Mtume na hata maswahaba wake. Hawa walikuwa ni miongoni mwa hao wanyonge wasioweza kuitangaza wazi imani yao. Na wala hawana njia wala upenyo wa kukimbia kutoka Makah kwenda Madinah kwa ajili ya dini yao. Lau basi vita vingeliuma baina ya pande mbili hizi, hapana shaka kwamba wengi wa wanyonge hawa wangelikuwa miongoni mwa wahanga wa vita hivi. Na waislamu wangeliwaua ndugu wao hawa wa imani pasina kuwajua na hili likawatia khasarani kwa kuwapoteza ndugu zao hao, tena kwa mikono yao wenyewe. Hivi ndivyo Allah Taala anavyolitaja hili kwa njia ya kumsumbulia na kumkumbusha neema hiyo Mtume wake na waumini wote kwa ujumla. Haya na tusome kwa mazingatio: "NA YEYE NDIYE ALIYEIZUIA MIKONO YAO KWENU, NA MIKONO YENU KWAO, KATIKA BONDE LA MAKAH BAADA YA KUKUPENI (Allah) USHINDI JUU YAO. NA ALLAH ANAONA (yote) MNAYOYATENDA. HAO NDIO WALIOKUFURU NA WAKAKUZUILIENI KWENDA KATIKA MSIKITI MTUKUFU (wa Makah baada ya kukaribia hapo kwa kiasi cha maili  48). NA WAKAWAZUILIA WALE WANYAMA (mliowachukua kwa ajili ya kuchinjwa) WASIFIKE MAHALA PAKE. NA LAU KAMA SI WANAUME WAUMINI NA WANAWAKE WAUMINI (walioko Makah wanaficha Uislamu wao), MSIOWAFAHAMU MSIJE MKAWASAGA BILA KUJUA, NA KWA HIVYO MKAPATA  MASIKITIKO KWA AJILI YAO (ingalikuwa si haya, Allah asingekuzuieni kupigana nao. Amefanya haya) ILI ALLAH AMUINGIZE AMTAKAYE KATIKA REHEMA YAKE. KAMA (waislamu na makafiri) WANGALITENGANA BILA SHAKA TUNGELIWAADHIBU WALE WALIOKUFURU MIONGONI MWAO ADHABU IUMIZAYO. PALE WALE WALIOKUFURU WALIPOTIA NYOYONI MWAO MORI, MORI WA UJINGA; BASI HAPO ALLAH ALITEREMSHA UTULIVU WAKE JUU YA MTUME WAKE NA JUU YA WAISLAMU. NA AKAWALAZIMISHA NENO LA KUMCHA ALLAH; NAO WALIKUWA NDIO WENYE HAKI ZAIDI NALO NA WALIOSTAHILI. NA ALLAH NI MJUZI WA KILA KITU. KWA YAKINI ALLAH AMEMUHAKIKISHIA MTUME WAKE NDOTO YAKE YA HAKI. BILA SHAKA NYINYI MTAINGIA KATIKA MSIKITI MTUKUFU INSHA-ALLAH KWA SALAMA MKINYOA VICHWA VYENU NA MKIPUNGUZA NYWELE (kama ilivyo wajibu kufanya hivyo wakati wa Hijah). HAMTAKUWA NA HOFU (wakati huo) NA (Allah) ANAJUA MSIYOYAJUA. BASI KABLA YA HAYA ATAKUPENI KUSHINDA (kwanza) KULIKO KARIBU (kuwashinda Mayahudi)". [48:24-27]

 



 | Tuandikie |