Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

I. MACHINJWAJI YA BANIY QURAYDHWAH NA ATHARI YAKE KATIKA NAFSI ZA MAYAHUDI

 Faida

         Kuuawa Baniy Quraydhwah kwa kuchinjwa , kulikotokana na amri ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kuliacha athari isiyofutika katika nafsi za Mayahudi, wakawa wametoshewa, wametunduwaa wasijue la kufanya. Moto wa ghadhabu na uchungu ukitokota na kuwaka mioyoni mwao, ukifunikwa na tabia ya unyonge na uoga iliyokita mioyoni mwao. Wakawa na hisia kali za chuki na uadui zilizo changanyika na hisia kina za khofu na utisho. Hapo hapo wakiwa na mapenzi makubwa ya kutaka kuangamiza na kuponya machungu na ghadhabu yao. Mapenzi yao haya yakawa yanasukumwa na hisia za kusonga mbele na kurudi nyuma na kuingia vitani kuliko kinzana na pupa ya kupenda mno uhai kuliko kufa. Mayahudi walikuwa na udhuru katika muhemeo huu, kwani walikwishapata kipigo kikali kisichosahaulika kutoka kwa Waislamu huko nyuma. Na uzoefu umewaonyesha kwamba adui yao huyu ni mtu wa kuogopwa asiye wa kawaida na mwenye nguvu nyingi. Na kwamba anapata msaada wa nguvu za haki zisizoshindika na nguvu ya kibinadamu. Kwa hivyo basi, sio jambo rahisi kuweza kushindana nae na ukafanikiwa kumshinda hata kama una nguvu kubwa kiasi gani. Pamoja na kuyatambua na kuyakiri yote haya, bado Mayahudi walitamani kuzima mioto yao ya moyoni. Kwa kulipa kisasi na kumuhilikisha adui yao huyu aliye wadhalilisha na kuondosha haiba na heshima yao machoni mwa walimwengu.

Historia sahihi na ya kweli inaonyesha kwamba siku zota Mayahudi ndio waliokuwa wachokozi wakianzisha shari. Na mara nyingi shari waliyoianzisha wao iliwarudia wao wenyewe kwa kushindwa vibaya katika mapambano waliyopata kuyawasha. Pamoja na kushindwa huku kwa mara kwa mara, bado Mayahudi hawakukoma na kuacha uchokozi wao. Kama ambavyo hawakuwaidhika wala kunasihika na matukio yaliyopita, wakauzingatia mustakbali wao kutokana na yaliyopita.na wala kushindwa huko hakukuzituliza wala kuzifuta mioyoni mwao hisia za chuki na uadui kuuelekea Uislamu na Mtume wake. Wakaweza kuishi na Waislamu kwa amani na matangamano mema, hili halikupewa nafasi walau kidogo nafsini mwao. Kinyume chake ni fikra moja tu ndio iliyozitawala akili na mawazo yao, fikra waliyousiana viongozi na wakubwa wao. Hii haikuwa nyingine zaidi ya kuutokomeza Uislamu na waislamu kadiri iwezekanavyo. Mara nyingine fikra hii ikusukumwa na hisia za hasadi na wivu kwa nini utume umehama kwao na kwenda kwa Waarabu. Wakati mwingine msukumo ulitokana na hisia za uadui na chuki binafsi na pengine ni yale mapenzi yao ya kutaka kuangamiza na kulipa kisasi. Kila walipoona wigo wa Uislamu unazidi kutanuka na kuimarika, ndio fikra hii ovu ilipozidi kujikita mioyoni mwao. Wakiburuzwa chini ya taathira zilizotokana na fikra hii, wakifikiri, wakipanga na kupangua namna ya kuitekeleza. Wakitafuta na kuvizia sababu watakazozifanya mlango wa kupitia na kuyafikia malengo yao.

 

  II.            Uadui wa tangu kale wakita mizizi nyoyoni:

           Neno/kauli aliyoitamka kiongozi wao; Huyay Ibn Akhtwa, tangu pale Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipowasili Madinah. Ikawa ndio desturi na kanuni waliyoshikamana na kuifuata Mayahudi wote kuwaelekea waislamu, kwa maneno mengine ikawa ndio sera yao. Hii ndio kauli yenyewe kama ilivyonukuliwa katika Rejea za Historia (tarekh): "Wallah ni uadui tu maisha yote". Naam, ni kweli kauli hii ikawa ndio msingi walioukumbatia Mayahudi wote tangu siku ilipotamkwa. Ikawa ndio sera waliyoitumia viongozi na waongozwa wao na matukio yaliyojiri yakaendelea kuichochea na kuiwasha mioto ya uadui huu. Na yakiudhihirisha katika mandhari inayo onyesha wazi chuki yao dhidi ya mafanikio wayapatayo waislamu. Kwani tangu pale waislamu walipopata ushindi dhidi ya mushrikina katika vita vya Badri. Mayahudi wakaanza kudhihirisha dhahiri shahiri uchungu uliomo mioyoni mwao kuelekea ushindi huu mnono wa waislamu. Mshairi wao mkubwa; Ka'ab Ibn Al-Ashraf akatunga na kupita akiimba mashairi ya maombolezo akiwaombolezea mushrikina waliouawa katika vita hivi. Na akiwahimiza na kuwachochea Makureishi kulipa kisasi na wakati huo huo akitoa maneno machafu dhidi ya wanawake wa Kiislamu. Kama alivyouachilia ulimi wake mchafu kuvinjari kinywani mwake kumtukana na kumvunjia heshima Mtume na akila njama za kumuua pamoja na Mayahudi.

Mshairi huyu mwenye ulimi mchafu alipopata jazaa yake sawia kwa kuuawa na waislamu. Mayahudi wa Baniy Qayunqaa waliinuka na kuonyesha upinzani dhidi ya waislamu na wakiwachochea kuingia vitani kwa kila kauli na matendo yenye kuumiza hisia. Waislamu walipowafurusha kutoka Madinah, kazi yao hii ikashikwa na Mayahudi wa Banin-Nadhwiyr ambao hawa walifanya jaribio lililoshindwa la kumuua Mtume. Nao walipofukuzwa Madinah, kiongozi wao; Huyay Ibn Akhtwab akaanza kukusanya makundi dhidi ya Mtume na waislamu. Na akiwahimiza na kuwachochea Baniy Quraydhwah kuwasaliti waislamu katika mazingira mabaya mno. Huyu nae alipopata ujira wa kazi yake hii chafu, nafasi yake ikashikwa na Abu Raafii; Salaam Ibn Abil-Huqayq. Huyu akajipanga upya na kuanza kukusanya majeshi shirika dhidi ya Mtume na maswahaba wake. Akiitumia mali na utajiri wake aliokuwa nao pamoja na mamlaka//sauti yake kuyaunganisha na kuyakusanya pamoja makabila kuwapiga vita waislamu. Huyu nae alipoulipia uovu wake, nafasi na dhima yake ikachukuliwa na Useir Ibn Rizaam. Huyu tofauti na watangulizi wake, akapanga mbinu zake mwenyewe zisizofuata nyayo za wenzake. Yeye akafungua ushirika na matangamano na Baniy Ghatwfaan ili wawe upande wa Mayahudi wakati Mayahudi wa Khaybar watakapoingia vitani na waislamu.

 



 | Tuandikie |